TENDWA: POLISI wanavunja sheria kuzuia mikutano ya vyama | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TENDWA: POLISI wanavunja sheria kuzuia mikutano ya vyama

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MAMA POROJO, Jul 25, 2010.

 1. MAMA POROJO

  MAMA POROJO JF-Expert Member

  #1
  Jul 25, 2010
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 4,966
  Likes Received: 27
  Trophy Points: 135
  22nd July 2010

  Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa

  Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amesema kitendo cha Jeshi la Polisi kukataa kutoa kibali kwa vyama vya siasa vinapoomba kufanya maandamano au mikutano ni ukiukwaji wa sheria.

  Tendwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya waandishi wa habari yaliyofadhiliwa na Mfuko wa kusaidia waandishi wa habari nchini (TMF).

  Alisema jeshi hilo kutotoa kibali kwa vyama vya upinzani kimesababisha kwa muda mrefu kuwepo kwa vurugu hasa kipindi cha uchaguzi na baadhi ya wapinzani kulitupia lawama jeshi hilo kuwa linapendelea Chama cha Mapinduzi (CCM).

  “Tatizo hili tumeliona kwa muda mrefu hasa kipindi cha kuelekea uchaguzi, ambapo wapinzani wamekuwa wakililalamikia jeshi hilo kuwanyima kibali wanapotaka kufanya mikutano yao au maandamano na matokeo yake kumekuwa kukitokea vurugu na wakati mwingine watu kupigwa na kuwekwa ndani,“ alisema.

  Alisema tatizo hilo limepelekea vyama vya upinzani kipindi cha uchaguzi kutokuwa na imani na jeshi la polisi pamoja na ofisi yake kwa kudhani kuwa CCM inapendelewa.
  Alisema juzi ofisi yake, jeshi la polisi, vyama vya siasa 18 na wadau wengine walikutana kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu mambo hayo hayatokei tena.
  Tuliona tumefikia miaka 18 ya mfumo wa demokrasia kwa nini tuendelee kupigana virungu, vurugu, kwa mfano, Chadema au CCM wavalishe mbwa fulana, ndio maana tulikutana juzi kuangalia kasoro za kiutendaji na kupelekea vyama vya siasa na dola kutoaminiana,” alisema.

  Alisema wajibu wa jeshi la polisi ni kutoa kibali cha maandamano au mkutano kwa vyama pindi vinapoomba hilo.

  “Huu ndio wajibu wa jeshi la polisi, kukataa kwao kutoa kibali ndio chanzo cha tatizo hili, sheria hiyo inasema ikiwa chama cha siasa kimeomba maandamano, jeshi la polisi halitakiwi kukataa, lakini kama eneo ambalo limeombwa kwa ajili ya mkutano linatumiwa na chama kingine au wanawasiwasi na eneo hilo, basi watoe ushauri kwa wahusika, lakini sio kuwanyima kibali,” alisema.

  Alisema ikiwa jeshi hilo litaendelea kuvinyima kibali vyama hivyo, litasababisha mgongano kuendelea.

  Katika hatua nyingine, Tendwa alisema katika mkutano huo, vyama vya siasa pamoja na jeshi la polisi kila mmoja na nafasi yake waliangalia jinsi gani watakavyoweza kuitekeleza sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi.
  Alisema wagombea watarajiwa au watetezi wa nafasi zao majimboni endapo wataenda kinyume na sheria hiyo watakamatwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).

  Alisema kupitia vyama hivyo waliwakumbusha wagombea wapya na wanaotetea viti vyao, kuhakikisha baada ya kuteuliwa wanawasilisha makadirio na mapato yao.
  Alisema endapo hawatafanya hivyo, ofisi yake itamfahamisha Mkurugenzi wa Uchaguzi na mgombea huyo atasimamishwa kuendelea na mchakato wa uchaguzi.

  “Mgombea atakaposimamishwa kwenye nafasi yake kutokana na kukiuka sheria basi nafasi yake itaendelea kuwa wazi na chama hakitaruhusiwa kumteua mwingine, hivyo ili kuepuka hili wanatakiwa kuifuata sheria hii,” alisema.
  Pia alisema katika mkutano huo, vyama vya upinzani vilitoa malalamiko yao dhidi ya CCM kuhusu kuwepo kwa mabango ya ushabiki ambapo jambo hilo kwa sasa ofisi yake inalishughulikia baada ya kupokea barua.

  “Uwekaji wa mabango ya uchochezi, au utumiaji wa lugha ya matusi ni kinyume cha sheria, vyama vyote vinatakiwa kuliepuka suala hili, wenzetu wa Unguja hutumia taarabu tena zenye mafumbo kwa nini huku bara tunayaweka hadharani matusi, pia tunavikumbusha vyama kuwa wakati wa kampeni bado haujafika wazingatie muda uliowekwa,” alisema

  Kwa upande wa vyombo vya habari, Tendwa alivikumbusha kufuata maadili ya uandishi wakati wa uchaguzi mkuu ili kuepusha uchochezi na kupelekea kuzuka kwa vurugu.
  Alisema ofisi yake inatarajia kutenga muda wa siku moja kabla ya uchaguzi kwa ajili ya kuwaelimisha waandishi wa habari kuhusu sheria ya uchaguzi ili wazielewe vizuri zaidi.
  Akiielezea sheria hiyo Tendwa alisema, wagombea na vyama vya siasa wanatakiwa kuwasilisha mapato na matumizi ndani ya siku saba baada ya kuteuliwa na baada ya kupita siku saba ofisi yake itaanza kazi ya kufuatilia nani ambaye hajawasilisha na kufungiwa kugombea.

  Alisema siku 180 baada ya uchaguzi, mgombea anapaswa kuwasilisha tena matumizi na mapato aliyotumia kinyume na hapo ndani ya siku 60 mgombea kama hakufanya hivyo atavuliwa nafasi alioyoipata kama hakushinda, atafikishwa mahakamani.

  Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Habari (Maelezo), Clement Mshana, amevitaka vyombo vya habari kuhakikisha kuwa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu, habari zitakazoandikwa hazilengi kuleta vurugu.

  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...