Tamko la Ummy Mwalimu kuhusu wananchi kushambulia madaktari na wauguzi

Egnecious

JF-Expert Member
Jul 8, 2015
875
960
Ndugu Wananchi,

Nachukua fursa hii nikiwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya nchini, kutoa tamko kuhusiana na matukio ya hivi karibuni yaliyoripotiwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusiana na vitendo vya kusikitisha wanavyofanyiwa watumishi wa sekta ya afya, wakiwemo Madaktari kama vile kushambuliwa kwa maneno na vipigo. Pasi na shaka, vitendo hivyo vitaathiri upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wanaopewa huduma hizo hususan wa kipato cha chini.

Matukio haya yanajumuisha tukio lililotokea tarehe 27.03.2016 katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, ambapo Dr Dickson Sahini alishambuliwa na ndugu wa mgonjwa aliyepelekwa hapo kuhudumiwa.

Napenda kutamka kwamba nimesikitishwa sana na tukio hilo, na ninalaani vikali matukio ya watumishi wa afya kushambuliwa kwa maneno au kwa vitendo na wananchi wanaopatiwa huduma. Jambo hili likiendelea litawavunja moyo watumishi wa afya na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Ningependa kuwafahamisha kwamba kwa ujumla wake sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi sana katika maeneo ya miundombinu, dawa na vifaa tiba, watumishi wa kutosha, pamoja na kuwa na watumishi wasiozingatia nidhamu, weledi na maadili katika kutimiza majukumu yao.

Ninatambua kwamba changamoto hizi zipo siku nyingi, na zimekuwa zikitafutiwa majawabu na Serikali za awamu zilizopita ikiwemo ile ya awamu ya nne. Lakini sote ni mashahidi kwamba Serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dr John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inachukua hatua za makusudi katika kutatua changamoto hizi, likiwemo pia suala zima la utendaji unaozingatia uwajibikaji.

Kwa hiyo ninawasihi sana wanachi wanaopatiwa huduma katika vituo vyetu vya afya kote nchini kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mikononi na kufanya vitendo vinavyoweza kuwakwaza watumishi wa afya. Kwa vile nchi yetu inafuata misingi ya utawala unaozingatia sheria, ni vyema wananchi wakafuata taratibu zilizowekwa wanapohisi kwamba hawakupatiwa huduma za afya wanavyostahili.

Aidha nachukua fursa hii kuvitaka vyombo na mamlaka husika kutosita kuwachukulia hatua wananchi wanaokwenda kinyume na matakwa ya sharia ili kuwahakikishia watoa huduma za afya usalama na amani wakati wa utoaji wa huduma hiyo.

Ninaagiza vile vile kwamba hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini ziweke utaratibu mwepesi wa wananchi kufikisha malalamiko yao pindi wanapoona kwamba hawakupatiwa huduma za afya kwa kiwango stahiki.

Napenda pia kuahidi kwamba tutajitahidi kutatua changamoto za kimfumo zilizopo katika utoaji wa huduma za afya nchini ili kuufanya utoaji wa huduma kuwa bora zaidi.

Ndugu Wananchi,

Ninatambua kwamba sehemu kubwa ya watumishi katika sekta ya afya nchini wanafanya kazi zao kwa ufanisi, upendo, uadilifu na kwa kuzingatia matakwa ya weledi (professionalism) na miiko ya taaluma zao (ethics). Pia ninatambua kwamba wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanatumia muda wa ziada kuendelea kuwahudumia wagonjwa hadi wanapoona wapo salama. Ninawapongeza kwa dhati watumishi hawa na ninawashukuru na kuwatia moyo waendelee kuwa na tabia hiyo nzuri, kwa maslahi ya Taifa letu.

Hata hivyo ninasikitishwa sana na tabia ya watumishi wa afya wachache ambao wanafanya kazi kinyume na maadili na matakwa ya weledi wa taaluma zao. Napenda kusisitiza kuwa Wizara yangu haitavumilia matukio ambayo watumishi wa Sekta ya Afya watakwenda kinyume na matakwa ya weledi na maadili ya taaluma zao katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Hivyo hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kudhibiti hali hii.

Nimeshaelekeza vyombo vya kusimamia maadili ya watoa huduma za afya nchini, yaani Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) kuchukua hatua mara moja, kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zao, juu ya watoa huduma wote wanaotuhumiwa kukiuka misingi ya weledi na maadili ya taaluma zao. Endapo tuhuma zao zitathibitika, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kufutiwa usajili au leseni zao ikibidi.

Hivyo kwa tamko hili ninawaasa na kuwaagiza watoa huduma wa afya wote nchini kufanya kazi zao kwa bidii, kwa nidhamu na kwa kuzingatia weledi na maadili ya kitaaluma kama inavyoelekezwa.

Ndugu Wananchi,

Napenda pia kukumbusha kwamba kazi hii ya usimamizi wa mahusiano mema kati ya watoa huduma za afya na wananchi, na usimamizi wa weledi na maadili katika vituo vya kazi, itafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Kamati za Usimamiaji wa Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya, Kamati za Usimamiaji wa Huduma za Afya za Hospitali, na Wananchi wote kwa ujumla katika kuwasimamia, kuwaelekeza na kutambua mapungufu ya kimfumo au yale yanayohusu watumishi wa afya yaliyopo na kuchukua hatua zinazostahili mara moja. Ni lazima tuzingatie Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutimiza jukumu hili. Wizara ya Afya itaendelea kuvijengea uwezo Mabaraza ya kitaaluma ya wataalamu wa afya ili kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Tufanye kazi kwa pamoja ili kutekeleza kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, inayosema ‘HAPA KAZI TU’.

Asanteni sana.


Imetolewa na:
Mhe. Ummy Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mtwara – Tanzania
29 Machi 2016
 
Haitoshi,inabidi aende Mtwara akaitishe mkutano na wananchi akajaribu kufanya damage control alioharibu PM wake! Aombe radhi kiutu uzim aone jinsi reaction ya wananchi ili aweze kuweka level nzuri kwa wauguzi na madaktari nchi nzima!....akaanzie Ntwara
 
Binafsi sijaelewa vizuri jinsi tukio lilivyotokea mpaka bwana mganga akapewa kichapo. Nataka kueleweshwa ili nione kwa upana. Serikali iko busy kulaani tuu pasipo kwenda kwenye hoja iliyopelekea kupigwa kwa huyo bwana mganga. sisemi kwamba kupigwa ni sahihi ila nataka kuona mazingira ya hicho kipigo. sekta ya afya nchini imekuwa ikitajwa kwa rushwa na ukiritimba usio na maana kwa jamii.
Mwenye kulielewa vizuri hilo tukio hilo tafadhari anijuze
 
Hili suala lichukuliwe kuwa ni uhalifu tu na lisihusishwe na masuala ya kisiasa, wapo trafik walioshambuliwa na madereva, wapo polisi walioshambuliwa na majambazi vituoni, wapo walimu waliodundwa na watoto watukutu. Uhalifu ni uhalifu na wala usihusishwe na masuala ya kisiasa. Wapo maafisa ardhi walioshikiwa kwa mapanga na wanakijiji wakiwa katika zoezi la upimaji ardhi.

Zipo hoja za msingi zinazopaswa kuelezewa na kamwe zisichukuliwe kisiasa, najua madakari ni watu wenye weledi na hatutegemei wafanye mambo kienyeji enyeji.
 
Walimu walikula mikwaju kwa mkuu fulan hvi. Spoke zile walirandwa umati haukuliona kuwa ni tatizo. Marais nao hupopolewa mawe huko nyanda za juu katika misafara yao watu hawakuchukulia kama ni ishu. Madaktar sasa wanapewa kipigo cha mbwa mwizi bado tunasuasua. Hzi alinifundisha Dr wangu mmoja pale udsm zinaitwa professional risks ambazo zikiendeleq huitwa hazards. Sasa ianzishwe posho kwa watumishi wa uma kila mwezi walipwe hiyo risks wanayo incur kwa kuhudumia wateja wao wananchi maana hamna namna sasa
 
Walimu walikula mikwaju kwa mkuu fulan hvi. Spoke zile walirandwa umati haukuliona kuwa ni tatizo. Marais nao hupopolewa mawe huko nyanda za juu katika misafara yao watu hawakuchukulia kama ni ishu. Madaktar sasa wanapewa kipigo cha mbwa mwizi bado tunasuasua. Hzi alinifundisha Dr wangu mmoja pale udsm zinaitwa professional risks ambazo zikiendeleq huitwa hazards. Sasa ianzishwe posho kwa watumishi wa uma kila mwezi walipwe hiyo risks wanayo incur kwa kuhudumia wateja wao wananchi maana hamna namna sasa
tuache mizaha isiyokuwa na tija, tujadili hoja kwa mapana. Mwaka 2013 wagonjwa waliotibiwa hospitalini walikuwa
56,988,781, lakini wahalifu waliofikishwa vituoni walikuwa 566,702. Jiulize nchi hii kati ya polisi na madaktari wapi wengi?
 
Back
Top Bottom