Tutakukumbuka daima rafiki mpendwa Furaha (Ohaa Masai)...!

Tutakukumbuka daima rafiki mpendwa Furaha (Ohaa Masai)...!

Mtambuzi

Platinum Member
Joined
Oct 29, 2008
Posts
8,809
Reaction score
15,442
Ilikuwa ni siku ya Jumanne ya Disemba 7, 2010, majira ya saa nne asubuhi niko ofisini, nikiendelea na kazi zangu kama kawaida. Nilikuwa na jukumu la kukamilisha ripoti yangu ya juma lililopita ambayo niliilaza kiporo kutokana na kutindikiwa na kazi nyingi siku ya Jumatatu. Nakumbuka nilijihimu sana kufika kazini, nilifika kazini saa kumi na mbili na nusu alfajiri, lakini sijui ni kutokana na uchovu au ilikuwa ni uvivu tu, nilijikuta mpaka kufika saa nne asubuhi nilikuwa sijakamilisha ripoti yangu.

Nikiwa bado naendelea na kazi zangu kivivu-vivu mara simu yangu ikaanza kuita, niliinyanyua na kuangalia jina la mpigaji, hakuwa mwingine, bali ni rafiki yangu aitwae Soudy. Nilipokea simu ile, lakini sauti ya rafiki yangu huyu ilikuwa ni ya huzuni na hata salamu yangu hakuijibu na badala yake alisema tu kwa kifupi "Sir Mtambuzi, Ohaa Masai hatunaye, amefariki hivi punde" nilibabaika sana na kujikuta nikimuuliza maswali mfululizo. Amepatwa na nini? Amepata ajali au? Ameugua? Lakini kabla Soudy hajanieleza sababu ya kifo chake simu yake ilikatika ghafla.

Nijipojaribu kumpigia simu yake ikawa haipatikani. Nilichanganyikiwa sana mpaka wenzangu pale kazini wakawa wananishangaa.
Nilianza kuwapigia watu wa karibu na Soudy lakini nilijikuta nikiwa ni mtoa taarifa, kwani hakuna hata mmoja ambaye alikuwa anazo taarifa hizo, na hata mmoja wa wajomba zake ambaye nilikuwa na namba yake ya simu ilikuwa haipatikani. Wiki iliyopita nilikuwa na huyu kijana niliyeambiwa kuwa amefariki, na nilikutana naye katika Grosary maarufu pale maeneo ya Tabata Bima barabara ya Umoja maarufu kama RN Grosary.

Furaha Laizer ndio jina lake kamili, Wakati anafikwa na umauti alikuwa ndio ametimiza umri wa miaka 19 na ndio alikuwa amemaliza kidato cha nne akisubiri majibu yake ya mitihani. Nakumbuka tulizungumza kwa kifupi sana kwa sababu aliniambia kuwa kuna mahali anawahi, na nilikuwa nimemuomba aje kwangu kuniwekea antenna ya TV, na aliniahidi kuwa angekuja mwishoni mwa juma ambapo hata hivyo hakutokea, na badala yake napokea taarifa kuwa amefariki dunia!
Nilikuwa nikijaribu mara kwa mara kumpigia Soudy simu lakini bado ilikuwa haipatikani. Majira ya saa sita nilifanikiwa kumpata Soudy na alinijulisha kuwa simu yake iliisha chaji kutokana na kuwapigia watu wengi kuwajulisha juu ya msiba huo mzito, na kutokana na habari hiyo kuwastua watu wengi aliowapigia, alikuwa na wakati mgumu kuelezea sababu iliyopelekea kifo cha Furaha Laizer maarufu kwa jina la Ohaa Masai.

Masudi alinijulisha kuwa siku ya Jumatatu ya tarehe 6 Disemba majira ya saa mbili asubuhi Furaha akiwa amelala. aliamshwa na bibi yake kwenda kumdhibiti mjomba wake ambaye ana matatizo ya akili, kwani alikuwa akifanya fujo mtaa wa jirani. Alikuwa anawafanyia fujo akina mama wauza chapati kwa kumwaga chapati zao. Furaha alifika katika eneo la tukio na wakati anamsogelea huyo mjomba wake, mjomba wake mwingine aliyekuwepo hapo alimwambia asimsogelee kwa kuwa alikuwa ameshika chupa mkononi, lakini tahadhari ile ilikuwa imechelewa kwani yule mjomba mwenye matatizo ya akili alirusha chupa ile na kumpata Furaha katika paji la uso upande wa juu wa jicho la kushoto.

Furaha alipepesuka na kukaa chini na kwa muda mfupi uso ulivimba kiasi cha jicho moja kufunga. Kwa kushirikiana na majirani mjomba yule mwenye matatizo ya akili aliweza kudhibitiwa na kufungwa kamba na kupelekwa nyumbani. Furaha aliongozana na mjomba wake aitwae Timber kwenda Kituo kidogo cha Polisi (Police Post) pale Tabata shule na alikuwa akitembea mwenyewe. Alipofika hapo kituoni aliandikisha malezo yeye mwenyewe na kupewa PF 3 ambapo alikwenda Tabata Hospitali pale pale Tabata shule na hakuonekana kama ameumia sana zaidi ya ule uvimbe.Alipofikishwa pale na mjomba wake ghafla alianza kupoteza nguvu na hivyo kulazimika kukalishwa chini.

Baada ya kumuona daktari walishauriwa wampeleke Hospitali ya Amana, iliyoko Ilala. Waliondoka Tabata na baadhi ya ndugu zake wengine wakiwemo majirani zao kadhaa. Walifika Amana majira ya saa nne asubuhi, na wakati huo alikuwa akitokwa damu mdomoni na puani na wakati mwingine alikuwa akitapika damu. Walipomuona daktari waliambiwa wampeleke akapigwe X-Ray.
Baada ya kupiga X-Ray, ikaanza dana dana kutoka chumba kimoja hadi kingine, na kila wanapoingia chumba cha daktari wanaambiwa wamekosea sio chumba hicho wanaelekezwa kumuona daktari mwingine na wakimuulizia daktari walioelekezwa kumuona wanaambiwa ametoka na wamsubiri.

Dana dana hiyo iliendelea hadi saa nane mchana bila mgonjwa kupatiwa matibabu, na hadi kufikia wakati huo Furaha alikuwa akizimia na kuzinduka mara kwa mara. Baada ya kuona hakuna msaada wowote wanaoupata tangu wamfikishe mgonjwa pale hospitalini.
Soudy aliamua kumpigia mmoja wa rafiki zake ili afike pale kusaidia. Rafiki huyo alifika majira ya saa nane mchana na baada ya kuona hali ya mgonjwa ni mbaya na hakuna msaada wowote wa kitabibu alitoa ushauri warudi Tabata katika Hospitali ya Madona. Walipofika Madona daktari aliposoma ile X-Ray akawashauri warudi Hospitali ya Amana, kwa kuwa ile kesi ni kubwa, lakini kutokana na kukatishwa tamaa na huduma za Hospitali ya Amana wakakata shauri waende Hospitali ya Temeke.

Walifika Temeke majira ya saa kumi na mbili jioni na baada ya kutoa maelezo daktari wa zamu alianza kumuhudumia mgonjwa kwa kumuwekea dripu. Lakini baada kuchunguza zile X-Ray akatoa rufaa mgonjwa apelekwe Muhimbili na alitoa ambulance ili mgojwa awahishwe. Walifika Muhimbili majira saa nne usiku na walikalishwa mapokezi mpaka saa sita usiku na ndipo wakaelekezwa wampeleke katika wadi ya Moi, na wakati huo mgonjwa alikuwa hajitambui kabisa ingawa kuna wakati alikuwa akipepesa jicho moja kwa sababu la pili lilikuwa limefunga kabisa kutokana na uvimbe.Daktari aliyempokea mgonjwa alichunguza X-Ray waliyokuja nayo na akashauri kuwa mgonjwa anatakiwa kufanyiwa uchunguzi mwingine na kifaa kiitwacho TC Scan.

Baada ya kutoa ushauri huo aliwataka wale waliomleta mgonjwa waondoke abaki mtu mmoja ambapo walitoka na kukaa nje na kumuacha mjomba wake na Furaha peke yake. Walikaa pale nje wodini hadi saa kumi alfajiri ndipo wakakata shauri warudi nyumbani.
Masudi anadai kuwa hadi anarudi nyumbani hakuwaza kuwa Furaha angefariki kwani yule daktari aliwatoa wasiwasi kwa kuwaeleza kuwa ile hali a kupoteza fahamu ni tatizo la muda tu kwani kuna wagonjwa ambao hupoteza fahamu kwa wiki nzima na huja kuzinduka na kupona kabisa.

Alipofika nyumbani alilala kidogo na aliamka majira ya saa mbili hivi, akiwa njiani kuelekea Hospitali majira ya saa nne alipigiwa simu na rafikie na kupewa taarifa kuwa Furaha amefariki muda mfupi uliopita, baada ya kupigania roho yake kwa takriban masaa 26. Baada ya vipimo vya mwili wa marehemu ilikuja kugundulika kuwa alikuwa amepasuka fuvu la kichwa na hivyo damu kuvuja ndani ya ubongo kitu ambacho, ni vigumu sana kupona, labda kwa miujiza ya mwenyezi mungu.
Tulimzika Furaha siku ya Jumatano Disemba 8, 2010 saa kumi na mbili jioni katika makaburi ya Mbagala, mahali ambapo niliambiwa ndipo walipozikwa babu yake na ndugu zake wengine.

Ni msiba ambao umenigusa sana na sitakaa nimsahau kijana huyu Furaha ambaye alikuwa na furaha wakati wote kama jina lake.
Mimi sipendi kutoa sifa za kinafiki eti kwa kuwa amefariki, lakini naomba nikiri kuwa Furaha alikuwa mtu wa watu, ingawa alikuwa ni mdogo kwa umri na mrefu kwa kimo lakini alikuwa amejijengea marafiki wengi wakiwemo wazee, vijana wa rika lake na pia hata wadogo kwake. Alikuwa akimuheshimu kila mtu na alikuwa tayari kutoa msaada pale anapohitajika kufanya hivyo.

Ni jambo la kusikitisha kuwa Dunia imepoteza nguvu kazi na tegemeo la kesho kwani pamoja na kuwa alikuwa akiendelea na masomo yake ya Sekondari lakini pia alikuwa akisaidiana na mjomba wake kazi za ufundi umeme na hadi kifo kinamkuta alikuwa ni fundi umeme mzuri japo hakuhudhuria masomo hayo chuoni.
Katika mojawapo ya mazungumzo yangu na yeye, aliwahi kuniambia kuwa anatarajia kusomea uhandisi hususan wa umeme, hiyo ndio ilikuwa ndoto ya kijana Furaha Laizer.

Ni kweli ametutoka na tutaendelea kumkumbuka daima, lakini pia ametuachia changamoto kuwa na tahadhari na watu wenye matatizo ya akili hata kama ni mtoto wako wa kumzaa. Pia kuna haja ya familia zenye watu wenye matatizo ya akili kuwapeleka katika hospitali zenye wodi maalum za kuwatunza watu hao, kwani kukaa nao majumbani ni sawa na kuishi na bomu ambalo litakuja kutulipukia hapo baadae.

Ni kweli tunawapenda na tungependa kuishi nao karibu lakini kuna hatari kubwa kuishi na watu wa aina hiyo.
Ni wengi wameguswa na msiba wa Furaha, na ni vigumu sana kuamini kuwa hatunaye, lakini ni vyema tukikubali matokeo kwani kazi ya Mungu daima haina makosa.

Leo hii ninapoandika Tanzia hii, Furaha ametimiza miaka miwili na siku kumi tangu afariki dunia. Namuomba Mwenye-Enzi Mungu ailaze roho ya marehemu Furaha Laizer mahali pema Peponi, Amina

furaha%2Bmasai.JPG
 
oh!REST IN PEACE FURAHA!
pole sana Mtambuzi !
mi katika vitu vinaniumiza kusoma huwa ni tanzia!yani huwa najikuta tu nalia maana tanzia huwa zinatoa bubujiko la kihisia la jinsi mtu alivojisikia kwa mtu aliye marehemu alipokuwa hai!
i wish ningeweza kusoma tanzia yangu!i wish!
 
Last edited by a moderator:
Pole sana.

Kusahihisha kidogo ni kwamba kitabibu kupasuka fuvu la kichwa(Skull Fracture) na damu Kuvujia kwenye ubongo(Intracranial/Intracerebral Haemorrhage) kwa sehemu kubwa ni tatizo linaloweza kutibika na mgonjwa akapona tena hapa hapa Tanzania.

Issue kubwa ni UHARAKA(Emergency), VIPIMO(CT scan) na VIFAA(Theotre, Instruments, Monitors) vingekuwepo tayari tayari naamini Furaha angekuwa hai leo tena akipost humu JF.

*WATAALAM wa afya kutibu hiyo issue wapo hapa hapa Tanzania.
 
daaaah... What a sad story... So saaad so saaaad... MAY HIS SOUL REST IN ETERNAL PEACE... This year angekuwa anamaliza form6...oooh nguvu kazi imeenda
 
Pole sana.

Kusahihisha kidogo ni kwamba kitabibu kupasuka fuvu la kichwa(Skull Fracture) na damu Kuvujia kwenye ubongo(Intracranial/Intracerebral Haemorrhage) kwa sehemu kubwa ni tatizo linaloweza kutibika na mgonjwa akapona tena hapa hapa Tanzania.

Issue kubwa ni UHARAKA(Emergency), VIPIMO(CT scan) na VIFAA(Theotre, Instruments, Monitors) vingekuwepo tayari tayari naamini Furaha angekuwa hai leo tena akipost humu JF.

*WATAALAM wa afya kutibu hiyo issue wapo hapa hapa Tanzania.

Nakubaliana na wewe mkuu, lakini maelezo tuliyopewa hapo Hospitalini ni hayo.............
 
Dah,,, baada ya kusoma kaparagraph ndo cha kwanza ndo nimemkumbuka,,, jamaa nlikuwa nakaa naye mtaa mmoja duh, ni miaka miwili lakini ni kama jana,, tunakumisi sana Furahaa
 
Pole sana.

Kusahihisha kidogo ni kwamba kitabibu kupasuka fuvu la kichwa(Skull Fracture) na damu Kuvujia kwenye ubongo(Intracranial/Intracerebral Haemorrhage) kwa sehemu kubwa ni tatizo linaloweza kutibika na mgonjwa akapona tena hapa hapa Tanzania.

Issue kubwa ni UHARAKA(Emergency), VIPIMO(CT scan) na VIFAA(Theotre, Instruments, Monitors) vingekuwepo tayari tayari naamini Furaha angekuwa hai leo tena akipost humu JF.

*WATAALAM wa afya kutibu hiyo issue wapo hapa hapa Tanzania.
Unalosema ni kweli ndg, uharaka ndio tiba ya mgonjwa....Wiki 2 zilizopita kuna mdogo wangu alipata ajali ya pikipiki na baada ya kufikishwa Amana haraka alihamishiwa muhimbili ICU nao kwa haraka wakamtuma Regency kwa kipimo cha CT scan within 3hrs walikuwa wameshagundua tatizo na kuanza operation ya kichwa iliyochukua muda mrefu kidogo, baada ya siku 3 aliamka usingizini na sasa ni wiki ya 2 yupo nyumbani ufahamu umeanza kurudi ila hawezi kutembea, bt madaktari wameshauri mazoezi baada ya mwezi yatamrudisha hali ya kawaida.....Ninachotaka kusema hapa watanzania tujue kuna tatizo ktk maswala ya afya, tunawazika ndugu zetu tuliostahili kuwa nao...Vp kama Amana pengekuwa na CT scan ni wazi Furaha tungekuwa nae...Fikiri leo hata Muimbili unaambia CT scan imeharibika....jamani tuwe makini tuache kuyumbishwa na wanasiasa.
 
Too sad indeed!! Ila nimejifunza kitu bro Mtambuzi ..kuishi kwenye nchi zetu hizi maskini ni kuishi zaidi kwa kudra tu aisee..lol...ndio maana wenzetu 'developed countries' wanaishi miaka kibao sababu 'longo longo' hakuna!...May his soul rest in peace!
 
Last edited by a moderator:
Nakubaliana na wewe mkuu, lakini maelezo tuliyopewa hapo Hospitalini ni hayo.............

Mkuu ni sawa kuambiwa hivyo but tujifunze pia kutumia akili zetu kutafakari kile tunachoambua na hao wataalam lengo sio ili tuwahukumu bali tujifunze kitu kuepusha madhara yanayojirudia.

*Kumbuka hata Daudi Mwangosi alipo uawawa na polisi yupo jamaa mmoja anaitwa Salum Hapi(Kada wa CCM) alikuja humu na upuuzi wake akidai kuwa ni 'utaalam', eti Daudi Mwangosi alikuwa amevaa bomu la kujitoa muhanga!!

Yote kwa yote pole sana.
 
Back
Top Bottom