Kutoka Tanzania Daima
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM (UWT) ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sofia Simba, amemsimamisha kazi Katibu wa jumuiya hiyo, Hasna Mwilima katika mazingira ya kutatanisha kwa madai kuwa ni maagizo kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete.
Waziri Simba ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa na mahusiano mabaya na katibu wake huyo, alifikia uamuzi huo mwishoni mwa wiki katika kikao cha Kamati ya Utekelezeaji ya UWT taifa, iliyokutana kwa dharura jijini Dar es Salaam.
Katika hali isiyo ya kawaida, baada ya kikao hicho kupitisha uamuzi wa kumsimamisha, wajumbe wanne walitumwa nyumbani kwa Hasna kupeleka barua wakati akiwa kitandani akijiuguza kutokana na homa iliyokuwa ikimsumbua.
Mbali ya Waziri Simba, wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho na kuridhia uamuzi huo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa UWT, Asha Bakari.
Wengine ni Shamsa Mwangunga, Hawa Ghasia, Zainabu Mwamwindi, Furahia Abdallah, Fatuma Tawafiq, Lucy Mayenga, Lediana Mngongo, Subira Mohamed na Zainabu Shomari.
Habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa kikao hicho zilisema wakati wa kikao hicho, Hasna hakuhudhuria kwani alikuwa mgonjwa.
Kweli kikao kilifanyika na kuamua kumfukuza kazi Hasna na mwenyekiti alisema lilikuwa ni agizo kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM taifa, alisema mmoja wa wajumbe hao.
Kwa mujibu wa habari hizo, barua ya kusimamishwa kazi kwa Hasna ilipelekwa nyumbani kwake na wajumbe wanne ambao ni Asha Bakari, Zainabu Mwamwindi, Furahia Abdallah na Subira Mohammed.
Hata hivyo walipofika pale, Hasna alikataa kuisaini kwa madai kuwa kikao kilichokaa hakina mamlaka kisheria kumsimamisha kazi, kilisema chanzo chetu cha habari.
Habari zaidi zinasema kuwa mbali ya kumsimamisha kazi, kikao hicho pia kiliamua kumnyanganya gari.
Hata hivyo, Sofia Simba jana hakuwa tayari kupokea simu kila alipopigiwa na gazeti hili, badala yake simu hiyo kwa zaidi ya mara sita ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni dereva wake na kudai kwamba yuko mbali na waziri huyo.
Mzozo kati ya Waziri Simba na katibu wake uliongezeka wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la UWT ambapo aliwaambia wajumbe hao hamtaki katibu huyo ambaye hajafikisha hata mwaka mmoja tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo akitokea wilayani Hai, alikokuwa mkuu wa wilaya. Hali hiyo ilisababisha Hasna apate shinikizo la damu na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, huku wajumbe wakigawanyika.