TAFAKARI; Kinachoendelea NCCR-Mageuzi

Nicholas J Clinton

JF-Expert Member
Mar 13, 2014
877
486
TAFAKARI; NCCR- Mageuzi NI MOJA!

Kumetokea makelele mengi kipindi hiki kwamba NCCR- Mageuzi kuna pande mbili, Hapana! NCCR- Mageuzi ni moja ila kuchagua mtazamo ni uwezo wa Akili yako kifikra!

Leo nataka tuache ushabiki na tutulize Akili na kujiuliza maswali kabla ya kuanza ushabiki wa kufuata Mkumbo. Jitihada kujipa muda wako kufikiria kabla ya kuongea! Akili kubwa hujadiliana Hoja na sio vijembe.

Kumsimamisha Kiongozi Au Mwanachama ndani ya NCCR- Mageuzi Katiba na Kanuni zinataka Mwanachama aitwe mbele ya Kikao, asomewe tuhuma zake na kupewa fursa ya kujitetea ndani ya siku 14 na kuwasilisha utetezi wake. Makosa ni lazima yawe ya ukiukwaji Katiba na Kanuni.

Kumetokea baadhi wakisema Mwenyekiti Taifa Ndugu James Mbatia amesimamishwa Nafasi yake na hadi kupelekea wengine kusema ‘Aliyekuwa Mkiti’ hao nashauri wakasome kiswahili kupata maana ya Aliyekuwa vinginevyo labda tayari wanamaamuzi mengine! Hili lakini limepita baada ya Barua ya Naibu Msajili wa Vyama vya siasa.

Nimejaribu kusikiliza na kusoma hoja za waliodai kumsimamisha Mkiti Mbatia.
Baadhi ya Hoja zao ni…

- Alimuita Rais Samia Dada badala ya Mama na hivyo kutengeneza mahusiano mabaya na Serikali.
Hii nimetafakari kosa lake sijaliona, labda nisaidiwe ufafanuzi zaidi maana hata Katiba ya Nchi haimuiti Mama! Kwahiyo kumuita Dada, Bibi, Rafiki ni wewe mwenyewe! Sitaki kupoteza muda kuongelea hilo la kuharibu mahusiano na Serikali!

- Mkiti ameuza Mali za Chama na kunufaika binafsi!
Kwenye hili Jiulize kwanza kama UnaiSoma na kuielewa Katiba ya Chama AU Upo nayo tu!!
Chukua Katiba yako na uisome kazi na majukumu ya Mkiti.
Mkiti hana dhamana yoyote ya Mali za Chama kwenye uwekaji saini popote pale iwe Bank Au mikataba, sasa Mkiti ameuzaje Mali za Chama?!!
Jiulize hizo Mali zimepatikanaje!?

Je umehoji kwa Katibu Mkuu na kupata uhakika wa vithibitisho wa Mali hizo?! Maana Katibu Mkuu ndiye Accounting General wa Chama na lazima awe na maelezo yake mkononi kwa ushahidi.

Iwapo shutuma hizo zinatolewa bila Katibu Mkuu kutoa ufafanuzi wa vielelezo, basi kuna shida kwenye hiyo nafasi.

Otherwise wenye dhamana ya mali za Chama ni Baraza la Wadhamini, je Kuna madai hayo yamepelekwa kwenye Baraza la Wadhamini?!! Majibu yao?

Kama haujasikia kote huko, basi tambua ni hoja mfilisi, Rejea kwenye Katiba yako kuangalia Majukumu ya Mwenyekiti Taifa halafu tuliza mhemko!

- Mwenyekiti hakumuhudumia Katibu Mkuu alipokuwa Mgonjwa!
Kwenye hili wala sihitaji kusumbua Akili yangu kuwaza sana!
Ni wapi kwenye majukumu ya Mkiti au Katiba inamtaka Mkiti kumuhudumia Katibu Mkuu akiwa mgonjwa?!?!
Hii hoja hata sijaelewa lengo lake!

- Katibu Mkuu alitekwa na kupelekwa kwenye chumba cha mateso Nyumbani kwa Mkiti Mbatia na kulazimishwa na wanaume watatu kujiuzulu nafasi yake huku wakijua anaumwa lakini walifanya hivyo kwasababu yeye ni Mwanamke!

Hili lina mengi ya kujiuliza;
Kwanza ni suala la kijinai. Hauwezi kutekwa, ukateswa kwenye chumba, ukatoka ukirudi Nyumbani kulala na kuchukulia Poa, unless haujitambui Mwenyewe!

Kwa kauli hii peke yake inashusha hadhi kwasababu ya kupima uwezo wa kujitambua, maana kama una Katibu Mkuu hajitambui Haki zake, vipi aongoze Chama cha siasa kama NCCR- Mageuzi?

Hii ni Police case iliyotakiwa kuripotiwa siku ileile! Vinginevyo kwahiyo kauli, sitashangaa kusikia kuna case ya Defamation atakayofungua Ndugu James Mbatia au Familia yake kwasababu imehusisha Makazi yake.

Kuna hoja nyingine hapo ya Jinsia Mwanamke!
Hili limekuwa likirudiwa rudiwa mara Kwa mara na Katibu Mkuu.
Katiba ya NCCR- Mageuzi hakuna ibara yoyote inayoeleza nafasi ya Katibu Mkuu ni Mwanamke. Tunapochagua Kiongozi yeyote hatuchagui kwasababu ya jinsia yake kwani huo ni ubaguzi, bali tunachagua kutokana na uwezo wako. Hauwezi kufanya makosa ukaachwa kwasababu tu ni Mwanamke, Nop!!

- Mkiti Mbatia amekaa Madarakani muda mrefu!

Jiulize muda huo alikaa Madarakani kibabe bila utaratibu, mfano Uchaguzi?!
Kila miaka mitano kuna Uchaguzi Mkuu ndani ya chama, mbona hamgombei ili mchaguliwe, mnataka kufanya shortcut ya kuingia Madarakani, nini lengo lako?

Kila Uchaguzi Mkuu Ndugu James Mbatia anachukua fomu ya Mwenyekiti wa Taifa na mara nyingi amekuwa akichukua siku za mwisho, mbona hamchukia fomu?!

Kumbe hapa hoja ni ya kutafuta uchochoro wa kihuni kumtoa badala ya kutumia njia ya kidemokrasia, je hili ndilo lengo la NCCR- Mageuzi kutafuta mabadiliko ya kiuongozi kwa Mapinduzi baada ya kushindwa kwenye Chaguzi?

Haya Mapinduzi yakitoka NCCR- Mageuzi mnataka kuyapeleka kumtoa Rais Madarakani kimapinduzi kwasababu amekuwa akitushinda kwenye uchaguzi Mkuu?!? Nini hasa lengo lenu, isije Ikawa mna matatizo personal zaidi ambayo wengine hawajui, mwisho wa siku mtagombana wenyewe kwa wenyewe, tumia Akili!

Sitaki kujichosha sana maana hoja zote sijaona hata moja, labda mniambie wenyewe, Nini hasa kosa la Mwenyekiti James Francis Mbatia katika utendaji wake kukiuka Katiba au Kanuni?!?!


Tuje sasa Upande mwingine tuhoji baadhi makosa ya Viongozi wengine!

Kamati Kuu iliketi Kikao na kuagiza Chama kishiriki Kikao cha TCD pale itakapojiridhisha na Ajenda na malengo hasa ni kuwataka Viongozi wakuu wa TCD yaani Summit kukutana kwanza na Rais na kuongea nae ili watakapokutana kikaoni wawe na ajenda zinazotokana na Kikao hicho. Actually kinachoendelea sasa kati ya Chadema na Serikali ndio ilikuwa hoja ya Kamati kuu ya NCCR- Mageuzi kufanyika kati ya Viongozi TCD na Serikali.

Baada ya Kamati kuu kubaini ajenda na malengo ya Kikao cha TCD na Rais ni yaleyale ya Kikao cha Baraza la Vyama na Rais na uwepo wa kikosi kazi na kukipongeza, Kamati Kuu ikashtukia Kikao kile ni kutumia TCD kuingiza kwa Mlango wa nyuma vyama ambavyo viligoma kushiriki Baraza la vyama, hivyo Kamati Kuu akaketi tena na kutoa Tamko la Chama kutoshiriki Kikao hicho cha TCD na kuwajulisha wahusika wote wakiwamo wajumbe walioteuliwa kuwakilisha chama pamoja na TCD wenyewe.

Baada ya tamko hilo, Mkurugenzi TCD akaanza kuhangaika kumpigia simu Mjumbe mmoja mmoja kwa kuahidi kumtumia usafiri wa kufika Dodoma na posho zao na wengine wakapewa tiketi za Ndege.

Inashangaza hasa ilikuwa nini nia yake, lakini ilikuwa ndio mwanzo wa kutengeneza mgongano wa Wajumbe na Uongozi kwani haiwezekani kauli ya chama inasema hakitashiriki halafu unaahidiwa mambo kama hayo!

Wajumbe wote 12 walioteuliwa walijulishwa kuzingatia Maagizo ya Kamati Kuu na waliahidi kutokuhudhuria!
Kwa mshangao mkubwa Ndugu Haji Ambari Makamu Mkiti Zanzibar, Ndugu Amir Mshindani Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ndugu Susan Masele Mweka Hazina, Ndugu Beati Mpitabakana Mjumbe Hkuu wao waliamua kukiuka Agizo la Kamati Kuu na kushiriki Kikao hicho cha TCD na Rais na kusema wametumwa na Chama. Kwahiyo kati ya 12 ni hao wanne walikiuka Maagizo ya Chama.

Mahudhurio yao yalikuwa ni msumari mbaya Kwa chama kwasababu ilileta sura ya mgogoro ndani ya chama na ndipo maneno yalipoanza kuonyesha chama kimepasuka Juu!

Mahudhurio yao yalipelekea kuiona NCCR- Mageuzi inakubaliana na kikosi kazi na maamuzi yote ya Baraza la Vyama na ndio sababu hata hoja yetu ya Viongozi wa TCD kufanya Mijadala ya Haki na Demokrasia na Serikali ikatutoa na kuachwa kwa Chadema na ndio sababu pia Rais alipokuwa USA alisema vyama vyote vinakubaliana nae kasoro chama kimoja tu, akimaanisha Chadema, ndipo wakamtaka aje kukutana nao.
Leo NCCR- Mageuzi tumewekwa kundi moja na vile Vyama vya kupongeza na kuabudu Serikali kwasababu tu ya hayo mahudhurio ya Viongozi wetu!

Hili la Makamu Mkiti Zanzibar Ndugu Haji Ambari sio mara ya kwanza kukiuka Maagizo ya Chama, kwani baada ya Uchaguzi Mkuu mbali ya Chama kupinga Uchaguzi ule na kutoa Hoja za ukiukwaji na kusema hakitashiriki kwenye uapisho, Ndugu Ambar akiwa Mgombea Mwenza akiwa Pamoja na Mgombea Urais Ndugu Jeremia walihudhuria na baadae Ndugu Ambari kuandika barua ya kuomba radhi.

Kukiuka Maagizo ya Vikao halali ya vyama ni ukiukwaji wa Katiba na Adhabu yake ipo kwenye Kanuni.
Kwakuwa ni wazoefu, walipogundua watahojiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu, nafikiri wakaamua kuipoza kwa kumsakizia Katibu Mkuu ambaye alikuwa anaumwa kuita vyombo vya habari na kuongea shutuma alizoandikiwa dhidi ya Chama na Mkiti ili kubadilisha upepo mjadala wao wa ushiriki TCD upoe na hili la kauli za Katibu Mkuu ndilo lichukue Mjadala Mkuu!

Naweza kusema ni move iliyotumika na wazoefu baada ya kutathmini uwezo wa Katibu Mkuu kuchambua mambo. Kama Katibu Mkuu angekuwa sharp asingeingia huo mtego kwasababu yeye Katibu Mkuu hakuwa kwenye mjadala wowote!
Wakafanikiwa kwenye hilo!

Sekretarieti iliketi na kuandaa ajenda za Kamati Kuu.
Kamati Kuu iliketi tarehe 15/05/2022 ikiwa na wajumbe wote na moja ya ajenda ilikuwa Hali ya kisiasa ndani ya chama.

Kwenye hiyo ajenda, iliibuka hoja ya Katibu Mkuu kuongea na vyombo vya habari kushutumu Chama na Mkiti huku akijua kufanya hivyo ni ukiukwaji wa Katiba na adhabu yake ipo kwenye Kanuni.

Sekretarieti nayo ilikuja na madai yao kuonyesha kutokuwa na imani na Katibu Mkuu ambapo waliorodhesha tuhuma mbalimbali za kikatiba.

Kikao kilimpa Katibu Mkuu nafasi ya kujitetea na aliomba apewe siku 3 ya kuwasilisha utetezi wake.
Kwakuwa Katiba inamtaka apewe siku 14, Kamati Kuu ikampa siku 14 kulingana na Katiba na ikamsimamisha muda huo kumpa nafasi ya kuwasilisha majibu na hiyo ni kwa mujibu wa Katiba.

Kamati Kuu kwa pamoja ikapendekeza tarehe ya Halmashauri kuu ijayo ifanyike tarehe 13/08/2022.
Kikao kikamalizika kwa wajumbe wote kuwa pamoja na kuondoka vyema ya kikao yaishie kwenye kikao na ndio sababu haikuvuja Kwa maslahi ya chama na kulindiana heshima.
Kumbe wengine humo walikuwa na ajenda zao zingine!

Wajumbe wote wa Halmashauri Kuu waliwasiliana na Makao Makuu kuwajulisha kuahirishwa Kikao hadi 13/08/2022.

Tarehe 20/05/2022 Msajili wa Vyama vya siasa akakabidhiwa muhtasari wa Kikao cha Kamati Kuu na maamuzi yake, hii lilifanyika Kwa mujibu wa sheria.

Aliyepokea barua hiyo ya Msajili ni Ndugu Sisty Nyahoza ambaye ni Karani Ofisi ya Msajili. Kumbe anapokea , mfukoni ana lengo lake!

Kesho yake tarehe 21/05/2022 Asubuhi tunamuona huyo Ndugu Sisty Nyahoza akihudhuria Kikao cha Halmashauri Kuu NCCR- Mageuzi iliyketi takribani dakika 40 na kutoa maazimio ya kumsimamisha Mkiti, Makamu Mkiti Bara na kuvunja Baraza la Wadhamini na Sekretarieti ya Chama na kusoma majina ya Baraza jipya palepale ndani ya muda huo!

Kuna Sinema zingine zikifanyika ukiamua kuwa mshiriki basi Angalia maudhui na Kiongozi wa hiyo Sinema vinginevyo utaishia kucheza Sinema zenye kipato cha andazi la leo wakati wenzako wanapiga pilau!

Mjumbe wa Hkuu unatakiwa uwe na uwezo wa kuhoji aina ya Kikao na malengo yake ili usiingie kukigawa Chama ambapo hautapata manufaa yoyote, labda kama binafsi hauna Mapenzi ya dhati na Chama.
Unajua Hkuu imeahirishwa, umehudhuria kwasababu ipi?

Umezoea ukiitwa kwenye kikao unaanzia Ofisini, mbona leo tofauti unakwenda moja Kwa moja kurasini kikaoni?
Umezoea malipo yako yanavyofanyika lakini leo utaratibu umebadilika, bado haujaohoji tu!

Unaelewa Vikao vya chama HKuu Mkiti wa Kikao ni Mkiti Taifa, haumuoni na Viongozi wengine hawaonekani, mbona hata kuhoji hakuna?

Unaelewa tuhuma zozote zinasomwa mbele ya mtuhumiwa na kupewa fursa ya kuwasilisha majibu, vipi tuhuma zinasemwa tena kutoka mdomoni sio kwenye maandishi pasipo watuhumiwa kuwapo kikaoni na uamuzi unasomwa hapohapo bila wajumbe kupiga kura mmoja mmoja kwa kuitwa jina?!

Hapo wajumbe halali mlioshiriki hicho Kikao mnaona kabisa mlifanya haki?! Usijibu kiushabiki bali kiuhalisia machoni mwa Mungu wako!

Katiba inasema Mkiti asipokuwapo, Makamu Bara anakaimu nafasi.
Ikatumika akili nyingine ya kiuzoefu, akasimamishwa Makamu Bara ili Makamu Zanzibar ashike nafasi na ndio lengo lake hasa!

Nikuulize Mjumbe wa Hkuu uliyeshiriki kumsimamisha Makamu Bara, kosa lake kikatiba ni lipi?!
Hapo utagundua ulitumika bila kujitambua kutimiza lengo watu.

Wamevunja Baraza la Wadhamini, sababu ni ipi ya kulivunja Baraza?! Je wamekiuka wapi majukumu yao?!
Halafu Baraza jipya linasomwa wajumbe tu pasipo kupigiwa kura wala kuelezwa mapendekezo hayo yametoka wapi?!?

Kama mnataka Chama kiendeshwe hivi, basi sio NCCR- Mageuzi, tafuteni Chama cha aina hiyo!

Kwa tathmini ya haraka haraka ni Akili ya uzoefu waliyoitumia Ndugu Ambari kuleta mtifuano kwenye chama ili apate fursa nje ya Vikao vya chama kuongelea Maridhiano ili makosa yake yaishie juu juu na sio ndani ya Vikao kwasababu kulingana na Katiba na Kanuni za Chama zipo wazi kabisa anaelewa kwenye Vikao itakuwaje na hataki ifikie hatua hiyo, ndio sababu akamtumia Katibu Mkuu kuvuruga Kamati Kuu, na akatumia baadhi ya wajumbe Hkuu pamoja na wakupachikwa kutibua tena Hkuu halali 13/08/2022 ili suala lao la wakosaji wanne lipanuke zaidi liwe la wengi bila hao wengine kufahamu!
Wao wanadhani wapo kwenye vita ya pamoja kumpindua Mbatia Kumbe mwenzao anawatumia kumlinda yeye asijadiliwe kwenye Vikao!

Chama cha siasa makini kinatakiwa kiwe na Viongozi makini wenye kuheshimu Katiba na Kanuni za Chama, NCCR- Mageuzi inaendeshwa kwa Katiba na Kanuni zake.

Ukifanya makosa usitafute uchochoro, tumia njia sahihi ya kusahihisha makosa yako na sio kuvuruga Chama.

Andiko ni Refu lakini ni kwa nia njema ya kukutaka utafakari kabla haujaanza kufikiria pande za Chama wakati kipo kimoja tu nacho ni NCCR- Mageuzi chini ya Mkiti wake Ndugu James Francis Mbatia, full stop

Pamoja Tutashinda!

Sam Ruhuza
Mdhamini NCCR- Mageuzi


IMG-20220614-WA0159.jpg
 
Naona NCCR Mageuzi inaelekea kushinda vita, msajili ajitafakari sana na matendo yake ya kuvuruga vyama vya siasa.
 
Back
Top Bottom