Ufisadi Wetu

MwanaHaki

R I P
Oct 17, 2006
2,401
705
Waheshimiwa Waungwana wa Jambo Forums,

Napenda kujitokeza kwenu kutoa ushauri wangu wa jinsi ambavyo tunaweza kuanza kuitumia taasisi hii nyeti katika kuleta maendeleo na mabadiliko pamoja na mawazo mbadala kwa Watanzania, pia kujipatia tija na manufaa ya kiuchumi.

Kwa mtazamo wangu, na singependa kunukuu vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu, muumba wa viumbe wote vilivyo hai (wasiomuamini Mungu mtanisamehe...), kwamba "usihukumu pasi na wewe kutaka kuhukumiwa pia..."

Sitakuwa nimekosea nikisema, kwa ujumla wetu (mimi nikiwa mmojawapo), tumekuwa na desturi ya kuwahukumu watu tunaowaona kwamba ni wakosefu, wahujumu uchumi na pia wafisadi. Tumekuwa tukipiga kelele kwamba kuna ufisadi mwingi ndani ya nchi yetu tuipendayo na kuwanyooshea vidole watu wengine, sio sisi wenyewe, hususan wale ambao wako kwenye madaraka kwenye taasisi za serikali na binafsi. Ni kweli, ufisadi huo upo tele, lakini, tumewahi kujiuliza kama sisi pia si mafisadi?

Nikitazama, mifano ya ufisadi wetu, ambao ninauita ufisadi jamii, ni mingi sana. Ufisadi wa namna hii una madhara kuliko hata huo wa wizi wa mali ya umma, kwa kuwa tunajua nani mkosaji lakini hata kumyooshea kidole na kumwambia ACHA hatufanyi. Mfano hai, vurugu za daladala, teksi na wakorofi wengine kwenye foleni za asubuhi na jioni jijini Dar es Salaam ni ufisadi wa aina yake, lakini mbona hatukemei? Mbona abiria wanaokuwa ndani ya hizo daladala, teksi na magari mengine hawapigi kelele? Wanaona dhahiri kwamba maisha yao yanahatarishwa na uendeshaji hatarishi kwa maisha yao (ajali haina kinga babu!), lakini wamekaa kimya. Wanaona dereva anawapeleka futi sita chini, wanamwambia Kanyaga tu! Mifano iko mingi.... nadhani mmenielewa.

Wazo langu mimi ni kwa wanachama wote wa Jambo Forums, kama ifuatavyo:

1) Kujitokeza watu 10, ambao kila mmoja ataandika sura moja, inayohusiana na mada moja. Sura hiyo isizidi kurasa 10. Lengo ni kupata kitabu chenye kurasa 100, ambazo zitajumuishwa na kuchapishwa kwenye kitabu kitakachoitwa UFISADI WETU!
2) Mada 10 zitatokana na maoni ya wanachama wa Jambo Forums, kila mada kupigiwa kura kwa muda wa siku 30. Tunayo poll system humu. Kila mwanachama anaweza kutoa mada yake kwenye thread hii, na ikionekana inafaa kuwa mojawapo ya mada kuu 10 zitakazoandikiwa kwenye kitabu hicho, moderators wataiweka kwenye poll ili ipigiwe kura. Demokrasia izingatiwe.
3) Mimi nanitolea taaluma yangu nikiwa kama msanifu vitabu na mhariri (graphic design, typesetting, layout and editing) kukifanyia kazi kitabu hicho BURE. Faida itakayopatikana kwa Watanzania ni zaidi ya mchango wangu huo mdogo.
4) Kitabu kitauzwa kwenye soko huria kwa bei nafuu, lakini nina hakika kwamba maoni ya wanachama wa Jambo Forums yatavuka hata mipaka ya Tanzania.

Ushauri wangu ni kwamba, tuangalie kujikosoa sisi, kuikosoa jamii ya Watanzania, KABLA ya kuwakosoa hao wanaotuibia kila siku. Wao wanaiba kwa kuwa sisi hatujui kwamba, kwanza, tunatakiwa kujifahamu vizuri zaidi, kasoro zetu zianikwe, ili wajue kwamba tunajijua, udhaifu wetu na uimara wetu. Baada ya hapo, kama wataendelea kutuibia, basi watakuwa wanatambua khasara watakayoipata baada ya sisi kuamua kuwachukulia hatua kali... za kisheria au zozote zile zitakazostahili.

Nchini Marekani kuna kitu kinachoitwa Citizen's Arrest, yaani, haki ya raia kumkamata mhalifu na kumchukulia hatua za kisheria, zikiwamo kumweka chini ya ulinzi na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria. Ndio, Tanzania tunachukua hatua kama hizi, lakini kibaka akipatikana anapigwa hadi kufa, kisha kuchomwa moto. Hao walioiba fedha za EPA mbona hatuwataji majina yao? Mbona hatuwakamati, hatuwapigi, hatuwachomi moto? Mbona hatuwafilisi? Tunawaachia wanapeta... nani mwingine wa kuwawajibisha, isipokuwa sisi? Huu nao ni ufisadi... tunaachia mabaya yatendeke pasi na kuyachukulia hatua.

Nimeanzisha mpango huu kwa kuwa wanachama wa Jambo Forums ni watu wenye busara, wenye uwezo mkubwa wa kuchambua masuala mbali mbali, na kuyafanyia kazi. Basi, kwenye hili letu sisi, udhaifu wetu, ufisadi wetu, tuufanyie kazi... tujikosoe, na maoni yetu yatatupa tija kubwa sana.

Mpango huu wa kuandika kitabu kwa pamoja ni mmojawapo wa mipango mbali mbali za kiuchumi ambayo mimi na mmojawao wa moderators (ingawa huu sijamshirikisha...) tumeamua kuiendesha kwa faida ya wanachama wa Jambo Forums. Sasa maoni yetu yalete tija... nasi tufaidike katika kuikosoa jamii yetu, si kuishia kwa akina Afande Mwema bila hatia!

./MwanaHaki
 
Back
Top Bottom