kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,685
Wiki moja iliyopita katibu wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Khamis Mattaka, akiwa mbele ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi alitoa kauli kali ya kukemea mawaidha na mafundisho yaliyotolewa na masheikh waliotoka Oman wakiwa mkoani Kigoma.
Mafundisho hayo yaliwataka Waislamu kuwaondoa watoto wao katika shule au vyuo vinavyotoa elimu dunia na kuwataka wawahimize zaidi kusoma pekee kitabu kitukufu cha Korani chenye habari za Mwenyezi Mungu. Sheikh Mattaka alibainisha kuwa hiyo ni kinyume na imani ya Uisalamu na pia ni kutowatendea haki Waislamu hapa nchini.
Katibu huyo alisema kuwa mafundisho hayo yana mrengo wa kundi la kigaidi kule Nigeria, Boko Haram, hivyo hayafai kufundishwa hapa nchini mwetu kwani ni upotoshaji dhahiri wa kiimani na kijamii pia na kuwataka Waislamu kote nchini kuyakataa mafundisho ya namna hiyo kwa nguvu zao zote.
Binafsi, naunga mkono hoja ya Sheikh Mattaka kwa imani kuwa ni haki ya kila muumini wa dini yoyote nchini kupata elimu nyingine licha ya kuijua dini yake. Kwa jumla, maisha yana manbo mengi yanayohitaji uelewa ili kukabiliana nayo na kwa hiyo hakuna haja wala sababu ya kuwaondoa au kuwazuia watoto kupata elimu.
Ninaamini, elimu ya dini pekee haitoshi. Ni dhahiri hatuwezi kuchimba madini, mafuta au gesi, rasilimali ambazo tunazo kwa wingi kwa kutumia elimu ya dini. Hatuwezi kuvumbua vyombo vya usafiri na hata kwenda sanjari na sayansi na teknolojia ya wakati huu kwa kuitegemea elimu ya dini pekee.
Ni kweli kwamba elimu ya dini ina umuhimu na mchango mkubwa katika kuyafanya maisha yenye amani na upendo ambayo ni mahitaji muhimu kwa mwanadamu yawepo katika jamii, lakini haiwezi kusaidia pekee kufanya utafiti baharini, angani au migodini. Tunahitaji tiba, uhandisi, uhasibu na hata teknolojia ya kutosha kulinda rasilimali zetu dhidi ya maharamia au kupambana na ugaidi.
Pamoja na maombi tunayoweza kuyafanya kupitia dini, lakini tunahitaji elimu ya kukabiliana na changamoto hizo zote na hili ni jambo muhimu sana. Kwa hiyo, ipo haja kwa Serikali kuingilia kati na kutolipuuza hili kwa kuwachukulia hatua za kisheria wageni wote wanaoingia nchini na kukiuka na kuvuka mipaka ya sababu walizoombea vibali vya kuingia kwao nchini kwa kuwa hilo linaweza kusababisha balaa kwa nchi yetu siku za mbele.
Suala muhimu katika kufanikisha hili ni wananchi kutoa taarifa zote zinazohusu watu katika mamlaka husika. Sheikh Mattaka alibainisha kuwa Boko Haram walianza taratibu na hakuna aliyewajali kwani mamlaka nchini Nigeria ziliamini kuwa hakuna atakayewaamini, lakini hivi sasa wamekuwa tishio la usalama na amani nchini humo na kwingine Afrika Magharibi na hivyo akaomba kila mtu kutimiza wajibu wake katika kulinda amani tuliyonayo.
Hata Mzee Mwinyi, aliyekuwepo katika kongamano hilo aliasa juu ya matendo maovu yanayofanyika katika jamii kwa kisingizio cha Uislamu na kufafanua kuwa hiyo ni dini ya mapatano isiyohitaji matumizi ya nguvu kuieneza au kuongeza wafuasi. Habari za mapigano au utekaji nyara unaofanywa sehemu nyingi duniani kwa maelezo ya kutokana au kuhusishwa na mafundisho ya dini tumekuwa tukiyasikia kupitia vyombo vya habari.
Hivyo, Watanzania hatuna haja wala sababu ya kuyakaribisha mambo hayo hapa nchini mwetu… tuyakatae na kuyapinga kwa nguvu zetu zote. Ni kwa masilahi ya nchi yetu ambayo siku zote imejitangaza kama kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano, hatuna budi kwa pamoja kuhakikisha tunu hizi zinalindwa kwa gharama zozote zile.
Lazima tutambue kuwa kama nilivyoeleza awali, nchi inaweza kupiga hatua na kujikomboa kutoka kwenye umaskini na matatizo mengine kama itashiriki kikamilifu katika kutoa elimu kwa watoto wote bila ubaguzi. Hakuna shaka, kwamba mafundisho kama hayo ya wahubiri kutoka Oman kule Kigoma hayana budi kupigwa vita kwa gharama zozote na badala yake waumini wa dini zote ukiwamo Uislamu wazidi kuwekeza nguvu, akili zao katika mifumo yote miwili ya elimu, yaani dini pamoja na kupata maarifa mengine.
Hivyo, kwa mtazamo wangu, nasema kuna haja ya kuwaunga mkono juhudi za Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu nchini za kukemea na kuchukua tahadhari dhidi ya mafundisho yoyote yanayoenda kinyume na matakwa ya imani na dini hiyo.
Chanzo: MWANANCHI