TACAIDS na Mpango wa Kujinasua

dazenp

Senior Member
Mar 11, 2009
101
12
TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) inaiomba Serikali ipandishe kodi ya vinywaji vikali ikiwa ni pamoja na mvinyo na bia, na pia kodi katika vocha za simu ili Tume hiyo ipate fedha za kuanzisha Mfuko wa Ukimwi Tanzania.

Maombi hayo yanakuja baada ya yale ya awali kwa makatibu wakuu kukataliwa, Tume hiyo ilipoomba asilimia tano ya makusanyo ya ndani, lakini ikaambiwa itafute chanzo kingine cha fedha.

Baada ya kufikiria sana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Tacaids, Beng’i Issa, anasema Tume imeamua iwakamue wananchi kupitia vinywaji hivyo na vocha za simu, ili ipate Sh bilioni 100 kwa ajili ya Mfuko huo.

Hapo ndipo mahali pekee ambako Tume inaamini itapata ahueni baada ya wafadhili kujitoa kuwafadhili asilimia 97 ya bajeti yake na kubaki na Global Fund pekee ambayo inafadhili
asilimia 91, lakini ikitarajia nayo kufunga virago mwakani na Tacaids kubaki yatima.

Ni kweli, kwamba Tacaids imefanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya Ukimwi, kuanzia maambukizi yake na jinsi ya kujikinga nayo, lakini pia kushiriki masuala ya utoaji ushauri nasaha na upimaji kwa hiari.

Naipongeza Tacaids kwa kuwafumbua wananchi macho, ingawa maambukizi bado yanaendelea lakini si kwa kasi kubwa kama ilivyokuwa awali. Bila shaka kama itaendelea
kuwezeshwa itapiga hatua kubwa zaidi na pengine maambukizi kukoma.

Lakini najiuliza hivi ni busara kuendelea kuwakamua wananchi kwa ajili ya kuanzisha Mfuko wa
Ukimwi nchini?

Ina maana ushauri nasaha unaotakiwa kutolewa hivi sasa unahitaji kiasi hicho cha fedha? Na kama zinahitajika, ni busara kuwabana wananchi watoe kwa lazima kupitia vinywaji na huduma ya simu za mkononi, ambayo ni muhimu kwa mawasiliano ingawa gharama zake bado ni kubwa?

Haya ni mambo ambayo Tacaids walipaswa kujiuliza kabla hawajawasilisha maombi yao kwa Kamati Maalumu Hazina ambayo itayapitia kabla ya kuyawasilisha katika kikao cha makatibu wakuu kabla ya kupelekwa Baraza la Mawaziri kupata baraka kama itawezekana.

Labda swali la kujiuliza ni kama kuna ulazima kwa wananchi wakamuliwe; na kama itakuwa hivyo, basi itaonesha jinsi wananchi wanavyoonewa hasa wakati huu ambao maisha yanaendelea kuwa magumu, kila kitu kinapanda bei na hivyo kuingiza na hili ni sawa na kuwatwisha mzigo mzito wananchi.

Kama kweli Baraza la Mawaziri litakubaliana na maombi haya ya kuwakamua wananchi, litachangia hasira kwa wananchi ambao wataamini kwamba pengine Serikali yao haijali matatizo wanayoyapata mpaka kuwatwisha mzigo mwingine.

Hakuna asiyeelewa mchango na umuhimu wa Tacaids katika kupambana na Ukimwi tangu uingie nchini katika miaka ya themanini na hakuna asiyejua jinsi Ukimwi ulivyotesa watu wengi wa Tanzania ambao kwa namna moja au nyingine, wameguswa na athari mbaya za ugonjwa huo.

Ndiyo sababu Tume hiyo inatakiwa kweli iendelee kusaidiwa ili itimize malengo yake iliyojiwekea, lakini inapaswa kufanya tathmini na kuona mahitaji yake ya msingi ni yapi
hata kuhitaji kiasi hicho cha fedha.

Inapaswa kuona ilikotoka, ilipo na inakokwenda na kujua umbali wa safari iliyobaki na kulinganisha na kiasi cha fedha inachotaka ipewe, kabla ya kuanza kuingia mifukoni mwa
wananchi kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kuwasababishia ugumu wa maisha.

Lakini si siri pia, kwamba Watanzania wengi wameshapata uelewa wa jinsi maambukizi ya
Ukimwi yanavyotokea na jinsi ya kujizuia nayo na hata jinsi ya kuishi na mtu mwenye Ukimwi.

Yote hayo ni mafanikio ya taasisi mbalimbali za kutoa elimu kwa wanachi na Tacaids ikiwa ni moja wa wadau hao. Kwa kuzingatia hili, bila shaka hata Baraza la Mawaziri litakapokuwa na hoja hiyo mezani, basi liangalie nafasi ya Tacaids katika muktadha uliopo wa mapambano
dhidi ya Ukimwi.

Suala hapa lisiwe ili mradi kuwa na Tume, bali kuangalia kama ipo haja kweli ya kuwa na Tume kwa wakati huu, au chombo kingine kidogo tu cha kufuatilia elimu iliyotolewa na utekelezaji wake, badala ya kutaka kuchangisha fedha kwa wananchi ambao hakuna asiyejua ugumu wa
maisha unaowakabili.

Kwa mazingira ya sasa nchini na hali ya uchumi ilivyo kwa mtu mmoja mmoja na hasa kuzingatia umasikini unaowakabili Watanzania ambao wanaamini simu za mkononi ni njia
ya kurahisisha mawasiliano baina yao na hata kutumia kupata fursa za ujasiriamali, wazo la kuwapandishia gharama ni kuwakosea haki.

Lakini pia tuepuke kudhani kuwa tukitaka kupandisha bei au gharama lazima tupitie kwenye vinywaji, tuelewe pia kuwa miongoni mwa Watanzania hao wamo wanaokunywa vinywaji hivyo kama sehemu yao ya burudani, baada ya kazi ngumu ya mchana kutwa ya kujitafutia riziki.

Hiyo pia ni sehemu ya mchango wao kupitia kinywaji kwenye kuongeza pato la Taifa, hivyo
watakapopandishiwa bei ya kinywaji chao, ina maana watakuwa sawa na kufukuzwa na hivyo kuacha kunywa na kupunguza pato la Taifa; yote haya yazingatiwe katika uamuzi
utakaotolewa katika kujaribu kuisaidia Tacaids.
 
Back
Top Bottom