Return Of Undertaker
JF-Expert Member
- Jun 12, 2012
- 4,572
- 26,885
========
Sakata la mali zinazodaiwa za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limeendelea kulitikisa bunge baada ya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) kuongeza nyingine.
Akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Selasini alisema Makonda amenunua jengo (apartment), lenye thamani ya Sh600 milioni.
“Makonda amenunua apartment pale Viva Towers kwa Sh600 milioni. Makonda amempa mke wake gari aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya Dola 250,000 za Marekani (Sh550 milioni) kama zawadi ya ‘Birthday’,” alisema Selasini.
Suala la utajiri wa Makonda, liliibuliwa bungeni kwa mara ya kwanza Februari 6 na Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Msukuma akitaka mteule huyo wa Rais achunguzwe kwa kujilimbikizia mali.
Kiini cha mbunge huyo kumshukia Makonda ilitokana na hatua yake ya kutangaza majina ya watu aliodai wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, huku akidai utajiri wake una shaka.
Msukuma Februari 7, mwaka huu aliomba mwongozo kwa Spika, akitaka Bunge litoe mwongozo kuhusu utajiri huo wa Makonda ndani ya muda mfupi.
Msukuma alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tu wa wadhifa wake kama mkuu wa mkoa, Makonda amejilimbikizia mali likiwamo gari aina ya Lexus, lenye thamani ya Sh400 milioni.
Mbali na mali hizo Msukuma alisema Makonda anamiliki magari mengine ya kifahari aina ya V8, anajenga maghorofa jijini Mwanza na amekarabati ofisi yake kwa Sh400 milioni bila kutumia utaratibu wa sheria ya manunuzi.
Mbali na hilo, Selasini alisema utaratibu unaotumiwa na Makonda kushughulikia tatizo la dawa za kulevya, umetoa mwanya kwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo kukimbilia nje ya nchi.
“Kama unawatangaza watu kwa utaratibu huu. Ni mfanyabiashara gani wa dawa za kulevya mjinga amebaki katika hii. Makonda amesaidia kuwakimbiza labda anashirikiana nao,” alisema.
Wakati huo huo Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), ameliomba Bunge kutoa mwongozo kwa kile alichodai ni hatua ya katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kupingana na maazimio ya Bunge.
Chanzo: mwananchi