TFF yarudisha Ligi Daraja la Pili

TFF yarudisha Ligi Daraja la Pili

kbm

JF-Expert Member
Joined
Oct 5, 2012
Posts
5,224
Reaction score
1,687
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Limerudisha Ligi Daraja la Pili na itaanza kuchezwa Novemba mwaka huu.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limerudisha Ligi Daraja la pili na itaanza kuchezwa Novemba mwaka huu.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana hivi karibuni kukubali mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya kurejesha Ligi hiyo.


Michuano ya Ligi Daraja la Pili iliondolewa na uongozi wa TFF uliopita chini ya Leodegar Tenga, jambo ambalo lilipingwa vikali na wadau wa soka.


Akizungumzia hatua hiyo jana Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Boniface Wambura alisema lengo la kurejesha ligi hiyo ni kuongeza wigo wa mashindano kitaifa ambapo itasaidia kushirikisha kundi kubwa zaidi la wachezaji kwenye mashindano makini yanayozingatia viwango na vigezo ili kuwapa wachezaji maendeleo ya kiuchezaji ikiwemo kuendelezwa vipaji vyao kitaalamu.


"Shirikisho limeridhia kurudisha Ligi Daraja la Pili ili kutoa fursa na wigo mpana wa mashindano ya kitaifa na kutoa fursa kwa wachezaji zaidi kuonesha vipaji vyao", alisema Wambura ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho hilo.


Pia alisema ligi hiyo itakuwa na timu 24 na itachezwa katika hatua ya makundi manne yenye timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ambapo mshindi wa kila kundi atapanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na timu ya mwisho kila kundi itarudi kwenye ligi ya mkoa wake.


Alisema, timu zilizoongoza makundi zitacheza mtoano nyumbani na ugenini na pia kutakuwa na fainali ili kutafuta bingwa katika ligi hiyo na mshindi atatambulika kama bingwa wa Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu wa mwaka 2014/2015.


Timu zitakazocheza SDL kwa msimu huu ni zile zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nane katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) katika makundi yao msimu uliopita, na tatu zilizoshuka kutoka FDL msimu uliopita.


Kundi A litakuwa na timu za Milambo FC (Tabora), Mji Mkuu FC (Dodoma), Mpanda United (Mpanda), Mvuvumwa FC (Kigoma), Singida United (Singida) na Ujenzi (Rukwa) wakati kundi B ni Arusha FC (Arusha), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), Mbao FC (Mwanza), Pamba FC (Mwanza) na Rwamukoma JKT (Mara).


Kundi C linaundwa na timu za Abajalo, Mshikamano FC, Navy FC na Transit Camp zote za Dar es Salaam), Kiluvya United (Pwani) na Kariakoo FC (Lindi), na kundi D lina timu za Magereza FC (Iringa), Mkamba Rangers (Morogoro), Njombe Mji (Njombe), Town Small Boys (Ruvuma), Volcano FC (Morogoro) na Wenda FC (Mbeya).


Wakati huohuo, Wambura alisema Ligi ya (FDL) msimu wa 2014/2015 itachezwa katika makundi mawili kwa mtindo wa nyumbani na ugenini kuanzia Oktoba 11 mwaka huu.


Alisema, kundi A lina timu za African Lyon, African Sports, Ashanti United, Friends Rangers, Kimondo SC, Kurugenzi Mafinga, Lipuli, Majimaji, Mlale JKT, Polisi Dar es Salaam, Tessema FC na Villa Squad.


Na kundi B lina timu za Burkina Faso, Geita Veterans SC, Green Warriors, Kanembwa JKT, Mwadui SC, Oljoro JKT, Panone FC, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora, Rhino Rangers na Toto Africans.

Chanzo: HabariLeo
 
Back
Top Bottom