Uhalali wa Muungano shakani

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Uhalali wa Muungano shakani

na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

UTAFITI uliofanywa na mwanazuoni aliyebobea katika sheria, Profesa Issa Shivji, ambao matokeo yake ameyachapisha kama kitabu, umeibua mambo yanayouweka uhalali wa kisheria wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika mashaka makubwa.

Katika kitabu hicho, kiitwacho ‘Pan-Africanism or Pragmatism?-Lessons of Tanganyika-Zanzibar Union,’ kilichotolewa mwaka huu, Profesa Shivji anabainisha kuwa hatua muhimu za kisheria za kuuhalalisha muungano huo ulioingiwa mwaka 1964, hazikufuatwa, aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya.

Isipokuwa, kikubwa kinachoonekana katika kufanikisha Muungano huo, ni msukumo wa kisiasa na dhamira ya viongozi wakuu wakati huo, Julius Nyerere na Abeid Karume, kujihakikishia usalama wao na wa nchi zao.

Akionyesha misingi dhaifu ya Muungano huo, Profesa Shivji anabainisha katika kitabu hicho kuwa hata katiba ya muda ya Serikali ya Muungano na sheria zake, zilipatikana si kwa kuandikwa upya, bali kwa kuzifanyia marekebisho Katiba na sheria za Tanganyika zilizokuwepo na kuzifanya ziweze kutumika pia Zanzibar.

“Hayo yote yalifanywa na rais, ambaye pia alikuwa anaongoza Muungano, ambaye kisheria alikuwa pia kiongozi wa Tanganyika. Kwa taathira inaweza kusemwa kuwa Katiba ya kwanza ya Muungano, hata ile ya muda, iliwekwa na mtu mmoja, rais,” anasema Profesa Shivji katika ukurasa wa 97 wa kitabu hicho chenye zaidi ya kurasa 300.

Inaelezwa kuwa katika mabadiliko ya katiba yaliyofanyika, licha ya umuhimu wake, hata Karume hakuombwa wala kuelezwa na kutakiwa kutoa maoni kutoka upande wa pili wa muungano.

Kwa upande mwingine, Profesa Shivji anasema kuwa mchakato wa kuunganisha Tanganyika na Zanzibar ulifanywa kwa siri sana, kiasi kwamba baadhi ya watu muhimu, kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati huo, hawakufahamu kilichokuwa kikiendelea hadi dakika ya mwisho.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kuhusiana na matatizo yanayoukabili Muungano hivi sasa, Profesa Shivji alisema anaamini kuwa umefika wakati kwa watu kuulizwa na kutakiwa kutoa maoni yao kuhusiana na Muungano.

“Ingawa Karume hakuwa na utaalamu wa masuala ya sheria, hata angeambiwa atafute msaada kutoka kwa wanasheria, asingefanya hivyo, kwa hofu yake kuwa iwapo suala hilo (muungano) lingejulikana kwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, lingepingwa,” anaandika Profesa Shivji.

Mbaya zaidi, Profesa Shivji anaeleza kuwa Karume hakujali sana masuala ya kisheria kiasi kwamba hata alipoelezwa na Nyerere kwa mara ya kwanza kuhusiana na kuungana, alisema kuwa yupo tayari hata wakati huo wakatangaze muungano, na kuwa Nyerere atakuwa rais.

Msomi huyo ambaye sasa anakalia Kigoda cha Mwalimu Nyerere, anabainisha zaidi kuwa uhalali wa muungano una mashaka makubwa kutokana na kufikiwa bila kuwahusisha wananchi wa nchi mbili zilizoungana.

“Chombo cha kutunga sheria Zanzibar hakikutunga sheria yoyote ya kuhalalisha muungano. Hata kikao cha Baraza la Mapinduzi, kilichofanyika Aprili 25, muda mfupi kabla ya kwenda Dar es Salaam, nacho hakikufikia makubaliano kuhusiana na suala la muungano,” anabainisha.

Mwanasiasa mwingine mwenye utaalamu wa juu kuhusiana na masuala ya muungano, Ismail Jussa, ambaye ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Wananchi (CUF), aliwahi kufanya utafiti kuhusiana na muungano huo na kubainisha kuwa haukuwa halali kisheria.

Jussa, ambaye pia ni mwanasheria, aliandika ripoti hiyo kama sehemu ya utafiti alioufanya wakati akisoma masomo ya juu katika chuo kikuu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Jussa alisema kuwa katika ripoti yake hiyo, aliyoiandika kama sehemu ya kukamilisha masomo yake ya shahada ya sheria mwaka 1999, alibainisha mambo kadhaa ambayo yanaufanya muungano usiwe halali.

Kwanza, alisema kuwa muungano huo haukupitishwa na chombio chochote cha kutunga sheria Zanzibar, na kwa mujibu wa mkataba wa Vienna unaosimamia mikataba ya kimataifa, iwapo hali hiyo inatokea, mkataba husika haupati uhalali.

Pili, Jussa alisema kuwa hata kama mkataba wa muungano ungepitishwa na Zanzibar, kuna vipengele vingi vya makubaliano ya muungano ambavyo vimekiukwa, jambo linalofanya mkataba huo kutokuwa halali.

Alivitaja baadhi ya vipengele hivyo kuwa kipengele kinachoipa Zanzibar nguvu ya kufanya maamuzi kuhusiana na masuala yasiyo ya muungano.

“Awali kulikuwa na masuala 11 tu ya muungano, lakini hivi sasa yameongezwa, hii maana yake ni kuwa uhuru wa Zanzibar kujiamulia mambo yake umeingiliwa, na hii inakiuka makubaliano ya muungano,” alifafanua.

Pia, alisema kuwa kwa mujibu wa makubaliano ya muungano, ilitakiwa iundwe tume ya kutunga katiba na Bunge la katiba, mwaka mmoja baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya muungano, lakini suala hilo lilifanyika mwaka 1977, miaka zaidi ya kumi tangu lilipotamkwa.

Jussa aliyataja mabadiliko mengine yanayoufanya muungano kutokuwa halali kuwa ni kumnyang’anya rais wa Zanzibar wadhifa wa kuwa mmoja wa makamu wawili wa rais wa muungano.

“Kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa, pande zenye uwezo wa kubadilisha makubaliano ni zile zinazoungana. Kwa maana hii, katika muungano, pande hizo ni Tanganyika na Zanzibar.

“Makubaliano ya awali ya muungano ni kuwa rais wa Zanzibar atakuwa mmoja wa makamu wa rais wa Muungano. Hili lilibadilishwa na Bunge la jamhuri ambalo kikatiba halina mamlaka ya kufanya mabadiliko ya mkataba wa Muungano, kwa sababu si sehemu ya waliofikia makubaliano hayo.

Hata hivyo, akiujadili muungano huo, mwanasiasa kijana nchini, Kabwe Zitto, alisema kuwa muungano unaweza kuchukuliwa kwa sura mbili za kisiasa na kisheria.

Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema kwa mtazamo wake yeye, muungano wowote, hasa wa Tanganyika na Zanzibar, ni wa kisiasa zaidi kuliko kisheria.

Akifafanua, mwanasiasa huyo kijana, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alibainisha kuwa hata katika kitabu hicho, Profesa Shivji amekosoa muungano huo na kubainisha kuwa si halali kisheria, lakini akaja kusema kuwa ni halali kisiasa.

Zitto alisema kuwa ingawa chombo cha kutunga sheria Zanzibar wakati huo hakikuhalalisha makubaliano ya muungano, lakini ushiriki wa Wazanzibari katika taasisi za Muungano kama vile serikali na Bunge, kunaufanya muungano huo kuwa halali kisiasa.

“Kwa hiyo mimi naamini kuwa muungano wetu ni halali kisiasa ingawa ukiangalia kisheria kunaweza kuwa na kasoro kadhaa,” alisema.

Muungano huo umekuwa ukipigwa mawimbi makali kwa miaka ya hivi karibuni na kila jitihada za kuweka mambo sawa zimekuwa zikionekana kugonga mwamba.

Katika matukio ya hivi karibuni, mjadala mkali uliibuka kuhusiana na hadhi ya Zanzibar katika Muungano, huku Wazanzibari wengi wakisisitiza kuwa hiyo bado ni nchi kamili ndani ya Muungano, jambo ambalo baadhi ya wanazuoni wanalipinga.
 
Back
Top Bottom