Tulizoeshwa vibaya katika kubembelezana

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
Mojawapo ya mambo ambayo bado inaonekana hayajakubalika vyema na baadhi ya watu kuhusiana na utendaji kazi wa Serikali ya Magufuli ni hili la kuchukulia na hatua za kinidhamu hadharani. Tumeona Waziri Mkuu na mawaziri wengine wakizungumza na watendaji mbele ya vyombo vya habari kiasi kwamba watendaji wasiokuwa na uhakika na mambo yao wanaanza kutoka jasho wenyewe wakati mwingine unahofia mtu anaweza kuanguka kwa shinikizo la damu.

Tumeona hili kuanzia ile ziara ya kwanza ya Waziri Mkuu bandarini na jinsi gani viongozi wa ngazi za juu ambao katika mazingira yote ya kawaida wanaitwa “vigogo” wakionekana kubanwa mbele ya viongozi wa juu serikalini. Tuliona mtu kama Rished Bade – akiwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania - alivyobanwa na Waziri Mkuu hadi unaona huruma.

Hata alipofanya tena ziara nyingine kwenye eneo la mafuta na kukuta mita za kupimia mafuta zimefungwa na kuanza kufunguliwa kiholela tuliona jinsi Mkurugenzi wa Vipimo alivyobanwa mbele huyo huyo Waziri Mkuu. Siyo yeye peke yake hata Mawaziri wengine nao wameonekana kuchukua mwendo huo huo wa kuchukua hatua bila kuoeneana haya. Kuanzia Mwigulu Nchemba hadi Kairuki na wengine kadhaa suala la kuitana chemba na kunong’onezana mafichoni inaonekana limepitwa na wakati na wapo watu hili limeanza kuwasumbua.

Kilele cha hili tumeona wiki iliyopita ambapo kibano hiki cha kukamatana hadharani nusura kiwageukie mawaziri wenyewe. Hili lilitokea baada ya taarifa kuwa kuna baadhi ya mawaziri na manaibu ambao walikuwa hawajatimiza matakwa kadhaa ya kisheria ambayo yanawataka kujaza fomu fulani fulani za masuala ya maadili. Waziri Mkuu Kassim “Tabasamu” Majaliwa alizungumza na vyombo vya habari na kuwataja kwa majina (kutekeleza maelekezo ya Rais) ya mawaziri hao na kuwa walipewa saa chache tu hadi jioni ya siku ile wawe wamerudisha fomu zile vinginevyo watakuwa wamejiondoa kwenye uwaziri.

Na tunajua uwaziri mtamu. Hakuna aliyezembea tena kwani walijua kitu kimoja kwa hakika kabisa; Magufuli hawatanii na hakuwa amewapiga mkwara mbuzi. Alimaanisha na kama wangetaka kujaribisha kama ni simba au paka wangeamua tu kutotekeleza hilo halafu wangejua.

Hili la juzi limezidi kuwakera baadhi ya watu kuwa kwa nini Magufuli anawadhalilisha viongozi wake tena kawateua mwenyewe. Kwamba, kwa nini asingewaita tu na kuwauliza kwa siri kwa nini hawajarudisha fomu hizo au kutoa maagizo ya kuwa warudishe kwa kuwapigia simu tu badala ya kuwataja mbele ya waandishi wa habari na Watanzania wote kuwajua.

Kuna vitu viwili ningependa tu niviseme kwani kwa watu ambao wamenisoma tangu tuyapinge mabadiliko yale feki wanajua msimamo wangu. Kwamba, nchi yetu ilihitaji uongozi mkali wenye kujenga nidhamu kwa watumishi wa umma tena ulihitaji miaka kumi na tano iliyopita. Leo hii kama tungekuwa na uongozi wa aina hiyo tusingekuwa tunahangaika na mambo haya. Tumepoteza muda mrefu kubembelezana, kunyamaziana na kupigiana simu kiasi kwamba hata hivi majuzi kuna watu wengine bado wanafikiria wanaishi jana. Kwamba, hata taratibu za kiofisi watu walishazisahau. Wapo watu walikuwa wanafanya kazi kana kwamba ni kibarua tu; wanaingia kazini siku moja moja na wakiwa kazini hata siku nzima kazi za umma zinafanywa kama ni ‘ziada’ kwani kazi zao za msingi za kuhakikisha miradi yao inaendelea vizuri wakati wananchi wanasubiria.

Tulikuwa tumefika mahali pabaya mahali ambapo kurudi kwake kusingewezekana isipokuwa kwa lazima. Lakini kubwa zaidi la kuelewa hili ni muhimu watu wakumbuke kuwa viongozi hawa ni viongozi wa umma; ni viongozi ambao wanapaswa kujua wanafanya nini. Mtu unapokuwa Mkurugenzi Mkuu wa chombo fulani maana yake ni kuwa watu wamekuamini kuwa unaweza kuangalia maslahi ya umma. Sasa kama huwezi au inaonekana hujui ufanye nini hadi viongozi wa juu wa serikali waje kwako ina maana ulipaswa kujiuzulu siku ile Magufuli anaapishwa.

Muda wa kuwabembeleza na kuvumulia viongozi na watendaji wabovu ulishapita. Taifa lina watu wengi ambao wanaweza kuongoza taasisi karibu zote na hakuna mtendaji yeyote ambaye anapaswa kujisikia salama ati kwa vile anakalia ofisi fulani yenye viyoyozi na kuendesha gari la kifahari. Muda wa watu kudhani sasa wamefika umepita; muda wa watu kujua na kukumbuka sasa wanalitumikia taifa umerudi.

Wanaoshangaa hili la kufokewa hadharani au kuchukuliwa hatua hadharani inabidi wajifunze nchi nyingine ambazo zimeendelea na waone kama zina tabia hii ya kuoneana haya na kuchukuliana hatua kwenye vyumba vya ofisi tu. Inapofika kiongozi mkubwa wa nchi anafika ofisini kwako na kukuta matatizo muda wa wewe kuitwa pembeni kuulizwa ‘ilikuwaje’ ulishapita.

Watu watajifunza tu na wataheshimu. Wale ambao wanaona yanaweza kuwakuta njia rahisi ya kukwepa huku “kudhalilika” ni kuamua kuandika barua zao za kujiuzulu kabla ya kufikiwa. Wanaweza kuziandika kwa siri huko huko na kuamua kuondoka kwenye utumishi wa umma. Wawape watu wengine nafasi ya kulitumikia taifa na ambao hawataona shida kuonesha matunda ya kazi zao hadharani na hawatokuwa na haja ya viongozi wa juu wa nchi kuwafuatilia kwa karibu kwani wanaonesha weledi na uwezo wao. Hao watapongezwa hadharani.

Raia Mwema
 
Back
Top Bottom