SITASAHAU (Kisa Cha Kweli)

SITASAHAU (Kisa Cha Kweli)

Abdallahking

JF-Expert Member
Joined
Mar 19, 2018
Posts
3,985
Reaction score
10,843
1.jpg



KISA : SITASAHAU (KISA CHA KWELI)
KISA HIKI KIMEKAMILIKA
KIMEANDIKWA NA : NIHZRATH NTANI
CHANZO : BURE SERIES


SEHEMU YA KWANZA


Kwa kumbukumbu ya wazazi wangu.

"Wakati mikono yangu haiwezi tena kuwagusa niwapendao, nitaendelea kuwakumbuka kwa sala zangu. Wakati macho yangu hayawezi tena kuwaona wapendwa wangu, sura zao kamilifu huibuka katika album ya picha ya familia yetu. Wakati masikio yangu hayawezi tena kusikia sauti tamu za niwapendao, bado minong'ono yao huendelea kama kitulizo na burudisho la muziki mtamu masikioni mwangu. Kweli wale tuwapendao hawafi kamwe bali huendelea kuishi kwa muda wote ambao tunawakumbuka , kuwaenzi na kustahimili ukiwa lakini bado tutaendelea kuwa pamoja nao
Uungwana na utulivu wao upo hai wakati wote, macho yao malegevu, lakini ya huruma yataendelea kuniangalia. Tabia zao za unyenyekevu na utaratibu nitazikumbuka. Nitakumbuka pia ushauri wao waliokuwa wakinipa na utaendelea kuwa kama mwongozo mzuri kwangu, familia yetu na marafiki pia. Wamekwenda, nitawaonaje mimi?"


Utangulizi: Nimekuwa mwanaume mtu mzima sasa, pengine ni wakati sahihi kuitoa simulizi hii ili jamii ipate kujifunza. Niliitaka simulizi hii niifanye kama riwaya, pengine hadithi nzuri ya kupendeza lakini yote ilishindikana kwa sababu kazi hii si ya kubuni ingenipa shida sana katika kutengeneza matukio ya riwaya. Nikataka kuandika kama tamthiliya lakini nako sikuweza kuzingatia muundo wa uandishi wa tamthiliya nikajikuta naandika simulizi isiyo tamthiliya, riwaya ama hadithi. Nina hakika mara tu utakapomaliza kuisoma simulizi hii utakuwa umejifunza jambo muhimu sana katika maisha yako. Majina yaliyotumika katika simulizi hii si ya kubuni lakini hayahusiani na simulizi hii. Majina halisi yamefichwa kwa sababu maalumu. Twende nami mpaka mwisho wa stori hii......

....................
Nikiwa ndio kwanza nimetoka kutuma barua ya maombi yangu ya kazi, kwenda kwenye kampuni moja inayohusika na usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi. Asubuhi hii ilinikuta niko maeneo ya Posta, jijini Dar es salaam. Kuwepo kwa mvua za rasha rasha zilinifanya nijumuike na watu wengi kujificha pembezoni mwa korido za ofisi zilizoko maeneo hayo. Hata hivyo, baada ya muda fulani mvua zile zilikata.

Nikaanza kujivuta kusogea stendi ili nipate usafiri wa kurudi nyumbani ninapoishi pale maeneo ya Ukonga Airport. Kwa muda ule wa asubuhi ya saa nne hakukuwa na shida yoyote ya usafiri kama ilivyo adha la jiji la Dar Es Salaam, magari yalikuwa mengi. Wakati nalifuata basi moja kati ya mabasi machache yaliyokuwepo kituoni hapo yanayokwenda njia ya Gongolamboto. Nikajikuta namgonga kwa bahati mbaya mdada nisiyemfahamu.Mungu wangu!
Bila kutarajia, macho yangu yakajikuta yakiangalia baadhi ya nyaraka zilizosambaa ardhini kutokana na kitendo kile nilichokifanya bila kukusudia, nikajikuta mwili wangu ukiinama na kuziendea nyaraka zile na kuzikusanya kwa uangalifu mkubwa. Sikuwa najua nini kilichoifadhiwa ndani ya nyaraka zile. Kwa unyonge niliyainua macho yangu na kumtazama binti yule kwa mara ya kwanza, nakiri kabla ya hapo sikuwa nimemtazama vizuri binti huyu.

Macho yangu yakatua kwenye uso wa binti yule, Lalaula! nikashtuka! ni kama nimeshikwa na bumbuwazi kwa muda wa sekunde chache, mapigo ya moyo wangu yalikimbia kwa maili nyingi. Kitendo kile kilifanyika kwa haraka mno. Hata hivyo niliweza kumkabidhi binti yule nyaraka zile, na alipozipokea tu alinisindikiza na tusi na msonyo juu yake, nikabakia kufadhaika kwenye macho ya watu wengi, mvulana mimi!.
Wakati macho yangu yakimsindikiza binti yule akitokomea ndani kabisa ya Bank ya CRDB tawi la Azikiwe lililopo jirani na eneo hilo la Posta hapa jijini Dar es Salaam. Nami nikajivuta na kuingia ndani ya Bus, na kukiendea kiti cha kati kati upande wa dereva kisha nikakaa hapo. Dakika chache baadae basi lile likaanza safari. Mawazo ya binti yule yakaanza kunitawala. Hakika alikuwa binti mzuri ajabu na mrembo hasa wa kupendeza ambaye nakiri sikuwahi kukutana na msichana mzuri kama yule kabla. Kila kitu kilichotokea kwa dakika zile chache zikawa zinajirudia mawazoni mwangu. Nikajikuta najiuliza kwanini binti yule atawale mawazo yangu?.Nikakosa jibu.

*****************
Milio ya 'coins' kama ilivyo ada ya makonda wengi wanavyozichezesha pesa hizi za 'silver' kwa mtindo wa kipekee kabisa, ilinigutusha kutoka katika lindi la mawazo kwa wakati huo. Konda alikuwa ananikumbusha nimpe pesa yake, huku macho yangu yakitazama nje, nikaja gundua tupo kwenye foleni ya kuvuka mataa pale Tazara. Haraka nikaingiza mkono wangu mfukoni ili nitoe akiba yangu nimlipe konda yule.

Hamadi! mikono yangu ilirudi patupu, hakukuwa na pochi wala pesa. Nikajikuta natafuta kila mahali ndani ya mifuko ya suruali yangu kama mtu aliyechanganyikiwa kwa muda huo lakini majibu yalikuja yale yale, pochi haikuwepo. Nikajikuta nababaika huku nisijue cha kufanya. Wakati huo huo konda alikuwa yupo makini na mimi akisubiria nimpatie haki yake. Kwa mara nyingine tena, nikawaza! nikawaza! nikahofu kufadhaika ndani ya Bus. Kwa ujasiri wa kiume nilimjibu konda yule, nimeibiwa pochi na pesa iliyokuwemo. Konda hakunielewa hata kidogo, akaanza kutoa maneno ya kashfa na ya udhalilishaji juu yangu, huku akisema ni tabia za vijana wengi kusingizia kuibiwa mara wanapodaiwa nauli. Nikafadhaika!
Maneno yale yalinifanya niwaze sana, nikaanza kujiuliza nikiwa msomi wa shahada moja ya elimu ya teknolojia, leo nadhalilika kwa kutokuwa na shilingi mia nne tu ya nauli? Konda yule akawa anaendelea kusisitiza kuhitaji nimlipe nauli yake. Dada mmoja kama malaika akajitokeza pasipo tarajia;...wakati nikiwa nimebakia nafikiria kumwambia konda anisaidie huku nikiwa na hofu kutokana na matamshi yake dhidi yangu, nikajikuta nadhamiria kumuomba anishushe.

Hata hivyo kabla ya kuyasema hayo, nikasikia sauti ya kike kutoka nyuma ya kiti changu ikimwambia konda akate nauli yake na yangu. Haraka niliyageuza macho yangu na nikajikuta yanagongana na ya msichana mrembo wa haja. Bahati kubwa hii? Nilijiuliza. Haraka nilimjibu "Asante" nae akaachia tabasamu machoni mwake huku akinijibu "husijali kaka", Wakati huo huo konda alikuwa anarudisha chenji kwa yule dada. Safari ikaendelea.
Nikajikuta mawazo yangu yanamkumbuka yule dada niliyemgonga pale posta, nikaanza kuhisi kuwa tukio lile lilipelekea kuibiwa pochi yangu bila kufahamu, sikumbuki ni muda gani nilibiwa lakini najua kuna mvulana alikuja na kumuuliza yule dada tatizo mahali pale. Wakati naendelea kuwaza...nikaanza kuwaza maisha yangu chuoni.

Nikawakumbuka marafiki ambao tulikuwa tukiambizana vyumbani wakati huo tukiwa hosteli kwa furaha na kupeana matarajio makubwa ya kuwa tukimaliza chuo, tutapata kazi nzuri, tutaishi maisha mazuri na hata kuwa na familia nzuri. Kila kitu kilikuwa kinakuja kama tamthiliya fulani ndani ya mawazo yangu, nikajikuta nachukia mfumo wa ajira ya nchi yangu hata mfumo wa elimu pia, elimu inayomfanya mhitimu afikirie kuajiriwa kuliko kujiajri. Walimu wetu chuoni hawatuambii ukweli hali halisi ilivyo baada ya kuhitimu elimu yetu. Nikajikuta najichukia mwenyewe badala ya walimu hao.
Nikaanza kuwakumbuka wazazi wangu waliokuwa kijijini mkoani Mbeya, wamejenga matarajio mema juu yangu,lakini ni mwaka wa pili sasa nahangaika kutafuta kazi bila mafanikio, kila mahali nilipotuma maombi yangu hakuna nilipoitwa kwa usaili. Maisha ya kuishi kwa watu yalielekea kunichosha, hata hivyo si mimi tu hata walezi wangu walianza kunichoka. Nikaanza kuchukia ni kwanini nilitumia muda wangu mwingi kusoma, kusoma kusiko na faida?

Kutokuwapo na kazi yenye kuniingizia kipato kukapelekea nimpoteze 'My Girlfriend' Binti yule wa Kimanyema niliyekuwa nafikiri ananipenda kwa dhati, kumbe alikuwa ananidanganya. Mwanamke niliyempata Chuoni, nilimpenda kweli kweli lakini baadae aliniacha kwa sababu sina pesa. Wako wapi wanaosema pesa haina umuhimu katika mapenzi?.Mnajidanganya.

Nikaanza kuyakumbuka matendo yake kwangu, nyakati fulani alilia kwa ajili yangu hasa nilipomuuzi, alinihakikishia kuwa mimi ni wake na yeye ni wangu mpaka ndoa na hakuna kitakachotutenganisha. Kumbe nilikuwa napumbazwa ndani ya dimbwi la mahaba. Mahaba yaliyokuja kuniumiza baadae. Nikajikuta nikiwachukia viumbe hawa wanaoitwa wanawake. Hata hivyo, bado moyo wangu haukuepa maumivu yale.
Sauti ya konda ilinigutusha kutoka katika lindi la mawazo yale, tayari gari limewasili kituoni, kituo kilicho pembeni na uwanja wa ndege. Haraka nilishuka nikaanza kutembea. Sijui ni kitu gani kilinifanya nigeuke nyuma kabla ya kuvuka barabara. Nikajikuta nabakia na mshangao mkubwa! .Ndio! macho yangu yakakutana na binti yule mwokozi wangu, binti aliyenionea huruma na kunilipia nauli ndani ya Bus . Haraka nilimpa tena asante kwa msaada wake, binti yule akanijibu "nisijali", nilimuuliza wapi anapoelekea, alinijibu yeye ni mgeni mahali hapo na amekuja kumsubiri mgeni wake kutoka nje ya nchi, hata hivyo amewahi sana, atafika hapo masaa mawili baadae.

Binti yule aliniomba nimuoneshe mahali panapopatikana chips nzuri apate kula, ni baada ya kumwambia mimi ni mwenyeji mahali hapo. Nikachukua jukumu la kumsindikiza, nilimpeleka kwenye Cafe zilizoko pale karibu na kituo cha tax. Baada ya kufika pale nilianza kumuaga kwa minajili ya kuondoka. Binti wa ajabu alipinga uamuzi wangu, akaniomba tuwe pale tupate wote chakula na kinywaji kisha angeniruhusu kuondoka kama sitajali. Kumbuka sikuwa nimetia chochote tumboni kwa wakati huo, hakika sikujivunga.....nikavuta kiti na kukaa.
Kuwepo kwangu na binti yule mahali pale kukapelekea kutambuana, alinifahamisha kuwa anaitwa Nadia, ni sekretari wa kampuni moja ya Bima nchini na yupo pale kwa ajili ya kumpokea rafiki yake mmoja. Nilijitambulisha kwake kuwa naitwa Richard Kamba. Nilimuelezea maisha yangu kwa ufupi, hata hivyo sikuwa natambua kwanini namuelezea maisha yangu mtu nisiyemfahamu? Hata hivyo nguvu fulani iliniambia nimefanya jambo sahihi kwa wakati ule.
Baada ya muda tuliachana na binti yule, alinipa 'Bussines Card yake', akinisisitiza kuwa nikifika nyumbani nimpigie, maana simu yangu nayo ilikuwa imeibiwa kwa tukio lile la Posta. Vile vile alinipatia noti ya elfu tano, bahati ilioje? kwa dakika zile nikajikuta nasahau yote uso ukajaa tabasamu. Nilipofika nyumbani nilioga na kupata chakula nilichokikuta, kazi ya kutazama vipindi vya television ikachukua nafasi yake kama ilivyo siku zote. Hiyo ndio ilikuwa kazi kubwa nikiwa nyumbani, kushinda kwenye tv.
Baadae nilipokumbuka kumpigia simu Nadia, nikatafuta 'Bussines Card' ile bila mafanikio, sikumbuki wapi nilipoiweka, nilitafuta mwishowe nilikata tamaa. Na sikuiona tena.

Maisha ya hapo nyumbani hayakuwa yenye furaha kwa upande wangu hata kidogo, sikuwa na kazi ya kufanya na muda mwingi niliutumia kukaa sebuleni na kutazama tamthiliya za kifilipino na baadhi ya filamu za Bongo movie yalikuwa maisha yangu ya siku zote. Maisha ya mtu hasiye na kazi.

Mwaka sasa, bado ningali natafuta kazi na hakuna mahali nilipowahi kuitwa hata kwenye usaili tu. Walezi wangu walianza kunichoka taratibu hapo nyumbani nilianza kufikiria kurudi kijijini, mahali walipo wazazi wangu, hata hivyo bado moyo wangu haukuwa radhi kurudi Tukuyu. Sikuweza kukata tamaa. Tukio la ajabu likatokea....

***********************
ITAENDELEA
 
SEHEMU YA PILI

Miezi miwili baadae nikapokea simu ya mdada mmoja huku akihitaji kuzungumza na Richard, bila shaka niliipokea simu ile na kuzungumza nae kwa umakini mkubwa, ndipo alipojitambulisha anaitwa Aisha ni Katibu Muktasari wa kampuni ya Tanzania Transport company, akinipa taarifa ya kuitwa kwenye usaili siku ya jumamosi ofisini kwao kutokana na maombi ya nafasi ya kazi niliyoomba miezi michache iliyopita. Hakika ilikuwa tukio lenye kuleta furaha sana kwa upande wangu. Nikaazimia kushinda usaili huo.

Jumamosi kwa upande wa Dar es salaam mara nyingi nyakati za asubuhi huwa hakuna shida ya usafiri, lakini mimi saa moja kamili ilinikuta nimeshafika Msasani mahali ilipo ofisi za Kampuni ile, nakiri kabisa sikuweza kupata usingizi usiku wa kuamkia siku yangu ya usaili. Hata hivyo niliwahi sana maana ofisi ile ilikuwa inafunguliwa saa mbili na nusu asubuhi na usaili ulipangwa kufanyika saa nne asubuhi, sikujali sana umbali wa muda huo. Nikasubiri kwa hamu kubwa.

Baada ya kuvumilia sana huku nimekaa na watu nisio wafahamu malengo yao, tukaja kuitwa wale wote waliotakiwa kufanyiwa usaili siku hiyo, ndipo nikatambua sikuwa peke yangu, tulikuwa kama watu sita hivi. Nikasogea na kukaa kwenye chumba ambacho kilitengwa maalumu kwa shughuli hiyo. Tukakaa kwenye benchi ya kisasa lililopo pembeni ya chumba kwa ajili ya kusubiriwa kuitwa. Muda Ukawadia na nikapigwa na bumbuwazi.
Nilikuwa mtu wa kwanza kuingia chumba cha usaili, ikiwa ni mara yangu ya kwanza kufanyiwa usaili tangu nilipoanza kutafuta kazi, hivyo suala la hofu sikuweza kuepukana nalo. Hofu ikanitawala. Ni wakati ambako nilisikia sauti kwenye masikio yangu ikiniambia "Richard ondoa hofu uliokuwa nayo, jiamini kwa sababu hii ni nafasi muhimu ambayo umeipata, shinda hofu hii" Kauli hiyo ilisambaa kwa kasi ya ajabu masikio mwangu, haraka nikashusha pumzi kwa nguvu zote. Wakati huo tayari nipo ndani ya chumba kizuri ajabu.

Chumba chenye kunakshiwa na rangi nzuri na vitu vya thamani kubwa. Chini ya chumba kile kulitandikwa zulia zuri jekundu, pembeni ya ukuta kulikuwa na tv nzuri ya kisasa iliyokaa vyema ukutani pale. Macho yangu kwa kasi ile ile yakaendelea kusawiri chumba kile. Hakika ni chumba kilichokuwa kinavutia sana kwa harufu nzuri iliyosambaa chumbani mle ,huku hali ya kiubaridi ikitawala eneo lile. Wakati ukawadia.
Wakati nikiendelea kustaajabu uzuri wa chumba kile ghafla sauti ya kike ikasikika " Naitwa Tayana Masenga ni Afisa Uajiri wa kampuni hii na nipo hapa na Afisa habari Mr Salim Mhando, karibu sana ndugu" Wakati huo nilimuona yule dada akivua mawani yake kwa utulivu husio kifani. Ni wakati huo huo macho yangu yalipokimbia maili nyingi kwa kasi ya ajabu na kutua usoni mwa msichana yule. Nikashtuka! Sikuamini macho yangu kwa wakati ule.
Haraka kumbukumbu zangu zikarejea kwa kasi ya ajabu, nikajiuliza wapi nilimuona binti huyu? wakati huo huo mapigo ya moyo wangu yakawa yameongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida. Ni wakati ambapo moyo wangu ukahisi hali ile ile, hali ambayo niliwahi kuhisi kipindi fulani uko nyuma. Naaam! haraka nikamkumbuka..."Ndiye huyu! ndiye yeye hasa" Nikajiambia...

.Ni binti yule yule ambaye nilikutana nae Posta na kumgonga kwa bahati mbaya tu kama nilivyohisi kwa upande wangu , ni binti huyu ambaye alinifanya nipewe maneno ya kashfa na konda. Ni binti huyu ambaye alinifanya nipoteze simu yangu ya thamani wakati wa tukio lile, kumbe anaitwa Tayana? nikajijibu. Badala ya kuanza kumchukia nikajikuta nabakia kutabasamu..tabasamu la uongo. Tabasamu la kihisia! nikajikuta najitambulisha..."Naitwa Richard Kamba na nipo mahali hapa kwa ajili ya usaili" Wakati najitambulisha macho yangu yalikuwa yanamtazama binti yule ambaye naweza kusema kwa wakati huo ni adui yangu. Hata hivyo sikuona chochote kilichobadilika usoni kutoka kwa binti yule mrembo. alionesha sura ile ile yenye kuvutia. Ajabu ilioje?

***************
Nilianza usaili ule kwa kujibu kila swali kwa umakini mkubwa na uwerevu wa hali ya juu, majibu yangu yalionekana kumfurahisha sana Afisa habari wa kampuni ile, wakati wote kila nilivyokuwa nikijibu kwa umahiri mkubwa alikuwa akibakia akitabasamu na huku akiandika kitu nisichokifahamu kwenye 'Note Book' yake. Ndipo binti yule mrembo aliponiuliza swali ambalo lilionekana kama la mwisho kwa upande wangu. Aliniuliza: " Unataka ulipwe mshahara kiasi gani?" Hakika lilikuwa swali gumu kulijibu na kuna sauti nikaisikia masikioni mwangu ikinisisitiza nilijibu swali hilo kwa uangalifu wa hali ya juu.

Nikajibu: " Napaswa kulipwa kutokana na kiwango ambacho kampuni hii imekitenga kwa ajili ya nafasi ninayoiomba. Napaswa kulipwa kutokana na utendaji wangu na kiwango cha faida nitakachokiletea kampuni. Pia napaswa kulipwa kutokana na kiwango cha elimu yangu" Nikamaliza kulijibu swali lile. Na kuwatazama wale watu wote wawili walio mbele yangu. Nilimuona yule afisa habari akitabasamu na kumuangalia binti yule kwa furaha hata hivyo sura ya binti yule ikabakia vile vile katu haikujibu tabasamu la afisa habari yule. Nikafadhaika!
Baada ya usaili niliruhusiwa kuondoka mahali pale huku yule afisa habari akinipa pongezi za kipekee na kunipa matumaini makubwa juu yangu ya kupewa ajira katika kampuni ile.Tofauti na yule binti mrembo yeye aliguna tu. kisha akafunga kitabu chake na kuvaa miwani yake ambayo ilionekana wazi ni ya matatizo ya macho. Nilitoka ndani mle nikiwa nusu nina furaha na nusu nikiwa na huzuni, hasa nikikumbuka kuwa binti yule mrembo alikuwa ni kama ufunguo wa ajira yangu, ni yeye ndie atakayeamua nafasi yangu. Nikasali! nikasali! nikasali kwa Mungu wangu nishinde usaili ule.

**************
Wiki zikapita, hadi miezi ikapita, sikuwahi itwa na kampuni ile kwa ajiri ya ajira. Hakika nilikata tamaa kabisa ya kuajiriwa na nikatamani kujiajiri mwenyewe hata hivyo nilikosa mtaji wa kuanzisha biashara. Mjini nikapaona pachungu huku manyanyaso yakizidi toka kwa walezi wangu. Maisha yalikuwa magumu sana kwa upande wangu. Mwanaume mimi nilikosa hata pesa ya vocha. Wakati mwingine nilitegemea chenji zinazotokana na mahitaji madogo madogo ninayotumwa kwenda kununua na kiasi kidogo kinachobakia ndio hutumia kununua vocha. Nilikata tamaa ya maisha. Nikazidi kuchukia muda wangu niliyoupoteza kuitafuta elimu. Wakati ukawadia.
Ni siku chache baadae nikaliona tangazo kwenye gazeti la serikali kuhusu nafasi za ajira kutoka shirika la Ethiopian Airline, ambalo limefungua tawi hapa nchini. Niliandika maombi yangu na kuambatanisha CV yangu yenye nyaraka kivuli za kuthibitisha kile nilichokiandika kwenye wasifu wangu na bila kuchelewa nikatuma. Wiki moja baadae niliitwa kwenye usaili.

Baada ya wiki moja kupita nilipokea simu ya kuhitajiwa ofisini kwa kupeleka nyaraka zangu halisi ni baada ya kuelezwa kushinda usaili niliyofanya. Kila kitu kilienda kama simulizi nzuri ya kuvutia ni kama kusoma vitabu vya Robson Kruso. Hatimaye nikaajiriwa rasmi kama Afisa wa IT yaani 'Information Technology' katika shirika hilo. Kumbuka nina shahada ya kwanza ya IT kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam. Maisha yakaanza kwa upande wangu.

Nilianza kazi kwa juhudi kubwa na kujituma kusiko kwa kawaida huku nikiazimia kufidia muda wangu nilioupoteza kwa kipindi chote. Miezi minne baadae niliomba kuhama na kuanza maisha ya kujitegemea. Ilikuwa jambo gumu kwa walezi wangu kunielewa hawakupenda kuhama kwangu kwa haraka kwa kipindi hicho. Nilijaribu kuwashawishi na mwishowe wakakubaliana na uamuzi wangu. Wakati huo huo nikaanza kujiuliza inakuwaje sasa wananipenda, wananililia nikae pale ilhali kipindi sina kazi walikuwa wananinyanyasa? Huku wakinishinikiza nirejee kijijini ....Nikagundua kuwa ni kwa sababu ya kazi yangu, nikasema kwa sababu ya pesa. Hakika pesa ni kila kitu "Nikawaza".
Nilipanga chumba na sebule eneo la Mbezi Kimara, mbali na mahali walipo walezi wangu. Sikutaka kukaa karibu nao. Nilitaka kuwa huru zaidi katika eneo jipya. Miezi michache baadae nilibahatika kupata mkopo ambao niliutumia kununua vitu vya ndani kama Tv, fenicha za kisasa na vingine vingi. Sasa chumba changu kikaanza kuwa na mwonekano mzuri na wenye kuvutia, chumba anachostahili kuishi mvulana wa kisasa. Pia ukumbuke kwa kipindi hicho sikuwa na msichana hata mmoja, hakika niliwachukia wanawake . Kila siku inayokwenda , nilimuomba Mungu anioneshe mke wangu kwa sababu wakati huo sikuwa nawaamini wanawake tena pamoja na kukutana na vishawishi vingi kwa wakati huo.

******************************
Mwaka mmoja baadae kupitia akiba niliyokuwa nikijiwekea nilifanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Kigamboni. Nilianza kufurahia maisha na hata mwonekano wangu ulianza kubadilika. Nilikuwa mvulana mtanashati sana, kila mmoja aliyepata kuniona kabla ya kuajiriwa alibaki akipigwa na bumbuwazi mara tu alipopata bahati ya kukutana nami kwa wakati huu. Nilikuwa mwaminifu na mtiifu sana kazini.

Uwezo wangu wa kufanya kazi bila kuchoka, ushirikiano wangu na wafanyakazi wenzangu uliwavutia wakuu wangu wa kazi. Hivyo nikajikuta nakuwa mwakilishi mzuri wa shirika sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi kwa muda mfupi. Kote huko nilipopitia shirika lilikuwa likipata sifa kubwa kupitia mimi. Nikafarijika sana na kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi. Jambo nisilotegemea likatokea!

Ni miaka miwili baadae yaani miaka miwili na miezi sita tangu niajiriwe kwenye shirika hili. Tukapata msiba mzito wa kuondokewa na Meneja wa shirika kwa upande wa Tanzania. Kifo cha meneja huyu kilikuja baada ya kupata ajali ya gari maeneo ya Tazara wakati huo akielekea nyumbani kwake Tuangoma -Mbagara. Ilikuwa pigo na huzuni kubwa kwa shirika na wafanyakazi ofisini hapo. Nakiri kwa muda mchache niliyomfahamu meneja huyu nilijifunza mambo mengi hasa ukarimu na busara zake bila kusahau ucha Mungu wake. Baada ya kumalizika shughuli nzima ya mazishi ya meneja wetu maana niliteuliwa na shirika kusimamia msiba huo. Wiki moja baadae nikaripoti kazini.

Niliwasili jumatatu ya asubuhi kama kawaida yangu na baada ya kuwasalimia wafanyakazi wenzangu nilielekea ofisini kwangu. Hata hivyo nilijikuta nikiwa na maswali mengi baada ya secretary wa ofisi ya meneja kunichangamkia kusiko kawaida huku akinitizama kwa tabasamu fulani lenye kumaanisha kuna jambo muhimu angependa kuniambia. Wakati huo bado miguu yangu na akili yangu nilishavielekeza kuelekea ofisini mwangu.
Niliingia ofisini mle kama ilivyo kawaida, macho yangu yakatua vema juu ya meza ya ofisi yangu na kuiona bahasha ikiwa imeandikwa jina langu, bahasha hisiyo ya kawaida kimuonekano. Nilikuwa napokea bahasha nyingi lakini hii ilikuwa tofauti, muonekano wake ulinisisimua . Nilishtuka sana, na kwa kasi ya ajabu haraka niliifungua barua ile na kuisoma kwa muda ule ule huku ningali nimesimama. "Mungu wangu!" Nilijikuta natoa sauti hafifu huku nimepigwa na butwaa. Mle ndani ya barua ile ambayo nimeisoma ilieleza imetoka makao makuu ya shirika likitoa taarifa ya kuteuliwa kwangu kuwa meneja mpya wa shirika la ndege la Ethiopia Airline. Kila kitu kilikuwa kama tamthilliya fulani ya kifilipino, nikajihisi kama nipo ndotoni. Nilifumba macho na kufumbua tena bado macho na akili yangu iliniambia kuwa sio ndoto. Ni ukweli halisi. Nikapagawa!
Uteuzi wangu ulienda sambamba na kupewa likizo yenye malipo ya wiki moja, kujiandaa na nafasi mpya ya umeneja ofisini hapo. Likizo yangu iliandikwa inaanza siku hiyo hiyo. Nikajikuta natoka nje kama mwehu. Kila mmoja miongoni mwa wafanyakazi wenzangu walikuwa wakinipa hongera kwa uteuzi wangu. Bado nilihisi nimo ndotoni.Ndoto nisiyotarajia. Nikajikuta najikana mwenyewe kusiko tarajiwa. Hapana sio mimi Richard. Nikarejea kuisoma upya bado jina lililomo kwenye barua hiyo lilikuwa langu. Bila shaka ni mimi niliyekusudiwa.
Nilianza kujiuliza kama nastahili cheo hiki?, wakati wapo wafanyakazi wa muda mrefu kuliko mimi. Kitu gani uongozi wamekiona toka kwangu hadi kufikia kustahili kupewa nafasi hii kubwa kabisa katika shirika? Maswali yangu kwa wakati huo hayakuwa na majibu katika kichwa changu. Nikaazimia kufanya kazi ambayo itawashangaza hata wakuu wangu. Kazi itakayokuwa na faida kubwa kwa shirika hili. Moyoni nikakubali uteuzi huo.

*************
ITAENDELEA

CHANZO : BURE SERIES
 
SEHEMU YA TATU

Ni baada ya kupata kazi ndipo nilichukua jukumu la kulea wazazi wangu, ulikuwa mzigo ambao katu sikuweza kuepa. Nikabeba majukumu. Majukumu niliyostahili kuyabeba. Haraka nilimsimamisha Baba na Mama yangu kulima kwa kutumia jembe la mkono, kisha nikawa naweka vibarua huku wao wakibakia kuwa wasimamizi tu. Pia nililazimika kuwawekea msichana ambaye muda mwingi atakuwa anawasaidia kwa kazi za pale nyumbani. Kila mwezi nilituma kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kununulia mahitaji ya hapo nyumbani. Wazazi wangu walifurahi sana na kila mara walikuwa hawachoki kuniombea mimi mtoto wao.
Pengine, ushirikiano wangu na upendo wangu kwa kila mtu pale kazini uliwavutia sana wakuu wangu,nilijiambia. Hata pia utendaji wangu kazini ulikuwa wa hali ya juu na hata kufikia kupata tuzo ya mfanyakazi bora wa shirika kwa miaka miwili mfululizo. Karibu wafanyakazi wengi pale ofisini walikuwa wakinipenda na kuwa karibu nami. Na hata aliyekuwa Meneja mkuu hayati mzee Johnson Ndeluma alikuwa ananipenda sana na siku zote alikuwa anapeleka ripoti kuhusu mimi makao makuu. Hapo ndipo maswali yangu ya kuteuliwa kwangu kuwa meneja mkuu wa shirika kwa upande wa Tanzania yalipopata majibu katika wakati sahihi. Nikatabasamu!

Baada ya kumaliza kila kitu na kukabidhi ofisi kwa mtu atakayekaimu nafasi yangu mpaka pale nitakapomaliza likizo yangu kisha kukabishi nyaraka za kitengo nilichokuwa mwanzo kwa msaidizi wangu wa kazi kama barua ile ilivyoeleza. Msaidizi wangu moja kwa moja anaenda kuwa ofisa wa IT ofisini hapo. Kila kitu nilikifanya kwa haraka kisha niliwasha gari yangu na kuelekea katika ufukwe wa Coco ulioko katikati ya jiji la Dar Es salaam ili angalau nipunge upepo na kufurahia kuwaona watoto waliotoka katika maisha ya tofauti wakijimwaga kwenye ufukwe huo.

Ufukwe wa Coco nilitokea kuupenda sana kwa sababu nilihisi ni sehemu sahihi kwa mtu mwenye msongo wa mawazo kufika hapo. Maana kila makundi ya watu hufika hapo tofauti na fukwe zingine ambazo huwezi kuingia mpaka ulipe kiingilio. Ufukwe huu ni bure na watu wa kila aina wanapatikana hapo.
Niliwasili katika ufukwe huo mida ya mchana, sikumbuki ilikuwa saa ngapi bali ilikuwa kati ya saa saba hadi saa nane mchana. Nikakijongea kiti cha plastic na kukaa hapo nje ya mgahawa na kuagiza kinywaji huku nikiwatizama vijana kwa watoto wakiogelea. Nilijisikia raha sana na kukumbuka nyakati nyingi zilizopita.

Wakati huo nilipokuwa mwanafunzi kule Tukuyu na kipindi fulani tulikuwa tunakwenda Matema beach kujivinjari. Kumbuka mpaka wakati huo sikuwa na mahusiano na msichana yoyote. Hata wale wafanyakazi wa kike waliokuwa wakijigonga ofisini waliishia njiani. Ilifikia hadi kupewa kashfa kuwa mie Jogoo halipandi mtungi. Binafsi sikujali kwa sababu niliufahamu ukweli.
Vile vile sikuwa mnywaji wa kilevi chochote na sikuwa mvutaji pia. Kinywaji changu pekee ni juice na soda tu. Baadhi ya marafiki zangu walikuwa wananidhihaki kwa kuniambia mie bado mshamba tu kwa sababu situmii kilevi kama wao. Nalo pia sikujali sana kwa upande wangu Kwa sababu kitu kimoja nilichokuwa nacho ni kusimamia kile ninachokiamini. Hicho ndicho kilichokuwa kinanisaidia.
Wakati nipo hapo Coco beach nikawaza sana na kisha nikajiambia likizo hii ya wiki moja yanipasa niende kuitumia Tukuyu pamoja na wazazi wangu ambako toka nilipohitimu chuo kikuu sikuwahi kwenda au niende sehemu nyingine nje ya Dar es Salaam?. Nikawaza sana. Wakati naendelea kuwaza jina la Zanzibari likapita kichwani mwangu. Ni hapo sauti mbili zikaanza kushindana na akili yangu katika maamuzi.

Upande mmoja ukaniambia ukienda Tukuyu ni sehemu sahihi zaidi kwako kwa sababu Baba na mama yako wana hamu kubwa ya kukuona. Na upande mwingine sauti ikanitaka nipuuze kwenda Tukuyu, na ikinitaka kuwa niende katika kisiwa cha Unguja kilichopo Zanzibari. Huko nitafurahia sana wakati wangu alafu pia kwenda Tukuyu ni vizuri niende na mchumba kumtambulisha. Sauti hizi mbili zikanifanya nibakie njia panda nisijue wapi ni sahihi zaidi. Mwishowe niliazimia kwenda Tukuyu mkoani Mbeya kuwaona wazazi wangu.
Baada ya kutosheka mahali hapo nikawasha gari na kurejea nyumbani kwangu Mbezi ya Kimara mahali ambako ndipo nilipopanga. Usiku huo kwangu ulikuwa mgumu sana, bado sauti ya kunishawishi nibatilishe uamuzi wangu wa kwenda Tukuyu na kisha niende Zanzibar haukukoma. Kila muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo nikajikuta naanza kushindwa kuutetea uamuzi wangu nilioufanya kabla...Uamuzi wa kwenda Tukuyu. Sasa akili ikatawaliwa na kwenda Zanzibari.

Bila kutambua nikajikuta nawasha Laptop yangu ndogo na kuitafuta Zanzibar. Nikaanza kuona uzuri na mambo mengi yakaanza kunivutia.Simulizi za marafiki zangu ningali chuoni hasa kwa vijana wale watokao huko visiwani vikanifanya niufikirie mara mbili uamuzi wa kwenda Tukuyu haukuwa uamuzi sahihi. Bila ajizi nikabadili safari ya Tukuyu huku nikikubali ushauri wa kuwa nitaenda huko nikipata mchumba ili wazazi wangu wafurahi. Nikaamua niende Zanzibar. Ni Zanzibari ndipo historia yangu ikabadilika.

Baada ya kufikia makubaliano na akili yangu, na kuazimia kwenda Zanzibari. Usiku huo huo nikajikuta nikivutiwa na Hoteli ya MELIA iliyopo Zanzibar tena ni baada ya kusoma tangazo lao kwenye Gazeti siku chache zilizopita na usiku huo nikajikuta naitafuta hoteli hiyo kwenye mtandao. Ilionekana ni Hoteli nzuri kwa upande wangu. Nikachukua mawasiliano yao na kuongea nao usiku huo huo.

Hakika niliongea na muhudumu na kunifanyia Booking ya chumba cha stahiki yangu. Baada ya yote hayo nikajiuliza ni usafiri gani ambao ningeutumia kwenda huko kati ya Ndege au Boat. Hapo nilikuwa na uamuzi wa haraka sana. Sikuwahi safiri na chombo chochote cha majini nikaona hii ni fursa ya kipekee kutimiza ndoto hizo. Usafiri wa Boti ukawa chaguo lisilo na upinzani.
Bila kuchelewa, asubuhi ya saa kumi na mbili nilikuwa barabarani naelekea bandarini kwa ajili ya safari hiyo. Kutokana na foleni kubwa ya Dar Es salaam nikajikuta nakosa usafiri wa saa moja. Hivyo nikapata usafiri wa saa tatu na nusu asubuhi. Ni baada ya kupata tiketi kutoka ofisi za Azam Merine zilizoko hapo hapo Bandarini.

Saa tatu na nusu tayari nimo ndani ya Boti ya Kilimanjaro nikielekea Zanzibari. Hakika ilikuwa safari nzuri sana kwangu ukizingatia ilikuwa mara yangu ya kwanza kutumia usafiri wa majini. Pia sikuweza kukaa ndani kutokana na hofu ya kutapika. Basi nikakaa juu kabisa ambako kuna hewa na upepo unapatikana kwa wingi. Upepo ambao ulinisaidia nisitapike.
Masaa mawili baadae nilikuwa nateremka bandarini Unguja, kila abiria alikuwa mwenye furaha kubwa ya kufika salama. Nje ya geti nikaiona gari yenye maandishi ya Hoteli ya Melia na pembeni yake kuna mwanaume ameshika bango lenye jina langu kuwa yeye ndiye atakayenipokea. Nikamuendea na kujitambulisha kwake huku nikitoa kitambulisho na kumkabidhi mtu yule. Haraka alichukua begi langu dogo na kuweka mlango wa nyuma ya gari lake kisha akanifungulia mlango wa mbele pembeni yake. Kitabia huwa sipendi kukaa mbele katika chombo cha moto labda mimi niwe ndie Dereva. Huwa navutiwa kukaa nyuma zaidi kwa imani kuwa inapotokea ajali ni nadra mtu wa nyuma kupata tatizo na hata akipata huwa bahati sana kufa. Imani niliyokuwa naishikilia kwa muda mrefu sasa.
Siku hiyo nilipenda kukaa pembeni ya dereva. Ni uamuzi huo uliokuja kunipa furaha kubwa maana niliweza kuyasawiri maeneo mengi ya Zanzibar. Huku nikistaajabu na hali ya ukimya niliokuwa naushuhudia barabarani. "Hakika Zanzibar ni mji wenye kuvutia sana" Nilijisemea. Wakati naendelea kuangalia mandhari ya mji wa Zanzibar nilikuja kushtukia tunafunguliwa Geti la Hoteli ya kisasa ya Melia. Kwa nje ilionekana hoteli nzuri sana kwa jinsi ilivyopambwa kwa namna ya kipekee kabisa. Jambo hilo likanifanya niwe na shauku ya kuingia ndani humo.
Ni baada ya dakika chache ya kufanya malipo, ndipo nilipokabidhiwa chumba cha kisasa kabisa ambacho kilinifanya niupongeze uamuzi wangu wa kuichagua Hoteli hii kwa ajili ya likizo yangu fupi. Nikajitoma Chumbani. Siku hiyo sikutoka nje ya Hoteli hiyo. Muda mwingi niliutumia kusoma na kutazama Tv. Siku zikasonga, muda ukatimia na majibu ya maswali yangu yakapata majibu.

Baada ya siku tatu tangu niwasili hapa Zanzibar na siku mbili nilizitumia kutembelea maeneo ya kihistoria. Nilianza kupapenda Zanzibari. Ilikuwa ni siku ya nne nyakati za asubuhi sana kama kawaida. Niliamka na kutoka nje ya Chumba changu kwa ajili ya kufanya mazoezi. Sikumbuki ilikuwa muda gani ila bado nakumbuka kila kitu. Ilikuwa kati ya saa moja asubuhi na saa mbili.
Nikiwa nimevalia mavazi ya kimazoezi baada ya kukimbia pembezoni mwa bahari na kuchoka sana. Ndipo nilipokuwa narejea taratibu kwa mwendo wa uchovu kutoka pwani ya Bahari mwa hoteli ya Melia. Macho yangu yakanasa kiumbe kilichokuwa kimejilaza kwenye kiti cha uvivu ambacho wazee wengi wa maeneo ya Pwani hupenda sana kuvitumia viti hivyo...viti vya kulala ambavyo mara nyingi vinakuwepo maeneo ya beach zile kubwa na za gharama. Msisimko wa ajabu ukatawala mwili wangu ,nikajikuta nashikwa na bumbuwazi!.

Na kwa mara ya kwanza moyo wangu ukavutiwa na kiumbe kilicholala kama mita arobaini kutoka nilipo. Sijui kwa namna gani macho haya yaliweza kunasa kiumbe hicho. Ni wakati ambapo nikaanza kupoteza kujiamini kwangu. Nikajikuta hisia za uwoga zikianza kutambaa mwilini mwangu kama vile kitu fulani kibaya nimekiona. Nikajikuta moyo na macho yangu yakihitaji kuendelea kumtazama kiumbe huyo. Huku akili haikuweza kuhama kwenda sehemu nyingine kutokana na hofu ya kukipoteza kiumbe kinachoonekana mbeleni mwangu. Kila kiungo changu kikawa kinafanya kazi kwa namna ya ushirikiano wa ajabu. Kiumbe kikaonekana.
Hatua za miguu yangu zikaongezeka atimaye nikakaribia kumfikia kiumbe hicho. Hata hivyo sikuweza kufika mwisho kabisa ya lengo langu kabla ya kupigwa na butwaa. Nikasita. Mungu wangu! nikashtuka!. Ulikuwa mshtuko mkubwa sana kwangu. Hapo hapo nikajikuta sina namna nyingine niende mbele au nibadili mwelekeo wangu. Hata hivyo sauti ndani yangu ikaniambia " wewe ni mwanaume, na siku zote mwanaume husifiwa kwa ujasiri. Onesha uanaume wako" Nikatii sauti hiyo. Nikasogea na macho yakatua kwenye mwili wa binti mrembo. Akiwa amejilaza mahali hapo huku macho yake yakiwa yamefichwa na miwani mikubwa ya urembo ambayo siku hizi vijana wengi wanapenda kuyatumia. Bado nywele zake zikawa kama zinakaribia kugusa ardhi. Ardhi hisiyo na huruma, ardhi iliyomeza miili ya binadamu wengi. Ndipo nilipomtambua.
Nikamtambua kiumbe huyo na haraka nikaanza kurudisha kumbukumbu zangu nyuma. Ndio! Ni binti yule ambaye niliwahi kumgonga kule Posta. Duh! . Ni wakati huo huo binti nae akivua miwani yake na kubakia akinishangaa. Sikuwa nafahamu kwanini alikuwa ananishangaa? Nikaanza kujiuliza amenionaje mimi, ni kwamba sistahili kuwa hapa au ameshtushwa uwepo wangu mahali hapa?. Mwisho nikajiona mpuuzi kuwaza vitu ambavyo sikuwa na uhakika navyo. Nikajikuta namsalimia kiumbe huyo. Jibu lake lilikuwa tofauti na nilivyofikiria.

Nilifikiri hasingeweza kupokea salamu yangu. Alinijibu kwa upole na huku akinisindikiza na tabasamu zuri lililonifanya nibabaike kidogo. Niliomba kujumika nae mahali hapo kama hatajali. Jibu lake lilinishangaza pia, hakika hakuwa na hiana hata kidogo alinikaribisha kwa uchangamfu wa aina yake. Nilivuta kiti ambacho hakikuwa mbali na eneo hilo. Tukazungumza.
Tulizungumza mambo mengi sana. Ni wakati wa mazungumzo hayo ndipo nilipouona uzuri maradufu wa binti huyo ambaye alinikumbusha jina lake kuwa anaitwa Tayana, Tayana Masenga. Hakika siku zote nilitambua ya wazi ni msichana mrembo. Hata hivyo sasa ndio nagundua ni msichana mrembo zaidi kuliko nilivyofikiri, zaidi nilivyomuona mbali kwa mara ya kwanza. Ni mrembo hasa. Alikuwa msichana anayeonekana ana akili nyingi huku akiwa ni mwanamke mwenye kujiamini. Nikagundua pia ni mwanamke anayejua nini anachokifanya. Tukaendelea kuzungumza.

Ni katika mazungumzo hayo ndipo alipoonekana kushtushwa na mabadiliko makubwa niliyonayo. Kiukweli tangu niajiriwe nilibadilika sana. Hata mwili ulianza kujiachia. Huwezi kuniweka kwenye kundi la wanene na pia huwezi kuniweka kwenye kundi la watu wembamba. Nilikuwa mtu mwenye mwili wa wastani. Hakika hakutegemea kunikuta mahali hapo ila kwa kauli yake aliamini kuwa siku moja tutaonana. Nilimuuliza kwanini yupo pale? Alinijibu kuwa yupo pale kwa ajili ya likizo yake ambayo kampuni ilimpa kwa ajili ya kupunguza mawazo. Ni hapo ndipo nilijawa na udadisi wa kujua kipi kilimsibu mpaka apewe likizo ya kuondoa "stress'' Maana si kazi rahisi hata kidogo.

******************
ITAENDELEA

CHANZO : BURE SERIES
 
SEHEMU YA NNE


Hakuniambia, akanijibu si wakati wake, ila siku moja ataniambia. Hakika siku hiyo tuliongea mengi zaidi na baada ya muda tukajikuta tumekuwa marafiki. Baada ya chuki faraja nikatambua. Hata hivyo kuhusu kazi yangu sikumwambia ukweli. Aliponiuliza kuhusu ninafanya shughuli gani kwa sasa? Nilimjibu kuwa nafanya kazi shirika la ndege la Ethiopian nikiwa mfanyakazi ninayehusika na mifumo wa mawasiliano ofisini hapo. Baada ya kutumia masaa machache hapo, sote kwa pamoja tukarejea hotelini.

Urafiki wetu ukadumu na kuimarika sana, kila mahali tulikuwa pamoja. Sasa nikahisi nimepata mwenyeji, mwenyeji binti mrembo. Kwa siku tatu hata wahudumu wa hoteli hiyo walikuwa wanatutania kuwa tumependeza sana kama mtu na mke wake. Maneno hayo yalikuwa yakituingia moja kwa moja ila sote tuliishia tukitabasamu kwa furaha, Tabasamu lenye kumaanisha jambo. Mpaka hapo tulikuwa marafiki tu.
Likizo ilipokuwa inafikia tamati. Likizo ya wiki moja ambayo nilipewa na shirika baada ya kupandishwa cheo kazini na nitakaporejea nirejee katika majukumu mapya. Makubwa zaidi niliyokuwa nayafanya mwanzo. Nilimweleza kila kitu Tayana kuhusu kuisha kwa likizo yangu hivyo nitawajibika kurejea Dar es salaam kuendelea na majukumu yangu ya kikazi.
Uamuzi wangu ulionekana kuwa wa ghafla sana kwake. Nikauona uso wake ukipoteza ile nuru ya furaha niliyoizoea siku zote huku akiachia tabasamu hafifu machoni pake. Nikahisi hakutegemea uamuzi wangu kwa kipindi kile. Kipindi ambacho alianza kusahau kila kitu kuhusu matukio ya maisha yake ya nyuma yaliyopelekea apoteze sio tu furaha yake hata amani ndani ya moyo wake.

Tayana akawaza sana kisha akanijibu kuwa kwa kipindi tulichokuwa pamoja ametambua wazi mimi nina umuhimu mkubwa kwake....ni mimi ndiye niliyemsahulisha na mawazo mengi yaliyopelekea kutaka kufupisha uhai wake hivyo katu hataweza kubaki peke yake yu radhi naye kufupisha likizo yake na kuongozana nami kurejea Dar es salaam kama tu nitakuwa radhi kuongozana naye. Machozi yalionekana yakimtiririka kwenye mashavu yake, nikashtuka! Nikajikuta namuuliza kwanini analia?


Ndipo aliponieleza kuwa alipewa likizo na kampuni kwa ajili ya kupunguza mfadhaiko uliomkumba baada ya kuachana na mwanaume aliyempenda sana. Mwanaume ambaye siku zote aliamini kuwa ndiye atakayejenga nae familia siku za usoni. Mwanaume ambaye siku zote alimuamini na kumpenda. Mwanaume ambaye alimfanya ajisikie mwenye furaha kila wanapokuwa pamoja. lakini kila kitu kilikuja kubadilika ndani ya usiku mmoja tu. Pale mwanaume huyo ambaye alimwambia kuwa kila kitu kati yetu kifikie tamati leo. Tayana hakuwa na namna tena, alilia na kuuliza sababu lakini mwanaume huyo akamjibu hana sababu. Maumivu ya moyoni yakamtawala kwa wakati huo. Mapenzi yakamuumiza Tayana .

Siku mbili baadaye tulikuwa sote mimi na Tayana tulikuwa ndani ya Boti ya Kilimanjaro kurejea nyumbani huku nyuso zetu zikitawaliwa na tabasamu lenye kuvutia sana. mazungumzo yetu yalitawaliwa na vicheko vya hapa na pale. Ni kama tunakutana kwa mara ya kwanza huku kila mmoja akimuhitaji mwenzake, kwa upande wangu halikuwa jambo nililowazia kwa wakati huo. Nikasahau kama tupo safarini. Tena juu ya maji....Safari ikawa fupi ajabu.
Masaa mawili kasoro baadae tuliwasili salama bandarini Dar es salaam. Baada ya kumaliza hatua zote muhimu tuliagana mimi na Tayana. Tukikubaliana kuendelea kuwasiliana kwa kadiri iwezekanavyo. Wakati anapoelekea kupanda gari iliyokuja kumchukua eneo hilo huku macho yangu yakimsindikiza binti huyo ghafla bila kutegemea, Tayana aligeuka nyuma mita chache niliposimama na mita chache iliposimama gari ikimsubiri. Tukatazamana! Macho yetu yakagongana ...macho yakatoa ishara , ishara ya kihisia. Nikatabasamu naye akanijibu kwa tabasamu. Tabasamu lake likanifanya nicheke naye akacheka. Nikampungia mkono kama ishara ya kumuaga kwa mara nyingine tena naye akapokea ishara yangu na kuingia garini.
Nami nilielekea kwenye gari iliyokuja kunichukua na kunipeleka nyumbani kwangu. Mawasiliano yangu na Tayana yaliendelea kuimarika kila siku. Ikafikia hatua siwezi kulala bila kusikia sauti ya Tayana naye pia hivyo hivyo hawezi kulala bila kusikia sauti yangu. Tukaendelea kuwa karibu zaidi huku kila wikiendi tulikuwa tukikutana sehemu mbalimbali.Mpaka kufikia kipindi cha miezi miwili hakuwa anapajua nyumbani kwangu, kila wakati aliniletea ombi la kuhitaji kunitembelea nyumbani kwangu kila mara nilitoa visingizio vingi. Sikutaka apajue nyumbani kwangu kwa wakati huo. Maana nilikuwa naendelea kumalizia ujenzi wa nyumba yangu kisha nihamie hapo na ndipo ningeweza kumkaribisha kwangu. Ndivyo nilivyopanga siku zote. Mpaka kufikia hapo hakuna aliyepata ujasiri wa kumueleza mwenzake hisia zake. Sote tukaacha matendo pekee yazungumze.


Miezi mitatu baadaye tangu kumfahamu na kujenga ukaribu kati yangu na Tayana. Nilikuwa mimehamia nyumbani kwangu. Nyumba yangu haikuwa imekamilika kila kitu kama nilivyotaka ila kwa kiwango ilipofikia haikunizuia kutohamia hapo. Hapo ndipo ndoto yangu ya kwanza ya kumiliki nyumba nzuri ya kisasa ikatimia.Nikasahau matatizo yote ya nyuma. Wakati mwingine nilipokuwa nayakumbuka maisha yangu ya nyuma nilijisikia kuumia sana. "Katu husiyakumbuke ya nyuma maana yanaumiza sana" Nilisikia sauti ikiniambia masikioni mwangu. Kumbuka mpaka kufikia hapo nilishaenda zaidi ya mara moja nyumbani kwa Tayana. Hakika Tayana alikuwa msichana wa kisasa, mwenye kumiliki nyumba ya kisasa katika umri wake ilikuwa jambo gumu kuamini. Zaidi ya hapo nilipigwa na butwaa baada ya kuyaona magari matatu ya kifahari yaliyopaki ndani ya uzio wa nyumba yake. Magari ya ndoto yangu, nilijisemea. Tukio la ajabu likatokea.........

Wiki moja sasa tangu nihamie nyumbani kwangu. Siku hiyo nilikuwa ofisini wakati nilipotembelewa na mgeni bila kutarajia. Nakumbuka ilikuwa mida ya saa tano asubuhi wakati katibu muhtasi wangu alipoingia na kuniambia nina mgeni anayehitaji kuniona nami... je amruhusu kuingia? Kwa sababu siku hiyo nilimwambia katibu muhtasari nahitaji muda mwingi wa kuwa busy na kazi hivyo hasimruhusu mgeni yoyote hasiye wa kampuni kuniona. Nina hakika kwa siku hiyo alitelekeza hilo lakini ilionekana mgeni huyu alikuwa mbishi sana kukubali kuondoka bila kuonana nami. Alisisitiza lazima aonane nami hata pale alipoulizwa je ana miadi ya kuonana na mimi? Mgeni yule alikataa na alihitaji kuonana na mimi kwa dharura.
Bila shaka niliruhusu katibu wangu amruhusu mgeni huyo kuingia ofisini. Ni wakati huo macho yangu yalikuwa yameukazia mlango huku nikijawa na shauku ya kumfahamu mgeni huyo mkorofi hasiyeheshimu kanuni za ofisi. Nilitaka kumuona kwa hamu kubwa macho yangu yakaendelea kuuelekea mlango kwa umakini mkubwa. Ndipo niliposhikwa na butwaa kwa kutoamini ninachokiona mbele yangu. Alikuwa Tayana akiwa ndani ya gauni zuri yenye rangi ya pink iliyomkaa vema mwilini.

Bila kutarajia macho ya Tayana yalitembea maili nyingi na kusambaa kwa kasi ya ajabu na niliyashuhudia yakitua kwenye kibao kilicho mbele ya meza yangu. Kibao kilinitambulisha "Manager Richard Kamba" Ni wakati ambapo macho ya Tayana yakionesha mshangao mkubwa kama mtu hasiye amini kitu anachokiona mbele yake . Nikamuachia tabasamu mwanana na kumkaribisha ofisini kwangu. Ni wakati alipokaa ndipo nilipogundua amepoteza hali ya kujiamini mbele yangu ni kama amepigwa na bumbuwazi . Haraka nilitambua kwanini yupo katika hali ile? Siku zote alinifahamu kama mfanyakazi wa kawaida tu katika shirika hili mpaka muda mchache uliopita ndipo alipotambua hilo hivyo kuja kwake ghafla ofisini na kunikuta mimi ndio meneja wa shirika hili ilibidi ajiulize maswali mengi zaidi bila kupata jibu.

Baada ya maongezi madogo alinieleza wazi hakupanga kuja hapa lakini ilitokea dharura kuja eneo la ofisi yetu akaonelea ni vizuri kunifanyia "suprise" kuja ofisini kwangu na alipata shida sana kufika hapa kwa sababu naliniulizia kama mfanyakazi wa kawaida lakini wote walisema hakuna mfanyakazi mwenye jina hilo zaidi ya meneja wa shirika. "Nikajikuta nafadhaika lakini nafsi yangu ilikuwa ngumu kukubali kushindwa ndipo nilipohitaji kumuona meneja huyo mwenye jina la mtu aliyeniambia anafanya kazi hapa. Nilipokuona wewe ndio meneja wa ofisi hii hakika nilipigwa na butwaa ni kama nisiyeamini kitu".
Maelezo ya Tayana yalinifanya nitabasamu kisha kwa mara ya kwanza nilimuomba nimpe mwaliko wa kunitembelea nyumbani kwangu wikiendi inayokuja. Nilimwambia hapo ofisini si mahali sahihi kuzungumza mambo mengi kati yetu ambayo si ya ofisi. Alinielewa huku akinisindikiza na tabasamu....tabasamu la kihisia! Tabasamu lenye kutuma ujumbe fulani mahususi....Nikang'amua anachomaanisha. Nilimuomba tukutane siku tatu baadae nyumbani kwangu.

=============================================================
Kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu tangu nilipoanza kumfahamu Tayana niligundua vitu gani anavipenda na mambo yapi hayapendi hata kwenye vyakula pia niligundua vyakula anavyovipenda. Siku hiyo ya jumapili nilitayarisha chakula anachokipenda Tayana, chakula hicho nilikiandaa kwa mikono yangu mwenyewe. Binafsi mimi ni mpishi hodari sana jikoni na siku zote nilipenda kupika mwenyewe. Saa sita kamili mchana Tayana aliwasili nyumbani kwangu baada ya kumuelekeza .
Alikuja na gari yake mwenyewe moja kati ya magari yake ya kifahari niliyowahi kuyakuta nyumbani kwake. Alishuka garini taratibu kama malaika fulani hivi ....hakika nakiri Tayana alipendeza sana siku hiyo...uzuri wake uliongezeka maradufu ndani ya gauni fupi lenye rangi nyekundu...Gauni la kisasa ambalo lilivaliwa ndani ya mwili wa msichana mrembo wa kisasa. Sikujali sana. Nilipenda alivyovaa alikuwa "amazing". Kwa mara ya kwanza mimi na Tayana alikuwa ananitembelea nyumbani kwangu, tukasalimiana kisha nikamkaribisha ndani mwangu. Ndani ya nyumba iliyopuliziwa marashi yenye harufu nzuri ya kunukia.Marashi anayoyapenda Tayana siku zote kuyatumia. Niliifanya siku hiyo kuwa maalumu kwa Tayana. Ndivyo nilivyotegemea.
Tulizungumza mengi na Tayana siku hiyo. Aliniuliza mahusiano yangu ya kimapenzi yalivyo. Tangu tulipoanza kuwa karibu hakuwahi nigusia jambo lolote linalohusiana na mapenzi lakini siku hiyo aliniuliza. Jambo hilo katu sikushtuka kwa sababu nililitegemea. Nilimueleza wazi kutokuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa sasa hasa chuki yangu kwa wanawake. Alinishangaa sana kwa kutoamini ninachomueleza. Aliniuliza kwa nini nawachukia wanawake? Ilinilazimu nimueleze Tayana bila kuficha ili apate kunielewa...Nikamueleza....

"Nilikuwa na mwanamke niliyempenda sana wakati ningali chuoni ni baada ya kuwa marafiki tulijikuta tukianzisha uhusiano wa kimapenzi, kila mara alikuwa akiniambia ananipenda sana. Na mapenzi yangu kwake niliyaamini. Na Nilimuamini zaidi aliponiambia anahitaji kujenga familia na mimi. Siku zote nilijenga matumaini makubwa juu yake. Miaka yote mitatu chuoni ilikuwa ya kusisimua sana kati yangu mimi na yeye, marafiki na wanafunzi wenzetu walituchukulia kama mfano mzuri wa mahusiano yao.

Nikajikuta nawekeza pendo langu ndani yake. Ni baada ya kuhitimu masomo yetu, haraka yeye alipata bahati ya kuajiriwa mapema nami ikanibidi nisote kutafuta kazi kwa muda mrefu...ni kipindi ambacho mpenzi wangu alipobadilika sana kitabia hasa baada ya kupata kazi akaanza dharau juu yangu. Miezi miwili baadaye alinitumia ujumbe kwenye simu yangu kuwa mahusiano yangu mimi na yeye yafikie tamati, aliniomba msamaha kwa kunipotezea muda wangu mwingi pia alinieleza wazi sikuwa mwanaume wa ndoto yake. Kwangu mimi alikuwa nami ili kupoteza muda na sasa amepata mwanaume wa ndoto yake. Alinieleza anatamani kubadilisha historia kati yangu mimi na yeye....anajutia uamuzi wake wa kuwa nami kimapenzi. Maneno yake yakaniumiza sana siku hiyo ilikuwa ghafla bila kutarajia...Mvulana mimi nikachanganyikiwa"
Jambo moja ambalo nililiamini.....Kila jambo hutokea kwa sababu, hili pia lilikuwa sababu. Sikutaka kupigania pendo langu kwake kwa sababu aliniambia ukweli..ukweli wenye kuumiza. Tangu wakati huo nilianza kuwachukia wanawake sikuwa na hamu tena ya viumbe hao. Niliyapigania maisha yangu kwanza.Lakini pia sikuweza kumsahau msichana huyo.Kwa ufupi nilimaliza kumuelezea Tayana mahusiano yangu yaliyopita.Muda wote Tayana alikuwa kimya akinisikiliza huku akiniangalia usoni kutambua ukweli wangu.Bila kutarajia....Nilimuona akinifuata mahali nilipo...nami nikasimama.....ujasiri umemuingia wakati huo Tayana.

ITAENDELEA

CHANZO : BURE SERIES
 
SEHEMU YA TANO ................ MWISHO


Aliponikaribia niliyaona macho ya Tayana yakimaanisha kitu..macho ya upendo huku mdomo wake ukihitaji kusema kitu ni kama ameshikwa na kigugumizi....Tukasogeleana!...Tukatazamana!....Tukajikuta tunakumbatiana. Kumbatio lenye kufungua ukurasa mpya wa urafiki...nikapigwa na bumbuwazi...nikapoteza kumbukumbu nzuri na kuwaza ni lini hasa mara ya mwisho mimi kukumbatia ama kukumbatiwa na sio tu kukumbatiwa na binti, binti mrembo? Nilihisi mwili wangu umepigwa na shoti ya umeme...shoti iliyokuwa inasambaa mwilini kwa wakati huo....akili haikutaka..zaidi ilikuwa uzoefu wenye kuvutia sana. " Nakupenda Richard, nakupenda sana Richard natamani uwe mume wangu Richard hata sasa" Alinitamkia Tayana bila woga. Nikashtuka!.... Nikavutwa! nikavutika! kizuri hapa ni kwamba tayari mimi nilishapenda tangu siku ya kwanza nilipomuona. Nikamjibu nampenda pia .....Tukaachiana.....
Tayana akaniita.."Richard? Nataka kukukabidhi moyo wangu, tangu sasa nakukabidhi moyo wangu siwezi kuendelea kuumiza moyo wangu...sitaki kuhisi nakupenda...nataka kukwambia nakupenda Richard. Hichi nilichokuwa nacho kitakuwa kwa ajili yako peke yako, naapa sitampa mwingine sitakuumiza na naomba husiniumize Richard..tazama ujasiri niliouonesha Richard kwako?....Ni wanawake wachache wenye ujasiri kama wangu wa kumtamkia mwanaume hisia zake..tafadhali kubali ombi langu Richard...Husinikatili Richard, mimi ni kiumbe dhaifu mbele yako Richard."
Nilimtazama Tayana kwa mshangao...nilivutiwa na ujasiri wake....bila kuchelewa nilimjibu...'Too late Tayana'...Nikamuona Tayana akishangaa! uso ukapoteza tabasamu lililokuwepo...nikagundua!.."sivyo ufikiriavyo Tayana" Nilimueleza.....akabakia ameshikwa na mshangao wenye taharuki! ... Nilikupenda tangu siku ya kwanza nilipokutia machoni Tayana. Nilipokuona siku ile kwa mara ya kwanza mwili wangu ulinisisimka na nikajua huyu ndiye mwanamke niliyekuwa namsubiria. Mwanamke wa ndoto yangu. Hata hivyo siku ile nilifikiri kama jambo hilo lisingewezekana milele...tofauti yangu na yako ilikuwa kubwa. Nikasahau mapenzi yana mambo mengi...mapenzi ni kama sanaa ambayo unaweza kuyatengeneza ukiamua karibu ndani yangu Tayana.....Sitakuumiza..nitakulinda Tayana. I don't know what happened........Hakika Tayana alivutiwa na mapishi yangu niliyomuandalia siku hiyo...

==============================================================
Miezi sita baadaye mkono wangu wa kiume ulikuwa umemshika Tayana pembeni yangu ndani ya kanisa ya St Joseph tukielekea kwenye antare kwa ajili ya kiapo cha ndoa....ndani ya kanisa hilo lililojaa pomoni....furaha ilinitawala kila nilipowaona wazazi wangu wakifurahia......nawatazama marafiki wakinishangilia...najikuta nikiamini mimi ndiye mwanaume mwenye furaha kuliko wote Duniani. Tayari ninaye mkononi mwangu mwanamke mrembo anayeenda kutimiza ndoto zangu. Ndoto ya kuwa na mke mzuri....mke mrembo mwenye kujivunia kwa marafiki. Baada ya kula kiapo nikamgeukia Tayana ambaye sasa ni mke wangu rasmi nikamwambia; " Uwepo wa mmoja haukamiliki mpaka uwepo wa mwenza..asante moyo..asante moyo kwa kupenda" Mwanamke aliyenipatia Mungu.
Mwisho wa Richard....Twende kwa Tayana naye tumsikilize kwa ufupi...ana lipi ambalo anahitaji jamii ijifunze kupitia yeye

Simulizi hii ni ya ukweli mtupu ila majina halisi yamefichwa kwa sababu maalumu....ni baada ya kumsikia Richard ilibidi nifunge safari hadi kigamboni mahali ambapo Richard anaishi sasa. Nimeikuta familia yenye furaha sana..nikikaribishwa kwa uchangamfu wa hali ya juu. Nipo kwenye ukumbi mdogo uliotengwa mahususi kwa ajili ya wageni kama mimi..mbele yangu kwenye sofa amekaa Mr Richard na kwenye sofa la upande mwingine amejimwaga Tayana huku pete ya dhahabu inayoonekana ya thamani kubwa iking'aa kidoleni mwake sasa mke wa Richard.....uwanja ni wa Tayana sasa......Tayana kwa ufupi sana anaeleza;


Nilizaliwa kwenye familia ya wazazi wasomi, wenye kujua nini maana ya familia. Mama yangu alikuwa daktari katika moja ya hospitali za rufaa nchini. Huku Baba yangu alikuwa mtumishi wa wizara ya fedha. Mama yangu na Baba yangu siku zote walikuwa wakinuia pamoja. Walipendana na kutulea kwenye misingi ya ucha Mungu na upendo wa hali ya juu. Tulijikuta sisi tukiwa watoto wenye heshima na adabu sana kiasi ambacho kikapelekea kusifiwa na jamii iliyotuzunguka mimi na kaka yangu. Sote wawili tulipenda imani yetu, tulipendana sana sisi kwa sisi kwa vile tulikuwa tumelelewa kimaadili kila mmoja alipata elimu nzuri. Kaka yangu alihitimu shahada ya mawasiliano ya umma katika chuo kikuu cha Nairobi kisha akaanza kusimamia biashara za familia. Mimi nina shahada ya Human resource kutoka chuo kikuu Mzumbe.
Miezi michache kabla ya kutunukiwa shahada yangu.....pigo kubwa katika familia yetu ikatufikia. Baba na mama yangu walifariki kwa ajali ya gari maeneo ya Tegeta wakati wakitoka kutembelea shamba ya familia yetu lililopo Bagamoyo nje kidogo ya mkoa wa Dar Es Salaam. Baba yangu alikufa pale pale huku mama akifia mikononi mwangu Hospitali ya Muhimbili baada ya kufikishwa hapo wakijaribu kuokoa maisha yake.

Kifo cha wazazi wangu Ilikuwa pigo kwangu na pigo la familia yetu. Baada ya kumaliza msiba wa wazazi wetu ilimlazimu kaka yangu achukue majukumu ya kusimamia mali za wazazi wetu ikiwemo kampuni ya usafirishaji. Na baada ya kumaliza chuo nikajiunga kufanya kazi kwenye kampuni yetu kama afisa wa Rasilimali watu yaani HR.
Siku moja nilikuwa nimetoka kuchukua nyaraka kwa mwanasheria wa kampuni yetu.....sikumbuki siku yenyewe ila bado kumbukumbu ile ingali ipo kichwani mwangu.....niligongana na Richard kwa bahati mbaya naweza kusema hivyo sasa. Kwa kipindi kile nilichukulia kuwa alifanya kusudi....inawezekana Mungu alipanga tukio lile liwe chanzo cha familia hii. Maneno yangu hayakuwa mazuri kwa Richard.....naumia nikikumbuka maneno yale..najutia kosa lile mpaka kesho.....nisamehe sana mume wangu nakiri nilifanya makosa makubwa mbele yako Richard.
Nilimuona Tayana akitiririkwa na machozi huku akiyapangusa kwa utulivu husio na shaka...ndipo alipotufanya sote tupigwe na mshangao.....aliendelea kueleza Tayana...

Nilikutana kwa mara ya pili na Richard ni wakati alipokuja kufanya usaili kwenye kampuni yetu. Katika kampuni ambayo mkurugenzi ni kaka yangu tumbo moja....Nilikuwa na maamuzi makubwa katika bodi ya kampuni. Nilimfanyia usaili Richard alionekana mvulana mwenye akili na mwerevu sana....alistahili kuajiriwa kwenye kampuni yetu na leo nakiri mbele yako...ulishinda usaili ule Richard lakini kwa wakati ule nilikuchukia sikutaka uwe sehemu ya wafanyakazi wa kampuni yetu kutokana na uadui uliojitokeza kati yetu. Ni mimi ndiye niliyeliondoa jina lako baada ya kupendekezwa na kwa alama nyingi na mwezangu.
Nikamuona Richard akitikisa kichwa kama ishara ya kuumia moyoni mwake.....inaumiza hakika
....Tayana akaendelea kuhitimisha...
Naomba unisamehe sana Richard...sikuwa natambua nikifanyacho kwa wakati huo. Leo naamini kila kitu kilichokuwa kinatokea kati yangu mimi na wewe kilipangwa kwa sababu maalumu...husichukie kwa kile nilichokutendea mume wangu. Nafikiri kama ungeajiriwa kwenye kampuni yetu ingekuwa vigumu mimi na wewe kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi. Ulipoteza kazi na ukapata kazi pia ukanipata mimi Richard. Yote haya hayakuja kwa bahati mbaya....Mungu alituonesha kupitia matukio yale na kuyatenda sasa. Nakupenda kuliko nilivyofikiria..nisamehe sana Richard.....
Nimefahamu historia yako ya mahusiano yako yaliopita Richard lakini kwa upande wangu niliwahi kukueleza kwa ufupi sana mahusiano yangu yaliyopita na hata hukuwahi kuhitaji nikueleze kwa kirefu nachukua nafasi hii kukueleza ili moyo wako uwe na amani siku zote mume wangu.
Nilikuwa na mvulana niliyempenda sana. Hakuna namna bora ya kuelezea machungu yangu aliyonisababishia kisha nikaeleweka. Nilimpenda sana Patrick, nilimpenda Patrick ilifikia wakati nikaamini atakuwa mwangaza bora katika maisha yangu. Niliamini yeye atakuwa nuru iangaziayo amani na furaha ndani ya moyo wangu. Katika kipindi cha furaha na huzuni. Mwisho aliniacha na kwenda kuoa mwanamke mwingine huku angali bado na mahusiano nami, ukatili husio na mfano. Jambo hilo likanifanya nichanganyikiwe kwa kiasi kikubwa.

Kwa ajili yake nimelia sana na ilikuwa ngumu kuamini kilichotokea na sikujua maisha yangekuwaje bila yeye..sikuona sababu ya kuendelea kuishi katika Dunia hisiyo na huruma ndani yake huku Patrick akifurahia maisha na mwanamke mwingine..Patrick alioa mwanamke mwingine angali bado yupo na uhusiano nami huwezi kuamini, Patrick aliniambia tuachane siku moja kabla hajafunga ndoa...ukatili husio semeheka...nikafikia maamuzi ya kunywa sumu....sumu ilikuwa suluhisho sahihi kwa wakati ule ili kuondokana na kadhia hii. Bahati nzuri dakika chache baada ya kunywa sumu rafiki yangu aliwasili nyumbani kwangu bila kunitaarifu ujio wake. Mpaka leo sifahamu kwanini alikuja kwangu kwa wakati ule.....ndipo nilipowahishwa hospitali....nilinyonywa sumu yote iliyokuwa inasambaa mwilini mwangu.
Kaka yangu alipigania maisha yangu kwa nguvu zote naweza kushukuru kwa hilo. Baada ya kupata nafuu nilipandishwa kizimbani kwa kosa la kujaribu kutaka kujiua.... Mwishowe nilihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita ni baada ya mwanasheria wetu kufanya kazi kubwa kuishawishi mahakama. Kisha nikapelekwa kwenye vituo vya ushauri Nasaa kwa washauri waliobobea katika masuala saikolojia na mahusiano ya kimapenzi ni hapo ndipo nilipojihisi kuwa kitendo nilichokuwa nataka kukifanya ni cha kipuuzi. Baada ya yote hayo nilipewa mapumziko ya wiki mbili katika kisiwa cha Zanzibar. Kaka yangu alinipeleka Melia hoteli ni huko ndiko historia yangu ilipobadilika. Ndipo mahala huzuni yangu ilipoishia na ndipo ambapo furaha yangu ikaanzia.
Wakati Tayana anamalizia kueleza simulizi yake, mume wake Richard hakuwepo sebuleni hapo......sikumbuki ni muda gani aliondoka? maana nilizama kwenye simulizi ya Tayana ila nafikiri wakati Tayana anamuelezea Patrick ndipo alipoondoka Richard...Ni wakati ambapo Tayana ananyanyuka na kumfuata Richard alipo....punde wote kwa pamoja wanarejea sebuleni...nabaki nawatumbulia macho yenye udadisi mwingi... Tayana mbele yangu anampigia magoti mumewe....
Richard mume wangu....ukweli nakupenda sana. Bila wewe mimi si kitu...Maneno na matendo yako yamenipa ujasiri wa kuamini sikuwa nimekosea kukupendekeza katika maisha yangu. Najua utakuwa malaika na waridi wa moyo wangu. Kila ninapokufikiria moyo wangu unakuwa ukifarijika kwa furaha na kuburudika kwa shauku ya kukuona kila wakati. Nakuona kama jicho au roho yangu. ingawa sina uwezo mkubwa mume wangu nitahakikisha kila ulichodhamiria ndani ya ndoto zako zikifanikiwa. Maisha yako yatakuwa yangu na naamini utayafanya maisha yangu kuwa yako.
Kwa ajili ya mapenzi yangu kwako kila muda nitatamani kuwa na wewe nahitaji kukufanya ucheke, ujidai na uone thamani na fahari ya kuwa na mwanamke kama mimi..mwanamke anayekupenda na kukuthamini Richard. Machozi yalianza kumtiririka Tayana..ndipo ambapo Richard aliposogea na kumkumbatia mkewe...kisha akamwambia...

" Wewe ni Mama wa watoto wangu wawili.....nimekusamehe kila ulichonifanyia. Nakupenda sana mke wangu nataka uwe wangu milele yote yamepita mke wangu...ni wakati wa kutuliza hamu zetu kaa kwangu daima, nikupende sana wewe niwe wako daima. Nyakati haziwezi rudi nyuma tugange yajayo mke wangu".

Yote niliyashuhudia yakitendeka mbele yangu. Simulizi yao ni kama tamthiliya fulani yenye kusisimua nikaadhimia kuicheza katika filamu simulizi hii ili jamii yote ipate elimu hii kupitia Richard na Tayana..wakati nikiendelea kuwatazama wapenzi hao wakiendelea kukumbatiana mbele yangu....."Mr and Mrs Richard" hatimaye niliwaita.....wote kwa pamoja waliachiana na kunigeukia huku wakinitazama kwa pamoja....nikatabasamu.....kisha nikawaambia...
"Kila aliye na mahusiano na mtu anayempenda huwa katu hawezi kutamani kumpoteza. Kuwa na mtu unayempenda kwa dhati ni zaidi ya raha ya kawaida unaweza kujikuta muda wote uko na furaha, japo mipango ya maisha yako haijawa ya kuvutia. Faraja na amani utakayoipata kwa kuwa na yule unayempenda kwa dhati huweza kutibu majeraha yaliyopita, hatimaye kuyaona maisha kuwa ni kitu bora cha kufurahisha" nikawaona wapenzi hao wakitazamana huku wametabasamu......falsafa wasiojua nilichomaanisha.....

Mlio wa mlango unaosukumwa ukatufanya sote tuyaelekeze macho yetu mlangoni kushuhudia kiumbe kinachoingia........watoto wawili mapacha wenye jinsia tofauti wenye umri kati ya miaka 2-3 walikuwa wanaingia eneo hilo huku yule wa kiume akimkimbilia mama yake na yule wa kike akienda kutua kifuani mwa baba yake. Tukio lenye kusisimua.....Bila shaka hawa ni watoto wao kutokana na mfanano wao..sikutaka hata kutambulishwa kwa jinsi walivyo fanana na wazazi wao....Atimaye wakanitambulisha watoto hao yule wa kike aliitwa Nadia nafikiri Richard alitaka kumuenzi Nadia binti wa ajabu aliyemlipia nauli kwenye bus huku yule wakiume akiitwa Johnson kwa heshima ya marehemu mzee Johnson Ndeluma"
Ilinilazimu kuwaaga na kuondoka....wakati namalizia ngazi ya mwisho ili nitoke nje nikakumbuka kuna jambo sijalisema ambalo nilitaka niwaambie nikarejea haraka ndani nikawaita kwa mara nyingine "Mr and Mrs Richard"......Naomba niwaambie siku zote watu hujifunza kwa mifano. Mifano huwakilisha kwa ustadi wa hali ya juu hisia na hali halisi ya jambo fulani kwa tafsiri maridhawa. Kukutana kwenu ilikuwa katika namna ya tafsiri. Na kilichotokea kitakuwa mfano kwa vijana wengi nchini. Asante kwa ushirikiano wenu. Nakuahidi Mr Richard nitafanya kila jitihada, kuwatafuta popote sitachoka kutembea mchana hata usiku ikiwa nitawapata Patrick na Nice nitawakutanisha tena ili muifanye familia zao na yenu marafiki.....tafadhali kubalini ombi hili..... "Bila shaka" Wote walitamka kama vile walikuwa na mawazo yanayofanana.... Nikacheka! Nikacheka! kwa kupata bahati ya kuifahamu simulizi hii.
Ni mwaka wa tatu sasa....naendelea kuwatafuta Nice na Patrick ili nitimize agano langu.....sijapata hata fununu za watu hawa walipo....najua simulizi hii itasomwa na watu hao bila shaka mtakapoisoma msisite kuwasiliana nami nahitaji kufahamu ukweli wenu....ukweli husiosahaulika.

Mwisho.

AHSANTENI SANA KWA KUWA NASI TANGU MWANZO MPAKA MWISHO WA KISA HIKI CHA KWELI. TUNATUMAI KUWA MTAKUWA MMEJIFUNZA JAMBO KWENYE KISA HIKI. TOA MAONI YAKO


CHANZO : BURE SERIES
 
Asante sana kwa hadithi nzuri. Inatufunza tusikate tamaa. Richard alisota mwisho alipata kazi. Na unaweza kuumizwa kimapenzi baadae ukampata mtu bora zaidi
 
Asante sana kwa hadithi nzuri. Inatufunza tusikate tamaa. Richard alisota mwisho alipata kazi. Na unaweza kuumizwa kimapenzi baadae ukampata mtu bora zaidi
Pamoja sana mkuu
 
Siku zote naamini sana katika kuipa moyo nafasi ya kusubiri hasa unapofikia hatua ya mahusiano ya kimapenzi. Simulizi ni tamu saan na nimejifunza kitu kikubwa saana. In god we trust na kwake hakuna kisicho wezekana na jina lake lihimidiwe. Hiyo familia bila shaka mungu ameiwekea ngao ambayo hakuna adui yoyote toka njee ataweza kuitingisha kamwe.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom