TANZANIA INAVYOPOTEZA NAFASI ZA KIUCHUMI AFRIKA MASHARIKI

de paymer

Member
Jan 4, 2016
41
27
Tanzania ndiyo nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki inayoongoza kwa kuwa na eneo kubwa, idadi kubwa ya nguvukazi, eneo kubwa la ardhi inayofaa kwa kilimo, rasilimali nyingi na imekuwa katika hali ya utulivu na amani.

Mazingira hayo yanatosha kabisa kuifanya iwe na uchumi mkubwa na kuvuta wawekezaji wengi. Hata hivyo, tafiti za kiuchumi zinaonyesha hali hiyo ni kinyume chake.

Ripoti za kiuchumi za kimataifa zinaonyesha Tanzania imekuwa ikipoteza nafasi yake ya kuongoza kiuchumi katika ukanda wa Afrika ya Mashariki mfululizo katika miaka ya karibuni.

Jambo hilo, limekuwa na athari katika kuvutia wawekezaji nchini na katika dhamira yake ya kufufua viwanda na kufanya mageuzi ya kiuchumi, licha ya kuwa na utajiri mkubwa zaidi wa maliasili na rasilimali kuliko nchi nyingine yoyote katika ukanda huu.

Tafiti zilizofanywa na taasisi za kimataifa, ambazo hutumika kila mwaka katika kulinganisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyofikiwa na nchi mbalimbali duniani zinaashiria kuna kila haja kwa Tanzania kujitathmini na kujipanga upya.

Takwimu za tafiti hizo zinaonyesha kuwa siyo za kuzisoma na kuzitupa bali wataalamu wetu wanapaswa kukaa chini, kuumiza vichwa vyao na kuangalia nini kifanyike kunusuru taifa lisiendelee kudidimia kiuchumi.

Hali inaonyesha kuwa, Tanzania imekuwa ikijipima kwa takwimu zake za hapa nchini, ambazo huipumbaza na kuifanya ijione iko katika hali nzuri za viwango vya kimaendeleo lakini ukweli ni kwamba ikijilinganisha na nchi nyinginezo duniani, iko nyuma.

Ripoti ya Kimataifa ya Mazingira Bora ya Ushindani wa Kiuchumi na Uwekezaji Duniani (GCI) iliyotolewa mwaka huu inaonyesha tathmini iliyofanyika mwaka 2015, Tanzania ilishika nafasi ya 120 kati ya nchi 140 zilizojumuishwa kwenye utafiti huo.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania imeshika nafasi ya nne kati ya nchi tano. Ya kwanza, ni Rwanda, ambayo imekumbwa na machafuko ya muda mrefu, yakiwapo mauaji ya kimbari 1992.

Kwenye ripoti hiyo ya nchi 140, Rwanda inashika nafasi ya 58, ya pili ni Kenya, iliyoshika nafasi ya 99 na ya tatu ni Uganda, iliyoshika nafasi ya 115. Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania inaizidi Burundi, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa. Tanzania ina kila sababu ya kujiuliza ni kwa nini ipo kwenye nafasi hii.

Mazingira mazuri kiuwekezaji

Serikali ya awamu ya tano, unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuipitia upya Sera ya Uwekezaji nchini ili iweze kuvutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi. Hii ni kutokana na tafiti kuonyesha kuwa haina mazingira mazuri ya kiuwekezaji ikilinganishwa na nchi za ukanda huu.

Utafiti wa Mazingira Mazuri ya Kibiashara (EDBI) unaonyesha nchi zenye Mazingira rafiki zaidi ya kufanya biashara duniani, Tanzania inashika nafasi ya 139 kati ya nchi 189.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania inashika nafasi ya nne kati ya nchi tano. Ya kwanza, ni Rwanda iliyoshika nafasi ya 62 kimataifa ya pili ni Kenya, iliyoshika nafasi ya 108, ya tatu ni Uganda, iliyoshika nafasi ya 122 ikifuatiwa na Tanzania na Burundi ni ya mwisho kikanda, ikishika nafasi ya 152 kimataifa.

Kikwazo kwa Tanzania

Wachunguzi wa mambo ya kiuchumi wanasema urasimu, kukithiri kwa rushwa na uelewa mdogo katika biashara za kimataifa, ni baadhi tu ya sababu zilizoikwaza Tanzania katika kuvutia wawekezaji wa kimataifa na wa ndani.

Teknolojia ya Tehama na ufisadi

Ripoti nyingine ya Kimatiafa ya mwaka 2014 ya Kupima Utayari wa Matmizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (NRI) nayo imeiweka Tanzania kwenye nafasi ya nne Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo imeiweka Tanzania kwenye nafasi ya 125 kati ya nchi 148 duniani, zilizoguswa na tathmini hiyo. Rwanda inaonekana kuendelea kuongoza Katika Afrika Mashariki ikifuatiwa na Kenya, Uganda na Burundi ni ya mwisho.

Katika Ripoti ya Viwango vya Rushwa Duniani (CPI), Tanzania inashika nafasi ya 119 kati ya nchi 175. Ripoti hii inaonyesha angalau Tanzania iko nafasi nzuri katika ukanda wa Afrika Mashariki.
 
Back
Top Bottom