Siri kali kwa kupindisha ukweli...

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,109
ndio yenyewe!...au kulikuwa na ripoti nyingine ya REDET ambayo hatukuiona!? Kwa nini hawa wanasiasa hawataki kuukubali ukweli bali wanaupindisha ili kukidhi nafsi zao!? :(

Serikali: Matokeo REDET safi

na Ratifa Baranyikwa
Tanzania Daima

SERIKALI imesema ripoti ya utafiti uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), imeonyesha kuwa watu wengi wanaridhika na utendaji wa Serikali na Rais Jakaya Kikwete kuliko inavyoelezwa na baadhi ya watu.
Tamko rasmi la serikali kuhusu ripoti hiyo ya Redet lilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib mbele ya waandishi wa habari.

Waziri Khatib katika tamko lake hilo alisema, matokeo hayo ya Redet yameonyesha pia kwamba, watu wanaoridhika na utendaji wa kazi wa serikali wanafikia asilimia 79.4, unapochanganya wale waliotengwa katika makundi mawili ya wanaoridhika sana na wanaoridhika kiasi.

Khatib alisema serikali imelazimika kutoa tamko hilo sasa baada ya kuwapo kwa maoni tofauti ya wananchi tangu Redet, walipotoa maoni yao hayo wiki mbili zilizopita.

Akizungumzia juu ya utafiti huo ambao lengo kubwa ni kuboresha utendaji wa shughuli za serikali na kuleta maendeleo kwa watu walio wengi na kuimarisha demokrasia nchini, Khatib alisema kuwa, kwa mujibu wa utafiti huo, serikali ya awamu ya nne imeona imepata mafanikio makubwa katika miaka miwili ya mwanzo ya uongozi wake wa miaka mitano.

Katika hilo, Khatib alisema kuwa katika uchambuzi uliofanywa na serikali, neno ridhika ambalo limetumiwa kuwahoji wananchi kutoa tathimini juu ya utendaji wa serikali ambalo lilitengwa katika vipengele vitatu, ambavyo ni ‘Naridhika sana’, ‘Naridhika kiasi’, na ‘Siridhiki’ lina maana moja.

“Kwa mujibu wa kamusi ya kiswahili sanifu, Toleo la pili mwaka 2004, neno ridhika linamaanisha kutosheka na maelezo au kufurahia kitu fulani, kwa mantiki hiyo basi “kuridhika sana” na “kuridhika kiasi” kote ni kuridhika,” alisema Khatib.

Akitoa mfano, Khatib alisema kuwa matokeo ya utafiti wa Redet juu ya utendaji wa kazi wa Rais Kikwete unaonyesha kuwa asilimia 44.4 walisema ‘naridhika sana’ na asilimia 35.0 wakasema ‘naridhika kiasi’.

Alisema kutokana na matokeo hayo, bila ya kujali maneno ‘sana’ au ‘kiasi’, utabaini kuwa wananchi wanaoridhishwa na utendaji wa serikali kinachoonekana ni kwamba wanaoridhika ni asilimia 79.4.

Pamoja na hilo, Khatib alikiri kuteremka kwa maoni ya watu kuhusu utendaji wa Rais Jakaya Kikwete pamoja na utendaji wa Baraza la Mawaziri kama ilivyoonyeshwa kwenye utafiti ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka jana ambako watu waliokuwa wakiridhika na utendaji wa Rais Kikwete ni asilimia 90.1.

Alielezea sababu za kuporomoka huko, kulitokana na kuwapo kwa tuhuma kadhaa dhidi ya serikali wakati utafiti huo ulipokuwa ukifanyika.

Mbali ya hilo, Khatib alisema utafiti huo ulionyesha kuwa idadi ya watu waliokuwa wakiridhishwa na utendaji wa Baraza la Mawaziri walikuwa asilimia 61.2 unapochanganya wale wanaoridhika sana 20.2% na wanaoridhika kiasi 41.4%.

“Kwa upande wa serikali za mitaa wananchi waliosema “Naridhika sana” ni asilimia 32.5 na waliosema “Naridhika kiasi” ni asilimia 47.1 hivyo wananchi walioridhika na utendaji wa serikali za mitaa ni asilimia 79.6.

“ Kuhusu Bunge wananchi waliosema “Naridhika sana” ni asilimia 21.8 na waliosema “ Naridhika kiasi” ni asilimia 42.5 kwa hiyo wananchi walioridhika na utendaji wa kazi za Bunge ni asilimia 64.3,” alisema Khatib.

Hata hivyo alisema kuwa kuhusu Watanzania wengi wasiosoma ambao wameonekana kuunga mkono utendaji wa rais kuliko wasomi, serikali ina wajibu wa kuwahudumia Watanzania wote bila kujali wenye elimu na wasio na elimu.

“Kwanza hao wachache wa chuo kikuu wanaomuunga mkono rais, chuo kikuu idadi yake ni ndogo sana,” alisema.

Aidha, kuhusu mengineyo, tatizo kubwa ambalo utafiti umeonyesha kwa wananchi kutoridhika na mahitaji kama ya afya, elimu, maji na miundombinu, serikali imesema kuwa inakubali sehemu hizo kuwa na matatizo na wananchi kutoridhika, lakini bajeti ya mwaka huu imelenga kuboresha maeneo hayo.

Khatib alisema kuwa kufuatia ufafanuzi huo wa utafiti uliofanywa na Redet, serikali inapenda kusisitiza kuwa imefanya mambo makubwa ya maendeleo ambayo yanaonekana wazi machoni mwa wananchi na Watanzania wanapaswa kuelewa kwamba, mkataba kati ya uongozi wa chama tawala (CCM) na serikali ni wa miaka mitano, na hadi hivi sasa serikali inaamini kuwa utekelezaji wa ilani ya chama hicho unaendelea vizuri na utakamilika kama ilivyokusudiwa.

Khatib alisema kuwa serikali inaipongeza Redet kwa utafiti wake, aidha inaipokea taarifa kama changamoto ya kuendelea kutekeleza ahadi mbalimbali za serikali kwa wananchi.

Aidha, serikali imeishauri Redet izidi kuendelea na tafiti mbalimbali za aina hiyo ambazo zitatoa changamoto kwa serikali iliyoko madarakani.
 
Back
Top Bottom