Ufisadi huu unatisha

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Ufisadi huu unatisha

Edwin Mtei
Tanzania Daima

NIMESOMA muhtasari (Executive Summary) wa Ripoti ya Kamati Teule ya Richmond na nilipata pia fursa ya kumsikiliza Mhe. Harrison Mwakyembe alipokuwa anaiwasilisha bungeni, licha ya kwamba umeme hapa kwetu ulikuwa unakatika katika kama kawaida.
Kwanza, nijiunge na Watanzania wazalendo wenzangu kuipongeza Kamati ya Mwakyembe kwa umakini, uzalendo na ujasiri walioonyesha katika kutayarisha ripoti hii. Nawapongeza pia waheshimiwa wabunge wote waliochangia siku ile ya mwanzo.

Walionyesha uzalendo na ujasiri na walijali masilahi ya taifa na hasa Watanzania wanyonge. Ni matumaini yangu kwamba mjadala huu utakaoendelea hata baada ya Bunge kumaliza mkutano wake wa 10.

Nimpongeze pia Mhe. Mizengo Pinda kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu na kumtakia kila la heri kwa dhati, katika majukumu haya mazito mapya aliyokabidhiwa na umma wa Watanzania.

Pili, nataka kusema, nakiri kwa dhati kabisa kwamba natishwa binafsi na ufisadi huu pamoja na ule ulioanikwa na ripoti ya wakaguzi wa kimataifa, Ernst & Young, kuhusu Benki Kuu ya Tanzania na matumizi ya akaunti ya EPA.

Nielewavyo ni kwamba bado kuna madudu zaidi yatafichuliwa Benki Kuu na katika mashirika mengine! Najiuliza: Tanzania tunaelekea wapi? Kwanza nashauri tusali, kumwomba na kumsihi Mwenyezi Mungu atuvushe katika majanga haya, kwa ama sivyo nchi hii inaelekea kulipuka.

Tatu, imethibitishwa kwamba kampuni hii ya Richmond inayojidai kutuzalishia umeme ni kampuni feki. Hata kule Houston, Marekani inapodai imesajiliwa, imethibitishwa kwamba jina hilo linatumiwa na kampuni ya uchapishaji wa bahasha na vifaa vya karatasi.

Richmond ilijidai ina uhusiano na Kampuni ya kimataifa ya Pratt & Whitney inayotengeneza mitambo ya umeme, lakini mjumbe wao ni laghai na hajulikani kwa kampuni hiyo.

Katika kutekeleza majukumu yake kulingana na mkataba, Richmond iliweza kuzalisha baada ya utata uliohusiana na mitambo kuwa mibovu na chakavu, umeme wa MW 20 tu badala ya MW 100. Kabla hata kutimiza majukumu kulingana na mkataba, Richmond ikakabidhi mkataba kwa kampuni ya Dowans kwa mtindo wa kiubabe na kutozingatia masharti na taratibu zilizoidhinishwa katika mkataba wenyewe.

Nne, kimaslahi mkataba huu wa Richmond ni wenye kugharimu Tanzania sana. Katika kutekeleza masharti ya mkataba, viongozi wetu serikalini wameonekana watu wasiojali gharama ama kwa kutojua, kuzembea au kwa makusudi kutokana na faida za kibinafsi.

Kwa mfano, pale Richmond walipotaka walipwe fedha za awali kwa Hati Muamana (Letter of Credit) ya dola za Marekani 30 milioni, benki mbili maarufu za Marekani zilikataa. Hii ilikuwa ni dalili au ushahidi tosha na onyo kwamba Richmond walikuwa ni kampuni isiyokopesheka.

Lakini wakubwa serikalini wakang'ang'ania na Benki Kuu kwa mantiki isiyoeleweka, ikatoa dhamana kwa CRDB na kuilazimisha kufungua hiyo Hati Muamana. Kwa hiyo hii kampuni feki ikaanza kulipwa.

Tano, kwa kuzingatia masharti ya mkataba wa kukodisha hiyo mitambo ya Richmond, bei ya umeme ilikuwa kubwa kuliko bei ambazo wale wazabuni wengine wangetoza. Lakini kwa sababu zisizoelezeka wakubwa wetu wakazikubali. Lakini baya zaidi ni kwamba mkataba unalazimisha TANESCO kulipia mitambo hiyo sh 152,000,000 kila siku (capacity charge)!

Mwanzoni mkataba ulikuwa unataka malipo ya capacity charge iwe ni kwa muda wa mwaka mmoja, lakini, bila kujali kwamba hizi ni gharama za ziada na ni kubwa sana kiasi cha kutisha, wakubwa wamekubali malipo haya yawe kwa miaka miwili.

Kwa maana nyingine ni kwamba kila siku, sisi wateja wa TaNESCO tunatozwa fedha za ziada sh 152 milioni zinazokwenda kwa Richmond kwa huduma hewa, pamoja na malipo ya umeme ikiwa mitambo ya Richmond inafanya kazi siku hiyo.

Kwa mwaka huu wenye siku 366 tutalipa sh 152 milioni x 366 = 55,632 milioni kwa umeme hewa kwa vile TaNESCO ni lazima watutoze ili walipe Richmond.

Bila shaka hii gharama ya ziada kwa Kampuni ya TANESCO ni sababu mojawapo ya kuongeza kuanzia Januari mosi mwaka huu, bei ya umeme kwa asilimia 21. Nyongeza hii haitoshelezi, kwa hiyo wanataka kuongeza tena kwa asilimia 40. Mhe. Karamagi, Waziri wa Nishati hata hakuona aibu kueleza wabunge na Watanzania kwamba hili ni ongezeko la lazima.

Halafu nikamsikia Mhe. waziri mmoja akieleza kwamba eti mfumko wa bei nchini umesababishwa na upungufu wa chakula!

Mbona ongezeko hili la gharama za umeme, pamoja na mabilioni yaliyoingizwa katika mzunguko wa fedha kutokana na wizi katika Benki Kuu hayatajwi kama sababu ya mfumko wa bei? Wataalamu wetu wa uchumi na fedha hawashauri hawa mawaziri?

Sisi tungeweza kukubali kuwa bei ya umeme ingeongezeka kutokana na mitambo na spea zake kugharimu zaidi. Tungeridhika pia kama bei ya mafuta ya kuendeshea mitambo ingepanda, au kodi itozwayo ingeongezwa.

Lakini ongezeko la bei ya umeme litokanalo na malipo ya ziada kwa kampuni feki ya Richmond kwa mitambo iliyosimama na isiyofanya kazi ni lazima lipingwe kwa kila njia kwa vile madhara yake juu ya mfumko wa bei yanaenea kote. Hayana mpaka. Kwa hiyo basi wale wote waliohusika kuidhinisha mkataba huu ni lazima waadhibiwe vikali.

Nasema kwamba hawa mafisadi waadhibiwe kwa vile matokeo ya bei ya kuruka ya umeme ni Watanzania wote, matajiri na maskini kutozwa bei kubwa kwa huduma hii muhimu. Viwanda kushindwa kuzalisha bidhaa au kupandisha bei ya bidhaa zizalishwazo. Ajira kupungua kutokana na viwanda au shughuli nyingine za uzalishaji kama kupampu maji ya kumwagilia kupunguza matumizi, kwa vile gharama zimepanda mno.

Hapa nazungumzia hali halisi inavyojitokeza sasa katika viwanda na mashamba yetu yanayomwagiliwa. Huduma za kielimu na za afya zinazohitaji umeme zinagharimu zaidi. Hata serikalini gharama za umeme zimeongezeka!

Baya zaidi na la kulaaniwa ni kwamba Richmond ni kundi la matapeli, likishirikisha viongozi wetu mafisadi, walio na uroho wa kujitajirisha haraka haraka na kutokujali kunyonya damu na jasho la Watanzania wanyonge.

Hawana huruma na Watanzania wanaokosa matibabu na elimu, na wanaomudu mlo mmoja tu kwa siku. Kutokana na fedha hizi za Richmond kulipwa nje ya nchi ni kwamba Tanzania inaendelea kutumbukia katika lindi la umaskini licha ya CCM kutangaza kwamba wananuia kuleta maisha bora kwa Watanzania wote. Hawa mafisadi washauriwe waunde chama chao wakiite "chama cha matapeli".

Fursa iliyojitokeza sasa ni lazima itumiwe kuchunguza kwa kina jinsi kila mmoja wao wa hawa mafisadi alivyojinufaisha binafsi na malipo haya yaliyotolewa kwa kampuni feki. Washiriki wao wote wa ndani na nje wachunguzwe kwa umakini; wale wa nje wakipigwa marufuku kuingia tena Tanzania, isipokuwa tu pale wanapoletwa kushitakiwa katika mahakama zetu kwa kosa hili la jinai.

Wote wa ndani wachunguzwe kwa nia ya kuwaleta mbele ya mahakama endapo inadhihirika hiyo ndiyo stahili yao. Endapo wanapatikana na hatia, si tu wafungwe, bali mali zao zifilisiwe katika juhudi za kurejesha angalau kwa Serikali ya Tanzania, fedha zilizolipwa kwa udanganyifu na ulaghai kwa hii kampuni hewa. Kama kuna wawakilishi wa Richmond ambao wanazurura Tanzania wafukuzwe kama haiwezekani kuwatia mbaroni.

Mwisho, kuna tetesi kwamba mkataba huu hauwezi kutupiliwa mbali eti kwa vile ulikuwa ni baina ya shirika la Tanzania na "mwekezaji" wa nje na hata Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC) kilitoa leseni au idhini kwa Richmond.

Sasa kama imedhihirika kwamba kampuni hii ni feki, na kwamba hata huko kwao Houston, Texas hakuna kampuni inayoshughulika na mitambo ya kuzalisha umeme yenye jina hilo, kwa nini mkataba huu usibatilishwe (abrogated) na malipo yanayofanywa na TANESCO kusimamishwa? Huu mkataba wa Richmond ni 'bogus'. Kama hakuna mtu atakeyetupeleka katika hiyo Mahakama ya Kimataifa, basi tuna kila sababu ya kuutupilia mbali mkataba wa Richmond. Hao wanaosemekana ni wamiliki wa mitambo chakavu iliyoletwa na kufungwa Tanzania, basi wajitokeze aidha wairudishe makwao au waiuze kwa mteja atakayejitokeza.

Pendekezo la kubatilisha (revoke) mkataba wa Richmond ni changamoto kwa Serikali iliyoundwa upya na Mhe. Rais Jakaya Kikwete Februari 12, 2008. Naamini matokeo yake ni kwamba wakubwa hawatathubutu tena kuingia katika ufisadi kwa vile mengi yatafichuliwa. Tanzania bila ufisadi na rushwa inawezekana!

0754 387 177.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom