UFISADI: Tatizo ni 'recycling' ya viongozi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

UFISADI: Tatizo ni 'recycling' ya viongozi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mbonea, Nov 13, 2009.

 1. Mbonea

  Mbonea JF-Expert Member

  #1
  Nov 13, 2009
  Joined: Jul 14, 2009
  Messages: 640
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  [​IMG]
  Selemani Rehani​
  [​IMG]
  [​IMG]Chanzo ni CCM kukaa madarakani muda mrefu
  YAPO mambo mengi yanapita katika jamii yetu. Mambo haya yanaibua maswali mengi sana vichwani mwa Watanzania. Ufisadi na rushwa. Ni mambo ambayo yanaigharimu sana jamii yetu.
  Labda, ni vizuri tutafakari chanzo cha matatizo haya ni nini. Hivi sasa kuamniana kumetoweka kabisa. Tuhuma zimekuwa ni nyingi sana. Kila mtu anamtuhumu mwingine.
  Katika miaka ya nyuma tuliweza kujenga jamii ambayo tuliaminiana. Wananchi waliwaamini viongozi wao. Tulikuwa na uongozi ambao uliaminika kwa wananchi. Wananchi waliwaamini viongozi kuwa maamuzi yoyote wanayoyafanya, wanaweka maslahi ya taifa mbele.
  Leo hii imani hii imetoweka. Kila mtu na yake. Hakuna kuaminiana tena. Kila mtu anasema lake. Kauli nyingi zinatoka kwa viongozi ambazo zinapingana. Hakuna maelezo wala majibu ya kuridhisha juu ya kadhia mbalimbali. Kila maelezo yanapotolewa ndio yanazuia maswali mengi zaidi.
  Kama jamii hatuna budi kutafakari na kutafuta chanzo cha matatizo haya. Nchi nyingi, pamoja na sisi wewe wenyewe, huko nyuma tuliweza kudhibiti vitendo vya rushwa kwa sababu tuliweza kutenganisha shughuli za siasa na biashara. Siasa haikuwa tasnia ya kujitayarisha, ilikuwa ni kazi ya kuwatumikia wananchi. Wanasiasa wengi waliishi maisha ya kawaida na kwa kweli wengi wao walikufa maskini.
  Siku hizi imekuwa ni ajira, imekuwa ni biashara na shughuli ya kujipatia utajiri. Wafanyabiashara walifanya biashara na wanasiasa waliwatumikia wananchi. Shughuli za siasa zilifadhiliwa na wananchi wenyewe kwa vipato vyao vidogo.
  Tofauti na sasa shughuli nyingi za vyama zinafadhiliwa na wafanya biashara matajiri wachache. Hiyo inaua demokrasia ndani ya vyama na pia inasababisha vitendo vya rushwa na ufisadi kuongezeka.
  Biashara na siasa ni shughuli ambazo hivi sasa zimefungamana sana. Kwa ufupi, tunaweza kusema kuwa wanasiasa ni watu wanaoshughulika na kuweka taratibu na sheria na kuzisimamia taratibu na sheria hizo na kuhakikisha kuwa haki inatendeka.
  Haiwezekani ukafanya shughuli hiyo na wakati huo huo ukawa mfanya biashara. Makundi haya mawili ni vyema yakajipambanua. Ni maoni yangu kuwa upo uhusiano mkubwa wa tatizo la ufisadi lilipo na mfumo wetu wa maisha ambao umejenga mahusiano ya karibu mno kati ya siasa na biashara.
  Tumeshuhudia wafanyabiashara kwanza wakianza kufadhili shughuli za chama kwa kutoa mapesa mengi, baadae wakaona hiyo haitoshi wakaamua kujitosa katika siasa huku wakiendelea kufanya biashara zao. Hali ya namna hii inasababisha kushamiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi.
  Kukosekana kwa ushindani wa kweli na wa maana katika mfumo wa vyama vingi nayo ni sababu kubwa inayochangia matatizo kadha, ikiwa ni pamoja na uongozi mbovu, rushwa na ufisadi, na uzembe.
  Kwa upande mmoja tuna chama tawala ambacho kimekuwa madarakani kwa muda mrefu sana. Chama hiki kina nguvu na bado kina ushawishi mkubwa na kinakubalika miongoni mwa wananchi wengi. Kina viti vingi bungeni, hivyo kinatwala bunge. Hili imepelekea tuwe na one party dominance.
  Kwa upande mwingine tuna utitiri wa vyama vya upinzani ambavyo ni vidogo, havina nguvu na bado havijakubalika na kuaminiwa na wananchi wengi kushika dola. Vinakabiliwa na matatizo mengi. Vimekuwa vikishindwa vibaya sana katika chaguzi toka kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.
  Takwimu zinaonyesha kuwa vyama vya upinzani bado vina kazi kubwa ya kuwashawishi Watanzania waviamini na kuvichagua. Hivi sasa dalili zinaonyesha kuwa vinazidi kuimarika na kukubalika miongoni mwa wananchi, hasa mijini lakini, uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika hivi karibuni bado unaonyesha kuwa safari bado ni ndefu sana.
  Mwaka 2000

  Chama
  Idadi ya viti
  CCM
  202​
  CUF
  17​
  TLP
  04​
  CHADEMA
  04​
  UDP
  03​
  NCCR - MAGEUZI
  01​
  Mwaka 2005

  Chama
  % ya kura
  Idadi ya viti
  CCM
  70.0%
  206​
  CUF
  14.3%
  19​
  CHADEMA
  8.2%
  05​
  TLP
  2.7%
  01​
  NCCR MAGEUZI
  2,2%
  0​
  UNDP
  1.4%
  01​
  Sura hii inadhihirisha kuwa vyama vya upinzania vimekuwa vikifanya vibaya katika chaguzi mbalimbali. Sababu za kufanya vibaya ni mada inayohitaji mjadala wake pekee. Chama kilichopo madarakani kinapokuwa na na dominance ya namna hii inakuwa ni vigumu kutokomeza na kupambana na rushwa na ufisadi. Tatizo hili ni kwa vyama vyote vya siasa duniani. Conservative ya Wingereza ilikaa madarakani kwa muda mrefu sana na matokeo yake ilijisahau na kuwa mbali sana na wapiga kura mpaka ilipondolewa madarakani na Labour chini ya Tony Blair.
  Ni vigumu sana kwa chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu sana kuepuka, kujitenga na kujipambanua na vitendo vya rushwa. Kama alivyowahi kusema hayati Baba wa Taifa, kuwa kimekuwa kokoro. Akimaanisha kuwa kuwa kokoro lina tabia ya kuvua si samaki tu bali kila kitu, chura, mawe na takataka zozote zile na hata samaki wadogo ambao hawatakiwi kuvuliwa.
  Chama kinachokaa madarakani kwa muda mrefu sana huwa na tabia kadhaa. Hukusanya wanachama ambao hawana maadili kabisa yanayoendana na chama chenyewe. Kwa kuwa chama nacho kinataka ushindi kwa gharama yoyote ile hushindwa kuwakataa wananchama ambao hawaendani na maadili ya chama chao. Chama hupoteza uwezo wa kuwafukuza au kuwavua madaraka wananchama wake ambao wanaonekana kukosa maadili ya chama. Wanachama hawa hujiunga na chama kwa lengo la kupata uongozi ili wakidhi maslahi yao binafsi au waimarishe biashara zao.
  Kupitia siasa hupata nafasi (access) ya kuwa karibu na viongozi wenye kufanya maamuzi, hivyo wanapata upendeleo ambao utawasaidia kupata faida maradufu katika biashara zao.
  Chama kinapokuwa madarakani kwa muda mrefu dhana ya uwajibikaji hupotea. Kwa sababu viongozi wa chama hicho hujikuta ni walewale. Wanazunguka toka nafasi moja kwenda nyingine. (Leadership recycling). Viongozi hawa huwa wanafahamiana, wametoka mbali, wamesaidiana katika mamabo mengi, wanajuana ni marafiki na hivyo inakuwa si rahisi kuwajibishana. Badala yake wanajenga msimamo wa kulindana kwa gharama yoyote.
  Chama kinapokuwa madarakani kwa muda mrefu hubweteka (complacency), na hasa kinapokuwa hakina hofu ya kushindwa na vyama vingine katika chaguzi. Ndio maana tunashuhudia matatizo na kadhia mbalimbali hazipatiwi ufumbuzi au angalau juhudi kufanywa kuondoa kadhia hizo.
  Yamekuwepo matatizo mengi kwa muda mrefu na ufumbuzi wake unaonyesha kushindikana. Matatizo ya migogoro ya ardhi, matatizo ya malipo ya walimu, wafanyakazi hewa ni baadhi tu ya mambo ambayo ufumbuzi wake bado kitendawili. Pia yapo matatizo katika taasisi mbalimbali ambayo yamekuwa ya muda mrefu sana. Kama tungekuwa na ushindani wa dhati, chama kilichoko madarakani kingeweka juhudi kubwa kutatua matatizo hayo kikiogopa kushindwa katika chaguzi zijazo.
  Matokeo yake ni nidhamu ndani ya chama kutoweka. Chama kinakosa uwezo wa kuwaadabisha wale ambao wanaenda kinyume na maadili ya chama. Badala yake majungu, fitna na chuki hutawala miongoni mwa wananchama wenyewe. Matatizo hayatatuliwi katika vikao. Badala ya kutatua migogoro na matatizo kwa njia ya vikao, matatizo hayo hupigwa danadana na kuahirishwa wakidhani kuwa kwa kufanya hivyo, watu wasahau au yataondoka yenyewe.
  Siasa ni muhimu sana katika kuweka mustakabali wa nchi na kujenga uongozi safi, madhubuti na imara. Siasa hufanyika katika vyama vya siasa. Viongozi hutoka katika vyama vya siasa. Kutokana na ukweli huo vyama vya siasa vina umuhimu mkubwa katika kutupatia viongozi safi ili kujenga jamii yenye haki, usawa na maendeleo.
  Vyama safi, huzaa viongozi wasafi, wanachama safi na hatimaye huweza kujenga Jamii ambayo haijagubikwa na vitendo vya rushwa; jamii ambayo inawaheshimu, kuwatambua na kuwazawadia wale wanaopata riziki zao kwa njia ya halali na kwa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na uzalendo.
  Hatuna budi kuangalia upya utaratibu wa kufadhili shughuli za siasa katika vyama vya siasa. Je wanaofadhili wanatoa wapi fedha? Ni fedha safi? Na labda upo umuhimu wa kuweka masuala haya wazi. Kwa mfano, watanzania wengi wangependa kujua vyama vya siasa; CCM, CUF, CHADEMA n.k. vilitumia kiasi gani katika uchaguzi wa 2005?
  Hivyo, ni muhimu sana kujenga ushindani makini, vyama makini ambavyo vitatupa viongozi makini ili waweze kupambana na changamoto mbalimbali ikiwemo rushwa na ufisadi. Hivi sasa ni idadi ndogo sana ya watanzania ambao ni wananchama wa vyama vya siasa. Kama tunataka kuondoa kero hizi na nyingine hatuna budi kuwa hai (active) katika masuala ya siasa, kushiriki kikamilifu ili kujenga vyama imara ili tuwe na uongozi madhubuti na tuweze kutokomeza rushwa na ufisadi.
  Vyama vibovu huzaa serikali mbovu, serikali mbovu hushindwa kupambana na rushwa na kibaya zaidi kama alivyowahi kusema kiongozi mmoja wa zamani, uongozi hutekwa na matajiri.
  Mwaka 1986 na 1987 wakati wa mradi wa kuimarisha chama Hayati Mwalimu aligundua kuwa, CCM ilikuwa imelala usingizi, viongozi wake walikuwa mbali sana na wananchi. Vitendo vya rushwa vilikuwa vimekithiri na viongozi kutumia nafasi zao kwa manufaa yao binafsi. Aligundua kuwa wananchi pamoja na kuwa walikuwa watulivu lakini walikuwa na manugÂ’uniko mengi na walikuwa hawaridhiki na mambo mengi.
  Marehemu Baba wa Tifa aliwahimiza wananchi kuwa wazi, kusema ukweli, mabaya na kukosoa. Inasemekana kuwa hiyo ni sababu moja wapo iliyomfanya marehemu Mwalimu aone kuwa mabadiliko ya mfumo wa siasa toka chama kimoja kwenda vyama vingi yalihitajika. Kuanzia hapo akaanzisha mjadala kwa kusema kuwa si dhambi kujadili mfumo wa vya vingi. Mwalimi alitarajia kuwa vyama vingi vitakifanya chama tawala kiamke na kiondoe tatizo la uongozi ndani ya chama. Bado hutujawa na ushindani wa maana, bado tuna chama kimoja chenye nguvu sana (One Party Dominance) katika hali hiyo uzembe na ufisadi ni lazima.
   
Loading...