Tutor B
JF-Expert Member
- Jun 11, 2011
- 9,025
- 6,617
UBOVU WA MFUMO WETU WA ELIMU
Vijana wetu wanakaririshwa vitu vingi pasipo kuwa na utambuzi wa kina juu ya mambo hayo. Niliwahi kuandika humu juu ya tatizo hili; kwamba nilikutana na mkufunzi akiwa na wanafunzi wake wakaihoji ni wapi nilipoipata Azolla – chakula cha mifugo kinachooteshwa kwenye mabwawa.
Yaani mkufunzi anawafundisha wanafunzi vitu ambavyo hata yeye havijui – hakuwahi kuviona kwa macho, anadownload picha na kuwafundishia wanafunzi kama yeye pia alivyofundishwa kupitia picha. Wanafunzi wakimuuliza ni wapi wanaweza kupata mimea hiyo anawatajia nchi kama Hindi Paraguay ambapo ni vigumu wanafunzi hao kufika huko.
Sasa ilitokea bahati nzuri tu kati ya wanafunzi hao alikuwepo mmoja wao ambaye anatumia vyema mitandao; aliwahi kuchart nami akitaka nimhakikishie kama kweli ninayo mimea ya azolla ndani ya Posh Garden – huyo ndo aliwaongoza wenzake na mkufunzi wao kuja kuona kwa macho.
Majuzi wakati natuma miche ya comfrey kwa mteja, nikiwa stand ya Nyegezi alikuja kijana mmoja ambaye ni kati ya wafanyakazi wa mawakala wa kusafirisha vifurushi. Bahati nzuri mzigo huo wa miche ulikuwa na majani yametokelezea kwa nje ya kifurushi. Kijana alipoyaona majani hayo alianza kuwaelezea wenzake kwamba majani hayo walifundishwa chuoni kuhusu mimea yenye uwezo wa kujikinga dhidi ya wadudu waharibifu – majani yana vinyweleo ambavyo vikikuguza kwenye Ngozi vinawasha sana. Maelezo ya kijana yalikuwa sahihi kabisa na ndiyo sababu nilipata hamasa ya kuanza mahojiano naye.
Katika mahojiano alieleza kwamba chuoni walijifunza aina nyingi za mimea ila majina yaliyotumika ni ya lugha za kigeni – akimaanisha botanic names. Kijana alidai kuwamba wakiwa chuoni walioneshwa mimea mbalimbali kwapicha wakafundishwa sifa na matumizi ya mimea hiyo. Nilipomuuliza kama anajua jina la mmea huo alilitaja na kunieleza mambo mengine mengi tu ambayo sikuyajua kabla.
Hoja yangu – ubovu wa mfumo wetu wa elimu unawarundikia vijana wetu vitu vingi vichwani ambavyo hawawezi kuvifanyia kazi. Ifike hatua sasa kila ngazi ya elimu wanafunzi wafundishwe mambo maalum ya kufanyia kazi; na program hii iandaliwe kikanda ili kuendana na uhitaji wa jamii yae neo husika. Nitoe mfano; ngazi ya elimu ya awali Watoto wanaweza kufundishwa namna ya kuotesha mbogamboga na maua bila kutumia udongo – yaani watumie makopo kupata mbogamboga.
Ngazi ya shule ya msingi Watoto wafundishwe ufugaji wa mifugo midogo midogo kama kuku, bata, sungura nk; Ngazi ya diploma wafundishwe uandaaji wa vyakula mbadala vya mifugo kama hydroponics fodder, silage, azolla, wadudu mbalimbali nk. Hawa wafundishwe kwa vitendo namna ya kutengeneza michanganyiko bora kwa ajili ya chakula cha mifugo. Ngazi ya digrii, hawa ni wakubwa – wafundishwe namna ya kupima virutubisho vinavyopatikana kwenye vyakula na mbolea mbalimbali.
Kwa mtindo huo, mfumo wetu wa elimu utakuwa umetengeneza vijana wanaojua mambo mengi ya kufanya ili kutatua changamoto mbalimbali zinazosumbua jamii. Vinginevyo tunaendelea kuzalisha kundi kubwa la wanaoitwa wasomi wakati hawajui lolote lakufanya. Na wale tunaowaita wasomi wakati wakati hawawezi hata kuandaa chips mayai – waandaliwe kozi fupifupi zitakazowawezesha kupata mambo ya kufanya kwenye jamii zinazowazunguka ili wajipatie kipato.
Nitoe mfano wa mwisho; kuna siku nilifanya ziara ya kumtembelea mfugaji wa Samaki anayetumia vizimba ziwani Viktoria; katika timu nzima ya wafanyakazi wake – kuna mtaalam mmoja tu wa ufugaji wa Samaki mwenye elimu ya digrii. Wengine wamejifunza shughuli hizo wakiwa hapo kambini; walioenda kujenga mabanda kwa ajili ya kambi na wenye fani zingine tofauti baada ya shugghuli hizo kukamilika walianza kufundishwa shughuli za ufugaji wa Samaki na sasa ni watu mahili sana kwenye shughuli hii.
Katika kambi hiyo vijana wanafanya mambo makubwa ambayo hata vituo vinavyomilikiwa na serikali hawafanyi mambo hayo; wapo wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali huenda kwenye kambi hiyo kwa ajili ya kujifunza kwa kuona. Hapa namaanisha kitu kimoja; kumuweka mwanafunzi chuoni kwa muda mrefu – miaka 2+ sio kumfanya aelewe. Tuandae kozi fupifupi zitakazowafanya vijana wetu kuwa mahili kwenye utendaji kazi na sio kwenye maelezo ya kwamba wanajua kila kitu – kweli vijana wanajua vitu vingi lakini hawawezi hata kujaribu kuvifanyia kazi.
Tufike wakati sasa, tupaze sauti kwa Pamoja ili wadau wa elimu wafanye mkakati wa maksudi wa kurekebisha mfumo wa elimu na mafunzo ili uweze kuleta tija kwa jamii ya watanzania.
Kwa Pamoja – tunaaweza.
Share hii kwa kadri uwezavyo.
Saint Baika