Sumaye ashangaa utaratibu wa Serikali kutumia michango ya rambirambi

ras mkweli

JF-Expert Member
Mar 12, 2012
280
104
Kwa ufupi
  • Sumaye, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza kushika nafasi hiyo kwa miaka kumi mfululizo, alisema hayo akitoa mfano kwa wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera pamoja na ajali iliyoua watu 35 wa Shule ya Lucky Vicent ya jijini Arusha Mei 6.
  • Fedha za misaada ya wahanga wa tetemeko la ardhi, takriban Sh7.5 bilioni zilitumiwa kukarabati miundombinu iliyoharibika, wakati za ajali ya basi la Lucky Vicent zimetumika kwa shughuli mbalimbali za kuaga maiti na mazishi na hivyo kuibua lawama kuwa baadhi ya matumizi hayakutakiwa kugharimiwa na fedha hizo.

Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ameitaka Serikali kuacha kutumia michango inayotolewa kwa wahanga wa majanga, kwa matumizi yake.

Sumaye, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza kushika nafasi hiyo kwa miaka kumi mfululizo, alisema hayo akitoa mfano kwa wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera pamoja na ajali iliyoua watu 35 wa Shule ya Lucky Vicent ya jijini Arusha Mei 6.

Fedha za misaada ya wahanga wa tetemeko la ardhi, takriban Sh7.5 bilioni zilitumiwa kukarabati miundombinu iliyoharibika, wakati za ajali ya basi la Lucky Vicent zimetumika kwa shughuli mbalimbali za kuaga maiti na mazishi na hivyo kuibua lawama kuwa baadhi ya matumizi hayakutakiwa kugharimiwa na fedha hizo.

Ajali ya Lucky Vicent iliua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja. wanafunzi watatu walionusurika, wamesafirishwa kwa msaada kwenda Marekani kwa matibabu zaidi, wakiwa pamoja na daktari, muuguzi na mzazi mmoja kila mwanafunzi.

“Tujuavyo, huwa tunachangia kuwasaidia waliopatwa na tatizo. Huu utaratibu mpya wa kuichangia Serikali kupitia misiba au majanga umeanza lini na ni chombo gani kimeupitisha?” alihoji Sumaye.

Kutokana na matukio hayo mawili na kilichofanywa na Serikali, Sumaye alisema utaratibu huo si sahihi kwa sababu unawadhulumu wale waliotakiwa kusaidiwa na kuwavunja moyo wachangiaji.

“Ni aibu kubwa sana kwa Serikali kufanya hivyo. Serikali iache kutumia mabavu kuchukua michango ya watu na kuitumia kinyume na watoaji walivyodhamiria,” alisema.

Licha ya mabadiliko ya matumizi yaliyofanywa katika rambirambi, mkuu wa mkoa wa Arusha aliagiza kukamatwa kwa watu waliojitokeza kwenda kutoa pole zao katika shule hiyo na kuzuia Sh18 milioni walizotaka kuikabidhi Lucky Vicent.

“Watanzania wapenda amani na wapenda haki lazima tulaani kwa nguvu zetu zote kitendo hicho cha uonevu, ukatili na uvunjifu wa haki za binadamu,” alisema Sumaye.

“Mtindo wa kutesa watu wasio na hatia kwa sababu za kisiasa ni chachu ya machafuko katika nchi na amani hii tuliyonayo ikitoweka, hakuna atakayepona.”

Hoja kama hiyo ilitolewa na mtafiti wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Profesa Haji Semboje aliyehoji sababu zilizoifanya Serikali isimamie rambirambi hizo wakati inaweza kuanzisha kwa utaratibu unaoweza kusimamiwa na wahusika wenyewe.

“Kama Serikali imeshindwa kukusanya kodi iliyopo kwenye mfumo, itawezaje kukusanya fedha hizo? kimbelembele cha Serikali ni kipi? Hata wahusika wangechangisha wenyewe, wangezipata,”alisema.

“Unaweza kujiuliza ni sababu gani zilizosababisha wakatumia rambirambi kwa matumizi mengine halafu hizi wasizichukue kwa matumizi mengine?

“Ukitoa rambirambi ya msiba eneo la nyumbani fedha hizo zitabakia kwa wafiwa nyumbani, lakini ukizitoa eneo la kanisani zinaweza kubakia kanisani. Lazima kuwepo mfumo wa ufuatiliaji ulio uwazi. Misiba mingine hakuna uwazi, wafiwa wanaweza wasipewe kabisa rambirambi,” alisema.

Profesa Semboja alisema ni muhimu kutambua mfumo wa ukusanyaji wa rambirambi yanapotokea maafa na pia madhumuni ya michango yanatakiwa yawekwe wazi ili kuepusha mizozo.

Sakata la rambirambi latinga bungeni

Suala la rambirambi zilizotolewa na wabunge kwa ajili ya wafiwa wa ajali ya wanafunzi wa Lucky Vicent pia lilijitokeza bungeni jana baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara aliomba mwongozo kuhusu fedha za rambirambi kutumiwa kwa makusudi yasiyokusudiwa, akiegemea kanuni ya 68(1) ya kanuni za kudumu za Bunge.

“Kwanza madaktari wamelipwa posho na nyingine zimeenda kwa wale watoto. Inaonekana zinaenda kujenga hospitali badala ya kwenda kwa waathirika waliokusudiwa,” alisema.

“Hizi fedha kwa kweli Bunge linahusika maana tulikatwa posho kwa maana ya kutoa rambirambi kwa wahusika. Lakini imekuwa ni tabia inayojirudia mara kwa mara ya kutumika isivyo,” alisema mbunge huyo.

“Fedha inachangwa kwa ajili ya rambirambi lakini Serikali inaipangia matumizi mengine, kitu ambacho kinatukwaza sana, hasa mimi mwenyewe.

“Tutakuwa tunachangishana fedha hapa, halafu wanaenda kufanya matumizi yake na kulipana posho.

“Naomba mwongozo wako. Hivi ni sahihi fedha inachangwa kwa ajili ya rambirambi, halafu inabadilishwa juu kwa juu bila kupelekewa wahusika?”

Akijibu muongozo huo, mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema hawezi kulitolea muongozo jambo hilo kwa vile halikutokea bungeni na kwamba mbunge huyo amesoma katika magazeti.

“Sisi hatuendeshwi humu bungeni kwa magazeti. Kwa heshima zote Mheshimiwa Waitara, kwa mila zetu, ukishatoa mchango wako wa rambirambi, unaiachia familia ile au chombo kile. Hayo yanakwisha,” alisema Chenge.

“Mimi kwa maoni yangu tusiendeleze hayo, lakini Serikali ipo, Bunge hili lipo, uongozi wa Bunge upo na unategemea mrejesho kwa michango ya Bunge.

“Mrejesho ni muhimu ili siku za usoni mtakapokuja kuombwa kufanya hivyo muwe na hiyari wa mwitikio. Lakini kuanza kuleta tuhuma kuwa hazijaenda huko, mimi nasema kidogo ni tatizo,”

Polisi yawaita wenye milioni 18 kuzifuata

Wakati hayo yakiendelea, polisi mkoa wa Arusha imewataka viongozi wa Tamongsco kwenda kuchukua Sh18 milioni zilizokuwa zinashikiliwa baada ya polisi kuzichukua kutoka kwa watu walioenda kuzitoa Lucky Vicent kama rambirambi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema mtu yeyote anapokamatwa na polisi akiwa na fedha uchunguzi ukibaini kosa analoshitakiwa nalo linahusiana na fedha zitatumika kama kielelezo, lakini kama hazihusiani ni haki yake.

Hata hivyo Kamanda Mkumbo alipotakiwa kueleza ni lini waliokamatwa watafikishwa mahakamani alisema hana taarifa za kutosha kwa kuwa alikuwa likizo lakini hakuna mtu anayeshtakiwa kwa kwenda kutoa rambirambi.

Katika tukio hilo la Mei 18, polisi waliingia shule ya Lucky Vicent na kuwaweka chini ya ulinzi waliokuwepo kwenye chumba kimoja ambao ni wazazi waliofiwa, waandishi wa habari, viongozi wa Tamongsco, Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro madiwani wawili na Mkuu wa Shule ya Lucky Vicent kwa kosa lililodaiwa kufanya kikao kisicho cha kibali cha polisi.

Jana, Lazaro aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kupata dhamana juzi, jana aliripoti polisi lakini ametakiwa kurejea tena Ijumaa.

Lazaro alisema hajui hatima ya shauri hilo, kwa kuwa jana alielezwa kuwa anatakiwa kurudi polisi Ijumaa.

Hata hivyo, Lazaro alieleza kupinga fedha za rambirambi kiasi cha Sh44.7 milioni kutumika kulipa posho za muuguzi, daktari na fedha za kujikimu ndugu wa majeruhi nchini Marekani.

Lazaro alisema watumishi wa umma, wana utaratibu wao wa malipo, hivyo ni jambo la aibu Serikali kushindwa kuwalipa watumishi wake posho za kuishi Marekani na badala yake kutumia fedha za rambirambi.

Alisema awali, mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu alisema watoto, ndugu na wauguzi watakuwa Marekani kwa ufadhili wa shirika la Siouxland Tanzania Education Medical Ministries (Stemm) na Samaritan’s Purse, inakuwaje wapelekewe fedha za rambirambi.

Sumaye azungumzia uteuzi

Katika mahojiano na Mwananchi, Sumaye pia alizungumzia uteuzi wa viongozi wa nafasi mbalimbali unaofanywa na Rais John Magufuli.

Sumaye alisema ni vizuri anafanya bila kubagua umri, lakini akatoa tahadhari kuhusu uhuru wa wateule hao.

“Kimsingi hakuna kosa kumpa kijana nafasi nyeti kama ana uwezo wa kuimudu. Tatizo linatokea pale mtu huyo anapokosa uwezo kwa sababu yoyote; iwe elimu, ujuzi au nyingineyo. Hata anapopewa maelekezo ya ziada yasiyoendana na mamlaka ya nafasi anayopewa,” alifafanua.

Alitoa mfano wa mkuu wa wilaya au mkoa anapokandamiza vyama vya siasa kufanya kazi zao za kikatiba, lazima atakuwa ndiye wa kwanza kuhatarisha amani anayotakiwa kuilinda.

Alisema hilo linaweza kusababisha kuvunja haki, kuonea hata kusababisha mateso kwa raia wasio na hatia kwa kutekeleza maagizo ya ziada nje ya madaraka aliyopewa.

Sumaye aliikumbusha CCM kwamba katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi hakuna chama kitakachotawala milele, hata kama kikifanya vizuri.

“Ni wajibu wa sisi sote kujenga upinzani wenye nguvu ili wananchi wasiwe na wasiwasi na uwezo wake wa kuongoza nchi,” alisema.


CHANZO:
Mwananchi
 
Nchi inaendeshwa kibabe...aibu sana kwa kweli.Titakuwa hatuchangii hadharani,unamtaimu mwathirika nyuma ya pazia unampa chake,ila ukigundulika selo inakuhusu.
 
Angekuwa ndani ya mfumo asingeshangaa. Hongera kwa kujitambua mzee wetu, but ajue serikali hawana kitu ndio maana wanakula michango
 
Sumaye hana moral authority ya kuongelea mambo kama hayo.
Mtu aliekwapua ardhi ya wananchi na kujimilikisha kote Tanzania,leo anatoka kuongelea michango?
 
Back
Top Bottom