SoC03 Tukizingatia kujiajiri na kuajiriwa inawezekana

Stories of Change - 2023 Competition

Eagle Minja

New Member
Jun 3, 2023
2
0
Ajira ni kazi au shughuli afanyayo mtu kwa ajili ya kujipatia kipato au fedha kama malipo ya hiyo shughuli hivyo inaweza kuwa ni ofisi za binafsi, serikali, shirika/taasisi kwa mkataba maalum kati ya mwajiri na mwajiriwa mfano; daktari, mwanasheria, mwanajeshi, askari polisi.

Kujiajiri ni hali ya kujishughulisha binafsi bila kuwa chini ya uongozi au sheria za mwajiri mfano mkulima mjasiriamali, mvuvi.

Hali halisi ya mazingira au maisha tuliyonayo yanaturuhusu au kutuhitaji kujiajiri au kuajiriwa? Kwasababu sisi kama vijana kwa asilimia kubwa tunategemea kuajiriwa kutokana na tabia/hali ya kuamini kuwa maisha mazuri ni mpaka uwe umeajiriwa isitoshe pia serikali yetu inashauri tujiajiri ingawa haijaweka mfumo madhubuti wa kutuwezesha kujiajiri.

Uhusiano uliopo baina ya Ajira na Jamii/Malezi, Kijana binafsi na Serikali katika kuhakikisha vijana tunaweza kujitegemea, kujiendeleza na kuwawezesha wengine;

Jamii/Malezi
Nikianza na jamii kwa nafasi ya familia kama kianzilishi/msingi wa jamii hadi kufikia kuwa taifa ina wajibu mkubwa sana katika kumuwezesha kijana kufikia malengo kupitia malezi.

Malezi ya sasa yameachiliwa kutolewa na wasaidizi wa nyumbani na watu baki kama ndugu badala ya wazazi hivyo mzazi kushindwa kutambua kipaji au karama ya mtoto tangu akiwa mdogo hivyo basi kumwongezea mwalimu jukumu la kujua mtoto anataka kuwa nani hapo mbeleni.

Hii ni kwa sababu ya wazazi kutingwa sana na shughuli za utafutaji kukidhi mahitaji ya familia. Kwa kiasi kikubwa hii hupelekea wazazi kuwalazimisha watoto wao kusomea fani wasizozitaka mfano kuwa mhandisi angali mtoto ana kipaji cha mpira au Sanaa ingawa anaweza kuwajibika katika nafasi zote ila sasa ile fani aliyolazimishwa na wazazi haitoifanya kwa ubora unaotakiwa au hata kumsababishia kufeli kwa kuwa hana wito nayo hivyo kutokufiti kwenye soko la ajira.

Pia wazazi wengi hawatoi malezi ya kumjengea kijana mazingira ya kujitegemea au kujiajiri hii inaweza kutokana na wazazi kuwa na wadhifa mkubwa kikazi au kwenye uongozi hvyo kuona kwamba mtoto wake hahitaji kujishughulisha sana kwani atarithishwa mali au nafasi kupitia jina la mzazi wake hivyo basi hata kijana pia hushindwa kuonyesha bidii katika kusoma au hata kazi.

Kutokuwa na utamaduni au mfumo wa wazazi kuweka akiba kwa ajili ya maisha ya baadae ya kijana endapo itatokea kuwa aidha mzazi/wazazi wamefariki hivyo kushindwa kujiendeleza kimasomo haswa anapokuwa mdogo hii huweza kupelekea migogoro ya kifamiliaa licha ya kuwa mzazi alikuwa na uwezo wa kifedha au mali baina ya ndugu wa wazazi na mtoto huyo ambaye atakuwa yatima ,pia hata itakapotokea kuwa amemaliza masomo na anahitaji kujiajiri na anakuwa na changamoto ya mtaji.

Nafasi ya serikali katika kumuwezesha kijana katika kuweza kuajiriwa au kujiajiri;
Katika kuhakikisha mfumo wa elimu wa sayansi unaboreshwa haswa kwa shule za sekondari maeneo ya vijijini kuwepo na maabara za kisasa na uwepo wa waalimu wa kutosha wa masomo ya sayansi kama hisabati, fizikia, kemia na biolojia.

Hii itawezesha wanafunzi kufaulu kwa kiwango kikubwa Zaidi na kuwa na maarifa Zaidi ya kuhusu majaribio ya kisayansi hivyo kuondoa mitihani inayokuwa ni mbadala wa kufanya majaribio kuwa mitihani ya kawaida na si kwa vitendo. Hii itasaidia kijana kuwa na maarifa na uwezo mkubwa katika fani ya sayansi iliyo na wasomi wengi.

Kuwezesha utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana na hata jamii kwa ujumla kwa gharama nafuu Zaidi tofauti na jinsi mataasisi yasiyo ya Kiserikali na watu binafsi wanavyotoa mafunzo hayo ili kuwawezesha wao kujiajiri. Hii ni kwa kupitia vikundi vya vijana ngazi ya mtaa, kijiji, kata, tarafa hadi mkoa hvyo kufikia wanajamii kwa kiasi kikubwa Zaidi.

Usimamizi na uboreshwaji wa bajeti ya mikopo kwa kundi la vijana Zaidi ambao ni nguvu kazi ya taifa na viongozi wa baadae ili kuwawezesha kujiajiri na sio kutegemea kuajiriwa kwani idadi ya vijana wasomi inazidi kuongezeka katika jamii huku ukosefu wa ajira ukizidi kuwa changamoto sio kwa Tanzania tu na ulimwengu kwa ujumla.

Muda wa kustaafu kwa waajiriwa upunguzwe ili kuwezesha vijana kuingia katika soko la ajira. Muda wa mwajiriwa tangu anapoajiriwa mpaka kufikia muda wa kustaafu umuwezesha kujiendeleza ili kuruhusu mfumo wa ajira kupokea nguvu kazi mpya ili kuleta mabadiliko zaidi katika uzalishaji na uboreshwaji wa huduma katika ufanisi zaidi kulingana na ukuaji wa sayanasi na teknolojia.

Nafasi ya kijana ili kujitegemea na kujiweka katika ushindani ndani ya soko la ajira;

Kuwa na bidii, juhudi binafasi na utayari wa kujifunza mambo mbalimbali yatakayotuwezesha kuwa na nafasi kubwa katika kujiendeleza licha ya kuwa na taaluma Fulani kama ya ualimu, udaktari, uhandisi na nyinginezo.

Mafunzo kama ujasiriamali, biashara, utoaji wa huduma ya kwanza, maswala ya afya ya jamii pia kuwa na mwanachama wa taasisi mbali zinazolenga kuhudumia jamii kama mwanachama wa Msalaba Mwekundu, Umati(chama cha malezi Tanzania)mwanachama wa vyama vya siasa pia hii yote ni kujiweka katika nafasi ya kukutana fursa mbalimbali kama kijana.

Kujitolea katika mashirika,ofisi na taasisi mbalimbali ili kuongeza ufanisi na uzoefu Zaidi katika fani aliyosomea, pia kushiriki katika shughuli za kijamii kama usafi na utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji hii itachangia kwa kiasi kikubwa kufahamiana na watu Zaidi wenye maarifa na mawazo chanya kuliko kukaa kwenye makundi wakilaumu serikali hakuna ajira na kuikosoa.

Kuchagua watu sahihi wa kuambatana nao watakao hamasisha mafanikio Zaidi kwa vijana ili kuwashawishi vijana wengine wasio na ajira kuona kuwa mafanikio yapo hata pasipo kuajiriwa. Pia kuelimishana juu ya madhara ya madawa ya kulevya na ulevi kwani vimechangia vijana wengi kupotelea huko hivyo kuwa mzigo kwa wazazi na hata taifa.

Hivyo basi kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwa ajili ya kumuandaa kijana kuwa na uwezo wa kujitegemea na kujiendeleza hii imepelekea ajira kuwa changamoto kwa kiasi kikubwa mno angali upo uwezekano wakupunguza tatizo hilo kwa kuzingatia yaliyoelezwa bayana.

Malezi bora yatolewe kwanzia utotoni wazazi wajitahidi kuwa mstari wa mbele kulea, serikali kuboresha mfumo wa ajira kwa vijana, mfumo wa elimu wa sayansi haswa kwa shule za sekondari zilizopo katika kata, uwezeshaji kwa vijana kupitia mikopo na mwisho ni kijana kuweza kujitambua na kuwa na utayari wa kujifunza na kujishughulisha binafsi.

IMG-20230614-WA0039.jpg
 
Back
Top Bottom