Tunataka Katiba mpya kwa ajili ya nani?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Tunataka Katiba mpya kwa ajili ya nani?

lC.gif
Lula wa Ndali-Mwananzela
Januari 19, 2011
rC.jpg

KAMA jibu lako msomaji ni kuwa “ katiba mpya ni kwa ajili yetu” basi inakupasa uendelee kusoma makala hii kwani yawezekana hukutumia sekunde kujiuliza nimeuliza nini hasa.
Kama bado unashangaa kosa lako ni nini katika jibu hilo basi nina uhakika inakupasa uache unachofanya na kutulia kusoma nitakachofafanua hapa kwani katika kelele na sauti za “katiba mpya, katiba mpya” tunaweza kukosa kile kilichofichika nyuma ya kilio hiki cha wananchi.

Tutafanya makosa makubwa sana kama katika kujadili na hatimaye kukaa chini na kuanza kuunda Katiba mpya tukajikita katika wazo kuwa katiba mpya ni kwa “ajili yetu”.

Nasema tutafanya makosa makubwa kama tutaangalia maslahi yetu sisi Watanzania tunaoishi sasa na kutoka kwayo tuamue Katiba yetu iweje. Kwa maneno mengine, tunapozungumzia suala la Katiba mpya tusifikirie limtanufaisha vipi Dk. Willibrod Slaa, Profesa Ibrahim Lipumba, John Bwana Mapesa Cheyo au Jakaya Kikwete, john Magufuli na Edward Lowassa ifikapo 2015. Ni muhimu kuondokana na wazo la “yetu” kwani tusipofanya hivyo tutaandika Katiba ambayo kwa hakika haitakuwa na matokeo tunayoyataka.

Jambo hili ni muhimu kwa sababu tukiandika Katiba kwa ajili yetu tutajikuta tunajipendelea au tunatoa mawazo yakiwa na lengo la kuwapendelea watu fulani au kundi fulani la watu. Binafsi ninaamini kuwa ili tuweze kuwa na Katiba nzuri tunayoitaka ni lazima tufikirie kuwa tunataka kuandika Katiba ambayo tunataka kuwaachia Watanzania wa kizazi kijacho.

Wazo hili la Katiba kwa ajili ya vizazi vijavyo vya Watanzania likituongoza basi tutaangalia masuala mbalimbali yatakayokuwa mbele yetu kwa mwanga wa maslahi ya Taifa zaidi kuliko maslahi “yetu” sisi wa leo.

Hii ina maana ya kwamba, tutakapokaa na kujadiliana kuhusu Muungano hatutaangalia kwa maana ya kumnufaisha CCM au CUF kule Zanzibar kama ilivyo sasa. Bali tutaangalia kama tunataka kuwarithisha watoto na wajukuu wetu Tanzania hii iliyoungana au tutaamua kwenda njia ya Sudan ambapo itabidi tufikirie kuwarithisha nchi mbili za Zanzibar na Tanzania (sipendi nchi ya Tanganyika!).

Tutakapokaa na kuzungumzia Muungano tutatakiwa kujiuliza katika nchi tunayotaka nafasi za uongozi zitakuwaje na zitagawanywa vipi na mfumo utakuwa wa namna gani. Hapo tutaamua si kuondoa “kero” tu bali kuon’goa “matatizo” ya Muungano kwa kizazi kijacho.

Hatuwezi kuwaachia watoto wetu waje kuamua hatima ya Muungano wakati sisi tunajua historia, na baadhi ya mashuhuda wa Muungano bado wapo hai. Hivyo, tukiongozwa na kufikiria Tanzania tunayotaka kuwaachia watoto wetu tutakuwa na hekima ya nini tufanye na nini tusifanye na kwa nini?

Lakini tukianza kufikira jinsi gani tutakayoamua yatawanufaisha wanasiasa wetu wa leo hii basi tutajikuta tunaacha viporo visivyo vya lazima.

Tukifikiria wazo la “kizazi kijacho” basi tutaangalia suala la mgawanyo wa madaraka na kusimamiana kwa mwanga mzuri zaidi kuliko ilivyo sasa.

Sasa baadhi ya watu watatoa mawazo ambayo watapendekeza madaraka yawe kwa ajili ya kuwanufaisha baadhi ya watu. Kwa mfano, mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yalifanywa ili kumuingiza madarakani Seif Shariff Hamad. Lakini, mtu yeyote akiangalia mara moja utaona kuwa kuna matatizo mengi kwenye mabadiliko yale kiasi kwamba hayawezi kudumu. Nitawaachia wengine wayajadili. Lakini kama ingefikirika jinsi gani mabadiliko yanufaishe wengine basi sina shaka wangekuja na mapendekezo tofauti na kuwa tayari kuishi na matokeo ya mapendekezo hayo.

Tutakapokaa na kuzungumzia nafasi ya Rais wa Tanzania, madaraka yake na majukumu yake, tutafanya makosa kama tutawafikiria wale watakaoingia 2015 ambao kimsingi ni mmoja wetu kati ya watu walio hai sasa hivi. Tutakapokaa kuzungumzia nafasi ya Urais kwenye hiyo Katiba mpya tusiongozwe na fikra za nani atanufaika na mabadiliko hayo 2015. Lazima tuongozwe na kanuni kuwa tunataka watoto wetu wasije kuwa na matatizo na Urais miaka hiyo inayokuja. Hivyo ni muhimu kuongozwa na kanuni ya kuwarithisha watoto mfumo mzuri wa Urais kuliko kujiridhisha sisi na wanasiasa wetu wa leo.

Naweza kuendelea na mifano mingine kwa mfano, tutakapozungumzia suala la Muundo wa Tume ya Uchaguzi tunaweza kufikiria kuandika kwa ajili ya uchaguzi wa 2015 lakini ninaamini mfumo mzuri ni ule tutakaofikiria ambao utawanufaisha watoto wetu huko mbele ya safarini. Uwe ni mfumo gani bora.

Hatuwezi kutengeneza mfumo wa uchaguzi ili kuwaridhisha wanasiasa wa leo hii au vyama vyetu vya siasa vya sasa hivi. Tukifiria kuwa tunataka kutengeneza mfumo wa kunufaisha wanasiasa wa sasa tunaweza tukajikuta tunapitisha mambo ya ajabu sana. Itakuwa ni kama CCM ilivyofanya mabadiliko ya 2005 na mabadiliko mengine huko nyumba ambapo katika kufikiria walikuwa wanafikiria kunufaisha CCM zaidi na ilipotokea kuwa ingeweza kuwagharimu wao wenyewe (kwenye uchaguzi wa 2010) ilibidi watumie “nguvu zaidi” kushinda.
Ninachosema ni kuwa ni vizuri kuimba “katiba mpya katiba mpya” lakini ni lazima tuone kama wengine walioona kabla yetu kuwa Katiba nzuri ni ile inayoweza kutosheleza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya sasa na inatarajia mahitaji ya vizazi vijavyo. Tukumbuke kuwa ni lazima iwe ni Katibu inayotokana na maisha na mang'amuzi yetu vile vile.

Ninaogopa kuwa baadhi ya watu wanaozungumzia “katiba mpya” wanazungumzia kwa kutumia mwanga wa siasa za Kimagharibi na wanatumia hizo kufikiria Katiba yetu iweje. Kama kweli ni Katiba ambayo tunataka kuwarithisha watoto wetu basi ni lazima iwe ni Katiba inayotokana na maisha na mang'amuzi yetu na kuakisi maono, tunu, na njozi zetu kama Watanzania. Vinginevyo, tunaweza kuandika Katiba nzuri kweli na inakila kitu ambacho kitasifiwa na nchi za Magharibi kuwa ni “katiba ya kisasa” lakini tukakuta kumbe haitufai.

Ni sawasawa na simulizi ya mtoto aliyelilia nguo “mpya mpya” na wazazi wakaenda kumnunulia nguo mpya. Aliifurahia na kulinga nayo kwa miezi michache na baadaye ikaanza kumbana. Akaanza kulia tena, “nataka nguo mpya, nataka nguo mpya”; wazazi wakamnunulia nyingine nayo baada ya miezi ikaanza kumruka. Ndipo wazazi wakaamua kununua nguo ambayo atakua nayo kwa muda zaidi na wakaweka na vitambaa vya ziada ili kuhakikisha wanaweza kufanyia marekebisho wakati utakapofika. Na alipoivaa mara ya kwanza aliona inapwaya pwaya lakini kwa kadiri alivyozidi kukua ndivyo ile nguo ilivyozidi kumkaa vizuri zaidi. Watu wakaanza kumsifia kwa jinsi alivyopendeza.

Ndugu zangu, tuwe na mawazo ya wazazi kwa watoto wao ambao huanza kuandaa mambo mbalimbali ambayo wakati mwingine hata watoto hawayaelewi lakini wanapokomaa na kuwa watu wazima wanaona fahari kuwa wazazi walichukua muda kuyaandaa kwa ajili yao. Lakini tukifikiria kwa ajili ya kujifurahisha sisi wenyewe tunaweza tukajikuta tunafanya ufisadi dhidi ya Katiba. Tuongozwe na kiu na hamu ya kutaka kuona Tanzania mpya inajengwa na kuwa Tanzania tuwarithishayo watoto wetu ni Tanzania bora zaidi kuliko ile ambayo sisi tunayo leo. Ni katika kufanya hivyo tu ndipo kweli wimbo wa “katiba mpya katiba mpya” kweli utakuwa na maana.
hs3.gif
 
Back
Top Bottom