nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,803
Habari
Waandishi Wetu Toleo la 295 22 May 2013
NDEGE yoyote itakayonunuliwa na Wizara ya Uchukuzi, inayoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, inaviziwa kutaifishwa kwa mujibu wa mikataba ya hovyo iliyoandaliwa na mtandao wa mafisadi na mawakala wao, ndani na nje ya nchi, Raia Mwema, linaripoti.
Mchezo huo wa kifisadi unahusisha si tu baadhi ya watendaji waliokuwa wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) bali pia baadhi ya wabunge ambao wakati shirika hilo likiendelea kutafunwa, miongoni mwao walikuwa washauri wakuu wa serikali.
Taarifa za uhakika zinafichua ya kwamba licha ya serikali kuwa na uwezo wa kununua ndege mpya kwa ajili ya ATCL, lakini mazingira ya shirika hilo kwa sasa yaliyowekwa na mtandao huo wa mafisadi na mawakala wao ni pigo kwa nchi.
Kwa muda mrefu sasa Watanzania wamekuwa na kiu ya kuona shirika lao la ndege likifufuliwa kutokana na kujali kwamba ni alama ya utambulisho wa taifa katika jukwaa la kimataifa, lakini kutokana na mazingira hayo ya kifisadi, uwekezaji mpya kwa sasa hautakuwa na tija hadi hapo mtego huo wa kifisadi uliowekwa unasuliwe.
Chanzo chetu cha uhakika cha habari kimefichua kwa kueleza; Ukinunua ndege mpya leo inakamatwa, ikienda safari za nje, hairudi....itakamatwa tu.
Chanzo hicho kinaendelea kubainisha kwa kusema; Baadhi ya viongozi waliomo serikalini pamoja na wabunge waliopata kushika nafasi za juu serikalini ni wahusika wakuu wa kufikisha ATCL hapo ilipo, lakini katika hali ya kushangaza nao leo hii wana ujasiri wa kuhoji serikali kutolifufua shirika hilo.
Taarifa hizo kutoka chanzo chetu cha habari kwa namna fulani zinathibitishwa pia na Waziri Dk. Mwakyembe ambaye ni Mwanasheria wa Shahada ya Uzamivu, pale alipowauma sikio wabunge hivi karibuni wakati wa hotuba yake ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/2014, hasa baada ya baadhi ya wabunge kuhoji sababu za serikali kushindwa kununua ndege mpya.
Katika kuwauma sikio wabunge, Dk. Mwakyembe aliwaambia mazingira ya shirika kwa sasa si muafaka kuingiza mtaji, kwamba serikali hivi sasa inahangaika kulisafisha shirika hilo kwanza, kuweka mazingira mazuri ndipo kuwekeza mtaji mpya.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, deni ni kubwa na mzigo kwa shirika hilo, na sehemu kubwa ya deni hilo halistahili bali lilitengenezwa na uongozi uliopita wa shirika hilo kwa kushirikiana na viongozi wengine ndani ya serikali.
Uthibitisho wa athari za deni hilo kwa uwekezaji mpya ni malipo ya bima ya ndege iliyopata ajali, ikielezwa ya kwamba zaidi ya asilimia 80 ya fedha zilizolipwa na kuingizwa kwenye akaunti za shirika hilo ilikatwa kulipia madeni ya shirika.
Shirika hilo lililipwa dola za Marekani milioni 10 kama bima baada ya moja ya ndege zake kupata ajali, lakini fedha hizo zilipoingizwa tu kwenye akauti za shirika hilo, zilizobaki kwenye akaunti hazikuzidi dola milioni mbili za Marekani, milioni nane zikiwa zimekatwa kulipia sehemu ya madeni ya shirika hilo.
Katika hali ya kuthibitisha kutokuwapo kwa uzalendo miongoni mwa waliokuwa watendaji wa shirika hilo na baadhi ya viongozi wa serikali, miongoni mwa mambo yaliyochangia kuua ATCL ni pamoja na ukodishaji ndege iliyokuwa gereji ikifanyiwa matengenezo, ukodishaji ambao umesababisha deni kubwa linalodaiwa kisheria kwa sasa na kama serikali itatumbukiza mtaji, basi mtaji huo utamezwa na deni hilo pamoja na madeni mengine feki.
Kinachoendelea ATCL
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kinachoendelea kwa sasa kuhusu ATCL chini ya uongozi wa Wizara ya Uchukuzi ni uhakiki wa deni, wahusika na kisha kuchukua hatua madhubuti za kusafisha shirika hilo, ikiwemo akaunti zake kwa kumaliza kwanza ulipaji deni lililohakikiwa, ili hatimaye shirika lianze kazi likiwa halina vikwazo vya uendeshaji.
Katika michango yao, baadhi ya wabunge walifikia hatua ya kuonyesha kujisikia vibaya kwa taifa kubwa kama Tanzania kukosa Shirika la Ndege la Taifa lenye nguvu wakilinganisha na nchi za Rwanda na Burudi, zenye mashirika yanayomiliki ndege.
Sio kwamba nchi kama Burundi au Rwanda zinatushinda.... kupanga ni kuchagua, wao wamechagua ndege na sisi tumechagua barabara, alisikika Dk Mwakyembe akijibu hoja za wabunge hao, huku taarifa za uhakika za Raia Mwema zikithibitisha bila shaka kwamba siri iliyopo ni pamoja na kuogopa ndege mpya zitakazonunuliwa kutaifishwa.
Hata hivyo, katika hatua inayowashangaza baadhi ya wabunge ni kwa baadhi ya vigogo wa CCM waliochangia kuua shirika hilo kuandaa mikakati ya kumdhoofisha Dk. Mwakyembe, wakitajwa kutafuta makosa ya kumhusisha nayo ili aonekana kuhusika na udhaifu uliomo kwenye ATCL na Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Mashirika hayo yalipata kuwa chini ya Wizara ambazo Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, amepata kuziongoza na pia Chenge, kabla ya hapo, amekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Mawaziri wengine kadhaa pia wamepata kuongoza wizara hiyo, ambao ni pamoja na Dk. Shukuru Kawambwa na Basil Mramba.
Njama za bungeni
Kwa upande mwingine, taarifa zaidi kutoka bungeni zinabainisha ya kwamba wakati wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi iliyojadiliwa kwa siku mbili katika Bunge, mmoja wa wabunge alijipanga kuendesha mashambulizi dhidi ya Dk. Mwakyembe wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, na ndiye aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali za juu nchini, ikiwa ni pamoja na kuongoza wizara hiyo.
Lakini katika hali iliyowashangaza wengi, alitoka nje ya ukumbi mara baada ya jina lake kutajwa kuwa miongoni mwa wachangiaji, na hata siku ya pili alipotajwa tena hakuchangia na badala yake, alionekana akionyesha ishara ya mikono kwa Mwenyekiti wa Bunge aliyekuwa akiongoza kikao cha siku hiyo, akiashiria kutokuwa tayari kuchangia.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya Bunge zinabainisha kuwa, hatua ya mbunge huyo kukwepa kuchangia ilitokana na hofu ya kuumbuliwa na madudu aliyoyafanya akiwa kwenye wizara hiyo, hii ikiwa ni baada ya kufahamishwa ya kuwa mkakati wake umeshitukiwa.
Kuvuja kwa mkakati huo unaohusishwa na harakati za urais mwaka 2015, na kati ya wanaoshirikiana kutaka kumhujumu Dk. Mwakyembe wakati wa mjadala wa bajeti yake ni pamoja kigogo wa Bodi ya Shirika la Reli Tanzania.
Kukwama kwa mkakati huo, ilikuwa ni kama vile mwendelezo wa kukwama kwa mikakati kadhaa iliyoandaliwa kumdhalilisha Dk. Mwakyembe wakati wa kujadili hotuba ya wizara yake.
Mikakati ya awali iliyokwama ni pamoja na ule wa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba ambaye taarifa yake ilikataliwa na wajumbe wake na kushinikiza iandaliwe upya na kamati ndogo.
Tangu asimamie Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la kashfa ya Kampuni ya Ufuaji Umeme ya Richmond, iliyosababisha Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu, sambamba na mawaziri wengine wawili, Dk. Mwakyembe amekuwa akipitia misukosuko kadhaa ikiwamo ya kiuongozi.
Misukosuko hiyo ni pamoja na ajali iliyotajwa kusababishwa kwa makusudi na lori dhidi ya Mwakyembe kwa wakati huo akiwa safarini kutoka Kyela kwenda Dar es Salaam, eneo la Ihemi, kilomita 40 kabla ya kufika Iringa Mjini.
Katika ajali hiyo iliyotokea Mei 21, mwaka 2009, Dk. Mwakyembe alikimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Iringa na baadaye kusafirishwa kwa ndege hadi Kitengo cha Mifuta, Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Utata katika ajali ulikuwa kati ya maelezo ya Polisi chini ya Mkuu wa Polisi Mkoa wa Iringa, Advocate Nyombi aliyesema ajali hiyo ilitokana na shimo lililokuwapo barabarani lakini Meneja wa Wakala wa Barabarani (Tanroad) Iringa, Paul Lyakurwa alishangaa na kusema shimo hilo la nchi mbili, haliwezi kusababisha ajali yenye madhara kiasi hicho.
Oktoba, 2011 Dk. Mwakyembe pia amejikuta akiugua ugonjwa wa ajabu, akivimba mwili na ngozi yake kuota magamba, nywele kupukutika sambamba na kucha, kwa wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, alipelekwa nchini India kwa matibabu ya miezi kadhaa.
Katika masuala ya kiongozi, amekuwa akipata misukosuko mbalimbali ikiwamo mivutano ambayo ni pamoja na kati yake na aliyepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile.