Taarifa kwa umma

Kidbwenga

Member
Nov 11, 2016
20
18
December 27, 2016

Mnamo tarehe 26 na 27 Desemba, 2016 baadhi ya mitandao ya kijamii imeandika taarifa zenye nia ya kupotosha Umma ambazo Sekretarieti ya Ajira inapenda kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo;-

1. Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa ufafanuzi kufuatia hoja iliyoandikwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii ya tarehe 27 Desemba, 2016 zenye vichwa vya habari vinavyosomeka “Waliofaulu usaili ajira serikalini kufutwa” na “Taarifa kwa waliokuwa wakisubiri kupangiwa vituo vya kazi kabla ya ajira kusitishwa serikalini” zikidaiwa kutolewa na Taasisi hii katika majibu ya hoja za mwezi Novemba, 2016 katika utaratibu wake wa kujibu hoja za kila mwezi kama ifuatavyo;-

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Sekretarieti ya Ajira tangu mwezi Juni, 2016 Serikali ilipositisha Ajira hapakuwa na orodha ya waombaji kazi waliokuwa wakisubiri matokeo ya usaili, kwa kuwa usaili wa mwisho ulioendeshwa na Sekretarieti ya Ajira ulifanyika mwezi Mei, 2016 na waombaji waliofaulu walipangiwa vituo vya kazi kwa idaidi ya nafasi zilizokuwepo.

Aidha, kwa wale ambao walifaulu na hawakuweza kupangiwa vituo vya kazi kutokana na kukosekana kwa nafasi zilizokuwepo walihifadhiwa katika kanzidata (Database) ambayo hudumu kwa muda cha miezi sita (6) baada ya matokeo ya usaili husika kutolewa.

Baada ya ufafanuzi huo hususani aya ya tatu Sekretarieti ya Ajira ingependa kufafanua zaidi namna kanzidata ya waliofaulu usaili inavyotumika ili kuweza kuwa na uelewa wa pamoja kwa wadau na jamii kwa ujumla ili kuepusha kupokea ama kusikia taarifa zisizo rasmi zenye nia ya kupotosha Umma zinazojitokeza mara kwa mara hususani katika baadhi ya mitandao ya kijamii.

Kanzidata ya waliofaulu usaili:

Kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa shughuli za Sekretarieti ya Ajira za mwaka 2016, Kanuni ya 21. (1) - (5) imefafanua juu ya kanzidata kama ifuatavyo;-

(1) Baada ya waombaji waliofaulu usaili kuwapangia vituo vya kazi, orodha itakayobaki itatunzwa na Katibu katika kanzidata ili pale itakapotokea fursa ya ajira orodha hiyo iweze kutumika.

(2) Orodha ya waombaji walioko kwenye kanzidata itatumika kujaza nafasi wazi kulingana na mahitaji ya Waajiri. Hata hivyo, wakati wa upangaji, Katibu atazingatia mpangilio wa matokeo ya alama za ufaulu wa mwombaji kwa aliyepata alama za juu zaidi ya wengine kufikiriwa kwanza.

(3) Sekretarieti itatangaza nafasi wazi za ajira na kufanya usaili endapo orodha iliyotunzwa katika kanzidata itakuwa imekwisha au haina mtumishi mwenye utaalam au sifa zinazohitajika na Mwajiri.

(4) Endapo katika orodha iliyotajwa kwenye Ibara ya 21(2) kutakuwa na waombaji waliopata alama zinazolingana, utaratibu ulioainishwa katika Ibara ya 14(1) utazingatiwa.

(5) Orodha ya kanzidata itadumu kwa kipindi cha miezi sita (6) tangu kuidhinishwa kwa matokeo na Wajumbe wa Sekretarieti.

2. Sekretarieti ya Ajira pia inapenda kutoa ufafanuzi kwa taarifa nyingine iliyoandikwa katika mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari kinachosema “Mhe Rais Magufuli nakuomba Sekretarieti ya Ajira uifute maana haina majukumu sasa hivi lengo la Sekretarieti ya Ajira ni kutangaza kazi na ........”. kama ifuatavyo;-

Ni vyema wadau wa Sekretarieti ya Ajira na Jamii kwa ujumla ikafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (1). Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (6) (a-f) na Sera ya Menejimenti ya Ajira toleo Na. 2 la mwaka 2008 Sekretarieti ya Ajira ina majukumu yafuatayo;-

i. Kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa (kanzidata) za wataalam hao ili kurahisisha utaratibu wa kuwaajiri pindi wanapohitajika,

ii. Kuandaa orodha ya wahitimu wa Vyuo Vikuu na Wataalam Weledi (Professionals) kwa madhumuni ya kurahisisha rejea na ujazaji wa nafasi wazi za ajira katika Utumishi wa Umma,

iii. Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazotokea katika Utumishi wa Umma.

iv. Kuhusisha wataalam maalum (Appropriate experts) kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji,

v. Kutoa ushauri kwa Waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na ajira,

vi. Kufanya kazi nyingine yoyote inayoendana na majukumu yake kadri itakavyoelekezwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma.

Kutokana na ufafanuzi huo Sekretarieti ya Ajira ingependa jamii ifahamu mbali na jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira ina majukumu mengine inayoyatekeza kama yalivyoainishwa hapo juu kwa mujibu wa Sheria.



Riziki V. Abraham

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Sekretarieti ya Ajira.

27 Desemba, 2016.
 
Back
Top Bottom