Tanzania na giningi inayokwenda kombo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tanzania na giningi inayokwenda kombo

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by George Maige Nhigula Jr., Mar 9, 2011.

 1. George Maige Nhigula Jr.

  George Maige Nhigula Jr. Verified User

  #1
  Mar 9, 2011
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 470
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  [FONT=&quot]:Mwandishi Edwin Igenge[/FONT]​
  [FONT=&quot]Mwandishi wa makala hii ni Wakili wa kujitegemea na Mwanaharakati jijini Dar es Salaam anapatikana kwa simu Na. 0714 - 547- 069[/FONT]​
  [FONT=&quot]Baruapepe: igenge05@yahoo.co.uk[/FONT]​

  [FONT=&quot]TANZANIA NA GININGI INAYOKWENDA KOMBO[/FONT]
  [FONT=&quot]Giningi[/FONT][FONT=&quot]ni neno ambalo mimi mwenyewe sijui asili yake wala sina uhakika kama ni neno la Kiswahili ila nina uhakika kuwa giningi ni neno la kibantu ambalo kwa mara ya kwanza lilitumiwa na mwandishi maarufu Bwana Said Mohamed aliyeandika Tamthiliya maarufu ya Kiswahili inayoitwa Kivuli Kinaishi ambayo niliisoma wakati nikiwa mwanafunzi wa kidato cha tano katika iliyokuwa shule ya sekondari ya Mkwawa ambayo sasa hivi imegeuzwa na wanaginingi kuwa chuo kikuu cha taaluma ya ualimu huko mkoani Iringa. Katika Tamthiliya hiyo mwandishi amechora wahusika wake kwa ustadi wa hali ya juu ambao ni Bibi Kilembwe ambaye ni mtawala wa kiimla-mwanamke katika nchi ya Giningi. Mtawala huyu ni dikteta ambaye anatawala nchi ya giningi kwa mkono wa chuma na mikono yake inanuka damu kwa mauaji ya ama wapinzani wake ama wakosoaji wake ama mtu yoyote anayesimamia ukweli mfano mwanamapinduzi Mtolewa aliuauwa kwa sababu za kupinga utawala wake. Muimla huyu wa kike licha ya utawala wake wa kidespotiki alipambana na vuguvugu la wanamapinduzi lililoanzishwa na jemedari Mtolewa. Katika Tamthiliya hii neno giningi lilitumika kitaswira kumaanisha tabaka tawala ambalo limejaa viongozi na wanasiasa wapenda tandabelua walio walafi, wafidhuli, wanaidhaya, wadhulumaji, waonevu wasio huruma kwa masikini, matajiri waliokithiri na kusheheni utajiri, wala rushwa na mafisadi wanao honyoa jasho la wananchi wasio bahati kuingia giningi. Neno hili lina maanisha watanzania wanaojiona wenye bahati ya kushikilia hatamu za uongozi au dola la nchi yetu wengine tangu uhuru wa nchi yetu bado wapo Giningi tu. Aidha Kwenda kombo ni kirai kitenzi katika lugha ya Kiswahili ambapo kamusi ya Kiswahili sanifu iliyotolewa na TUKI-Dsm toleo la mwaka 2004 na kuchapishwa na Oxford University Press katika ukurasa wa 133 neno kombo linatafsiriwa kama kivumishi chenye maana ya kitu kisichonyooka au kitu kilichopeteka yaani kitu kinachokwenda upande kikiashiria hatari au kupata matatizo mbele ya safari au kutofika mwisho wa safari. Ninaposema 'Tanzania na giningi inayokwenda kombo' nina maana kwamba watawala wetu wameshindwa kutawala nchi wanaipeleka kombo kama tunavyoshuhudia sisi sote.[/FONT]

  [FONT=&quot]Aidha jina la makala hii linaweza kuwa kali sana au maudhui yake yanaweza kutia jelezi kwa wenye nasaba na giningi hatimaye kuwakasirisha watanzania wanaojiona wenye bahati ya kushikilia hatamu za uongozi au dola la nchi yetu.Pia maudhui ya makala hii yanaweza kuwafikirisha na kuibua hisia za kimageuzi hatimaye kuwaambukiza watanzania wasio bahati walio nje ya hatamu za giningi , watanzania ambao hawana nasaba na dola lililopo madarakani, watanzania ambao wamezaliwa katika hizi zama za elektronika, zama hizi za facebook na twitter, watanzania ambao ni wajuzi wa mambo ya ndani na nje ya dola letu,watanzania ambao wanajua kuwa nchi yao haiendeshwi chini ya misingi ya haki na usawa,watanzania wanaochukia sana ghiliba za wanasiasa walio walafi,

  wafidhuli,wanaidhaya,wadhulumaji,waonevu wasio huruma,matajiri waliokithiri na kusheheni ukwasi, wala rushwa na mafisadi ambao wameibeba nchi yetu mgongoni mwao na ndio wanaoipeleka giningi kombo.Maudhui ya makala hii yanaweza kuwaambukiza watanzania virusi vya mapinduzi viitwavyo nguvu ya umma vilivyoanzia Tunisia na kusambaa Misri,Yemen ,Bahrain,Moroko hadi Libya kwa mfalme wa Afrika Mohammar Gaddafi ambako hadi sasa watu zaidi 184 wenye virusi vya nguvu ya umma wameshauawa.Mfalme huyu wa Afrika miaka miwili iliyopita akitembelea nchi ya Uganda ambako alifungua misikiti iliyojengwa kwa pesa ambayo yeye anaita yake lakini ni pesa ya walibya alishauri waganda kuwa hawana haja ya kuwa na demokrasia na kufanya uchaguzi wa kumchagua Rais kwani Jemedari mwenzake wa kijeshi Yoweri Kaguta Mseveni anatosha.Hapa nadhani Kanali huyu wa Kibedui alisahau kuwa uongozi ni ridhaa ya watu siyo utashi wa mtu na ridhaa ya watu inapopuuzwa basi nguvu ya umma hutumika kurudisha ridhaa ya watu ndiyo maana walatini husema vox populi vox goduswakiwa na maana kuwa sauti ya watu ni sauti ya mungu.Hakuna giningi itakayodumu giningini ikiwa giningi hiyo inapuuza kilio cha watu wake au haijishughulishi na umasikini wa watu wake . Hiki ndiyo chanzo cha kuzuka kwa virusi vya nguvu ya umma katika nchi za kiarabu ambazo karibu zote zimekuwa zinatawaliwa na familia ya mtu mmoja au ukoo fulani unaojiita ukoo wa kifalme ndiyo maana kwa mfano nchini Libya katika maandamo yanayoendelea mmoja wa watoto wa Kanali wa kibedui Gadafi ndiyo alitoa tamko kuhusu uandamanaji wa wananchi.Hii yote ni ushahidi kwamba giningi za mataifa haya zilianza kwenda kombo pale wanasaba wa giningi hizi walipopuuza vilio vya wengi ,wala hawakuchukua hatua za makusudi kuleta demokrasia ya kweli na uongozi bora,bali giningi hizi ziliendelea kuchakachua maisha na haki za msingi za wananchi wake hatimaye zikaanza kwenda kombo hivi sasa tunazishuhudia zikisambaratika kama kinyesi cha kale japo waswahili husema hakinuki.Wahenga walisema ukiona mwenzako ananyolewa wewe tia maji nywere zako vinginevyo utanyolewa kavukavu.Watawala wetu wamefanya machache sana kuwashawishi watanzania ndiyo maana walatini husema : " Minimum est nihilo proximum" wakimaanisha machahe hufuatia ziro kwa kiingereza "The least is next to zero " .
  [/FONT]

  [FONT=&quot]Maswali ya msingi kujiuliza hapa ni kwamba: Je, Giningi ya Tanzania nayo inakwenda kombo kama nchi za uarabuni na kwingineko duniani? Je, Giningi ya Tanzania imeanza lini kwenda kombo, tangu uhuru? Kwa nini Giningi ya Tanzania inakwenda kombo? Je ni akina nani wanaifanya Giningi ya Tanzania iende kombo? Makala hii itajaribu kujibu maswali haya kwa kina na kufafanua kwa kina dhana ya Giningi ya Tanzania kwenda kombo.[/FONT]

  [FONT=&quot]Ninaposema Giningi ya Tanzania inakwenda kombo nina maanisha kuwa nchi yetu imekosa uongozi thabiti na mwelekeo mahususi, nchi yetu haina maadili au nchi yetu haina miiko ya uongozi au itikeli , kila kitu kinakwenda kombo.[/FONT]

  [FONT=&quot]Wanasiasa ambao baadhi yao tumewapa dhamana au kibali cha kwenda Giningi ili watuoneshe njia matokeo yake hawatuoneshi njia bali wanakwenda kombo kwa kuacha njia halisi, giningi nzima inakwenda kombo na wananchi nao sasa wanakwenda kombo hatimaye nchi nzima itakwenda kombo. Viongozi waandamizi serikalini nao wanakwenda kombo kwa sababu giningi inakwenda kombo.Tunashuhudia mabosi walioshika nyadhifa mbalimbali serikalini wasivyo na maadili wala itikeli ya taaluma zao. Hawa ndiyo wataalamu wetu wanaotekeleza sera mbalimbali za serikali .Siku hizi ni jambo la kawaida kusikia bosi ana mahusiano ya ngono na katibu muhtasi wake ambaye ana ndoa yake ,au ana mahusiano ya kingono na mfanyakazi aliye chini yake.Tunaona mabinti wengi wanaomaliza shule au vyuo wanavyobakwa au kudaiwa rushwa ya ngono na waajiri kwa kisingizio cha ukosefu wa ajira.Wanarubuniwa kwa kupewa upendeleo kazini kama vile safari za kikazi au kimasomo nje ya nchi au kulipwa posho za kijungu jiko au safari mbalimbali za ndani ya nchi zenye viposho vya hapa na pale. Wale waliokomaa kimaadili hukataa ushenzi huu lakini wengi wao hupata msukosuko wa kimbunga cha Katrina kiasi kwamba wachache wao huacha kazi .Ofisi za umma zinatumikia umma wa watanzania na ngono za wanaginingi .Siku hizi ni kawaida kabisa kusikia eti kiongozi au mwanasiasa fulani mwandamizi anatembea na visicha-vitoto vya shule au chuo,wengine wanaonekana wanakata viuno na kukumbatia wanawake katika kumbi za starehe usiku ,wengine wanawageuza wasichana hawa nyumba ndogo.Wengine hutumia magari ya kifahari ya serikali yanayoendeshwa kwa kodi za watanzania kutafuta visichina vidogo.Wengine wamewageuza madereva wao kama makuad wa kuwatafutia visichina vidogo.Wengi wa wasichana hawa ama hutoka familia masikini ama familia tajiri.Licha ya mambo haya kuwa ya aibu yanafanyika waziwazi mchana kweupe bila kificho na hakuna hatua zozote zinachukuliwa dhidi ya viongozi hawa.Kuchakachua utumishi wa umma ni kuchakachua maisha yetu .Tunahitaji watu wenye maadili kwenye utumishi wa umma kwani serikali ni tofauti sana na utumishi wa umma,serikali zinakuja na kuondoka muda wake ukiisha , lakini utumishi wa umma upo milele zote. Kinachonisikitisha ni kwamba afya za wengi wa viongozi hawa ni za kuchakachua ama kwa kumwaga damu na kujaza damu ama kwa kutumia ARV. Hii ni hatari kwa afya za uzazi za watoto wetu.Mtu unaweza kufikiria labda haya anafanyiwa mtoto wa jirani yako lakini ukimwi wa jirani yako au wako mwenyewe unaweza pia kumpata mwanao wa kuzaa. Hii ni aibu pia kwa Taifa kama Tanzania ambalo watangulizi wake kama Mwalimu Nyerere na wenzake walilijengea heshima kubwa ndani na nje.Mwalimu alichukia sana viongozi kukosa maadili ndo maana aliwahi kukemea katika moja ya hotuba zake kali kuwa kiongozi asiye na maadili mema hatufai….aende akaendeshe shamba lake huko au akafanye umalaya wake huko kwani mabarabara yamejaa tele… atuachie uongozi wetu. Juzi juzi hapa nchini Rwanda waziri mmoja kijana alikutikana amepiga picha zinazoashiria hisia za kimahaba na wasichana kadhaa amelazimika kujiuzulu. Hapa kwetu Tanzania viongozi wakware ni wengi lakini hawawajibishwi ! Mwalimu Nyerere wakati wa uongozi wake hatukuwahi kusikia wala kusikika vijiweni akisemwa eti fulani ni nyumba ndogo yake au fulani ni hawala yake amezaa nae mtoto kwani hakuwa na muda wa kutafuta au kutembea na mahawala wakati majukumu ya kitaifa aliyopewa na watanzania yamemganda aliwaogopo watanzania pia alichukia sana nchi kwenda kombo ikiwa chini ya utawala wake.Katika giningi ya Tanzania hususan baada ya Mwalimu ni aibu tupu viongozi waandamizi wa chama na serikali ama mawaziri ama wabunge ama wakurugenzi ama madiwani wote hawachaguliwi "on merits " yaani kwa sifa na umahiri au weledi katika taaluma zao .Sifa za msingi zinajikita katika mahusiano ya kingono ama udugu ama ukabila ama kuoleana.Mwanamke anapoteuliwa kuwa mkurugenzi au kushika wadhifa fulani basi sifa ya msingi ni kuwa na mapambaja mazuri au maungo mazuri ya kiuno au mabepa kadri yanavyomvutia mteuaji. Teuzi nyingi hazizingatii uwezo wa wanaoteuliwa kitaaluma au kiutendaji matokeo yake ni kuifanya giningi iende kombo athari zake zinarudi kwa watanzania hasa masikini kwani kiongozi mzigo ni mzigo wa waliomchagua. Hali hii inapelekea baadhi ya watu kutokuwa na imani na wanawake wanaoteuliwa kuwa wabunge kupitia viti maalum kwa mjibu wa katiba yetu ya mwaka 1977.Wengi wa wabunge hawa ukiwatazama kwa jicho pevu na kutafakari kwa umakini kabisa utagundua kuwa ni warembo wote hata ukifuatilia mchango wao bungeni ni dhaifu au hafifu. Je kweli hawa ni wabunge wa viti maalum au vitu maalum?Jibu la swali hili sisi wapiga kura hatuna kwani hatuwapigii kura wabunge hawa,wenye kuweza kujibu swali hili vizuri ni wale waliobuni na kuingiza kifungu hiki katika katiba yetu au wale wanaokitekeleza kifungu hiki kwa kufanya uteuzi wa wabunge wa viti maalum kupitia vyama vyao.Hizi siyo zama za kuwa na wabunge wa viti au vitu maalum bali ni zama za kuwa na wabunge wanaotokana na ridhaa ya umma.Hii ina maana kwamba maamuzi mengi ya watawala wetu yamejaa msukumo wa maslahi binafsi au ngono. Hizi ni dalili za giningi ya Tanzania kwenda kombo.[/FONT]

  [FONT=&quot]Aidha, hivi karibuni tumeshuhudia tandabelua ndani ya chama tawala ambacho ndicho watanzania walikipa dhamana ya kutuonesha njia ingawa kuna malalamiko mengi tu kuwa walichakachua kura na matokeo .Tandabelua yenyewe inatokana na msimamo wa chama tawala kuhusu suala la malipo ya DOWANS ambayo imepewa tuzo na mahakama ya kimataifa kuwa ilipwe shilingi za Tanzania bilioni 94 kutokana na kuvunja mkataba. Chombo chenye maamuzi ndani ya chama tawala ni central Committee (CC) kilikaa mahali walipokaa na kutoa msimamo wa kuilipa Dowans uliotofautiana na tamko la Umoja wa vijana wa CCM(UVCCM) waliosema serikali isiwalipe Dowans. Ikiwa bado hakujakucha vizuri chama hicho hicho kimoja kinakuwa na kauli tatu tofauti yaani kilipoenda kitandani kinasema Dowans wasilipwe kwani ilitokana na Richmond ambayo haipo wala haijawahi kuwepo, kilipoanza kusinzia na kuota kwa sababu ya shibe ya miaka mingi maadarakani kikasema Dowans walipwe. Je hii siyo giningi inayokwenda kombo? Wahenga husema milunzi mingi humchanganya mbwa wa msasi ! Aidha, kama hilo halitoshi Rais wa nchi yetu alijitokeza hadhalani na kukiri kwamba yeye hawafahamu dowans wala hana maslahi yoyote nao. Rais katika nchi yoyote ile ni kiongozi wa ngazi ya juu kabisa na ya mwisho ambaye pia ni mamlaka na Taasisi.Chini yake kuna vyombo mbalimbali vinavyomsaidia kutekeleza majukumu yake ya kila siku kama Rais. Vyombo hivi ni pamoja na usalama wa Taifa, Majeshi yote, TAKUKURU na kadhalika. Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kwamba ikiwa Rais pamoja na vyombo vyake vyote hivi hamjui mmiliki wa DOWANS je ni mtanzania gani pale kijiji cha izizimba Kwimba au msoga Chalinze mwenye uwezo wa kufahamu mmiliki wa Dowans ambayo tunaambiwa mara imesajiriwa Nchini Costa Rica mara Tanzania mara Oman?Je Rais Kikwete ni Mfalme Nebukatuneza wa kwenye biblia aliyeshindwa kusoma maneno "mene mene tekeli tepeli" ? Kama hivi ndivyo basi Giningi ya Tanzania inakwenda kombo kwa sababu yake. Mbona serikali ina haraka sana kutaka kutekeleza hukumu ya Dowans? Mbona kuna hukumu nyingi tu ambazo zimetolewa na mahakama zetu za ndani dhidi ya serikali lakini serikali haina haraka wala nia ya kulipa? Mfano mzuri ni hukumu ya kesi zifuatazo nitataja chache kwa ufupi : Mosi ni kesi ya D.P Valambia dhidi ya Transport Equipment Ltd kesi ya madai Na.210 ya mwaka 1989 ambapo serikali iliamuriwa na Mahakama Kuu ya Tanzania DSM kulipa kiasi cha pesa Dola za Marekani 202,922,191.55 kwa mleta maombi ,serikali haikulipa mpaka leo. Pili kesi nyingine ni ya Ali Juma Mwangomba na wengine dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kesi ya madai Na.144 ya mwaka 1996 ambapo mahakama kuu ya Tanazania DSM iliiamuru serikali kuwalipa waleta maombi fidia ya kunyang'anywa ardhi yao Tshs 3,583,993,579.00 hadi leo hii serikali haijawalipa na kesi ya tatu ni kesi ya Bodi ya Tumbaku Tanzania dhidi ya Kiwanda cha sigara ,Tabia njema na wengine,kesi ya madai Na.10 ya mwaka 1996 Mahakama Kuu DSM ambapo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamuriwa kuwalipa wahusika ,mpaka leo hii bado hawajalipwa wengine ni wazee wa Afrika Mashariki ambao tumeshuhudia wanapigwa danadana hawalipwi haki zao.Kwa ushahidi wa kesi hizi ni dhahiri kwamba chama tawala na serikali yake havijawahi wala hakina utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria kama Kapt.Chiligati alivyodai. Kwa utamaduni wao tunapatwa na mshangao kuona wanakimbilia kulipa pesa za Dowans ambazo nazo ni nyingi kama tulizoona kwenye kesi tajwa hapo juu! Kwa nini serikali isitumie ujanja iliotumia kukataa kulipa wadai katika kesi hizo,hii haraka ya kutaka kuwalipa dowans sisi tunaona ina maslahi binafsi ndani yake zaidi kuliko kuheshimu utawala wa sheria na uamuzi wa mahakama.Ikiwa serikali ilishindwa kuheshimu uamuzi wa mahakama kuu ambayo ni kiumbe cha Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,.katiba ambayo ndiyo serikali inatokana nayo iweje leo hii serikali ikimbilie kuheshimu uamuzi wa mahakama ya kimataifa ambayo si kiumbe cha katiba yetu moja kwa moja? Malipo kwa Dowans yataleta balaa kama siyo janga la kitaifa kukosa umeme na kukaa gizani . Watanzania hatukuzaliwa kuzoea shida na umasikini, tunahitaji kuondokana navyo . Huu wote ni utashi wa giningi inayokwenda kombo. Mahali popote duniani hakuna wananchi watakao kaa kimya huku giningi inakwenda na kuwapeleka kombo.[/FONT]

  [FONT=&quot]Watanzania wa leo hasa huko vijijini wana malalamiko, manung'uniko na simanzi zisizo kifani za umasikini. Mwaka 2009 nilipata bahati ya kutembelea Delta ya mto Rufiji ambayo kwa kiasi kikubwa inaundwa na vijiji vya Mbwela, Kiasi, Kiechuru, Nyamisati, Pombwe, Ruma, Dima na vijiji vingine ambavyo ndivyo vinaunda eneo zima la delta ya mto Rufiji kwa kweli watu ni masikini lakini wanaishi juu ya ardhi yenye rutuba kuliko ardhi zote Tanzania! Watu ni masikini kuanzia nywere mpaka unyayo huku wanaginingi wetu wanaogolea katika utajiri usio kifani. Cha ajabu ni kwamba hakuna kiongozi anayejali au kuguswa na umasikini wa hawa watanzania katika delta ya mto Rufiji nakubaliana na Jimmy Carter Rais wa zamani wa Marekani katika kusema: " life is not fair ,and we hasten to add especially to the poor ,the downtrodden,and the wretched of the earth ". Mfumuko wa bei na gharama za maisha zinapanda kila kukicha ukiangalia jitihada ya giningi yetu kupambana na mfumuko wa bei ni sawa na jitihada ya mbwa anayeukimbilia mkia wake aukamate .Hata kule Tunisia ,Bahrain,Misri ,Yemen ,Moroko na Libya wanaginingi wa huko wanaogolea katika utajiri wakati raia wao wanazama katika lindi la umasikini.Matajiri wanatibiwa na kula ulaya au Marekani ,masikini wanafia vijijini kwa kukosa huduma muhimu kama vile matibabu,malazi ,chakula na elimu.[/FONT]

  [FONT=&quot]Shuleni kuanzia msingi hadi sekondari nilifundishwa katika tasnia ya jiografia kwamba ardhi yenye rutuba popote duniani inapataikana katika eneo ambalo lina delta. Delta zijulikanzo duniani ni mabonde yenye utajiri na mali asili kwa wakazi wake na taifa kwa ujumla, mfano bonde la Indo Ganges huko Asia ni maarufu kwa kuzalisha mpunga, Bonde la Irawaadi ni maaarufu kwa kilimo cha pamba huko Burma. Je, bonde la mto Rufiji linazalisha nini na ni maarufu kwa kilimo gani? Hakuna kitu zaidi tunaona viongozi wafidhuli, wala rushwa na mafisadi wanavuna misitu ya mikoko katika delta ya Rufiji kwa faida binafsi huku wananchi wa bonde hili wakiachwa masikini. Hivi sasa kuna mtindo wa viongozi waandamizi wa serikali kuu na serikali za mitaa kupora ardhi ya bonde la mto Rufiji kutoka kwa wananchi masikini hii ni hatari kabisa.Nasikia Mamlaka ya usitawishaji wa bonde la mto Rufiji (RUBADA) iko katika mazungumzo na mchakato wa kubinafisisha bonde la mto Rufiji kwa wawekezaji kutoka Korea Kusini.Je giningi yetu imepanga kuwapeleka wapi wakazi wa bonde hili ambao ni masikini? Mwalimu Nyerere hakuacha mambo haya kwani nchi wala giningi ilikuwa haiendi kombo, hivi leo kama Mwalimu Nyerere angerudi akaona utajiri mkubwa waliojilimbikizia wanaginingi wetu wandamizi serikalini na kwenye chama, nina amini mwalimu Nyerere angekufa tena, safari hii bila kupata ugonjwa.Mwalimu Nyerere alikuwa mfuasi wa falsafa ya Mtakatifu Ambrose kama alivyomnukuu katika kitabu chake cha Binadamu na Maendeleleo kilichochapishwa mwaka 1974 na Oxford University Press katika ukurasa 100 aya ya tano Mtakatifu Ambrose anasema : " You are not making a gift of your possessions to the poor person,you are handing over to him what is his.For what has been given in common for the use of all you have arrogated to yourself…….." That is private property does not constitute for anyone an absolute and unconditioned right.No one is justified in keeping for his execlusive use what he does not need ,when others lack neccesities…" Hapa Mtakatifu Ambrose anawambia matajiri kuwa wanapomgawia hoehae sehemu ya mali zao wakumbuke kwamba hawatoi zawadi kwa masikini huyo bali wanarudisha kwake mali zake walizomnyang'anya kwani hakuna mtu hapa duniani mwenye haki ya kujirundikia lundo la utajiri wakati wengine wanapungukiwa.Hii ndiyo CCM ya nyerere ndivyo ilivyokuwa inaamini.[/FONT]

  [FONT=&quot]Aidha, Mwalimu Nyerere aliacha chama tawala kikiwa na mwelekeo mahususi wala hakikuwa na matajiri , hata akifufuka leo hii ataikana CCM ya leo kama Petro alivyomkana bwana yesu. Kwa kweli giningi ya leo ni Tandabelua tupu kila kiongozi anapigania kujilimbikizia utajiri huku wananchi wakiachwa kwenye lindi la umasikini, Watanzania wengi hawana uwezo wa kujipatia mahitaji kama vile chumvi, shuka, vyandarua, sukari n.k. Watanzania wengi wanakufa kwa magonjwa yanayotibika ama kweli giningi ya Tanzania inakwenda kombo.Watanzania wamejeruhiwa wana makovu ya umasikini na nawaambia wanaginingi kwamba wasidhani mwenye kovu kapona au mla ndizi ni rahisi kusahau,lakini mtupa maganda huwahasahau.Baada ya miaka 30 ya mateso wananchi wa Misri waligundua makovu yao bado ni vidonda wala hawakusahau hadithi ya mtupa maganda,bega kwa bega waliambukizana virusi vya nguvu ya umma na kuiangusha giningi ya Dikteta Hosni Mubaraka.[/FONT]

  [FONT=&quot]Nchi imepigwa roba ya mbao na wala rushwa pamoja na mafisadi ambao ndio giningi . Hawa wametumia gharama kubwa kununua nasaba na dola na ndio wanaoipeleka nchi yetu kombo. Rais kama siyo sehemu yao basi tunaomba awakemee na atuoneshe njia ya kupita. Angali mahospitalini rushwa tupu tumefikia hatua madaktari bingwa kabisa , kwa kuwa hawapati ujira wa kutosha kujikimu kimaisha wanaomba rushwa kwa wagonjwa, mgonjwa anapasuliwa kichwa badala ya goti la mguu au mgonjwa anakatwa mguu ambao ni mzima hauna ugonjwa badala ya kiungo chenye ugonjwa. Tumefikia mahali mgonjwa anafanyiwa upasuaji wa tumbo halafu baada ya wiki moja ndipo madaktari hukumbuka kwamba walisahau mkasi tumboni mwake .Wagonjwa wanaokumbwa na mikasa hii ni wale wanaotoka tabaka la watu masikini ambao hawana uwezo wa kutoa chichiri kwa madaktari,Giningi ya Tanzania inakwenda kombo![/FONT]

  [FONT=&quot]Hebu tazama mahakamani, kumejaa sheria tu lakini hakuna haki kwa wanyonge na walala hoi. Tanzania imegeuka jamii ya matabaka, tabaka la wenye pesa ndio wenye haki katika mahakama zetu, Masikini hawana haki ambao wengi wao wako vijijini.Masikini katika nchi hii hawako salama huonewa, hudhulumiwa , hunyanyaswa, hudhalilishwa na kufanyiwa madhila ya kila aina. Hivi uhuru wa nchi yetu ulikuwa kwa faida ya matajiri wenye nasaba na dola tu kwani ndio wanaofaidi matunda ya uhuru wetu ? Napenda kutoa rai kwa watawala wetu kuwa wanayo dhamana ya kuiweka giningi ya Tanzania katika mstari isiende kombo na isiache njia, wakichelea hili umma wa watanzania utaambukizwa virusi vya nguvu ya umma na kuchukua jukumu kama tunavyoshuhudia Afrika kaskazini, Tunisia, Misri ,Libya na kwingineko duniani. [/FONT]

  [FONT=&quot]Watanzania wanakabiliwa na madhila mengi , wakigeuka kaskazini umasikini, wakigeuka kusini ukimwi ,wakigeuka mashariki njaa na wakigeuka magharibi mabomu na rushwa .Haya mabomu yanayolipuka kila kukicha na kuua watanzania wasio na hatia huko mbagala na gongo la mboto,tuliyanunua kwa pesa ya walipa kodi wa Tanzania sasa yanapoteza maisha ya watanzania wenzetu kuna rafiki yangu mmoja yuko Bukoba idara ya usalama wa taifa alikuwa anatania kwamba yale mabomu ya mbagala na gongo la mboto kuliko kupotea kipuuzi kwa kuua watanzania wenzetu si bora tungeomba vita ya kirafiki na nchi ya Rwanda,Somalia au Burundi tungeyapoteza tumejipima uwezo wetu kivita na kijeshi.Tazama miongoni mwa waliokumbwa na mlipuko wa mabomu iwe mbagala au gongo la mboto hakuna mwanaginingi hata mmoja…ajabu mbona mabomu yanaua masikini tu?[/FONT]

  [FONT=&quot]Wajita kabila mojawapo katika mkoa wa Mara wilaya ya Bunda wana msemo usemao "Obhujuzi ni mwalimu wakisi kusiga ielimu iene" wanasema "ujuzi ni mwalimu mzuri kuliko elimu yenyewe".Ushindi wa kuchakachua matokeo au wa kutumia nguvu hauwezi kuisuluhisha mioyo ya wananchi bali utazidi kuivimbisha na kutafuta kisasi. Hali kadhalika machafuko au vita ni mbaya kwa pande zote aliyeshinda na mshindwa kwa aliyeshindwa huleta hasara kubwa na kwa aliyeshinda huandamwa na kisasi siku zote za maisha yake ndiyo maana Rais Ben Ali ailikimbilia Saudi Arabia ili kukimbia kisasi cha walioshinda ambao sasa ni watesi wake yaani mtesi wa zamani sasa ni mteswa. Watawala wanahitaji ujuzi utakao wawezesha kujenga jamii mpya yenye haki na usawa kwa watu wote. Siyo kama tunavyoona sasa, viongozi wanadiriki kutumia njia za uongo katika kupata kura, wengine huchakachua kura na matokeo yake. Hizi ndizo itikadi za kitaifa? Mgombea anayejua kuchakachua ndiye huchaguliwa na kutangazwa mshindi.Mgombea anayegawa pesa nyingi ndiye anayepigiwa kura nyingi. Hapa namkumbuka tena mwandishi wa Tamthiliya ya "Kivuli Kinaishi" Bwana Said A. Mohamed ambaye anaielezea kwa mapana na marefu nchi ya Giningi inayotawaliwa na viongozi wala rushwa, wasiopenda demokrasia ya kweli, waonevu, na wadhulumaji. Mfano wa utawala wa nchi hiyo ya Giningi uliwajengea wananchi wake hofu na kuogopa kuhoji baadhi ya mambo ya msingi kwa uongozi wao. Falsafa iliyokuwa inatawala katika nchi ya Giningi ilikuwa ni kuwa : "Ukweli ndio uongo na uongo ndio ukweli" Giningi hii ilikwenda kombo hatimaye ikakombolewa na mwana mapinduzi Mtolewa. Hata hapa Tanzania falsafa hii ya ukweli kuwa ndiyo uongo na uongo kuwa ukweli inatawala sana mtu anayependa ukweli hapendwi : muongo, tapeli na mpotoshaji ndiye hushabikiwa sana .Giningi yetu imejaa waongo, wezi, majambazi na wahalifu . Watawala wa Tanzania bado wanayo fursa ya kutosha kurekebisha mambo ili Tanzania isiende kombo, vinginevyo watanzania akina mtolewa watakao kuja kuiweka Giningi yao isiyo kombo kwa maslahi ya watanzania wote. Waswahili husema hata nyoka hauawi hivi hivi tu bali ni kutokana na jina lake baya. Kama sisi ni waadiliu katika kazi zetu na matendo yetu tunahofia nini? Kama tumejenga jina baya kama akina Hosni Mubaraka wa Misri ya wakati huo au Ben Ali wa Tunisia ya wakati huo, basi majina yetu ni mabaya yatafanya tuuawe kama nyoka.[/FONT]

  [FONT=&quot]Giningi ya Tanzania isije ikabweteka na ule usemi wa wahenga kuwa tone moja la maji haliwezi kuleta gharika katika nchi nzima. Hii si kweli maandamano nchini Tunisia yalianzishwa na muuza genge, hali kadhalika yale ya Misri yalianzia katika mkoa mmoja yakasambaa nchi nzima. Hivyo katika zama hizi za elektroniki tone moja la maji linaweza kuleta gharika kama ya Nuhu katika bara zima wala si nchi tu.[/FONT]
  [FONT=&quot]Watawala wowote wale ni zao la jamii yao lakini pia wao ni sehemu ya jamii yao, hivyo hawapaswi kuipuuza jamii inapokuwa ina lalamika. Wanajamii ndio wanaofahamu utawala kuliko watawala wenyewe. Watawala wasidhani kwamba kwa kuwa wao ni watawala basi wanachofanya ni sahihi machoni pa watawaliwa: wahenga husema kukaa karibu na mahakama siyo kujua sheria wala kuishi karibu na chuo kikuu siyo kufahamu kiingereza. Watawala wanapaswa kusoma alama za nyakati kwani alfajiri humtia mtu majaribuni wakati magharibi humuhukumu. Magharibi ya giningi isiyosoma vizuri alama za nyakati i karibu.[/FONT]

  [FONT=&quot]Aidha ni wakati wa watawala makini kung'amua kwamba mamlaka au madaraka waliyopewa na wananchi hayakuwapa sheria, bali sheria ndizo zilizowapa mamlaka au madaraka hayo, hivyo wataadhibiwa na kuhukumiwa na wananchi kutokana na matumizi mabaya ya mamlaka au madaraka waliyokuwa nayo ukweli ni kwamba hata ukimiliki nguvu za dola haziwezi kukusaidia kufa kifo chema. Watawala wanapaswa kujifunza kwamba kila zama na watu wake, walikuwapo wafalme waliokuwa na mamlaka na majeshi yenye nguvu kupindukia watawala walioitawala dunia kwa upanga wa moto. Leo hii wako wapi? Hawako tena. Wamekwishapita! Yuko wapi Dikteta Salazaar wa Ureno? Yuko wapi Benito Mussolini wa Uitaliano? Yuko wapi Adolf Hitler wa Ujerumani? Yuko wapi Dokta Hasting Kamuzu Banda wa Malawi? Yuko wapi Dikteta Generali Sitoyeni Mobutu Seseko Kukumbendu wa zabanga wa Zaire?Yuko wapi Sani Abacha wa Nigeria?Yuko wapi Charles Taylor wa Liberia?Yuko wapi Kabulu P.Botha wa Afrika Kusini? Yuko wapi Josip Tito wa Yugoslavia? Yuko wapi mfalme Hussein wa Jordan ? Hata watawala wa hivi leo wanaweza kupita. [/FONT]

  [FONT=&quot]Katika nchi yetu tofauti ya kipato kati ya masikii na tajiri ni kubwa sana. Uchumi wa nchii hii unahodhiwa na watu wachache wengine wageni, wengine maswahiba wa watawala na wengine watawala wenyewe. Kufumbia macho tofauti za kijamii ni kukalia bomu ambalo likilipuka litawadhuru wananchi zaidi, maana hao wageni na maswaiba watarudi makwao huko ughaibuni. Haya yote ni mabomu yanayotika watawala wanatazama kimya. Hii ni Giningi inayokwenda kombo.[/FONT]

  [FONT=&quot]Vilevile tumeona jinsi watawala walivyoshughlikia mgogoro wa Arusha, hatimaye watanzania wasiokuwa na hatia walikufa , lakini bado watawala wanadiriki kusema uongo kwa kutumia falsafa ya nchi ya Giningi ambako ukweli ni uongo na uongo ndio ukweli.Polisi wa nchi hii hawana leseni ya kuua watu, polisi wakumbuke kuwa bunduki au risasi au panga vyote havijui kiwiliwili au shingo ya aliyevitengeneza. Bunduki haiwezi kugoma kufyatuka eti kwa sababu imeelekezwa kwa aliyeitengeneza. Tunataka jeshi kama la Misri ambalo litagoma kuwaua raia linao walinda. Watawala wetu hawana mamlaka ya kuweka alama ya kuuliza mahali ambapo Mwenyezi mungu aliweka alama ya kituo. Ni mtawala wa namna gani ambaye atapeleka askari wengi wa kutuliza ghasia zisizokuwepo mahali ambapo hakuna ghasia na kuua watu? Ukiona upepo unavuma ujue una mahali unaanzia na kuna mahali unaishia. Iko siku watanzania wataikataa na kuikana Giningi inyowaletea taabu , mateso , dhuluma ,umasikini na kukosekana kwa haki.[/FONT]

  [FONT=&quot]Uhusiano wa watawala na watawaliwa umegeuka kuwa wa kinyonyaji siku hizi . Mtawala anamwombea mtawaliwa azidi kuwa masikini na yeye mtawala anomba aendelee kutawala ili azidi kujilimbikizia mali na utajiri mwingi. Watawala wetu siku hizi wanasali sala kama ya mchonga majeneza ambaye kutwa nzima anaomba mungu amjalie maisha marefu na ayafupishe ya wenzie ili apate wateja wa kutosha wa kununua bidhaa yake ambayo ni majeneza. Utandawazi na uzalendo havitangmani kama lila na fila, kibaya ni kwamba kwa viongozi wetu utandawazi ni sawa na imani yao kidini, ndio unaoipeleka kombo Giningi yetu. Viongozi ambao kwao madeni, mikopo au misaada toka ughaibuni kwao ni ufahari hawatufai kabisa.[/FONT]

  [FONT=&quot]Mwandishi maarufu wa Riwaya toka Ghana Bwana Ayi Kwei Armah aliwahi kuandika kupitia riwaya yake yenye jina la "The Beautyful Ones Are Not Yet Born" kwa kiswahili Wazuri Bado Hawajazaliwa ambayo ilichapishwa na "African Writers Series" mwaka 1969. Mwandishi huyu ingawa alikuwa anaikosoa serikali ya Rais Kwame Nkrumah pia alikuwa anaelezea uezo na ufisadi uliokuwa unazikabili serikali za kiafrika baada ya kupata uhuru kiasi kwamba wananchi walikosa matumaini na imani kwa watawala wao, hadi kupelekea jeshi kupindua serikali ya kiraia na kushika hatamu za uongozi, mwanzoni wananchi waliunga mkono mapinduzi ya kijeshi kwa kuwa walikuwa na matumaini kwamba jeshi lingejenga jamii mpya isiyokuwa na matabaka, rushwa, dhuluma na uonevu lakini ikawa kinyume chake, ndiyo maana mwandishi anasema viongozi wazuri wa jamii zetu bado hawajazaliwa kwa sababu vijana wasafi kabisa waliopo wameharibiwa na mfumo uliopo ambao umeoza, mfumo unaotukuza uongo kuliko ukweli. [/FONT]

  [FONT=&quot]Katika Riwaya hiyo kulikuwa na mhusika mmoja aitwaye "The Man" ambaye alikuwa masikini kwa sababu ya kukataa kupokea rushwa lakini alifurahia sana matunda yatokanayo na rushwa alifananishwa na ndege chichidodo ambaye anachukia sana kukanyaga kinyesi lakini anapenda sana kula funza wanaostawi katika kinyesi. Rafiki yake "The Man" ambaye walisoma chuo kikuu pamoja kwa jina aliitwa Joseph Khomsoon ambaye alichorwa kama waziri katika serikali ya Ghana ambaye alikuwa mla rushwa mwandamizi na tajiri anamwambia rafikiye "The Man" nanukuu maneno yake kwa kiingereza : " You can't remain uncorrupt in a corrupt society, if you do, you must remain poor forever" . Hapa anasema ni vigumu mtu ambaye hapendi wala hapokei rushwa kuendelea kuchukia rushwa katika jamii ya wala rushwa na kama atafanikiwa kubakia msafi lazima atakufa masikini. Huu ni ukweli usiopingika kwani uko dhahiri katika jamii yetu ambayo nayo imo katika ubatili wa kutoa na kupokea rushwa yule ambaye hatoi rushwa anachukiwa wala hapati huduma yoyote na yule anayepokea rushwa anasifiwa na kupongezwa.Mfano mtu ambaye alikuwa kiongozi mkubwa akaacha madaraka bila kuwa na mali hudhihakiwa au kubezwa na jamii yake . Katika jamii ya namna hii huwezi kupata The Beautiful Ones anaowasema mwandishi Ayi Kwei Armah katika riwaya yake, hata miongoni mwetu hakuna The Beautiful Ones.[/FONT]

  [FONT=&quot]Aidha Tanzania ya enzi za Mwalimu Nyerere ilikuwa na dira sahihi, ilikuwa na maadii , miiko na itikeli . Kwa mfano ni kweli kwamba Azimio la Arusha halikuwaondolea watanzania umasikini lakini liliwapa matumaini ya maisha na uzalendo pamoja na utaifa wa kuona kwamba watawaliwa na watawala lengo lao moja ni kujenga nchi moja . Hivi leo kila kitu kimesambaratika kama anavyosema Profesa Chinua Achebe kupitia Riwaya yake ya "Things Fall Apart" iliyochapishwa kwa mara kwanza mwaka 1958. Katika Riwaya hiyo mwandishi anawachora watu wa jamii ya Umuofia wakiwa wamoja wanazungumza kwa sauti moja kabla ya kuja kwa wakoloni hatimaye tunaona umoja wao ulisambaratika wakaishia kutawaliwa wote na mtawala mmoja mkoloni. Hivi ndivyo ilivyo kwa taifa lolote lile linalokwenda kombo badala ya kufuata mstari ulio wima . Kuna mwanasalsfa mmoja wa ki-nigeria aliwahi kusema kuwa unapokuwa na jamii ya matabaka ya walionacho na wasiokuwa nacho, hasa mwanya kati ya masikini na matajiri ukawa mkubwa basi katika jamii hiyo usiku masikini hawalali usingizi kwa sababu wana njaa hali kadhalika matajiri nao hawalali usingizi usiku kwa sababu masikini hawalali na mwisho wa siku katika jamii ya namna hiyo kila mtu halali usingizi usiku. Swali la msingi la kujiuliza hapa ni: Je katika jamii yenye mfumo wa namna hii kimaisha nani anafaidi masikini au tajiri ikiwa wote hawalali usingizi? Bila shaka jamii ya namna hii inahitaji kujengwa upya na kuondoa matabaka yote. Matabaka ni adui wa utaifa, umoja, usawa na uzalendo katika jamii. Haya siyo mambo ya kunyamazia uwe kiongozi uwe mwananchi wa kawaida kama anavyoonya Profesa Wole Soyinka wa Nigeria ambaye alisema maneno haya alipokuwa jela kwa kupinga utawala dhalimu wa Nigeria nanukuu :[/FONT]

  [FONT=&quot] " The Man dies in all who keep silent in the face of tyranny" .Hapa Profesa anasema mwanadamu anayekaa kimya katikati ya udhalimu hutoweka kabisa.[/FONT]
  [FONT=&quot]Giningi inayokwenda kombo itambue kwamba haiwezi kupendwa na watawaliwa wake, mwisho wake ukifika italazimishwa kwenda uhamishoni. Profesa Chinua Achebe katika Riwaya yake ya "Things Fall Apart" katika ukurasa wa 94 anaeleza sababu za watawala wanaosubiri waondolewe madarakani kwenda uhamishoni anasema nanukuu " A man belongs to his fatherland when things are good and life is sweet, but when there is sorrow and bitterness he finds refuge in another land[msisitizo ni wa kwangu]"Profesa anasema mwanadamu ( mtawala) ataishi katika jamii ya baba yake ikiwa mambo au utawala wake unakubalika na wengi katika jamii hiyo ,ikiwa hauendi vizuri basi atalazimika kutafuta hifadhi katika jamii nyingine husasani anakotokea mama yake" [/FONT]

  [FONT=&quot]Mwisho namalizia makala yangu kwa kutoa rai kwa watawala wetu walioko Giningi tayari,wanaotafuta kuingia giningi na watakao kuja , kwamba giningi inayokwenda kombo kwa kawaida huwa haidumu ili giningi ya namna hiyo iweze kudumu lazima ijitahidi kujenga jamii mpya yenye haki na usawa kwa watu wote watawaliwa na watawala, masikini na matajiri, wazee kwa vijana, wake kwa waume. Vinginevyo jamii mpya itajengwa na kizazi cha sasa , kizazi cha mtandao wa facebook na twitter ,kizazi cha akina Lenin, Karl Marx, Engels, Che Guevara wa kileo ambao huambukizana virusi vya kimapinduzi viitwavyo nguvu ya umma ambavyo ni tishio kwa walioko giningi .[/FONT]
   
 2. Makanyaga

  Makanyaga JF-Expert Member

  #2
  Mar 9, 2011
  Joined: Sep 28, 2007
  Messages: 2,498
  Likes Received: 127
  Trophy Points: 160
  Ndefu mno, inachosha.
  Halafu maneno aliyoambiwa mfalme Nebkadnezzar yalikuwa "Mene Mene Tekeli na Peresi", siyo kama ulivyoyatoa wewe. Yalimaanisha kuwa ufalme wake umehesabiwa, umepimwa kwenye mizani ukaonekana umepungua, umegawanyika na utakomeshwa kabisa. Mwenye Mamlaka ndiyo alitoa hayo maneno
   
 3. George Maige Nhigula Jr.

  George Maige Nhigula Jr. Verified User

  #3
  Mar 9, 2011
  Joined: Mar 14, 2008
  Messages: 470
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Watanzania ni wazembe wa kujisomea, hii makala sio ndefu, ni kutokana na mfumo wetu wa elimu ambao hautufunzi kujenga mapenzi ya kujisomea.
  Mtu akisha graduate chuo wala hana interest ya kujisomea tena, ndo maana hata makazini tunakuwa very incompetent kwa sababu ni wavivu wa kujisomea na hata mikataba yote hii mibovu inayosainiwa ni kutokana na wanasheria wetu hawaisomi na kuichambua ili kujilidhisha kama ina maslahi kwa taifa,

  Jamani, tukubali kujisomea sio makala tu hata vitabu mbalimbali, ama kweli ukitaka kumteta mtanzania mwandikie!

  Nahukuru kwa marekebisho nadhani mwandishi atayazingatia
   
 4. g

  geophysics JF-Expert Member

  #4
  Mar 9, 2011
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 904
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Sasa wewe una post kitabu kizima na hali ya maisha yenyewe unaiona mgawo wa umeme...(computer na simu zinaisha umeme) foleni za magari (wenzio twachelewa kurudi nyumbani) printer wino bei mbaya kuchapa nakala. Si unge andika kwa ufupi ukaelekeza anaependa kufuatilia afuate link fulani? Hata hivyo tunakushukuru.
   
 5. Jaslaws

  Jaslaws JF-Expert Member

  #5
  Dec 24, 2014
  Joined: May 31, 2011
  Messages: 5,129
  Likes Received: 2,186
  Trophy Points: 280
  Jf imekufa sikuhizi uwezi kukuta waandishi kma hawa..sikuhizi kumejaa ma sijui babe nani sijui swt nani..!!ovyo!!@back jf
   
Loading...