Tamko la CHADEMA kanda ya Pwani kuunga mkono Operesheni UKUTA

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
1.0. UTANGULIZI

Ndugu waandishi wa habari, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Pwani inayojumuisha mikoa ya Pwani na mikoa ya kichama ya Ilala, Kinondoni na Temeke, kwanza kabisa, tunasikitishwa sana na kulaani viashiria vya wazi vya utawala wa kidikteta ( Autocratic Rule) inayoendelezwa hapa nchini na Rais John Magufuli na Serikali yake ya CCM.

Pili, CHADEMA Kanda ya Pwani tunaunga mkono Kauli na Tamko la Kamati Kuu CHADEMA kuhusu utawala huu wa kidikteta na msimamo wa kuupinga, na kwamba CHADEMA Kanda ya Pwani tutashiriki kikamilifu katika Operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) uliobuniwa na Kamati Kuu na ulioanza kutekelezwa nchi nzima na itafikia kilele chake tarehe 01/09/2016.

2.0. UTAWALA WA KIDIKTETA (AUTOCRATIC RULE)

Ndugu waandishi wa habari, kwa faida yenu na ya watanzania wengine, labda tutoe tafsiri ya kawaida ya "autocratic rule" kwa kiingereza:-

"Autocratic rule is a leadership style characterized by individual control over all decisions and little input from other citizens. Autocratic rulers or leaders typically make choices or decisions based on their ideas and judgments and rarely accept advices from subordinates or other people".

Tafsiri fupi na rahisi ya "autocratic ruler" kwa kiswahili ni kwamba huyu ni mtawala au kiongozi dikteta ambaye mamlaka yote ni ya kwake, na hufanya maamuzi kwa kuzingatia utashi wake bila kusikiliza au kushauriwa na anaowaongoza.

Utawala tunaoushuhudia hapa nchini wa Rais Magufuli kwa hakika ni utawala wa kidikteta (autocratic rule/leadership).

3.0. "UDIKTETA UCHWARA" NI NINI?

Udikteta ni aina (mbaya) ya utawala, na wala sio tusi. Kwenye nchi zenye madikteta wa kweli (autocratic rulers) kwa kawaida wanafuta kabisa utawala wa kidemokrasia na hata mfumo wa vyama vingi vya siasa haukubaliki. Sasa unapokuta watawala ambao bado nchi zao zina Katiba na Sheria zinazotambua mfumo wa demokrasia na vyama vingi vya siasa lakini wanaendesha nchi zao kidikteta, huu unakuwa ni unafiki wa kiuongozi kwa sababu wanatangaza demokrasia lakini wanaendesha nchi zao kidikteta (They preach democracy but practice dictatorship/autocracy). Mfumo huu wa utawala wa kinafiki wa kuwa na demokrasia kwenye sheria/kauli lakini kunakuwa na udikteta kwenye uendeshaji wa nchi, unaweza kuuita "udikteta uchwara", kwa kukosa maneno mazuri ya kiswahili. Hili nalo sio tusi wala uchochezi.

Huu ndio utawala tunauona nchini Tanzania toka Serikali ya Magufuli iingie madarakani takriban miezi kumi iliyopita.

4.0. UMUHIMU WA KUKUZA DEMOKRASIA NCHINI

Historia inaonyesha kwamba pamoja na baadhi ya madikteta duniani kufanya mambo mazuri ya maendeleo kwa nchi zao na wananchi wao, lakini walikuja kushindwa na kung'olewa, wengine kwa aibu kubwa, kwa sababu ya kufinyanga demokrasia. Hii ni kwa sababu binadamu hata ukimfanyia mazuri kiasi gani kama ukimnyima uhuru wake wa kusema, kushirikiana na watu, na kutoa maoni kwa mambo yanayohusu maisha yake na ya jamii yake, hawezi kufurahia hayo maendeleo mengine na lazima ataasi mwisho wa siku. Uhuru wa mtu ndio maendeleo yake namba moja!

Toka aingie madarakani mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli amechukua hatua kadhaa nzuri za kuleta maendeleo ya watanzania kama kudhibiti rushwa, kubana matumizi ya ovyo, kukusanya kodi na kuwabana wazembe kwenye utumishi wa umma. Mambo haya yamefurahiwa na wananchi walio wengi hata kama baadhi yake yamefanywa bila kufuata taratibu nzuri na Sheria. Lakini Rais atambue kwamba haya mazuri yote yameanza kumezwa na kufutwa na hili baya sana la kuvunja Katiba na kuminya demokrasia na uhuru wa watu kukusanyika, kutoa maoni na kukosoa Serikali.

5.0. UVUNJAJI WA KATIBA NA SHERIA ZA NCHI

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaeleza wazi, kwenye Misingi yake, kwamba Katiba hiyo imetungwa kwa madhununi ya kujenga jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia, ujamaa na isiyokuwa na dini.

Ibara ya 3 ya Katiba inatamka kwamba Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. LAKINI tumeona jinsi Rais anayojaribu kuua demokrasia ya vyama vingi kwa kukataza na kuzuia mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani huku yeye kama Mwenyekiti wa CCM akiendelea na mikutano kama hiyo.

Ibara ya 4 ya Katiba inaelezea mgawanyiko wa madaraka kati ya mihimili mitatu inayojitegemea ya Serikali, Mahakama na Bunge. LAKINI tumeona jinsi Bunge linavyoingiliwa na Serikali kwa kutumia kiti cha Spika na wingi wa wabunge wa CCM, na kuzuia matangazo ya moja kwa moja (Live Coverage) ya majadiliano ya wabunge.

Ibara ya 20 ya Katiba inatoa uhuru wa watu kukutana na watu wengine kwa hiari na amani na kutoa mawazo yao hadharani. LAKINI tumeona jinsi Rais Magufuli alivyopiga marufuku wapinzani kukutana kwenye mikutano ya hadhara huku akiwatisha kwamba wakikaidi, hatua hiyo itakuwa ni kumjaribu na ati yeye hajaribiwi na atawashughulikia. Na kweli amewaamuru Polisi ambao wanatekeleza amri hiyo kwa kuwakamata, kuwadhalilisha, kuwaweka ndani na hata kuwafungulia mashitaka ya ovyo mahakamani wapinzani wanaotoa mawazo yao hadharani na wanaokosoa utendaji wake. Mifano ya kukamatwa mara kadhaa na kufunguliwa mashitaka Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Mhe. Tundu Lissu na viongozi kadhaa wa CHADEMA imeonekana kwa kila mtu. Hii ya mikutano CHADEMA kanda ya Pwani tumeathirika pia ambapo mikutano kadhaa iliyoandaliwa maeneo mbalimbali ya Kanda hii ilizuiwa na Polisi. Hata pale ambapo mkutano wa hadhara uliruhusiwa na Polisi kufanyika pale Chalinze mkoa wa Pwani wiki iliyopita lakini muda mfupi kabla mkutano kuanza Polisi hao hao wakauzuia. Ni wazi Mkutano huu ukizuiliwa kwa sababu ulikuwa uhudhuriwe na Mhe. Frederick Sumaye ambaye ni mkazi wa mkoa wa Pwani. Lakini Polisi wakadai mkutano ulizuiliwa kwa sababu ulikuwa uhudhuriwe na viongozi wa CHADEMA kutoka nchi nzima! Tunajiuliza, hivi Mhe. Sumaye ndiye CHADEMA nchi nzima?

Ibara ya 63 ya Katiba inaelezea pia madaraka ya Bunge kuisimamia na kuishauri Serikali. LAKINI tumeshuhudia Uhuru wa Bunge ukizimwa na wabunge, hasa wa upinzani, wakizuiwa kutoa mawazo yao ya kuikosoa na kuisimamia Serikali na hata kuadhibiwa kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge.

Lakini pia Sheria ya Vyama Vya Siasa ya mwaka 1992, Kifungu cha 11 imekuwa ikivunjwa na Rais na Polisi kwa kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani; huku Jeshi la Polisi likitumia vibaya Kifungu Na. 43 (3) cha Sheria ya Jeshi la Polisi, Sura 322 kwa kuzuia mikutano kwa kisingizio cha hali ya usalama na taarifa za kiintelijensia. Kwa sasa Rais na Polisi wameweka sharti la ajabu la kutaka mikutano ya hadhara kutohudhuriwa na mtu asiyetoka eneo husika. Huo ni ubaguzi wa aina mpya na unyimaji wa uhuru wa watanzania kwenda mahali popote nchini na kushirikiana na wenzao kwenye shughuli mbalimbali zikiwemo za kisiasa. Aidha agizo la kutambua walioshinda uchaguzi tu kwamba ndio wanasiasa wa kufanya siasa na wengine wote kupigwa marufuku ni kichekesho kikubwa katika utawala wowote wa kidemokrasia. Hata viongozi na wanachama wa vyama vilivyokosa madiwani na wabunge ni wanasiasa na lazima waendelee kufanya siasa.

Mbaya zaidi Jeshi la Polisi linazuia hata mikutano ya ndani ya vyama vya upinzani na makongamano, na hata mahafali ya wanafunzi wenye itikadi za upinzani, huku likitambua kwamba mikutano kama hiyo ya ndani haiwezi kuleta uvunjifu wa amani kwa walio ndani wala nje ya kumbi hizo.

Katika hili la mikutano ya ndani CHADEMA Kanda ya Pwani tumeathirika pia baada ya wiki jana mikutano ya ndani kuzuiwa kufanyika kwenye kumbi za kukodi za PTA Sabasaba na Bandari kwa sababu tu Mhe. Lowassa alikuwa ashiriki kwenye vikao hivyo. Ni wazi Serikali hii inawaogopa sana Lowassa na Sumaye! Lakini hii haishangazi kwa namna mawaziri wakuu hawa wanavyojadiliwa na kusemwa sana kwenye vikao vya CCM hata kuliko viongozi na makada wa chama hicho tawala.

Kutokana na Serikali ya Rais Magufuli kubaka wazi wazi demokrasia nchini, na katika kuunga mkono Tamko la Kamati Kuu, CHADEMA Kanda ya Pwani imeazimia kushiriki kwa nguvu zote kwenye Operesheni UKUTA katika mikoa, wilaya, kata, matawi na misingi yote ya Kanda ya Pwani siku hiyo ya tarehe 01/09/2016 yatakayohitimishwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano. Nia ni kupinga ukandamizaji wa demokrasia na uhuru wa vyama vya upinzani kufanya siasa kama Katiba na Sheria za nchi zinavyoruhusu. Tayari CHADEMA Kanda ya Pwani imetoa maagizo kwamba kuelekea Septemba mosi ngazi zote za Chama zipange mikakati mbalimbali ambayo wameshaelekezwa ya kujiandaa kwa Operesheni UKUTA tarehe 01/09/2016.

6.0. HITIMISHO

CHADEMA inamwambia Rais Magufuli na Serikali yake kwamba Operesheni UKUTA lazima itafanyika Septemba mosi mwaka huu, na ikiwa Rais akitaka tusitishe Operesheni hii, achukue hatua zifuatazo kabla ya tarehe hiyo:-

(1) Rais aanze mara moja kuishi Kiapo chake cha kulinda, kuhifadhi na kuifuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara zake zote 152.

(2) Rais aache mara moja dhamira yake inayoonekana wazi ya kutaka kuua demokrasia ya vyama vingi hapa nchini ili nchi irudi kwenye mfumo wa chama kimoja.

(3) Rais aache utawala wa kibabe na wa kidikteta (autocratic leadership) ambao utapelekea nchi hii kuwa nchi isiyokuwa na utawala wa kisheria (anarchical state).

(4) Muhimu na haraka, Rais Magufuli atoe tamko la kuacha vyama vya upinzani vifanye siasa, mikutano ya hadhara na maandamano halali na ya amani bila kizuizi chochote na wala masharti yoyote.

....La sivyo, tukutane kwenye UKUTA Septemba mosi, 2016!


Casmir Juma Mabina
KATIBU WA KANDA YA PWANI (CHADEMA)
 
Back
Top Bottom