Dar es SalaamSerikali imesema itasaini mkataba na mkandarasi baada ya wiki mbili kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati itakayotumia treni ya umeme, kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro ambayo itatumia saa 1:30 kwa safari.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo jana alipokuwa anahutubia wahitimu kwenye mahafali ya 32 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
“Naomba kwa sasa msiniulize ni mkandarasi gani atasaini ila wakati ukifika kila kitu kitakuwa hadharani, reli hii haitatumia gari moshi ni umeme,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema reli hiyo itakuwa na mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa.
Januari 26 mwaka huu, Rais John Magufuli alipokuwa anazindua mradi wa magari yaendayo haraka (BRT) maarufu kama mwendokasi alisema Serikali inapitia zabuni ili kumpata mkandarasi atakayejenga reli hiyo yenye urefu wa kilometa 200.
CHANZO: Mwananchi