Simulizi ya mapigano ya kijasusi na upelelezi

Simulizi ya mapigano ya kijasusi na upelelezi

Rajonce John

New Member
Joined
Apr 14, 2025
Posts
3
Reaction score
5
HADITHI:LUKUNGU(UPANDE WA PILI WA SARAFU)
MTUNZI: RAJONCE JOHN
MWANDISHI: RAJONCE JOHN
WHAT'SAPP:0673049321
UMRI:MIAKA 18+
SEHEMU YA KWANZA.
Usiku mmoja wenye upepo zaidi ya siku nyingine za wiki hiyo, ulipelekea wakazi wa jiji la Dalaba kurejea majumbani kwao mapema, ungepita mitaani siku hiyo ilikuwa tofauti sana na siku nyingine kwani kawaida ya jiji hilo huwa na watu wa kuranda huku na kule wenye kufanya kazi masaa ishirini na manne. Shughuli nyingi za jiji hilo zilisimama kufuatisha maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu, kitengo cha kushughulika na majanga ya dharura hasa yale ya asili. Taarifa zilizotolewa na mamlaka ya hali ya hewa ya nchi ya Tikali ni kuwa siku hiyo kutakuwepo na kimbunga Kelvin kitakachovuma kutokea upande wa bahari ya Hindi kuelekea nchi kavu. Kuanzia majira ya saa kumi na moja jioni upepo ulizidi kuwa katika mwendo wa tofauti, vumbi jingi, lilifunika jiji la Dalaba watu wengi walishauriwa kufunga milango na madirisha kuzuia kuezuliwa kwa mapaa ya nyumba zao.

Jiji la Dalaba linapatikana ndani ya nchi ya Tikali iliyopo upande wa mashariki mwa nchi ya Tanzania. Mhasisi wa nchi hiyo changa ni aliekuwa waziri mkuu wa zamani wa nchi ya Tanzania,John Senyagwa, kuzaliwa kwa nchi ya Tikali kulipunguza fukuto la mapigano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi ya Tanzania. Miaka thelathini na tano iliyopita nchi ya Tanzania ilipitishwa kwenye moto mkali wa mapigano ambayo yalianza kama kipele baada ya kukikuna kilizalisha kidonda kidogo na mwishoni likawa donda ndugu ambalo tiba yake aliileta John Senyagwa.

Kwa wakati huo nchi ya Tanzania ilikuwa chini ya raisi Wakute Wakute raisi ambae aliingia madarakani baada ya kuondolewa kwa raisi Hashimu Maganga(Tuliona kwenye kitabu cha ANGUKO KUBWA). Raisi Wakute Wakute na serikali yake waliwekeza nguvu nyingi za maendeleo upande wa magharibi mwa Tanzania kwani raisi huyo alikuwa anatokea mkoa wa Tabora. Tabora ilikuwa kitovu cha miradi mingi iliyostahili na isiyostahili yote ilipelekwa Tabora, huduma zote za kijamii zilipatikana kwa wingi Tabora,kipato cha mtu mmoja mmoja kiliongezeka sana huko Tabora, watu walipewa mitaji ya kuendesha maisha yao na kuufunika umaskini uliokuwa kwa miaka mingi ya zamani kabla ya utawala wa raisi Wakute Wakute. Upande mwingine ambao ulipewa nguvu zaidi ni mikoa ya kaskazini huko palikugunduliwa visima vya mafuta ambavyo vilipata uwekezaji mkubwa sana kutoka makampuni ya nje. Upande wa mikoa mitatu ya mashariki Dar es salaam, Pwani na Morogoro iliachwa solemba, miundombinu ilikuwa mibovu sana, maji na umeme vilikuwa vya mgao. Licha ya wananchi kupiga kelele na kulalamika serikali iliwageuzia mgongo hakuna ambae alijali tena kuhusu mikoa hiyo, wananchi walichoka kupigia kelele mitandaoni, uoga waliuficha kwapani waliingia mitaani kuandamana, kudai haki ya kutekelezewa mahitaji yao.

Serikali iliwajibu kwa ukali askari wenye silaha waliwafuata huko huko kwenye barabara walizokuwa wanachoma vitu mbalimbali. Askari walitumia nguvu zaidi, wananchi waliachiwa majeraha makubwa na vilema vya kudumu. Vilio vyao vilimfikia John Senyagwa aliekuwa uhamishoni nchini Kenya. John Senyagwa alijitahidi kumtafuta raisi Wakute Wakute ili wazungumze lakini mtu huyo alimfungia vioo. John Senyagwa alirejea nchini Tanzania kwa Siri sana akikwepa kukamatwa na vikosi vya raisi Wakute Wakute. Hali haikupoa maandamano yalizaa vita kati ya jeshi la serikali ya Wakute Wakute na watu wa John Senyagwa. Mapigano yalichukua muda mrefu miezi kumi na tatu mbeleni umoja wa mataifa kupitia ujumbe wake kwenye jumuiya ya umoja wa afrika na mashariki waliwaita mezani wababe hao wawili.

Majadiliano yalifanyika nchini Uganda kwa lengo la kuleta amani nchini Tanzania, vikao vizito viliendeshwa kwa siku mbili mfululizo na maazimio yaliyoamuliwa ni kuigawa nchi ya Tanzania. Mikoa mitatu ya upande wa mashariki yaani Morogoro, Dar es salaam, na Pwani iliunda nchi mpya, nchi ya Tikali na kukabidhiwa kwa John Senyagwa. Mikoa mingine ilisalia chini ya raisi Wakute Wakute ambae alikubaliana na jambo hilo kutokana na kubananishwa kwenye kona ya kutaka kufunguliwa mashitaka kwa uarifu wa kivita na ukatili dhidi ya binadamu, salama yake ilikuwa kukubali mikoa hiyo kuondoka Tanzania kwa upande mwingine mikoa hiyo mitatu haikua na faida yeyote kwake, alishaua bandari ya Dar es salaam, meli kubwa za mizigo zilitua Tanga na Mtwara, jiji la Tanga liligeuka kitovu cha biashara kwa nchi ya Tanzania. Mafuta yaliyochimbwa Mwanza yalisafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia bandari ya Tanga. John Senyagwa akiwa na miaka sitini na tisa alianza kuijenga nchi, kwanza alibadili majina ya mikoa na yote kuyapa hadhi ya majiji. Dar es salaam iliitwa Dalaba, Pwani iliitwa Labe na Morogoro iliitwa Gutemala. Raisi John Senyagwa aliongoza kwa miaka mitano pekee na kuwaachia viongozi wengine miaka thelathini na tano mbeleni inatufikisha katika mwanzo wa Simulizi yetu hii bingwa.

MELLOW APARTMENT
Ni makazi yaliyojengwa na serikali ya nchi ya Tikali, kwa lengo la kuwasaidia watu wa kipato cha chini kuishi kwenye majengo hayo kwa kulipia gharama nafuu. Makazi hayo yalikuwa kwenye mpango wa shirika la nyumba la Tikali, mpango wa kulipanga upya jiji la Dalaba pia kuinua uchumi wa watu ambao uliharibiwa wakati wa vita dhidi ya nchi ya Tanzania. Kwenye makazi hayo chumba namba mia nane tisini(890) alionekana mwanaume mmoja akishtuka usingizini. Simu yake ilikuwa inatetemeka sana baada ya kuingia ujumbe, alipeleka mkono mezani na kuichukua simu kwa mkono mmoja, mkono mwingine alitumia kufikicha macho yake kuondoa tongotongo ili apate nafasi ya kuona vizuri.

"KINDEGE KIMENASA" ujumbe ulisomeka namna hiyo, mtumaji akiwa amehifadhiwa Kwa jina T072.
"Ooooouuuuuuuuuuuuuh hii nchi haiishiwi mambo" aliongea huku akijinyoosha viungo vya mwili mpaka pale vilivyokaa sawa alishuka chini. Macho yalikuwa ukutani kutazama saa, mshale mfupi ulikuwa kwenye nne na ule mrefu kwenye tatu( saa kumi na robo usiku).

Jonathan Sakewa alipenda kuitazama saa ya ukutani, kuliko saa ya kwenye simu, akiwepo nyumbani alifanya hivyo kuipa nguvu akili yake uwezo wa kuanza uchakatuaji mapema. Alieleleka chooni aliporejea alikuwa na mambo matatu ya kuyafanya, hiyo ilikuwa kawaida yake pale siku mpya inapoingia kwanza alifanya sala kwa Mungu anaemtambua kisha alifanya mazoezi ya kujiweka imara, mwili ulipopata joto na kujiona yuko sawa alikimbilia bafuni alioga, alipotoka alikaa mezani kupitia kurasa ishirini za kitabu cha KIU kilichoandikwa na mwandishi Rajonce John, alipenda kusoma sana maandishi ya mwandishi huyo kuchangamsha akili kwa visa mafumbo vilivyochorwa katika vitabu vyake mbalimbali vyenye umaarufu sana barani afrika na duniani kote.
"Mifuko ya watu ina fedha nyingi, huwezi kuhesabia fedha zilizopo kwenye mifuko ya watu wengine lakini unaweza kuzifanya ziwe zakwako. Hakikisha kila unachokifanya kifanye kwa umaridadi zaidi ya kawaida ya watu wengine, amini fedha zitakujia, mabenki makubwa yanawalipa wataalamu wenye uwezo mkubwa wa kompyuta ili walinde taarifa zao za kibenki.

Wasanii wakubwa huwalipa fedha nyingi wazalishaji wa midundo(producer) endapo wanauwezo wa kuzalisha midundo mikali zaidi ya wazalishaji wengine na nyimbo ikaenda mbali zaidi. Watu hawakupi pesa Kwa huruma wanakupa pesa endapo utajua mambo, yaani utatumia akili na uwezo wako wote kuleta kitu kipya hapo utahamisha fedha kuja kwenye mifuko yako" Jonathan Sakewa alisoma maneno hayo ya mwisho na kukifunika kitabu chake, tayari alishaongeza kitu juu ya maisha ya utafutaji kuwa anapaswa kutumia uwezo wake wote ili kuhamisha fedha kutoka kwenye mifuko ya watu kwenda mfukoni mwake. Saa kumi na moja na dakika tano alikuwa ndani ya mavazi makuu kuu, suruali kubwa lenye matobotobo na shati kubwa lililouzidi mwili wake mara mbili, usoni alikuwa na sura tofauti na ile aliyoamka nayo kitandani, alikikamata kiroba kwa mkono wa kulia na kukilaza mgongoni alifunga mlango na kushuka chini kwa kutumia ngazi za jengo hilo, alitembea kwa hatua ndefu ndefu alipofika mahali fulani alitoa fimbo kwenye kiroba chake fimbo ilikuwa ndogo aliivuta na kuongezea urefu, mwendo ulibadilika, alitembea taratibu akipapasa njiani kwa kutumia fimbo kuepuka mashimo na vitu vya hatari njiani, alikuwa ndani ya upofu wa kuigiza lakini ilikuwa ngumu sana kwa mtu kumbaini. Kweli mjini akili mafanikio huja yenyewe, alitembea mpaka nje ya jengo kubwa la kuuza pikipiki liliitwa Kamota Motorcycle, jengo hilo lilikuwa likitazamana na tawi la benki ya TMB(Tikali Microfinance Bank) alitandika kiroba chake karibu na ombaomba wengine waliokuwa na ulemavu maeneo mbalimbali, alikaa juu ya kiroba kwa kukunja miguu yake vizuri mikono ilikuwa hewani kuombaomba Kwa watu waliokuwa wanapita mahali hapo.

"Nisaidieni, nisaidieni chochote ndugu zangu, Mwenyezi Mungu atawalipa, Mwenyezi Mungu atawaongeza" Jonathan Sakewa alipaza sauti yake maradufu akiamini itawafikia wapitaji. Jiji la Dalaba lilishaingia kwenye harakati zake za kila siku, watu walikuwa katika mbio za kuenda sambamba na muda ili jioni itakapoingia wawe na sababu ya kuingiza mkono kinywani, wapitaji waliosikia sauti ya Jonathan Sakewa waliangusha chochote kama sadaka ya kupalilia upambanaji wao wa siku. Ilikuwa asubuhi,mchana na jioni ilifikia jua lilielekea magharibi ya mbali, juu ya kiroba cha Jonathan Sakewa kulikuwa na sarafu nyingi sana. Ombaomba mwenye mguu mmoja alizitazama fedha hizo kwa macho ya uchu, alizitazama zake aliona amezidiwa parefu sana, alinyanyua magongo yake mawili alijikongoja mpaka alipokuwa amekaa Jonathan Sakewa. Aliyaweka magongo pembeni na kuchuchumaa mbele ya kiroba cha Jonathan Sakewa, alianza kuokota sarafu moja baada ya nyingine. Jonathan Sakewa aliekuwa anamwona ombaomba huyo, alimkamata shingo kwa nguvu na kuanza kumkaba, omba omba alijitahidi kuondoa mikono imara ya Jonathan Sakewa lakini hakuweza, Jonathan Sakewa alipoona anaweza kuua alimsukumiza kwa nguvu.

Ombaomba alianguka mzima mzima huku akikohoa baada ya kukabwa vilivyo, watu waliokuwa wanatazama malumbano hayo ya ombaomba waliishia kuangua vicheko, baada ya kushindwa jaribio lake ombaomba mwenye tamaa aliokota magongo na kurudi mahali pake. Jonathan Sakewa hakuwa na cha kupoteza alikusanya kila kilichokuwa cha kwake, fimbo ilimwongoza kuondoka eneo hilo, alitokea mtaa wa pili alitembea mpaka kwenye duka moja la nguo, muuzaji alipomwona alimpokea huku akitazama huku na kule, kisha waliingia ndani hakukua na mtu mwingine zaidi yao walielekea kwenye chumba cha kubadili nguo.
"Kuna jambo gani huku kiongozi wangu" Muuza duka aliongea akiwa ameinamisha kichwa kutoa heshima mbele ya Jonathan Sakewa.

"Kindege kimenasa Madiwe ndio maana nimekuja huku, naomba nguo za kubadili"
"Sawa kiongozi lakini usalama mlizingatia maana usalama wa taifa wanafanya kazi zaidi ya uwezo wao wa kawaida" Madiwe aliongea huku akimkabidhi kiongozi wake nguo za kubadili.
"Unahofu na uwezo wangu Madiwe?"
"Hapana kiongozi nisamehe"
"Ondoa hofu kila kitu kipo kwenye mhimili wake" Jonathan Sakewa alivaa suti ya rangi ya bluu, suti ilimkaa vyema mwilini, alichukua mafuta fulani na kuyapaka baada ya dakika tatu sura bandia ilitutumka, aliimenya na kuiondoa alikuwa kwenye sura yake halisi.

"Ninaelekea studio, huko nitatoa taarifa ambayo inaweza kutikisa jiji au nchi nzima, jiandae kwa lolote ambalo litatokea maana taarifa inaweza kuwagusa wengi ambao wanaweza kurusha mawe kutokea gizani au kwenye mwanga"

"Sawa Mkuu nimepokea" Madiwe alijibu huku akiinamisha kichwa kutoa heshima. Jonathan Sakewa aliaga na kutoka nje, kidani alichochukua kwenye shingo ya ombaomba ambae alikuja kumwibia kilikuwa mkononi mwake BMW nyeusi ilikuwa nje ikimngojea aliingia ndani yake. Mwendo wa dakika sabini kutokana na foleni ya jiji la Dalaba hasa usiku kutokana na watu kurudi nyumbani muda huo, aliweza kufika studio za redio maarufu WAKITAA FM. Jonathan Sakewa alikuwa ni mwajiriwa na mtangazaji bingwa kabisa wa redio hiyo, alipoingia ndani ya jengo hilo alikutana na meneja wa vipindi na matangazo wa redio hiyo, walipeana mikono kusalimiana baada ya salamu Jonathan Sakewa alikuwa na maneno ya kuzungumza.

"Meneja samahani naomba uzungumze na wafanyakazi wote, waaambie warejee nyumbani na asibaki mtu hata mmoja, hata hao walinzi wa nje wakapumzike na familia zao, Kuna kipindi nahitaji niendeshe nikiwa peke yangu ili asitokee yeyote akapoteza maisha kwasababu yangu, sitaki damu ya yeyote ilie juu yangu" Jonathan Sakewa aliongea maneno makavu, yakilenga dhumuni lake la kuwa mahali hapo.

"Jonathan umeanza tena, ni juzi tu tumefunguliwa kutoka kwenye kifungo cha miezi sita, leo unataka kuturudisha kule kule, hapana aiseeh tafuta mahali pengine pa kutolea taarifa yako" Meneja aliweka ugumu.
"Meneja hii taarifa niliyokuja nayo ni muhimu kuliko hata kazi yako, kama redio itafungiwa na wewe utaendelea kupokea mshahara shida iko wapi?"

"Mimi ni kiongozi wako, naomba nikupe kauli mbili, kauli ya kwanza maneno ya boss ni msahafu hayapingwi wala kuulizwa ulizwa na kauli ya pili rejea kwenye kauli ya kwanza"Meneja alisisitiza kuwa yeye ndio boss na maneno yake yalipaswa kufuatishwa.

"Mmmmh meneja nimekupa heshima kwa kukutaarifu ninachotaka kukifanya lakini naona unajiinua zaidi ya kimo chako na kusahau kuwa sisi wote ni waajiriwa, zungumza na mkurugenzi yeye ndie ataamua kipindi kiruke au kisiruke" Jonathan Sakewa aliongea bila hofu yeyote.

Meneja akiwa amefura kwa hasira alivuta simu na kuipiga kwa mkurugenzi wa redio, baada ya simu kupokelewa aliiweka sauti kubwa Ili maneno ya Mkurugenzi yasikike vizuri na wote wawili, baada ya salamu Meneja alianza kutema kilichomfanya apige simu.

"Bwana Jonathan Sakewa anataka kuturudisha kwenye vita ambayo hatujui faida ya kupigania, anataka kutupeleka kwenye kifungo cha redio kwa mara nyingine, muda huu anataka niwarudishe wafanyakazi nyumbani kisha yeye afanye ujinga wake wa kuvigusa visivyogusika, mimi nimeongea nae sana lakini moto wake hauzimiki naomba wewe kiongozi wetu zungumza nae labda atakusikiliza mkuu" Meneja aliongea kwa kushadadia.

"Mruhusu afanye kipindi chake, kama ametaka ninyi msihusike kwenye mabalaa yake, rudini nyumbani mwacheni yamkute mwenyewe"
"Lakini boss hii ni hatari sana"

"Nimesema mruhusu aondoke kwanza kesho ni siku ya kuwalipa mishahara yenu, nenda kapumzike na familia yako kungojea mshahara wa kesho" Mkurugenzi wa redio aliongea na kukata simu. Meneja aliondoka kwa hasira, maneno ya Mkurugenzi yalionesha kumpendelea Jonathan Sakewa na kumzalilisha yeye aliekuwa anatetea uhai wa redio yao. Jonathan Sakewa aliingia studio na meneja aliwapa taarifa wafanyakazi kuwa warudi nyumbani wakapumzike, redio ilibaki na mtu mmoja Jonathan Sakewa alikuwa mbele ya kipaza sauti saa tatu kamili alikuwa anawaarika wasikikizaje wake kutokea kona mbalimbali za nchi ya Tikali. Jonathan Sakewa akifahamika kwa jina la utangazaji Msago wa Mapulo aliendesha kipindi maarufu kinachofahamika kama Mapulo(Marungu), kipindi kiliegemea kwenye ufichuzi wa mambo ambayo watu wengi hawakuyafahamu, mambo ambayo yalifunikwa kwenye kiroba cheusi ambacho ilikuwa kazi kwa watu kuyafahamu kirahisi. Wasikikizaji walitega sikio Kwa umakini wakitaka kujua Msago wa Mapulo amekuja na jambo gani jipya ambalo lingefungua masikio yao.

"Moyo moyo moyo ni kiungo kidogo sana kwenye mwili wa mwanadamu ukubwa wake hauzidi hata ngumi ya mkono wake lakini ajabu unaweza kuyabeba na kutunza mengi ambayo hata mkono hauwezi kuyabeba, waliosema moyo ni pori nene hawakukosea, moyo wangu umebeba mengi sana ambayo leo nitawapunguzia machache, nitayasema kwasababu sitaki kufa na kihoro cha hili jambo kubwa niteme nisiteme" Jonathan Sakewa aliongea namna hiyo akiamini wasikikizaji wake upande wa pili watasema ateme maneno ambayo alikuja nayo usiku huo, Msago wa Mapulo alikuwa mbele ya wakati Kwa mambo mengi sana hivyo wasikikizaji walishindwa kumeza hata mate kwa shauku iliyowajaa mithiri ya kutaka kufulumia.

"Usiku huu, usiku huu ndani ya dakika kumi na tano zijazo benki ya TMB (Tikali Microfinance Bank) tawi la karibu jengo la Kamota Motorcycle, benki itavamiwa na kuporwa fedha zake zote, fedha za wana Tikali waliohifadhi mahali hapo zinakwenda kuchukuliwa na watu wasio na utu wala huruma ya kujua watu wa Tikali wamepambana vipi kuzipata fedha hizo. Taarifa hizi sijazitoa kwa chombo chochote cha Ulinzi na usalama kwani siwezi kushtaki kesi ya nyani kwa ngedere, vyombo vya Ulinzi na usalama mkiona kuna umuhimu wa ninyi kuokoa mamilioni ya wana Tikali kazi kwenu nendeni mkafanye kazi yenu ya kikatiba, ndugu zangu wasikilizaji kwa leo naomba tuishie hapo, tukutane wakati mwingine ahsanteni sana" Jonathan Sakewa alizima kipaza sauti chake na kufungulia muziki Kwa kuweka playlist kali ambayo wasikilizaji wanaopenda kukesha wazingepata shida ya burudisho la moyo, baada ya hapo alikagua milango yote na kuhakikisha kama imefungwa kisha aliufunga wa nje na kurejea kwenye gari lake, dereva aliondosha gari baada ya mita kadhaa walikutana na kizuizi cha magari mawili, dereva alitaka kugeuza gari na kutafuta njia nyingine. Jonathan Sakewa alimzuia asikimbie bali atulie, waliendelea kuyapa umakini magari ya mbele yao baada ya dakika mbili alirushuka mwanaume mrefu mwenye mwili mkubwa alishuka na kuwafuata, alitumia vidole kugonga kioo cha gari. Dereva alivuta bastola yake kuwa tayari kwa vulumai lolote ambalo watu hao wangeleta.
"Tulia kijana wangu, tulia tuwasikilize kwanza" Jonathan Sakewa alimzuia dereva kisha alimtaka afungue mlango wa upande wa kushoto aliokuwa yeye.

"Bila vurugu wala mapigano yoyote ya kuumizana naomba unifuate, mkuu anataka kuzungumza na wewe" mwanaume huyo alitoa amri.

"Mmmh MFF mmekuwa wa moto na haraka sana, huu muda mlionifuata hapa si mngeenda kuzuia fedha za wana Tikali siziende kwa mikono ya watu ambao hawatozipa thamani za matumizi kwangu hawajui zilipochumwa" Jonathan Sakewa aliongea huku akitabasamu wakati anashuka, alimgeukia dereva na kumtaka aondoke zake wala asimfuate. Jonathan Sakewa alimfuata mwanaume huyo mpaka kwenye gari mbili waliingia ndani yake na gari ziliondolewa kwa kasi eneo hilo. Huu ndio mwanzo wa kigongo chetu hiki naomba uwe pamoja nami mpaka mwisho.
 

Attachments

  • Screenshot_20250414-190149.jpg
    Screenshot_20250414-190149.jpg
    155.3 KB · Views: 24
HADITHI:LUKUNGU(UPANDE WA PILI WA SARAFU)
MTUNZI: RAJONCE JOHN
MWANDISHI: RAJONCE JOHN
WHAT'SAPP:0673049321
UMRI:MIAKA 18+
SEHEMU YA PILI.
ENDELEA NAYO.
TMB(TIKALI MICROFINANCE BANK)
Majira ya saa tatu na dakika kumi usiku, Askari wawili waliokuwa wanalinda ndani ya benki walipokea simu ya upepo kutoka kwa wenzao wakiwapa taarifa ya benki kutaka kuvamiwa, walipewa tahadhari hiyo wakitakiwa kuwa makini kwa wakati huo ikiwezekana wakabiliane na wavamizi wakati msaada upo njiani unakuja kuongeza nguvu na kuwakabili wavamizi, askari walitii kuwa wapo tayari kukabiliana na chochote kitakachokuja, ilipofikia saa tatu na dakika kumi na tano, gari mbili zilisimama na kutimua vumbi baada ya madereva wake kulazimisha breki ya haraka karibu na geti la kuingia ndani ya benki. Polisi wawili waliokuwa wanalinda walikuwa macho kutazama getini ambapo milio ya gari na kishindo cha breki kilisikika, askari wa kwanza alifyatua risasi ambayo ilitua vyema kwenye kifua cha mtu wa kwanza kujitokeza akiwa na silaha mkononi, risasi ilimshusha chini mzima mzima, askari wa kwanza aliruka kutoka kwenye kibanda chao cha ulinzi macho yake yalikuwa makini kutazama getini na eneo zuri ambalo angejificha kwa lengo la kukabiliana na wavamizi. Kitendo cha kumpa mgongo askari wa pili alifyatua risasi ambayo ilitua kwenye kisogo cha askari wa kwanza, lilikuwa ni tukio la kustaajabisha lakini ilikuwa mbinu ya kufanikisha uvamizi, Kundi la kigaidi la Ligojo linaloongozwa na gaidi Dungo liliingia ndani baada ya kusikika mlio wa risasi, walijua askari wanaoshirikiana nae amesharahisisha mpango wa kwanza. Askari wa pili aliekuwa mshirika wa karibu wa mkakati mzima wa kuiba benki alifungua mlango wa kuingia ndani ya jengo la benki, alikuwa mwongoza ramani waliufuata mlango wa kuingia kwenye korido ya kuelekea chumba cha kuhifadhia fedha hapo alionesha mlangoni kitambulisho chenye mfanano wa kile anachomiliki meneja wa benki, kupitia kitambulisho hiko alifanikisha kufungua milango miwili, milango ambayo haivunjiki wala kupitisha risasi, waliingia ndani mpaka chumba chenye mashine ya kuhifadhia fedha, mtaalamu wa kompyuta wa Kundi hilo alitoa kompyuta yake na kuanza kuchezea system za mashine, aliziweka namba ambazo zilikuwa kwenye mashine, baada ya dakika mbili alimtaka Dungo azungushe machuma ambayo yalikuwa kwenye mashine, Dungo akiwa mwingi wa tabasamu alizungusha kushoto mpaka mwisho akairudisha kulia mpaka mwisho na mara ya tatu aliirudisha kushoto mpaka katikati, mashine ilitoa mlio kisha mlango mdogo ulifunguka noti noti nyingi zilimwagika chini.
"Hahahahhahahahahahahahahhahahahahaha" Dungo alicheka kwa sauti ya juu, alichota noti kwa viganja vyake na kuzirusha juu, ulikuwa mwendelezo wa furaha kila mtu alikuwa mwingi wa furaha, hakuna ambae anapenda kukimbizwa kilomita kibao na umaskini noti nyingi zilizokuwa zimemwagika ilikuwa ishara ya mwendelezo wa kuupiga ngumi za uso umaskini. Mabegi yaliletwa, noti ziliwekwa Kwa mpangilio, mabegi saba yalijaa na bado noti hazikuisha waliweka kwenye mifuko yao na bado noti hazikuisha, ilikuwa ni mvua ya minoti ambapo walikosa mpaka sehemu ya kuziweka, gafla simu ya Dungo ilianza kuita, aliipokea.
"Naam naam ongea nakusikia"
"Mkuu kuna shida umbali wa mita mia naona gari za polisi zikija kwa kasi uelekeo ni hapa tulipo" mtu aliekuwa juu ya ghorofa la jengo la Kamota Motorcycle akiwa msoma ramani, alitoa taarifa kwani hatari ilikuwa karibu kutokea, polisi walikuwa kasi kuzuia wizi huo mkubwa wa fedha.
"Yapo magari mangapi?" Dungo aliuliza, upande wa pili wa simu haukujibu zaidi ya kusikika mvunjiko wa kitu ukifuatishwa na kishindo cha kuanguka Kwa mtu.
"Sikitu, sikituuu kuna magari mangapi?" Dungo aliuliza Kwa sauti ya juu zaidi, Sikitu hakujibu tayari mdunguaji wa jeshi la polisi alishapita na kichwa cha Sikitu. Milio ya risasi ilianza kusikika, mapigano yalizuka kundi la Ligojo walikabiliana vilivyo na jeshi la polisi kupitia kikosi chake maalumu cha kukabiliana na uharifu MFF(Mobile Field Force), cheche ziliwaka hakuna upande uliokaa kinyonge wanaume walipigana haswa.
"Hebu kuja hapa nioneshe njia ya siri ya kutokea hapa" Dungo alimvuta askari mshirikiana kwa kumshika shingoni, hakutaka kukamatwa wala fedha walizoiba kuchukuliwa na jeshi la polisi ingekuwa kazi bure kwa jitihada zao zote, kuanzia kuweka mpango,gharama walizotumia ingekuwa hasara kubwa kwa kundi zima.
"Niachie Kwanzaa,punguza ubabe hautasaidia chochote, mimi ndio mwenye ramani nzima ya kutoka ndani ya hili jengo kuwa mtulivu tutoke salama" askari alijitetea huku akijaribu kufurukuta kutoka kwenye Kono nene la Dungo.
"Haraka tuoneshe tuondoke, unaleta siasa kazini" Dungo alimwachia askari, Dungo na vijana wake bila kusahau mabegi yenye fedha waliongonza njia kutoka nje ya chumba.
"Kata kulia fungua huo mlango nenda kushoto" Askari alitoa maelekezo ya namna wanaweza kutoka salama bila kukamatwa na jeshi la polisi, baada ya hatua chache askari alitoa bastola macho yake yalikuwa kisogoni Kwa Dungo alifanya jambo ambalo halikutegemewa alifyatua risasi ambayo ilimfika vyema Dungo, hakuna ujanja, ubabe wala ukaidi mbele ya risasi Dungo alienda chini, roho yake ilikimbia maili nyingi kuicha dunia, vijana wa Dungo waliotikisika, askari alifanya unyama aliwaangusha wanne kwa risasi, vurugu za askari hazikuwa za kutosha mmoja kati ya wengi nae alimiminiwa risasi za mwilini, alichakazwa na kuanguka chini, vijana watatu wa Dungo walimfanyia umafia, walibaki vijana watatu wa kundi la Ligojo, chini kulikuwa na miili minne ya wenzao na watano ulikuwa wa boss wao, mpaka wa utii na mali ulisimama dede wachukue mwili wa boss na kuacha mabegi kadhaa yenye minoti, aaaah sio kweli walifanya ambacho hata, Mimi nawewe tumewaza walibeba mabegi saba huku na huku hakuna ambae alikuwa na akili ya umaskini tena, ngamia walitaka kupenya kwenye tundu la sindano wafike kwenye kisima chenye maji mengi jangwani, hawakuacha kitambulisho bandia chenye mfanano na kile cha meneja milango ilifunguka na kutokea nyuma ya jengo waliruka ukuta lakini hawakuweza kuwaruka askari polisi waliokuwa katika idadi kubwa, wawili walijisalimisha baada ya mmoja alietaka kukimbia na begi kuangushwa kwa risasi, polisi walikuwa kazini waliwakamata, pingu mikononi mzobe mzobe kwa karaha na vibao walipakizwa kwenye gari, uvamizi wa benki ulizimwa kwa mtindo huo wa kibabe, jeshi la polisi lilitangaza limefanikiwa kuzima tukio zima,ilivyo ajabu sifa humfuata ziliemchagua ndio maana watu husema wakati mwingine jitihada sio mafanikio kuna kuzidiana kwa nyota, sifa kedekede kutoka kwa watu zilipelekwa kwa mwandishi wa habari Msago wa Mapulo kwa kutoa taarifa hizo, alizidi kujenga mizizi ya kupendwa kwenye mioyo ya watu,hiyo ilikuwa hatari sana kwa maisha ya Jonathan Sakewa kwani kilipochema king'aacho hukaribisha mabaya ili kukififiisha ili kisiwazidi wenye mamlaka na wamiliki halali wa sifa.
*****
MOBILE FIELD FORCE HEAD QUARTER (MFF HQ)
Makao makuu ya kitengo maalumu cha polisi, kitengo hiki kiliundwa na askari polisi waliopewa mafunzo zaidi ya askari wa kawaida, lengo lake kuu ni kupambana dhidi ya uharifu uliovuka mstari wa kiarifu.
Moja ya matukio makubwa ambayo yalipelekea kuundwa Kwa kikosi hiko ni kuinuka kwa vikundi vya waharifu ambao walikuwa na umri mdogo miaka miwili baada ya vita ya nchi ya Tikali dhidi ya Tanzania.
Makundi hayo yalikuwa zao la vita, vijana wadogo ambao walihusika katika vita kwa kufundishwa namna ya kushambulia na kujilinda kwa mbinu za juu, vita vilivyomalizika vijana walibaki na ujuzi wao kichwani, kujenga nchi sio jambo la siku moja nchi ya Tikali ilipitia katika umaskini mkubwa vijana walikosa ajira hali ambayo iliwapelekea kuunda vikundi vya kiharifu walipora mali, walijeruhi watu ambao walikuwa wabishi kutoa vile ambavyo walivihitaji, wakati huo saa kumi na mbili jioni watu walikuwa ndani wakihofia kukutana na makundi hayo vijana makatili ambao walipachikwa majina mengi ya ajabu kama vile kombakomba, kutokana na vitendo ambavyo walikuwa wanavifanya. Raisi wa nchi kwa wakati huo John Senyagwa aliamua kufanya maamuzi magumu kwa kumteua luteni kanali Tabu Wambano kuwa mkuu wa kikosi kipya cha MFF(Mobile Field Force) na kumkabidhi majukumu ya kuirejesha nchi katika usalama, walichaguliwa askari ishirini kutoka ndani ya jeshi la polisi walipelekwa kwenye Kambi moja ambapo walipigwa msasa wa nguvu ndani ya miezi miwili waliiva, mioyoni walikuwa na kiu ya kuirejesha nchi kwenye usalama, jioni ilipofika waligawana mitaa, vikundi vya kiharifu vilipigwa haswaa, hawakuwaacha waliwakamata na kuwapeleka eneo maalumu la mateso, eneo ambalo liligeuka tishio kwa vikundi vya kiharifu eneo lilinuka damu, liliitwa Gotogoto, ilikuwa dhambi Kwa kijana mharifu kupelekwa Gotogoto na kurudi nyumbani mzima, wazazi waliokota miili mingi ya vijana hao waarifu ikiwa haina pumzi, ndani ya miezi sita vikundi vyote vilifyata mkia Kwa kujisalimisha kwa jeshi la polisi ili kuepuka kukamatwa na kikosi cha MFF ambao walikiita chinjachinja, nchi ilirudi kwenye usalama wake lakini kikosi cha MFF kilisalia kushughulika na atakae leta fyokofyoko kwa kutaka kuhatarisha usalama wa nchi.
Ndani ya chumba cha mahojiano makao makuu ya kikosi cha MFF, mlango ulifunguliwa na askari na kuingia ndani kwa lengo la kufanya mahojiano na Jonathan Sakewa ambae alihifadhiwa eneo hilo tangu usiku uliopita baada ya kutoa taarifa ya benki ya TMB kuvamiwa na Kundi la Ligojo, meza iliyokuwa katikati ndiyo iliwatenganisha Jonathan Sakewa na askari huyo wa MFF.
"Naitwa Troy Daniel ni askari wa MFF, niko hapa kwa lengo la kufanya mahojiano nawewe, ushirikiano wako ndio unahitajika mahali hapa kuliko chochote kile ambacho umewahi kipatia umuhimu, unafahamu kwanini uko hapa?" Afande Troy Daniel aliuliza baada ya kujitambulisha.
"Mmmmmmmmh futa jasho kwanza, mwili wako unatiririsha sana jasho na chumba kimejaa kiyoyozi cha kutosha, utaweza kuwahoji magaidi wakubwa wakati mimi nisie na chembe ya uharifu unatetemeka namna hiyo mpaka unarowanisha nguo zote" Jonathan Sakewa aliongea baada ya kufumbua macho yake na kutazamana na Troy Daniel.
"Usiruke kwenye kile nilichokuuliza, kama hujui kwanini uko hapa, bhasi nakuuliza na nahitaji majibu yaliyoshiba ulipata wapi taarifa za benki kuvamiwa? na wewe ni nani? unauhusiano gani na kundi la Ligojo?" Afande Troy Daniel aliuliza maswali mfululizo baada ya kugundua mtu alie mbele yake si mwepesi na asipokuwa makini atampoteza kwenye ramani ya maswali yake, alikaza macho kumtazama zaidi Jonathan Sakewa alieonekana kuwa mjanja mjanja.
"Afisa kutoa taarifa ambazo zimelisaidia jeshi lenu kufanya kazi yenu ya msingi ya kulinda mali za raia ni kosa? yaani kuwapa taarifa ambazo hamkua nazo na kuzipata kwenu ingekuwa kwa kuchelewa sana bado ni tatizo kwa nchi hii, nimewapa jukwaa la ninyi kupata sifa kedekede na kurejesha imani yenu kwa wananchi, bado unanikandamiza kwenye meza ya uharifu aiseeh hii nchi nimeinyanyulia mikono, kuna mambo nahitaji kuzungumza na mkuu wako, wewe bado kijana mdogo kuyabeba, unaweza tumia huu muda kufuta jasho, mwilini mwako" Jonathan Sakewa aliongea maneno ambayo yalimchefua Troy Daniel uvumilivu ulimshinda alikamata shati la Jonathan Sakewa na kulivuta kwa nguvu, walikuwa wanatazama, kama watu wanaotaka kupigana kwa vichwa.
"Sikia wee mpuuuzi nitakuua, nimesema nitakuua mimi sio pimbi wa kuchezewa chezewa najua wewe sio mtu wa kawaida kuna mengi unayafanya nyuma ya mgongo wa uandishi wa habari, macho yangu yapo juu yako kila wakati" Troy aliongea kwa sauti ya kukaza, hakutaka dharau kazini kwake, alitaka kukikata kiburi cha Jonathan Sakewa ambae hakuonesha kutikisika.
"Ouuuuuuuuuuuuuuuuuuh aaaaaaaah" Troy aliachia pumzi ndefu na kumwachia Jonathan Sakewa, alipiga meza kwa nguvu kupunguza hasira aliyakumbuka maneno fulani ambayo yalimfanya atulie.
"Utakapokuwa chumba cha mahojiano na mtuhumiwa akakuwahi hatua kadhaa mbele kwa kukwambia maneno ambayo yatakoleza moto wa hasira ndani yako, ukalipuka nao, bhasi hakuna taarifa utaweza kuambulia, unapaswa kumhoji mtuhumiwa ukiwa huna hasira na ukishindwa kujizuia ni bora kuacha kila kitu na kutoka nje" Troy Daniel aliyakumbuka maneno ya mwalimu wake wa somo la upelelezi wakati akiwa mafunzoni.
"Una hasira za karibu kama baba yako, na umekua sana siku baba yako atakuona atafurahi sana" Jonathan Sakewa aliongea maneno ambayo yalimvuruga Troy Daniel.
"Baba yangu? unamjua baba yangu?" Troy Daniel aliuliza maswali mfululizo, ni kama alijaa kwenye mfumo wa Jonathan Sakewa ambae hakujibu chochote zaidi ya kutabasamu tu. Troy aliendelea kusimama akiwa mwenye kujiuliza maswali juu ya mtu huyo, sauti ya mlango ilimshtua na kugeuka nyuma.
"Hebu nipishe nizungumze nae" Mkurugenzi wa MFF Sebastian Mroka aliongea baada ya kuingia ndani, aliona jambo lilishakua maji marefu kwa kijana wake ni kheri aingilie mwenyewe. Troy Daniel alitoa heshima na kutoka nje, Sebastian Mroka alivuta kiti na kukaa ukimya ulichukua dakika mbili wakitazamana tu.
"Mwandishi Msago wa Mapulo, nimekuita jina lako sababu nimeshafahamu maana yake kuwa ni kusagwa sagwa kwa kitu na marungu vipi nimekosea mahali?"
"Ni sahihi kabisa kama ungekuwa mtihani umepata alama za juu sana, naomba usizunguke sana nieleze ulichoniitia hapa nahitaji kwenda kushughulika na mambo mengine huko uraiani maana kukaa hapa dakika moja ni sawa na kuyasimamisha mambo yangu mara elfu moja"
"Mambo gani? kuna mambo unafanya gizani mbali na huo uandishi wa habari? utanijibu maswali hayo siku nyingine japo ninauhakika nitakujua tu. Ninahitaji kufahamu jambo moja kwa sasa ulifahamu vipi benki ya TMB itavamiwa pamoja na kujua muda wake halisi" Sebastian Mroka aliuliza.
"Ukifahamu utanipongeza kwa kitendo changu Cha kishujaa kwa wana Tikali?"
"Naam itakapobidi utapata zawadi sasa zawadi inaweza kuwa tamu au chungu, uchungu unaweza kukufikia endapo utakuwa unahusika kwenye hizo njama za kuvamia benki, hakika hatutakuvumilia utanyooshwa balabala hebu niambie tufanye wewe ni raia mwema ulijua vipi?"
"hahahahahaha jeshi la polisi bhana halijawahi kuaminika duniani kote, kizazi chetu kitapita na hata kijacho pia, bado jeshi halitakuwa na nguvu ya kuaminika kwenye kitabu kimoja cha mwandishi Rajonce John kinachoitwa Paka la mtaa, alielezea kisa kimoja cha mama fulani ambae aliwaita polisi nyumbani kwake kwa kuhisi kuna watu wabaya wananyemelea kumwibia, siku hiyo polisi waliwahi kufika tofauti na kawaida yao, cha ajabu polisi mmoja alimfyatulia yule mama risasi nusu saa mbeleni akidai kuwa alihisi ni jambazi baada ya umeme kukatika ndani ya dakika mbili, yule mama alifariki pale pale, kijana wake aligeuka paka la mtaa, aliua kila askari polisi aliekatiza mbele ya macho yake, kama sehemu ya kulipa kisasi cha kifo cha mama yake aliedhulumiwa uhai na moja ya askari wa jeshi la polisi na hakuna sehemu alipata haki yake kwani yule askari muuaji alibadilishiwa kituo cha kazi ili kuendelea kufukia maovu. Kupitia kisa hiko cha mwandishi Rajonce John umejifunza nini Mkurugenzi?"
"Hakuna kitu nimejifunza na mambo mengi ya kiharifu huwa hayatokei nchini kwetu sababu harufu yake tu ikinuka, hukutana na makucha yetu, tunayararua na kuyamaliza kabisa"
" Hahahahahaha siku moja usiishi kwenye vioo vya gari, vioo vya maghorofa yenu, nenda mtaani kabisa kule kwenye kiini cha maisha ya kawaida, utapata kujua madudu ya jeshi lenu utawaona askari wanaoshirikiana na waharifu kuiba pikipiki za bodaboda, utawaona askari wanaopokea rushwa ushuru Kwa wamama wauza gongo, na mwisho utaona lawama za watu kupotea mfululizo, ndio utajua kuwa hujui kitu kuhusu hii nchi na mateso yake, watu wana maumivu makali ni vile tu wameamua kuishi kama samaki ndani ya bahari, ngoja nikupe taarifa ya namna nilijua kundi la Ligojo watavamia benki kwasababu kwa sasa sina matumizi nayo". Jonathan Sakewa alifungua mdomo na kutema memory card na kumkabidhi Sebastian Mroka ambae alisita kuipokea.
"Usiogope Mkurugenzi sio bomu hilo, siwezi kuhatarisha maisha yangu wakati nayapenda kuliko unavyoyapenda yakwako, sikiliza sauti iliyopo humo ndani" Jonathan Sakewa aliongea alijua kilichokuwa kinakwenda kutokea. Sebastian Mroka aliekuwa kamuamini Jonathan Sakewa kwa asilimia kadhaa alichukua redio na kuipachika memory card, kisha aliongeza sauti, redio ilianza kutetemeka na kuongezeka joto ambalo Sebastian Mroka alishindwa kuishika aliiangusha juu ya meza ili isiendelee kumuunguza, redio ilikuwa inatikisikika sana mpaka meza nayo ilitikisika.
"Hahahahahaha hahahaha hahahaha hahahaha" Jonathan Sakewa alianza kucheka kwa sauti ya juu, sauti ilikuwa kali na kumuumiza masikio Sebastian Mroka ambae aliyaziba kwa nguvu. Mtikisiko ulizidi na redio ililipuka moshi mzito ulitanda ndani ya chumba cha mahojiano. Kizaa zaa kipya ndani ya makao makuu ya kikosi cha MFF kilizuka, askari polisi walipowahi ndani ya chumba cha mahojiano hawakumkuta Jonathan Sakewa wala Mkurugenzi wao Sebastian Mroka, walihamaki walifunga milango yote ya dhalura, Jonathan Sakewa hakutakiwa kuondoka mahali hapo akiwa amemteka Mkurugenzi wa kitengo Sebastian Mroka. Tushikilie hapo, tujinyooshe kidogo tukutane sehemu inayofuata hiki chuma kila mmoja atakishika na kuenea. Nikushukuru sana,kwa kusoma pamoja namimi Mungu akubariki sana tukutane sehemu inayofuata ya kigongo chetu hiki cha Upande wa pili wa shilingi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom