Ujinga waongezeka kwa 30%

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
IMEELEZWA kwamba asilimia 30 ya Watanzania hawajui kusoma wala kuandika, hali ambayo husababisha kupungua kwa kasi ya maendeleo nchini.

Hayo yamebainishwa bungeni na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya (CCM), aliyetaka kujua kiwango cha Watanzania wasiojua kusoma wala kuandika.

Mbunge huyo katika swali lake la msingi alisema kuwa idadi ya watu wazima wasiojua kusoma wala kuandika ni kubwa na walimu wanaojitolea kufundisha watu hao wamekuwa wakilipwa kiasi cha sh 20,000, kiwango ambacho ni kidogo ambapo aliitaka serikali kuainisha hatua inazochukua katika kurekebisha hali hiyo.

Akijibu swali hilo Mahiza alisema katika kupunguza idadi hiyo serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha idadi ya watu hao inapungua kwa kuendesha elimu ya watu wazima nchini.

Alisema ipo mikakati iliyowekwa na serikali katika kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kuandaa waraka kuhusu wale wanaomaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika na ambao hawajawahi kusoma shule.

Alisema waraka huo utatolewa kwa umma mara utakapokamilika na kupitishwa na mamlaka husika.

Mwantumu alisema wizara kwa kushirikiana na serikali ya Cuba inatekeleza Mpango wa Maendeleo ya Kisomo wa ‘Ndiyo Naweza’ kwa njia ya redio na televisheni.

“Mpango huu utajikita katika stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu pamoja na maarifa yanayohusiana na maisha ya kila siku, wizara ipo katika hatua za mwisho ya kutoa mafunzo kwa wawezeshaji wa mpango huo,” alisema Mahiza.

Aidha, alisema utekelezaji wa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA), Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) na Ndiyo Naweza itaongeza idadi ya watu weanaojua kusoma na kuandika.

Alisema pia mipango hiyo itafuta ujinga na kujenga uwelekeo sahihi kwa wananchi kuendelea kujielimisha maisha yote.

Mahiza alisema kutokana na ufinyu wa bajeti, halmashauri nyingi hazitengi fedha za kutosha kulipa wawezeshaji wote, hali inayosababisha baadhi ya vituo kufungwa kutokana na walimu wa kujitolea kutolipwa kwa wakati.
 
Back
Top Bottom