TFF ya Malinzi, Hadi mahali pa kuweka ofisi ni maelekezo ya FIFA?

Yombayomba

JF-Expert Member
Aug 23, 2006
818
214



Na Saleh Ally
NCHI hii raha sana, watu wengi sana wanaishi kwa ujanjaujanja na bado wanapata heshima mbele ya jamii na kuonekana ni watu wenye mchango kwenye jamii.

Bila kupindisha nazungumzia wale wanaojiita wasaidizi na washauri wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, kwamba ni watu ambao hawana msaada wowote.

Inawezekana kabisa, TFF inayoongozwa na Malinzi ipo katika hatua za mwisho kuzama na kuweka historia mpya ya kuwa na uongozi uliokuwa ukitumainiwa na wengi kwamba unaleta mabadiliko ya soka nchini, kumbe hauwezi hata kujua ofisi sahihi kwao ni ipi.

Kama mtu hajui hata ofisi yake inapaswa kuwa wapi ambapo ni sahihi kutokana na kipato anachoingiza, ataweza vipi kuleta mabadiliko kwenye kitu husika?

Nani anategemea maendeleo yapatikane kwa TFF hii ya Malinzi iliyojaa wasaidizi kibao ambao hawana tija na si wataalamu sahihi wa sehemu husika walizowekwa?

Yupi anaweza kusema kuna mafanikio ya soka yanakuja huku mamilioni ya fedha yakitumika kwa ushauri usio sahihi na watu hao bahati mbaya hawataki kukosolewa?



Kuna msaidizi mmoja wa Malinzi amenitumia salamu kupitia kiongozi mmoja wa soka, kwamba anataka kunitumia chatu. Hii inaonyesha kiasi gani watu bado wanaishi na mawazo ya zamani, ingawa pumzi wanayovuta ni ya sasa.

Huyo anayetaka kunitumia chatu ni kwa kuwa tu nilihoji uhalali wake wa kuwa TFF. Namsubiri huyo chatu na leo ninaendelea kuhoji Malinzi kuwa na rundo la wasaidizi au washauri ambao hawana msaada.

Wanalipwa fedha na nani, kwa nini fedha hizo zisitumike kwa ajili ya maendeleo ya mpira badala ya kuwapa watu hao ambao wanafanya mambo yao kiujanja?

Kuna ule msemo; "dunia siyo mbaya, walimwengu ndiyo wabaya." Inawezekana Malinzi pia anaweza asiwe mbaya, lakini ‘wapambe' anaowajaza TFF kwa ajili ya ‘ushkaji', kuridhishana kwa kuwa walimsaidia kwenye uchaguzi, ndiyo watakaomuangusha na kuuangusha mpira wetu.

Wakimuangusha Malinzi, haitakuwa biashara ya Watanzania kwa kuwa amepita kwingi kuanzia akiwa promota wa ngumi. Akaanguka na kuinuka na maisha yakaendelea, hilo litamhusu yeye na hao ‘washikaji' zake.

Lakini kuuangusha mpira wa Tanzania kwa ajili ya kuwafurahisha ‘wapambe' au ‘washkaji' kitakuwa si kitu rahisi kukubalika, hasa kwa Watanzania ambao hawapo tayari kuona wanaendelea kudidimizwa na watu wanaotaka kujifaidisha badala ya kuufaidisha mchezo wa soka.

Mfano ambao unaonyesha TFF chini ya Malinzi haijui njia sahihi ya kupita, ni suala la Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuingilia hadi wapi shirikisho hilo linapaswa kuweka ofisi.

TFF iliamua kuhamia mjini kwenye ghorofa la PPF Tower ambako lilikuwa likilipa hadi Sh milioni 15 kwa mwezi. Likaacha ofisi zake kwa madai pale kuna mpango wa uendelezaji wa eneo hilo, kukawa na taarifa NSSF ndiyo wameingia mkataba na TFF kwa ajili ya ujenzi.

Sasa ni zaidi ya miezi minne, TFF hakuna inalolifanya katika eneo la Karume huku mamilioni ya fedha ambayo yangetumika kwenye soka la vijana na lile la wanawake, yakitumika kulipia hilo jengo la PPF.

Washauri au wasaidizi wa Malinzi wako wapi? Vipi hawakuona kwamba hilo ni tatizo na kumshauri? Hadi imefikia Fifa wamekuja nchini na kugundua hilo ni tatizo na kuitaka TFF irejee Karume ambako haitalipa hata senti, kweli Malinzi na ‘vijana' wake wamerejea Ilala!

Hili jambo linasikitisha, linaumiza na inaonekana mwendo wa TFF hii ya Malinzi ni majanga katika soka nchini na kama mtawaachia waende hivi, tutakwisha.

Maana yake Fifa wasipoona kuna jambo baya, wao hawawezi kuliona. Hatukaki kurejea katika enzi za utumwa, kuwa watu tunaoagizwa au kuamrishwa tu kama watwana au nyampara anayewaeleza nini cha kufanya wafungwa wenzake.

Kikubwa ni kujitambua, kusimama kama Watanzania ambao tunataka kuleta maendeleo kwenye mpira wetu. Malinzi lazima akubali kupokea changamoto na kupambana kwa maendeleo ya soka kwa manufaa ya Watanzania.

Malinzi, mliondoka Karume mkisema kuna suala la kuboresha, vipi, liko wapi? Wakati Fifa wanawaambia mrejee mbona hamjasema kuna programu ya uendelezaji? Hasara ilikuwa kiasi gani?

Fedha mlizopanga PPF Tower zilikuwa kiasi gani na zingesaidia soka yetu kwa kiasi gani? Kuna hatari ya Tanzania kuzidi kuporomoka na yale mabadiliko yaliyojitokeza wakati wa uongozi wa Leodegar Tenga nayo yakayeyuka halafu tukarudi kule enzi za Fat.

Kuna kila sababu Malinzi aone kuna tatizo, abadilike na aachane na hao watu wanaotaka kuwatumia watu chatu au majini, kisa wamewakosoa.

Aachane na watu wanaotaka nchi ijaze watu waoga, wanaohofia kusema ukweli, kisa wataumizwa au kutumiwa chatu! Hapa kwa lengo la kujenga na si kuwaacha kina fulani waendelee kuharibu. Acha wengine wakae kimya, lakini Tanzania hii si ile ya wale akina nanihii waliokuwa wanafanya wanavyotaka.

Tunahitaji maendeleo, mkumbuke kama chatu wenu akimla Saleh Ally, kuna Watanzania wengi wanajua, wanaelewa nao watapambana kuhakikisha maendeleo yanapatikana na si ujanjaujanja tu. Nasisitiza, hatuhitaji hadithi, tunahitaji maendeleo, ikishindikana, kaka Malinzi kaa kando!

Source: SalehJembe
 
Wameondoka Karume na haraka zote kumbe mipango yenyewe bado. Wanataka ufahari wa kuwa na ofisi mjini. Kibaya zaidi, wakaenda kupanga ofisi za PPF wakati wanategemea NSSF ndio iwasadie katika mradi wao wa Karume. Kwa nini wasipange NSSF kuonyesha nia ya ushirikiano? Haya nayo mpaka FIFA waje wawaambie kwamba PPF na NSSF ni washindani kibiashara?

Yote haya lawama kwa Tenga kuachia wakati uwezo wa kuedelea kuongoza bado anao.
 
Back
Top Bottom