Siri za Rais Mstaafu Kikwete na Singasinga wa IPTL zafichuka

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
SIRI kati ya Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete na Harbinder Singh Sethi (Singasinga), aliyekwapua mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Tegeta Escrow, zimeanza kuvuja.

Mabilioni ya shilingi yaliyochotwa katika akaunti ya Escrow, ndani ya Benki Kuu (BoT), yalitoroshewa nchini Austria, kupitia Afrika Kusini na Dubai, MwanaHALISI linaweza kuripoti.

Mkakati wa kukwapua na kutorosha mabilioni hayo, ulisukwa kwa ustadi mkubwa na Singasinga kwa kushirikisha vigogo waandamizi serikalini na Ikulu.

Vyanzo vya taarifa kutoka serikalini na Ikulu vinasema, Sethi "alitoa rushwa kila mahali, ikiwamo Ikulu," ili kufanikisha mpango wake huo.

"Alihonga kila mtu. Alitoa rushwa kwa kila aliyeona faili la Escrow. Hadi maofisa wa Ikulu na viongozi waandamizi serikalini walihongwa," ameeleza mmoja wa viongozi waandamizi kutoka wizara ya fedha.

Amesema, "…hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga alitembeza mlungula. Ni BoT pekee, ambako hakuhonga au kuombwa rushwa."

Kampuni ya IPTL – Independent Power Tanzania Limited – ilijifunga katika mkataba na serikali wa miaka 20, wa kuzalisha megawati 100 za umeme wa dharura na kisha kuuza umeme huo kwa shirika la umeme la taifa (TANESCO).

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa mwaka 2004 baada ya serikali kubaini udanganyifu katika gharama za ununuzi wa umeme na mtaji wa IPTL.

Kampuni hiyo binafsi ilidai kuwa gharama za umeme zilikuwa asilimia 22.3; na gharama za mtaji asilimia 30 zilikuwa dola za Marekani 38.16 milioni. Hata hivyo, Mahakama ilithibitisha kuwa gharama halisi za mtaji wa IPTL, zilikuwa chini ya dola za Marekani 1,000.

Hadi Novemba 2014, akaunti hiyo ilikuwa imehifadhi zaidi ya dola 120 milioni. Mamilioni hayo ya dola yaligawanywa mithili ya "shamba la bibi" kwa aliyejiita mwekezaji mpya wa IPTL, kampuni ya Pan African Power (PAP).

Mabilioni ya shilingi yalilimbikizwa na Tanesco, katika akaunti hiyo, baada ya kuibuka mgogoro juu ya malipo ya gharama ya uwekazaji wa mitambo na gharama za kuweka mitambo (Capacity Charge), kati ya IPTL na Tanesco.

Lakini fedha hizo zilichotwa kabla mgogoro huo haujapatiwa ufumbuzi na katika mazingira ya udanganyifu; na kwa kutumia baadhi ya nyaraka ambazo zilikuja kugundulika kuwa ni za kugushi.

Sethi aliwasilisha serikalini nyaraka zinazomuonesha kuwa ndiye mmiliki mpya wa IPTL. Alidai kuwa amenunua kampuni hiyo kupitia kampuni yake ya Pan African Power (PAP).

Hata hivyo, Sethi alishindwa kuweka uthibitisho wowote kuwa kampuni hiyo inamiliki hisa za kampuni ya Mechmar Limited ya Malaysia ndani ya IPTL.

Kampuni ya Mechmar inamiliki asilimia 70 ya hisa katika IPTL. Mmiliki mwingine, ni VIP Engineering ya jijini Dar es Salaam, iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa.

Jitihada za kupata viongozi serikalini wakiwemo wa Wizara ya Fedha, zimeshindikana. Na simu ya Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile iliita kwa muda mrefu mara kadhaa bila kupokewa.

Taarifa zinasema, Gavana Ndullu alichukua tahadhari zote juu ya fedha hizo, ikiwamo kumjulisha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi, Dk. William Mgimwa (sasa marehemu), umuhimu wa kumjulisha Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu malipo hayo.

Anasema mtoa taarifa, "Kwa kuwa BoT ilipewa jukumu hili kwa makubaliano, uwajibikaji wake na mipaka ya uwajibikaji huo unabaki kuwa ni uleule ulioelezwa katika makubaliano hayo."

Lakini gavana anaripotiwa kwenda mbali zaidi, akitaka kupata hakikisho kwamba utekelezaji wa uamuzi wa mahakama, pamoja na makubaliano ya kukabidhi fedha, unapata baraka za wakuu wa nchi kama vile Rais na Waziri Mkuu.

"Pia BoT ilihakikisha kwamba mahitaji yote ya msingi kama vile, makubaliano ya kuhamisha fedha, kinga dhidi ya madai au mashitaka baada ya malipo, na suala la kodi ya ongezeko la thamani (VAT), vinapata ufafanuzi, baraka na mwongozo unaostahili," ameeleza mtoa taarifa.

Anasema BoT iliamua kuchukua hatua hizo, ili kujinasua na madai mapya ambayo yangeweza kuibuka baada ya fedha kuhamishwa kutoka benki.

"Gavana alimkatalia Dk. Mgimwa kuchukua fedha mpaka kwanza amjulishe rais. Alikataa hata maelekezo ya mwanasheria mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema, aliyetaka fedha hizo zilipwe, hata bila benki kujihakikishia usalama wake," ameeleza ofisa wa serikali.

Kwa mujibu wa nyaraka, BoT ilihamishia mabilioni hayo ya shilingi kwa PAP kupitia akaunti yake iliyoko benki ya Stanbic baada ya Sethi, anayedai kuwa mmiliki wa IPTL, kumuelekeza gavana.

Waraka wa Sethi kwenda kwa gavana Ndulu ulielekeza fedha hizo kulipwa kwa akaunti Na. 9120000125324, iliyopo benki ya Stanbic, tawi la Tanzania.

Sethi alimwandikia gavana tarehe 28 Novemba 2013, zikiwa siku 37 (21 Oktoba hadi 28 Novemba 2013) tangu mkataba kati ya serikali na PAP kufungwa.

Mkataba wa upelekaji fedha katika akaunti ya Escrow ulifungwa tarehe 21 Oktoba 2013.

Malipo hayo kwa PAP yalifanyika bila Waziri wa Nishati, Prof. Sospeter Muhongo, wala BoT kuhakiki uhamishaji wa hisa kutoka Mechmar kwenda PAP; bila PAP kusajili hisa zake nchini; bila PAP kuthibitisha kujisajili Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC); na bila kuwa na hati ya mlipa kodi (TIN).

Mkataba kati ya serikali na IPTL ulielekeza fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow, zilipwe kwa kampuni ya PAP kupitia tawi la Tanzania la United Bank Limited (UBL) – yenye matawi zaidi ya 1,300 katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Qatar, Yemen, Marekani, Pakistani, Uingereza, Uswisi, Oman, China na Tanzania.

Mkataba huo uliagiza fedha hizo zilipwe kupitia akaunti mbili za PAP; ambazo ziko katika benki ya UBL; hizo ni zile zenye Na. 010-0016-0 – ambayo ni ya fedha za Tanzania na 060-0016-7 ya dola za Marekani.

Hata hivyo, gazeti hili limeelezwa kuwa kilichofanya fedha hizo kutolipwa katika akaunti ya UBL, ni kukosekana kwa fedha katika Akaunti ya Escrow.

"Serikali ililazimika kukopa "kwa siri" kiasi hicho cha fedha kutoka Stanbic kwa kuweka dhamana ya hati fungani, ili kufanikisha upatikanaji wa fedha za kumlipa Singasinga wa IPTL," ameeleza mmoja wa maofisa wa Stanbic ambaye ametoka katika benki hiyo hivi karibuni.

Anasema, "…fedha zote zilizopaswa kuwepo, kiasi cha dola 122 milioni, zilikuwa zimewekezwa na BoT na kiasi kingine cha dola128 milioni, zilikuwa hazijawasilishwa na Tanesco kwa muda mrefu."

Taarifa zinasema, BoT iliwekeza dola za Marekani milioni 22 nchini Ufaransa na Sh. 148,071,613,572.93 iliwekeza katika Hati Fungani (Treasury Bills) za siku 182 .

Kigogo huyo anasema, "kwa vile wakubwa walishapanga kumlipa Sethi, kabla ya kumalizika Desemba 2013, ikabidi wakope benki kwa kuweka dhamana hati fungani zilizoshushwa bei (discounted treasury bills)."

Anasema, katika muhamala huo, Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania, ilitengeneza faida ya kitita cha dola za Marekani 18 milioni (Sh. 39 bilioni).

"Ile haikuwa biashara ndogo kwa benki. Yaani siku moja, unapata biashara inayokupa faida ya dola 18 milioni. Hizi ni fedha nyingi sana; na ambazo hakuna benki ambayo inaweza kuziachia," anaeleza.

Anasema, "kile ambacho kinaniumiza moyoni, ni kuona taifa linakopa ili kumlipa mtu ambaye mpaka leo kuna utata juu yaumiliki wake katika IPTL."

Taarifa zinasema, katika kiasi hicho cha dola 180 milioni, dola takribani 100 milioni, kilitoreshewa nje katika nchi za Falme za Kiarabu, huko Dubai na Afrika Kusini, kabla ya kuhamishiwa tena nchini Austria.

Nchini Austria, taarifa zinasema, ndiko ambako mtoto wa mmoja wa waliokuwa viongozi wajuu serikalini, amefungua akanuti.

Anasema, "Austria ndiyo imechukua nafasi ya Uswisi…nchi hiyo haina mkataba wa aina yoyote wa kuibana kufichua taarifa za kibenki za wateja wake na ndiyo maana fedha zilipelekwa huko."

Anasema, taarifa za kukopa fedha ili kumlipa Sethi na PAP zilifanywa kuwa siri kwa hofu kwa vile taratibu nyingi zilikiukwa, hali ambayo ingeweza kuibua tena mjadala mwingine juu ya sakata la Escrow.

Anasema, "mnachokiona kwenye maandishi ni nyaraka tu toka BoT kwenda kwa Sethi; fedha zilitoka Stanbic kwa makubaliano maalumu ya kuuziana hati funganizi lizoshushwa thamani."

MwanaHALISI limeelezwa kuwa katika mradi huo, Benki ya Stanbic, ili kufanikisha ukwapuaji wa dola milioni 250 (Sh.550 bilioni), ililazimika kupata baraka kutoka makao makuu nchini Afrika Kusini.

Kibali kutoka nchini Afrika Kusini, kimesainiwa na Bw. S. J Kok ambaye ni mkuu wa hazina wa kanda ya Afrika Mashariki na Malcom Low.

Fedha ambazo zilichotwa kwa njia ya uuzaji wa hati fungati, zingetosha kununua madawati milioni tatu na nusu (yanayohitajika nchi nzima); na kiasi kingine kujenga barabara ya urefu wa kilomita 50, kingebakia mikononi mwa serikali.

Taarifa hizi zinakuja kukiwa na kigugumizi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufikisha mahakamani watuhumiwa wote wakuu wa wizi katika akaunti ya Escrow, licha ya uchunguzi kukamilika miaka miwili iliyopita.

Mara baada ya mabilioni hayo kuingizwa katika akaunti, kiasi cha dola 70 milioni, Sethi alikilipa kwa Rugemalira.

Kiasi kingine cha fedha kilichosalia, wanufaikaji walikibeba kwa magunia na mifuko ya plastiki.

Baada ya Rugemalira kupewa kiasi alichohitaji, Sethi alibakiza kiasi cha dola 180 milioni, pamoja na mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL aliopewa kama sadaka.

Mbali na fedha hizo, Sethi na PAP wameendelea kulipwa kiasi cha Sh. 6 bilioni kila mwezi na Tanesco.

Sethi ameanza kulipwa mabilioni hayo ya shilingi, tokea Januari 2014, licha ya Bunge kuamuru malipo hayo kusitishwa.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, mkataba wa kugawana fedha kati ya serikali na IPTL, ulisainiwa na Eliakim Maswi. Alikuwa katibu mkuu wizara ya nishati na madini.

Wengine waliosaini mkataba wa uhamishaji fedha, ni Singasinga Sethi na Joseph Makandege, ambaye ni mwanasheria na katibu wa kampuni ya PAP.

Hadi sasa, wote wanne, hawajafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za wizi wa fedha za umma.

Bunge ambalo lilijadili ripoti ya uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lilimtaja Sethi kuwa mhalifu aliyekubuhu; anayepaswa kukamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Vyombo vya habari, ikiwamo mitandao ya kijamii, vimeripoti kuwa Singasinga "alitokea ikulu" kabla ya kukwapua mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya Escrow katika Benki Kuu.

Bunge limeagiza kufanyika taratibu za kisheria, kuitangaza benki ya Stanbic kuwa ya utakatishaji fedha haramu.

Mkataba wa malipo kati ya IPTL na serikali, umeambatana na muhtasari wa kikao cha pamoja cha uhakiki wa malipo ya tozo kati ya kampuni hiyo ya kigeni na Tanesco.

Chanzo: MwanaHalisi
===================

KANUSHO: IPTL yakanusha Tuhuma za Rushwa na Taarifa za Uongo Zilizochapishwa na Gazeti la MwanaHALISI
 
Kuna mengi sana yamejificha ndani ya carpet.

Na ni muda umefika sasa wa yote kuweka juu ya carpet. Wakati wa kampeni CCM walisema kuwa WAPINZANI WATAISOMA NAMBA SASA NAONA WAMEANZA KUISOMA NAMBA CCM. MATUMBO MOTO WANAKOSA USINGIZI.

WANAJUTA KUCHAGUA MAGUFULI KWANI YUPO UPANDE WA UPINZANI KATIKA KULETA MABADILIKO TULIYOKUWA TUNAIMBA WAKATI WA KAMPENI.

HONGERA MWANAHALISI KWA HABARI ZA UCHUNGUZI. WATAISOMA NAMBA MWAKA HUU.

Kitanzi.jpg
Kitanzi.jpg
 
Jamani mzee wa msoga alikuwa anatafuta hela ya kutosha ili akitaka kupanda ndege wakati amestaafu asipate shida ya nauli, nyie mnamjua mzee wetu anavyopenda kupanda ndege
 
Inaonyesha all system ilikuwa corrupt hivyo kutatua tatizo kwa kusite wahusika ni muhimu lakini pia kutafuta kiini cha tatizo kiko wapi.

kama serikali nzima ilihongwa je bunge lilikuwa wapi?

tusiseme tu bunge lilitunga maazimio ya kumuwajibisha fulani na fulani lazima tujiulize bunge lilitimiza wajibu wake au yawezekana kuangalia taratibu zinataka nini then kinafanyika kitu cha kuonyesha fulani katimiza wajibu wake kumbe hakuna kuwajibishana.

tulishuhudia jinsi mahakama iliyotakiwa kutoa haki ilivyokuwa hata ikitumika kuzuia bunge lisijadili????.

tatizo ni nini?

hapa utaona hakukuwa na msimamizi kwa maana ya bunge kusimamia haki, wala mtoa haki kwa maana ya mahakama kuangalia haki za watanzania ziko wapi. bali vyombo vyote vilishirikiana katika kufanya mambo haya.

na kwa msingi huo mimi niliwahi kusema tanzania tuna mhimili mmoja tu kwa maana jinsi mihimili hii inavyoundwa na utendaji wao wa kazi kunawapa nafasi ya vyombo kutekwa ama kutokana na nguvu ya mhimili mmoja kushinda mihimili mingine na hivyo kuona anayekushinda nguvu bora kuungana naye.

nani angemkemea serikali kama wangebaini serikali inafanya mambo haya? kwa nguvu ipi na je kama serikali ingekaidi wangechukua hatua gani? je wana nguvu au ni kuishia kuongea tu.

hawa waliotakiwa pengine kukemea serikali je wengine waliteuliwa na nani? na je unaweza kumteua mtu ambaye atakuja kukuzibia riziki?

je wale ambao hawateuliwi na hao tuliowapa madaraka makubwa je kuna peremende wanaweza kupewa ambazo zinaweza kuwafanya wanyamaze kutokana na peremende mtu aliyopewa jana au anayoweza kupewa kesho? hapa namaanisha nani hataki kuteuliwa kuwa waziri au mkurugenzi au mtu yeyote katika nafasi zilizowekwa katika uteuzi wa wale tuliowapa madaraka makubwa ambaye anaweza kusimama bungeni kusema haya yanayofanyika lazima yakemewe?

tumewahi kujiuliza ni kwa nini wale wasio na nafasi ya kupata teuzi wao wamekuwa mstari wa mbele kukemea na hawa walio na uwezekano yawezekana taratibu zetu zinawafunga midomo kwa kupima kutumikia tumbo au wananchi?

mihimili mitatu haikuwekwa kwa mantiki ya kuweka vitengo tu katika utwala bali iliangaliwa dhana ya ukimpa mmoja mali zako zote aendeshe na kukupa faida je siku moja akikugeuka utamshitaki wapi wakati hakuna kitu kilicho juu yake cha kuweza kumtia adabu?

wazee hao wa zamani waliona hiyo ni hatari sana maana mwenye mali anaweza kugeuka mtumwa.

wakaona suluhisho ni kuunda vyombo vitatu kuviweka juu vyenyewe visimamiane. yaani mayai huweki kwenye kapu moja ili kuhakikisha kapu moja yakivunjika basi kwakuwa tuna makapu matatu makapu mawili yatasaidi. maana kama ni madaraka ukivipa vyombo vitatu madaraka kimoja kikikugeuka basi bado una madaraka kupitia vyombo viwili na unaweza kurudisha mambo kwenye mstari.

sasa sisi watu wa leo ambao tunaamini tuna akili kushinda watu wa zamani maana inaaminika duniani maarifa yanaongezeka kadiri mda unavyokwenda, tunaunda vyombo hivi vitatu kwa majina lakini mifumo tunayoitumia kuviunda kimantiki kinabaki kuwa chombo kimoja.

matatizo kama haya ya serikali nzima kuongwa ndipo tungeona bunge linarudisha mambo kwenye mstari lakini kwa utaratibu wetu tuliokubaliana kupitia katiba unamfanya bunge kuwa mshirika wa serikali badala ya msimamizi. mahakama ndiye muangalizi wa haki lakini akiwa na jukumu la kumbakizia mamlaka mwananchi ili kukitokea chombo kimengeuka mambo yanadhibitiwa lakini kwa mfumo tuliouweka mahakam ni taasisi ndani ya serikali.

hili tatizo lilikuzwa na muundo wa mihimili ulioko kwenye katiba.

bila kuwa na kichwa cha nchi chenye viungo vitatu kila kimoja kikiwa na madaraka yake kamili katika kufanya kazi na kuwajibika kwa wananchi moja kwa moja upo uwezekano mkubwa wa kichwa hiki kutekwa na mjanja mmoja kwa kutumia peremende.

tuangalie kosa alilolifanya mtoa peremende na waliopokea peremende na kuchukua hatua lakini pia tuangalie sisi wenyewe tulifanya makosa gani yaliyosababisha hakuna hata mmoja aliyekaa upande wetu kipindi hicho wakati tulivitenga vyombo hivyo ili hilo lisitokee na tuchukue hatua pia.
 
JK hamia Ukawa watakusafisha... Nyumbu walimwandama Mzee Lowassa hivihivi mwishowe amekuwa rais wa mioyo yao
Kwa madudu yanayoibuliwa na mshirika wake magufuli, huyo JK wenu hasafishiki hata akienda kujiunga na shetani shetani lazima amkatae maana kamzidi maarifa.
 
Magufuli akirudi toka Rwanda kuna watu wata nyooshwa hapa. Week mbili hizi kuna mambo mengi yameibuka na Magufuli amekuwa kimya. Tusubiri vumbi la Kimbari limuingie vizuri. Ifike mahali tukubali mabadiliko, Na mabadiliko sio kwenye furaha tu bali hata kwenye kuumia na kuwajibishwa kwa faida ya Taifa. Surgeon Magufuli wagonjwa wapo theatre tayari, Rudi mapema ufanye kazi yako..!!!
 
Mi siku hizi siliamini gazeti hilo la mwanahalisi tena, tangu walipotuaminisha kuwa Lowasa ni fisadi ghafla Kubenea akaghairi na kumsifia Lowasa kwenye kampeni! Sina hamu nalo kabisa.
 
Back
Top Bottom