TUHUMA DHIDI YA CCM

security guard

JF-Expert Member
Sep 27, 2011
799
603
Ni ujinga mkubwa kudai eti CCM ina viongozi

wenye visasi, wezi, wala rushwa na roho mbaya


Na Charles Charles


“MAGUFULI anaweza kusafisha hekalu lake hata likang’aa na kurejesha heshima ya Tanzania, jipu moja tu ni pale atakaposafisha kwanza CCM na kufanya mabadiliko makubwa kwa kuondoa viongozi wezi, wala rushwa, wapiga dili, wenye roho mbaya na visasi, wambeya na wanafiki wa kisiasa”, anasema mhariri wa gazeti moja kupitia toleo la Jumapili Februari 28, 2016 na kujitetea kwa uongo:


“...Bahati mbaya sana baadhi yetu tunapozungumza lugha hii ya kuchukizwa na matendo (yote mabaya) ya CCM tunaonekana kama ni watu tusiokitakia mema chama hicho”.


Nimefuatilia kwa muda mrefu makala nyingi za mhariri huyo na kugundua ukweli kuwa ana chuki zake mwenyewe dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali yake na viongozi wake, hivyo anachofanya siku zote ni kuandika uzushi, uongo, upotoshaji na kila aina ya majungu na visasi ili kupoza machungu ya itikadi zake za kisiasa.


Anafanya hivyo kila inapofika Jumapili ya kila wiki kwa kutumia vibaya kabisa madaraka aliyopewa katika chombo hicho cha habari, mwandishi aliyethibitisha waziwazi kuwa ana chuki zake kubwa kwa CCM, hivyo hakuna hata siku moja ambayo chama hicho kwake kimewahi kufanya zuri lolote isipokuwa vinginevyo.


Ndiyo maana pia katika makala yake hiyo yenye kichwa kinachosema “Kwa vyovyote salama ya Magufuli ni kuisafisha CCM” aliandika kwa hasira zilezile, chuki zilezile, uongo uleule, uzushi uleule na usugu wa kupotosha kwa kudhani kuwa huenda wasomaji wake wote hawana akili timamu au ni mazuzu!


Sipendi kutumia lugha kali dhidi yake mwenyewe, fikra zake ama upeo wake wa kisiasa, lakini inawezekana nikafanya hivyo kwa vile nimechukizwa kwelikweli na juhudi zake chafu kwa chama changu, viongozi wangu na taifa langu katika ujumla wake.


Ndiyo maana ninasema kwamba ni ujinga uliopitiliza kichwani kwa mtu kudai kuwa CCM, tena kwa haraka inatakiwa isafishwe na Rais Dk. John Magufuli akishakuwa Mwenyekiti akichukua nafasi inayoachwa wazi na mtangulizi wake, Jakaya Mrisho Kikwete.


“Kimsingi mambo mengi ambayo wengi tunayaona kama ni ufisadi ulioota mizizi ndani ya mifumo ya serikali yameanzia ndani ya Chama Cha Mapinduzi”, anasema mhariri huyo katika makala yake hiyo, uongo ambao kwa namna zote ile ni kama ujinga mkubwa kabisa wa kufikiri kichwani!


Nafahamu kuwa hakuna gazeti lenye katiba, mfumo au ialani ila yana sera ambazo hata hivyo hazitekelezwi kwa sababu hata wafanyakazi wake ambao ni pamoja na wahariri kama yeye, waandishi wa habari na wengine kwa kawaida hawazijui kwa vile hutumika tu ili kusajilia magazeti na kufungiwa kabatini na mmiliki wake.


Hatua hiyo inafuatiwa na mmiliki huyo mwenyewe kuwaelekeza kwa mdomo tu wahariri wake kuwa “katika gazeti langu sitaki kuona kikiandikwa hiki au kile” katika upande wa kwanza, na kisha huwaelekeza itikadi yake ya kisiasa kwa kuwapiga marufuku “kumwandika fulani, fulani na fulani” isipokuwa fulani na fulani.


Ndiyo maana mhariri huyo mwenyewe, waandishi wake na gazeti lake hilo tulishuhudia wakati wote wa mchakato wa kutafuta mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, kisha wakati wote wa kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015 wakipambana kwa nguvu zao zote kumpigania Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa, Edward Lowassa ili aibuke mshindi.


Tulimuona mhariri huyo akipambana kwa nguvu zake zote, tena kwa uzushi na uongo wa kisiasa kupitia makala zake hizo, nyingi zikilenga ‘kumbeba’ Lowassa aliyekuja kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alipokatwa jina lake na Kamati Kuu ya CCM.


Bila wasiwasi na hata aibu usoni, mdomoni mwake, mikononi mwake na hata vinginevyo, mhariri huyo alikuwa mstari wa mbele kabisa kumpamba Lowassa ili aibuke mshindi wa kiti hicho, kazi iliyokwenda sambamba na kumponda Magufuli na CCM ili wananchi wamchukie na kutompa kura zao.


Hata ilipokuja vibaraka wa kisiasa wa Lowassa kama akina Kingunge Ngombale – Mwiru, Frederick Sumaye na kadhalika nao wakahamia Chadema, mhariri huyo alijitahidi kwa namna zote kuwapamba au kuzipa nafasi kubwa kauli zao, kazi ambayo hata hivyo ilimalizika kwa aibu kwa sababu upambe wake huo wa kisiasa ulisambaratishwa kama kishada kilichokwenda harijojo.


Ndiyo maana leo haishangazi anapokuja na uongo wake mpya, upotoshaji wake mpya, uchochezi wake mpya na kila aina ya hadithi ya uzushi dhidi ya CCM.


Mbona hatuambii ni kiongozi yupi wa CCM ambaye alianzisha ufisadi katika chama hicho na ilikuwa lini na upi? Mbona hasemi ni nani kati ya viongozi waliopo katika chama hicho wanaofanya ufisadi ili wananchi wawajue kwa majina?


Hata akiambiwa atutajie kiongozi yeyote wa serikali aliyekuwa CCM na kufanya ufisadi hawezi hata akielekezewa mtutu wa bunduki iwe ya aina ya Sub Automatic Rifle (SAR), Sub Machine Gun (SMG), Light Machine Gun (LMG), AK 47 ama bastola usoni kwake.


Inawezekana hawafahamu pia hata viongozi waandamizi wa serikali waliowahi kushika nafasi kubwa iwe CCM au ndani ya jumuiya zake tatu ambazo ni Umoja wa Wazazi, Umoja wa Vijana (UVCCM) ama Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) isipokuwa wachache mpaka afanye kwanza utafiti huo baada ya kuisoma makala yangu hii.


Hawezi kututajia ni kiongozi yupi wa CCM anayejua kuwa ni mwizi, na kwamba anaweza kutueleza pia alichoiba iwe fedha taslimu, hundi ama wizi wa kuaminiwa na ilikuwa wapi na shilingi ngapi.


Hawezi kututajia kiongozi yeyote wa CCM anayekula rushwa na kueleza ilikuwa wapi, lini na kutoka kwa nani, kwa tenda gani au kutoka kampuni gani, taasisi gani, shirika gani na endapo suala hilo lilifikishwa mahakamani au liliishia mtaani kwake.


Hawezi kututajia ni kiongozi yupi wa CCM anayeishi kwa kupiga dili iwe kuingia mikataba ya kampuni zenye utata kama ilivyokuwa Richmond Develoment LLC iliyomfukuzisha kazi Lowassa, na pia hawezi kutuambia ilikuwa lini, wapi na ilikuwaje ila mimi ninaweza kumtolea mifano iliyopo Chadema ambayo amekuwa mstari wa mbele kuitetea sana.


Hawezi kututajia ni kiongozi yupi wa CCM mwenye roho mbaya, visasi, mmbeya au mnafiki na kueleza ubaya wa roho yake, visasi alivyowahi kuvifanya na ilikuwa lini, wapi au kwa nani kama ambavyo hawezi kututolea mfano wa nani anayefanya umbeya, namna gani ama kusema unafiki wowote wa kisiasa anaofanya.


Pamoja na kutotaka kulumbana naye, lakini nafahamu kuwa baadhi ya wahariri wa magazeti yanayomilikiwa na watu binafsi nchini waliahidiwa vyeo na Lowassa endapo angeshinda na kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo huenda bado kuna wengine hawataki kukubali kwamba alishindwa na kuanza kuiandama CCM ili kumalizia hasira zao huko.


Kabla sijahitimisha makala yangu hii ninaomba kumtajia mifano ya viongozi wa Chadema ‘yake’ ambao ni wazushi sana, waongo sana, wambeya sana, wachochezi sana na wanafiki wakubwa kabisa wa kisiasa ambapo wanaongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.


Yumo pia Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Mnyika; Mbunge wa Iringa Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Peter Msigwa na hata Lowassa mwenyewe na kadhalika.


Kama siyo muongo na mzushi namuomba naye afanye hivyo pia ili wananchi wawafahamu hao aliowapa sifa hizo za kutunga akilenga kuichafua CCM, lakini anachofanya hasa ni kuanza ‘kuichafua’ kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2020 akiamini kwamba itafika kipindi hicho ikiwa tayari ‘inanuka’.


Ndiyo maana ninasema kifua mbele kwamba ni ujinga mkubwa kudai eti CCM ina viongozi wenye roho mbaya, visasi, wezi, wambeya au wala rushwa ila hili la kuwaita wanafiki wa kisiasa linategemea zaidi na itikadi iliyomo kichwani mwake.


Wale wanaoichukia CCM akiwemo mhariri huyo anayeitungia mpaka uongo, uzushi na upotoshaji ninaomba katika ujumla wao wote kabisa washindwe na walegee!


Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0787 088 870
 
Back
Top Bottom