Tume: Watanzania hawapati haki zao ipasavyo

R.B

JF-Expert Member
May 10, 2012
6,296
2,573
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema asilimia kubwa ya Watanzania hawapati haki zao zote kama sheria zinavyoelekeza. Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu, Amiri Manento.

Alisema si rahisi kila mwananchi kupata haki zote, kutokana na muundo ulivyo wa Serikali, miundombinu ya nchi na mazingira yake na wananchi kuwa na tabia ya kutosimamia na kudai haki zao.

“Mtakumbuka baada ya vita kuu ya pili kumalizika na kuacha madhara makubwa kwa binadamu na mali zao, Umoja wa Mataifa (UN) uliona iko haja ya kulinda na kutetea haki za binadamu ulimwenguni kote.

“Licha ya Tanzania kuwa ni mwanachama wa UN na Katiba yetu ya mwaka 1977, inatambua hilo lakini bado asilimia kubwa ya wananchi hawapati hazi zao kama inavyostahili,” alisema Jaji Manento.

Alisema Tume hiyo inashindwa kufanya kazi yake vizuri, kutokana na ukosefu wa rasilimali za kutosha ambazo zitaiwezesha kukidhi matarajio ya watu na mahitaji yatokanayo na majukumu yao.

Alisema ndani ya miaka 10, hawajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi akidai haki yake bali malalamiko mengi yanatoka kwa wafanyakazi wa Serikali na kampuni katika masuala ya ajira, nakala za hukumu, ukiukwaji wa mikataba, promosheni na mambo mengine.

“Mazoea ya wananchi kutokuwa na tabia ya kudai haki zao, ndio yanachangia utendaji wa taasisi kushindwa kuwa na ufanisi kutokana na wananchi kuwa na usiri.

“Katika maadhimisho hayo kutakuwapo na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wakala wa Usajili na Udhamini (RITA), Sekretarieti ya Msaada wa Kisheria (LAS).

“Nyingine ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Kurekebisha Sheria, Wizara ya Katiba na Sheria ambapo kila mmoja atawajibika kutoa ufafanuzi kupitia viongozi wake.

“Pia kila taasisi hizo zitakuwa na kauli mbiu yake kwa mfano kauli mbiu ya THBUB inasema, sauti yangu inachangia, hivyo tunawaomba wananchi wafike na kupata elimu ya kuwasaidia kuishi kwa kudai haki yao,” alisema Jaji Manento.
 
Back
Top Bottom