Maximo aongezewa mkataba Stars
na Wilbert Molandi
Tanzania Daima
March 19, 2009
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limerefusha mkataba wa kocha mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo wa kuinoa timu hiyo.
Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga, alisema jana ya kwamba, Maximo ameongezewa muda wa miaka miwili, lakini kocha huyo kwa hiari yake ameomba apewe mwaka mmoja kwanza.
Kwa mujibu wa Tenga, Maximo ameomba kipindi hicho cha mwaka mmoja kulingana na programu yake kabla ya kuongeza mwaka wa pili.
Tenga alisema, makubaliano yaliyopo ni kwamba, Maximo ataendelea na mwaka mwingine wa pili kama Stars itapata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini au Mataifa ya Afrika nchini Angola mwaka 2010.
Tangu Maximo aanze kuinoa Stars Agosti 19, mwaka 2006, Stars imecheza mechi 26 za ushindani na kirafiki na kushinda tisa, sare 11 na kufungwa sita.
Tenga alisema, kama upungufu kwa Maximo, utakuwa ni wa kawaida kama ilivyo kwa binadamu yeyote, hivyo kwa kipindi chote ambacho kocha huyo amekuwa na Stars, amekuwa mtu muhimu katika kujenga kikosi bora.