singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mjini Dodoma Januari 21, 2016.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-(OR-TAMISEMI) kuhakikisha inaisimamia vizuri Mikoa na Halmashauri ili serikali iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa.
Akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI alipoitembelea ofisi ya TAMISEMI mjini Dodoma leo, Mhe. Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.
“Hatukubaliani na uzembe kwenye idara na halmashauri za wilaya kwakuwa hivi sasa serikali ya awamu ya tano inasimamia utumishi wa uadilifu hivyo kila mmoja ahakikishe anasimamia vizuri eneo lake” alisema Mhe. Majaliwa
Alisema serikali ya awamu ya tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia serikali imeanza kuwajenga watumishi wa serikali kutambua na kukumbuka kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema.
“Lazima tujenge moyo wa huruma wa kuwahudumia wenzetu, anapokuja mwananchi msikilize, muhudumie na mwelekeze eneo sahihi ili aweze kupata huduma. Lazima tusimamie na kuona maeneo yote yanafanya kazi kama ilivyokusudiwa, ili kupata matokeo tarajiwa iwe ni wajibu ya kila mmoja kuhakikisha kuwa anatoa usimamizi thabiti katika eneo lake.” alisisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. George Simbachawene alisema TAMISEMI wapo tayari kubadilika na kufanya kazi kama kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli –HAPA KAZI TU-.