Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,883
James Lembeli
Kwa ufupi
- Hii ni baada ya baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na idara za Serikali kumweka kiti moto Diwani wa Sabasabini, Emmanuel Makashi wakimhoji sababu za kusimamia ujenzi wa barabara kwa fedha zilizotolewa na Mbunge wa zamani wa Kahama, James Lembeli aliyehamia Chadema.
Kahama. Wakati Rais John Magufuli akisisitiza kila mara kuwa maendeleo hayana itikadi za vyama huku akiwahimiza Watanzania kushiriki na kusaidia miradi ya maendeleo, hali inaonekana tofauti kwa baadhi ya viongozi na watendaji wilayani hapa.
Hii ni baada ya baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na idara za Serikali kumweka kiti moto Diwani wa Sabasabini, Emmanuel Makashi wakimhoji sababu za kusimamia ujenzi wa barabara kwa fedha zilizotolewa na Mbunge wa zamani wa Kahama, James Lembeli aliyehamia Chadema.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita moja kutoka Kijiji cha Mseki, Kata ya Burugwa hadi Kituo cha Afya Burungwa, imejengwa kwa gharama ya Sh1.5 milioni, kati ya hizo Sh800,000 zikiwa zimetolewa na Lembeli.
Kiwango kingine kilitokana na michango ya wakazi wa kijiji hicho na wafanyabiashara waliokuwa wakiathirika kwa ubovu wa barabara hiyo, ambao kwa hiari walichangisha Sh500,000 kwa ajili ya mafuta ya greda ili kuunga mkono juhudi za Lembeli.
Miongoni mwa waliomweka kiti moto Diwani Makashi ambaye pia ni mfanyabiashara wa eneo la Mseki, ni Diwani mwenzake wa Burungwa ilipo barabara husika, Joseph Masaluta (CCM).
Waliochukizwa
Katika orodha ya waliochukizwa na kitendo cha diwani wa CCM kusaidia na kusimamia ujenzi wa barabara kwa fedha zilizotolewa na Lembeli, wamo baadhi ya watendaji wa Serikali na mbunge mmoja wilayani Kahama.
Akizungumzia sakata hilo, Masaluta ambaye barabara hiyo ipo ndani ya kata yake, alisema kitendo cha mwenzake kusimamia ujenzi huo kwa fedha zilizotolewa na mpinzanim siyo tu usaliti dhidi yake, bali hata kwa CCM.
“Tayari nimewasilisha jambo hilo ngazi za juu za chama na Serikali. Lazima hatua zichukuliwe,” alisema Masaluta.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Michael Matomola alionekana kupingana na wanaohoji sababu za diwani huyo kusimamia mradi huo unaohusisha michango ya wananchi, akiwamo Lembeli ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mseki.
“Sioni tatizo kwa Lembeli kama mkazi wa Mseki kuungana na wenzake kujichangisha fedha kujenga barabara hiyo, kwa sababu ni rai ya Serikali kila mwananchi kushiriki kuchangia miradi ya maendeleo eneo lake,” alisema Matomola.
Akijibu tuhuma dhidi yake, Makashi alisema huo ulikuwa uamuzi wa wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo ambao baada ya kuchanga fedha walimuamini na kumkabidhi dhamana ya usimamizi.
“Lembeli ni mkazi wa Mseki, anawajibika kushirikiana na wananchi wenzake kuchangia miradi ya maendeleo. Tofauti zetu kiitikadi hazipaswi kuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi,” alisema Makashi.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Paulina Ndutu aliyempongeza Lembeli kwa kuwa tayari kushirikiana na wanakijiji wenzake kutatua kero ya barabara.
Akizungumzia sakata hilo, Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa aliunga mkono kitendo cha Lembeli kuunganisha nguvu na wananchi kujenga barabara hiyo, lakini akasema fedha hizo zingewasilishwa ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ambaye ndiye angesimamia utekelezaji wa mradi huo.
Chanzo: Mwananchi