Sitta ajitwika zigo la CCM
Send to a friend Thursday, 16 September 2010 07:41 0diggsdigg
Samweli Sitta
Waandishi Wetu
MAKOMBORA ya Dk Willibrod Slaa dhidi ya spika anayemaliza muda wake, Samuel Sitta, yamezidi kuongeza joto la kampeni za uchaguzi baada ya kada huyo wa CCM kutangaza kuwa anataka mdahalo wa wazi na mgombea urais huyo wa Chadema ili kuondoa kile alichokiita siasa za ulaghai na upotoshaji.Vyama vya Chadema na CUF vimekuwa vikitaka mdahalo wa pamoja na mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete lakini chama hicho tawala kimesema kuwa mgombea wake hana haja ya kitu kama hicho na kikaenda mbali zaidi kwa kutoa waraka wa kupiga marufuku wagombea wake wa ubunge na udiwani kushiriki kwenye midahalo hadi kwa maelekezo maalum.
Lakini jana, Sitta aliiambia Mwananchi kuwa yuko tayari kushiriki mdahalo na Dk Slaa baada ya katibu huyo mkuu wa Chadema kumshambulia kuwa ni mnafiki kutokana na kupinga sera ya chama hicho cha upinzani ya kutoa elimu bure kwa wote.
Dk Slaa alimshambulia Sitta juzi akiwa mkoani Mara ambako alisema katika uongozi wake wa uspika alizima kashfa nzito za ufisadi, likiwemo sakata lililotikisa nchi la zabuni ya ufuaji wa umememwa dharu iliyokwenda mikononi mwa kampni ya Richmond Development LLC, wizi wa fedha kwenye akaunti ya EPA, ufisadi wa kampuni za Deep Green Finance na Meremeta.
Dk Slaa, ambaye alipata umaarufu kutokana na kuibua kashfa mbalimbali, alimuelezea mbunge huyo wa Urambo Mashariki kuwa alimzima wakati alipokuwa akipinga mishahara mikubwa ya wabunge na kumwita kuwa ni mnafiki.
Jana, akizungumza na Mwananchi kutoka jimboni kwake, Sitta alisema: "Kwanza namuonea huruma sana Dk Slaa; siasa zake za ghilba zinaonyesha ni mtu aliyekata tamaa kwamba atashindwa na hafai kuwa rais. Anafanya siasa za ulaghai.
"Yeye ndiyo mnafiki mkubwa na mlaghai. Anasema mbunge anapata mshahara Sh7 milioni, lakini katika miaka 15 ya ubunge hajawahi kusamehe mshahara hata mwezi mmoja. Kusema bila vitendo ni unafiki, hilo analosema lingekuwa dhamira ya kusaidia umma, basi angekataa kuchukua mishahara miezi yote."
Kwa mujibu wa Sitta, ambaye alisifika kwa kuruhusu mijadala mizito dhidi ya serikali, kauli anazotoa Dk Slaa kuomba kura kwa wananchi zinamkera kwa sababu zimejaa upotoshaji na ulaghai na kuongeza kusema: "Natamani ningefanya mdahalo naye leo hii."
"Ningekuwa Dar ningeomba kufanya mdahalo na Dk Slaa ili aeleze hayo anayosema nami nifafanue. Bahati mbaya nipo kilomita takriban 1,000 kutoka Dar. Lakini, ili kuondoa ulaghai wake kwa wananchi nataka mdahalo na Dk Slaa; mimi ndiyo saizi yake si Kikwete. Kikwete amwache apige kampeni tu," alitamba Sitta.
Kuhusu hoja ya mishahara mikubw aya wabunge, Sitta alidai Dk Slaa anapotosha umma anaposema mbunge anapata mshahara wa Sh7 milioni. Alisema kuwa mbunge anapata mshahara kamili wa Sh2 milioni, akiwa katika daraja la saba la mshahara wa viongozi (LSS).
Hata hivyo, alisema hesabu za Dk Slaa zinajumuisha fedha nyingine ambazo ziko nje ya mshahara, ikiwa ni pamoja na fedha za mafuta, kuendesha ofisi ya mbunge ambazo ni za jimbo.
"Dk Slaa aonyeshe hati ya malipo ya mshahara unaoonyesha mbunge analipwa mshahara halisi wa sh 7 milioni," alisema Sitta.
Sitta, ambaye amemaliza kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya kuongoza chombo hicho cha kutunga sheria, alisema: "Kujumuisha fedha za kuendesha ofisi na mshahara ni sawa pia na kujumuisha fedha za kuendesha ofisi ya katibu mkuu wa wizara katika mshahara, huu ni ulaghai tu... wala hii haingii akilini."
Alisema mbunge anapata mshahara mdogo kuliko hata mkuu wa wilaya ambaye yuko daraja la LSS6 na "sijui kama anafanya utafiti, lakini alipaswa kuzikataa fedha za mshahara; mbona alikuwa anapokea? Alianza kujenga hoja hii baada ya kuona anataka kugombea urais, Slaa aache ghilba".
"Ndiyo maana, nasema nina wasiwasi Dk Slaa anatoa ahadi ambazo hakuzifanyia utafiti. Unajua huwezi kuwaambia watu tu kwamba utatoa elimu bure ya hadi kidato cha sita. Hebu waeleze wanatarajia kuanza na wanafunzi wangapi, wamekokotoa hesabu watatumia shilingi ngapi kwa kuanzia na malengo hayo ni kwa muda gani na mtoto mmoja gharama yake ni shilingi ngapi," alieleza.
"Kwabababu kufanya siasa za ulaghai kwa wananchi ili upate madaraka ni kosa baadaye itakuja kuleta matatizo. Sina tatizo na watu kusomeshwa bure, lakini tunataka ahadi zilizofanyiwa utafiti ambazo zitamkomboa mwananchi kweli."
Dk Slaa kuipiga bei ndege ya Rais
Naye Dk Slaa, ambaye anaendeleza na ziara zake za kampeni, jana aliendelea na sera zake za kupunguza matumizi ya serikali alipoeleza kuwa ataiuza ndege ya rais ambayo alidai kuwa Kikwete amekuwa akizurura nayo nje ya nchi kufanya anasa kwa kodi za wananchi.
Akihutubia wananchi wa Sirari mkoani Mara, Dk Slaa alisema ndege hiyo imekuwa ikitumia kiasi cha Sh6 milioni inaporuka kwa saa moja kitu ambacho ni cha kifisadi
.
Dk Slaa alisema kuwa Kikwete amekuwa akifanya safari za kupindukia nje ya nchi tangu aingie madarakani mwaka 2005 na kulitia taifa hasara, kitu ambacho alisema ni hatari.
"Anadai kuwa anatafuta wawekezaji lakini cha kushangaza nchi inazidi kushuka kwa ubora kiuwekezaji... sasa imekuwa nchi ya 131 kutoka 121," alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema kutokana na ndege hiyo kutumia fedha nyingi ambazo hazina tija kwa Watanzania, akiingia ikulu ataiuza na kununua helkopta ambayo inaweza kutua kila kijiji na kutoa huduma kwa wananchi tatizo linapotokea.
"Helkopta haitumii gharama kubwa kama ilivyo ndege hiyo, hivyo ni bora kuiuza kwa kuwa ni ya kianasa zaidi," alisema.
Alisema Kikwete hufuatana na msafara mkubwa wa watu ambao wamekuwa wakilipwa fedha nyingi na kulala hoteli za gharama kubwa zisizokuwa na msingi katika maendeleo ya taifa ambalo wananchi wake ni masikini.
"Katika safari yake ya mwisho kwenda Marekani ambayo alipitia Dubai, mmoja wa maofisa wake alinunua magari mawili baada ya kurejea nchini kutokana na posho za safari hiyo.
Hii ni hatari na haifai kabisa na mbaya zaidi amekuwa akifikia na msafara wake wote katika hoteli za gharama ya dola 5,000 za Kimarekani kiwango ambacho ni cha anasa," alidai Dk Slaa.
Akiwa Kata ya Nyamongo ambako uko mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick, Dk Slaa alisema kuwa atafumua mikataba ya migodi hiyo mara atakapoingia madarakani kwa kuwa wananchi wanaishi karibu na migodi hiyo hawafaidiki na maisha yao ni duni.
"Rasilimali za taifa hili ni lazima tuzirudishe kwa wananchi ili tuweze kuboresha maisha yao, hivyo nitahakikisha migodi hii na mikataba yake inafumuliwa ili tufaidike wote,"alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa hata polisi ambao wamekuwa wakiwapiga wananchi wanaokaa karibu na mgodi wa North Mara hawataweza kufanya hivyo tena kwa kuwa mgodi huo utakuwa mali ya wananchi wa Nyamongo na Tanzania kwa ujumla.
Dk Slaa pia alimtaka Kikwete aache kuwa mnafiki kama Sitta kutokana na kueleza kuwa elimu ya bure haiwezekani wakati wanajua ukweli kuwa inawezekana.
Alisema kuwa wanaujua ukweli kwa kuwa enzi za mwalimu walisoma bure na ndiyo maana leo wanaringa kwa kuwa walisoma bila tatizo lolote.
"Simuelewi Kikwete kwa kuwa haeleweki na hajui anachosema... ni mtu wa kuona noma (haya) kusema ukweli mbele ya wananchi, hivyo aache kuwadanganya kwa kuwa hivi sasa hawadanganyiki," alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema kuwa Kikwete anakumbuka wakati alipokuwa waziri alipitisha sheria ya kusamehe kodi kwa miaka mitano kwa wawekezaji, kodi ingeweza kutumika kuwasomesha wananchi bure.
"Kikwete yuko tayari kumwezesha mzungu na si Mtanzania masikini anayeishi maisha duni," alisema.
Dk Slaa pia alisema risiti ya malipo ya kumkodishia ndege ya serikali Mama Salma Kikwete zilizoonyeshwa na meneja wa kampeni za CCM, Abdulrahaman Kinana zina shaka na inabidi zichunguzwe.
"Waichapishe kwenye magazeti yote ili wananchi waione lakini pamoja na hayo nikiingia ikulu nitaichunguza," alisema Dk Slaa.
...CCM wajibu mapigo
Katika hatua nyingine, CCM imejibu tuhuma zilizotolewa dhidi ya Mama Kikwete anayedaiwa kufanya matumizi mabaya ya fedha za serikali ikiwemo ndege za serikali katika kampeni zake, ikisema kuwa ndege hizo hukodishwa kwa Wakala wa Ndege za Serikali.
Mratibu kampeni wa CCM, Abdularhaman Kinana aliwaambia waandishi jijini Dar es Salaam ndege hiyo hukodishwa na chama hicho.
"Ndege za Wakala wa Ndege za Serikali zinakodishwa kwa mtu yoyote ili mradi ratiba zisiingiliane na za viongozi. Mara nyingi watu huzikodi kwa ajili ya kufanikisha mazishi... ni ruksa kukodi ndege hizo ili mradi umudu kulipa gharama zake," alisema.
Alisema taasisi hiyo inajiendesha kibiashara kwa kujitegemea.
"Ukiiona ndege ya serikali inasafiri ufahamu kuwa imekodishwa, hata gharama zake ziko wazi, kila mahali unaposafiri ukifika ofisini kwao watakueleza gharama zao," alisema.
Kinana aliwaonyesha waandishi wa habari risiti ya kukodi ndege ya serikali 5HT GF iliyompeleka Mama Kikwete Musoma akitokea Dar es salaam. Inaonyesha kuwa gharama za kukodi ndege kwa safari hiyo ni Sh.22 milioni.
Alisema mbali na ndege za serikali, huwa pia wanakodi ndege binafsi kwa ajili kumsafirisha mke wa rais kwenda katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kampeni.
Alisema Mama Kikwete ataendelea kufanya kampeni kwa kwa gharama zozote za chama hicho kwa vile kimeona kuna tija kwa yeye kampeni.
Kinana alisema Dk Slaa anaonekana kuishiwa hoja kwa kuwa alitakiwa kufanya utafiti kwanza kabla ya kutoa tuhuma ambazo hazina ukweli wowote.
"Tunasikitika kuona kila siku Dk Slaa anafikiria namna ya kufungua kesi na kutoa tuhuma badala ya kuelekeza nguvu zake katika kunadi ilani ya chama chake. Hii inaonyesha jinsi mgombea huyo alivyoishiwa kisiasa," alisema.
CCM yaivimbia Nec
CCM pia imesema kamwe haiwezi kuondoa mabango yake sehemu mbalimbali nchini kama inavyoelekezwa na Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kwa vile ujumbe uliopo kwenye mabango hayo unaonyesha namna chama hicho kilivyotekeleza ilani yake.
Alisema wameiheshimu Nec kwa kuondoa mabango mawili yanayomwonyesha Rais Kikwete akiwa na majaji na nyingine lenye picha ya mgombea huyo akikagua jeshi.
"Tunasema tumeondoa mabango hayo, lakini hatuwezi kuondoa mabango mengine kwa vile hatuoni sababu kwa kuwa rais anaonyesha namna alivyotekeleza ilani ya chama chake," alisema.
"Mbona kuna mabango ya wagombea urais wa Chadema na CUF ambayo yanawaonyesha kuwa ni marais badala ya kusema wagombea urais, ina maana Nec haiyaoni," alihoji Kinana.
Source: Mwananchi
Taarifa hii imeandikwa Ramadhan Semtawa, Boniface Meena na Raymond Kaminyoge.