Treni Reli ya Kati kuanza tena Jumatatu ijayo

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Uongozi wa Kampuni ya Reli (TRL) umetangaza kuanza tena huduma za usafiri wa Reli ya Kati kuanzia Jumatatu ijayo.

Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo kwa vyombo vya habari, uamuzi huo umetokana na tathmini ya wahandisi wa ujenzi na wataalamu wa reli katika daraja lililoelezewa kuharibika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotumwa jana, ukarabati wa daraja hili lililopo kati ya stesheni za Bahi na Kintinku, unatarajiwa kukamilika Jumamosi ijayo.

“Kutokana na makisio hayo, huduma ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma iliyopangwa kufanyika Ijumaa, sasa safari hiyo imesogezwa mbele hadi Jumatatu saa 11 jioni,” ilisema taarifa hiyo.

Pia TRL imetangaza kuwepo kwa haduma maalumu ya usafiri wa abiria katika reli hiyo, ambapo treni itaondoka Tabora Jumatatu jioni, kwenda Kigoma na kugeuza siku ya pili yake saa 11 jioni kurejea Dar es Salaam.

“Hivi sasa kazi ya ukarabati zinaendelea kwa saa 24 ili lengo la kufungua njia kabla ya Januari 17, lifikiwe.

Uongozi wa kampuni ya reli unawataka wadau na wananchi wote kuwa na uvumilivu wakati huu mgumu ambao kampuni inafanya kila njia kurejesha huduma zake katika hali ya kawaida,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa abiria wote 1,846 waliokuwa wamekwama katika stesheni ya Kintinku wakitokea Kigoma, walisafirishwa kwa mabasi na basi la mwisho la 29 lilifika katika stesheni ya reli jijini Dar es Salaam saa 5 asubuhi jana.
 
Back
Top Bottom