Tamaa za wanasiasa wetu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tamaa za wanasiasa wetu

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Jumakidogo, Oct 30, 2010.

 1. Jumakidogo

  Jumakidogo R I P

  #1
  Oct 30, 2010
  Joined: Jul 16, 2009
  Messages: 1,859
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 0
  Tamaa ya uongozi na idadi kubwa ya ahadi zisizotekelezeka
  Na Juma Kidogo
  Ni siku na wakati mwingine tena tunakutana ndugu zangu wapendwa katika ulingo huu wa siasa ili kujadili mambo mbalimbali kuhusiana na tukio kubwa kabisa linalotarajia kufanyika katika wiki chache zijazo. Ni tukio adimu kutokea kama yule mnyama maarufu
  “Kakakuona”
  ambaye huonekana kwa nadra sana machomi mwa watu. Tukio ambalo huambatana na mambo mengi ya kupendeza na, kuchukiza pia. Matusi, kejeli, dhihaka na dharau huu ndiyo wakati wake. Uvumi, vurugu pamoja na idadi ya kesi mahakamani huongezeka katika kipindi hiki. Tukio hilo ni uchaguzi mkuu wa Raisi, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mnamo tarehe 31/10/ mwaka huu wa 2010.

  Lakini pamoja na yote hayo, lipo moja kuu ambalo ndilo la msingi zaidi katika wakati huu wa kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi huo mkuu. Jambo hilo ndilo msingi mkuu wa kampeni za wagombea zinazoendelea kutifua vumbi nchi nzima hivi sasa. Hilo ndilo mtoto aliyezaliwa kutoka katika Ilani za uchaguzi za vyama mbalimbali vya siasa nchini, Jambo hilo ni ahadi kwa wananchi na wapiga kura kwa ujumla ambazo zinaendelea kutolewa na wagombea wa ngazi mbali mbali za uongozi nchini.

  Kwa uelewa wangu finyu nilitegemea kuwa viongozi hawa watarajiwa watakuwa wakiahidi kusimamia mambo ambayo yameainishwa katika Ilani zao za uchaguzi tu, lakini kumbe mambo yamekuwa tofauti. Wagombea wamekuwa wakiahidi mrundikano wa mambo ambayo uwezekano wa kuyatekeleza yote katika kipindi cha miaka mitano hiyo ya uongozi wanayoipigania ni sawa na ndoto za mchana ambazo huwa hazina ukweli wowote. Uchaguzi mkuu wa mwaka huu umekuwa na msisimko mkubwa sana kiasi cha kufikia mashabiki na wanachama wa vyama mbalimbali kutupiana makombora makali ya maneno kwenye mikutano yao ya kampeni.
  Eidha kumekuwa na ukosolewaji wa moja kwa moja kwa viongozi ambao hawakutimiza ahadi zao baada ya kupewa dhamana ya kuongoza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hiyo ni dalili tosha inayoonyesha kuwa watanzania wa sasa hawadanganyiki, ni dalili tosha inayoonyesha kuwa watanzania wa sasa ni makini na wameanza kuwa na muamko wa mfumo huu wa vyama vingi vya siasa. Kutokana na hali ya kisiasa ilivyo sasa nchini wagombea hawa wanatakiwa wawe makini, wasome alama za nyakati na wayatambue mabadiliko haya ya kisiasa nchini. Sifa mojawapo ya kiongozi bora anayefaa kupewa dhamana ya kuongoza ni kusema ukweli pamoja na uadilifu.Kuzungumzia sera za vyama pamoja na kuwaeleza wananchi ni jinsi gani watayasimamia mambo yaliyo katika Ilani ya uchaguzi ya vyama vyao.
  Watanzania wanaokwenda kushiriki mikutano ya kampeni na kuwasikiliza wagombea wao wanapaswa kuwa makini na ahadi zinazotolewa majukwaani kuliko kuwa washangiliaji wenye mbwembwe bila kujua kuwa wanachokishangilia ni upuuzi mtupu.

  Binafsi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu sikuwa nimedhamiria kuwa miongoni mwa washiriki wa kusikiliza mikutano ya kampeni kwa sababu kuu moja. Wagombea ambao ndiyo chaguo langu niliopanga kuwapigia kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu tayari ninawafahamu na nilishawaandaa kabla hata ya kampeni hazijaanza kutokana na misimamo yao madhubuti. Hiyo pekee ndiyo ilikuwa sababu kuu ambayo kimsingi ilinifanya nichukuwe uamuzi wa kutoshiriki mikikimikiki ya mikutano yoyote ya kampeni.

  Hata mikutano ya wagombea wanaokihusu chama ninachokiunga mkono ambacho ndicho chaguo langu nayo niliamua nisihudhurie kwani ilani yao ya uchaguzi tayari nilikuwa nayo. Lakini si Ilani hiyo tu, hata Ilani ya vyama vingine pia nilikuwa nazo. Pamoja na hayo yote nimeamua kubadili msimamo wangu na,kuanza kushiriki mikutano yote ya kampeni bila kujali itikadi ya chama.

  Tena ikibidi nitafanya chini juu kuandamana na wagombea pindi wapitapo kijiji hadi kijiji, kata mpaka kata ikiwezekana na utekelezaji wa uamuzi wangu huo tayari umeshaanza. Nimeamua kufanya hivyo baada ya kugundua kuwa asilimia kubwa ya wagombea wetu hawa wanaweza kuwa waongo wa kupindukia huku wakitumia pesa nyingi kufanya kampeni haramu za kuwaahidi wananchi mambo ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza. Siku kadhaa zilizopita nikiwa katika harakati zangu za kutafuta ridhiki kwa bahati mbaya au nzuri pengine, jioni ya siku hiyo nilijikuta nimeibukia mahali palipokuwa pakifanyika mkutano wa kampeni wa mgombea wa ubunge wa chama kimoja. Kwa kuwa ilikuwa ni jioni nami nikaamua niwe miongoni mwa wananchi waliojitolea na kuwa wasikilizaji na washiriki wa mkutano huo. Muda ulipofika mgombea yule akaanza kuhutubia.

  Katika hotuba yake hiyo akatoa kipaumbele cha mambo saba kutoka katika Ilani yao ya uchaguzi ambayo aliahidi kuwa atayasimamia kwa nguvu zake zote.La kwanza lilikuwa ni miundo mbinu,hapa aliahidi kuwa barabara zote katika jimbo lake atahakikisha kuwa zitajazwa vifusi na angalau ziweze kupitika kwa msimu wa mwaka mzima bila kuharibika. Kama hilo halitoshi pia akaahidi kuwa barabara zote zilizo katika makao makuu ya jimbo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
  La pili elimu,hapa aliahidi kuwa atamalizia madarasa yote ambayo hayajamaliziwa kujengwa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya walimu hasa hasa wa masomo ya sayansi katika shule za Sekondari zote za kata.Suala la afya lilikuwa la tatu katika mambo aliyokuwa ameyanukuu katika kijikaratasi chake

  .Hapa aliahidi kuwa atajenga vituo vya afya katika kila kata na kuhakikisha madawa yanaletwa kutoka serikali kuu na kutolewa bure.
  La nne lilikuwa suala la maji,akaahidi kuongezwa kwa mashine moja yenye nguvu ya kusukuma maji ili kuondoa kabisa tatizo la maji jimboni mwake. Jambo la tano akasema kuwa atahakikisha anapambana na ufisadi pamoja na kuutokomeza ili jambo hilo libaki kama historia. Jambo la sita akaahidi atasimamia nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi.
  La saba na la mwisho akaahidi kuhakikisha anafufua kilimo na kuhakikisha mazao yaliyopotea yanarudi tena.Wakati akiyasema hayo wapigakura walikuwa wakimshangilia kwa mbinja,makofi mengi huku akina mama wakipiga vigeregere kwa fujo.Ki msingi ni ukweli kwamba kuyatekeleza mambo yote hayo katika kipindi cha miaka mitano tu ilikuwa ni ndoto za halinacha.

  Baada ya mbwembwe zake hizo, ndipo wananchi wakapewa fulsa na nafasi ya kuuliza maswali. Kwa bahati mbaya kulikuwa hakuna utaratibu wa kuuliza maswali yatokanayo na ahadi za msingi ambazo mgombea aliahidi kutokana na Ilani yake ya uchaguzi. Ndipo nilipogunduwa kuwa dhambi ya uongo ya wagombea hawa huanzia hapa.Swali la kwanza lilikuwa hivi,nanukuu “mheshimiwa pamoja na hotuba yako nzuri yenye ahadi tamu kwetu, lakini kuna hili suala la watoto yatima wanaozagaa hovyo mitaani bila ya kupata msaada wowote.
  Tunaomba utuambie pindi tukikupa kura utalitatuaje ili nao wawe kama wenzao wenye wazazi? Hilo lilikuwa swali jipya ambalo halikuwepo katika ile orodha ya mambo saba ambayo mgombea aliahidi katika hotuba yake kuwa atayashughulikia. Nikashangaa sana mgombea akisimama na kujibu tena kwa mbwembwe nyingi akiahidi kuwa atahakikisha anajenga vituo viwili vya kuwalea watoto hao katika jimbo lake pamoja na kuhakisha wanakwenda shule na kupata elimu sawa na wenzao. Hiyo ikawa ni ahadi nyingine mpya, watu wakapiga makofi na kushangilia. Swali lililofuta lilikuwa jipya pia, muulizaji akauliza kuwa “miaka ya nyuma kulikuwa na kiwanda cha mvinyo cha uma katika jimbo hilo. Lakini kilikufa kutokana na uongozi mbovu wa wakati huo. Kama yeye atapewa madaraka atafanya nini ili kuhakikisha kiwanda hicho kinafufuliwa tena?
  Mgombea tena akasimama kwa mbwembwe zilezile kama mwanzo na kuahidi kuwa hilo ni jambo dogo sana kwake kwani anavyojua yeye ni kuwa, mitambo iliyopo katika kiwanda hicho kwa sasa ni chakavu sana hivyo haifai tena kutumika. Kama atachaguliwa yeye kuwa mbunge wa jimbo hilo.
  Atahakikisha mitambo mipya inanunuliwa, tena mitambo ya kisasa kutoka nchini Italia ili kukifufua upya na kufanya wananchi waendelee kuburudika na mvinyo kama kawaida. Wananchi safari hii wakashangilia kwa nguvu zaidi. Mgombea huyo hakuishia hapo, kwenye mikutano yake mingine pia aliendelea kutoa ahadi za ziada ambazo zilitokana na maswali ya wananchi ambayo hayatokani na ahadi za msingi katika hotuba ya mgombea. Baadaye nikagunduwa kuwa tatizo hilo lipo kwa wagombea wote wa vyama wanaogombea ngazi mbalimbali za uongozi.
  Hizo ni ahadi hewa na mbinu chafu za kuwahadaa wananchi ili wao wapate madaraka kwa manufaa yao ya binafsi na familia zao pia. Lakini baada ya kufanya majumuisho ya fikra na mawazo yangu, baadaye nikagundua tatizo. Tatizo kubwa inawezekana lipo katika uandaaji wa Ilani hizi za vyama.

  Inawezekana kuwa Ilani hizi haziandaliwi mapema kwa kuwashirikisha wananchi ili mambo wanayoyahitaji kutekelezewa yaweze kuingizwa kwenye vijitabu hivyo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua madhubuti za utekelezaji. Huwezi kukurupuka kuahidi jambo ambalo kwa vyovyote vile hukuwa umejiandaa kulitolea uamuzi. Ushauri kwa viongozi wa vyama vya siasa waache kuandaa ilani zao maofisini na badala yake wafanye utafiti kwanza wa nini ambacho wananchi wanataka. Inawezekana pengine katika ilani yako ya uchaguzi umechaguwa kuwa kwa mwaka wa kwanza utawaletea maji wananchi katika jimbo lako. Kumbe wenzio kwa mwaka huo wa kwanza wanahitaji uwaletee pombe tu. Unaweza ukajikuta umekosa kura kwa sababu hukufanya utafiti mapema na kujua shida ambazo zinawakabili wapiga kura katika jimbo lako. Suala la mwisho ni kwenu nyie wagombea, jaribuni kusimamia yale mambo ambayo mmechagua kuyasimamia kutoka katika ilani ya uchaguzi ya chama chako.
  Kama sera zako umeamua kutekeleza mambo saba. Hakikisha unayanadi hayo mambo yako saba katika mikutano yako yote ya kampeni. Epukeni kuulizwa maswali ambayo hayatokani na ahadi zenu za msingi. Huko ni kujibebesha mizigo ya lawama, dhambi na kupoteza imani kutoka kwa wapiga kura wenu pindi uchaguzi mwingine utakapowadia.

  Ni bora uwafurahishe wapiga kura wako kwa kuwaahidi mambo mawili au matatu ambayo utakuwa na asilimia miamoja ya kuyasimamia pindi utakapooingia bungeni kuliko kuahidi mambo mengi na matokeo yake ukaishia kuuchapa usingizi kwenye viti vile vyenye sofa za kupendeza. Nasikia kuna mgombea wa jimbo moja ambalo halina mto wa kudumu achilia mbali hata bwawa alijisahau na kuwaahidi wapiga kula wake kuwa atahakikisha analeta meli jimboni mwake ili kukabiliana na tatizo la usafiri.Hayo na mengine mengi ndiyo vibweka vinavyoendelea katika wakati huu wa kampeni.
  Raia mwenye uchungu, huenda kupiga kura,
  Kuyaepuka majungu, chagua kilicho bora,
  Ulichopewa na Mungu, chagua pasipo hira,
  Huenda kupiga kura, raia mwenye uchungu.

  jumakidogo@yahoo.com
  0764-561078, 0712120740
   
Loading...