SEHEMU YA 03
Niliwaona wamesimama nje ya mlango wa chooni. Nikawafuata kulekule ambapo mama alinielekeza nifike pale kwa kutembea vilevile tulivyoelekezana awali. Nilisimama, nikageuka na kuanza kutembea kinyumenyume mpaka pale.
Mama na yule mwanamke waliniingiza chooni na kunisimamisha jirani na bomba la maji kisha wakasema natakiwa kuwa pale nikiwa nimesimama wima hadi watakaporudi. Wakati wanaondoka, mama aliniambia kazi yangu itakuwa kupokea vitu watakavyokuwa wanavileta pale na kuvishika kwa kusubiri maelezo mengine.
Baada ya muda, yule mwanamke alikuja, akanikabidhi watoto wachanga wawili. Akaniambia wakitaka kulia tu, niweke mikono juu ya vichwa vyao ili watulie, kisha akaondoka.
Niliwashika wale watoto kwa umakini kwani walikuwa wazito sana. Baada ya muda, alikuja tena yule mwanamke, alikuwa amebeba watoto wawili, akanikabidhi, lakini nilikuwa sina pa kuwaweka, akasema niwabebe mgongoni. Alinisaidia kunibebesha halafu wale wawili nikaendelea kuwashika mkononi.
Dakika kama tatu baada ya yule mwanamke kuondoka, aliingia mgonjwa mmoja, akawa kama amenikazia macho mimi. Nilimnyooshea kidole kisha nikakielekezea kwenye mlango wa choo kimoja, naye akaingia huko.
Pale nilichofanya, niliishika akili yake na kuielekeza iingie kule kwenye choo. Wachawi wengi hufanya hivyo. Pale wanapokumbana na kikwazo mbele yao, hujihami kwa vidole, mchawi akikunyooshea kidole kisha akakielekezea kwenye moto mfano, utajikuta ukienda.
Ndiyo maana kuna watu wanagongwa na magari njiani kisha wanaoshuhudia wanashangaa kwamba, jamaa ilikuwaje akasogea barabarani wakati gari lilikuwa linatoka kwa mbele yake?
Kinachofanyika ni kwamba, kama kuna mchawi ametumwa kwako akumalize na ni ‘mwepesi’, yaani huna kinga yoyote, basi akishakupatia shabaha, anakuelekezea mahali pa hatari. Iwe kwenye moto, barabarani au hata kwenye maji, lazima utaelekea huko tu kwani wenyewe wanasema wanashika akili.
Basi, yule mwanamke aliingia kule chooni. Akafunga mlango na kujisaidia. Baada ya muda alitoka, akageuka kuangalia niliposimama mimi, nikamnyooshea tena kidole na kukielekezea mlango mkubwa, akatoka. Huku nyuma nikasonya.
Niliendelea kuwa pale nikiwa na wale watoto wachanga. Lakini huku nikiwa na maswali mengi, kwani uchawi wa kupata mazao mengi shambani kupitia watoto nilikuwa siujui. Mawazo yangu yaliamini kwamba, wale watoto tutaondoka nao kwenda nyumbani ili kuufanya huo uganga kumbe sivyo.
Baada ya dakika chache tena, alikuja mama, naye alibeba watoto wawili, akasema nikae chini ili niwapakate. Kulikuwa na ugumu kwani sasa nilikuwa na watoto wawili mgongoni na wawili mkononi nikiwa nimekaa chini.
Baada ya kuwakumbatia wale watoto, mama akaniambia nivumilie kwani bado mawili tena. Akasimama na kuondoka kwenda kuungana na yule mama.
Baada ya dakika tano, mlango ulisukumwa, akaingia mwanamke mmoja akiwa anavua gauni, akajisaidia nje ya mlango wa chooni. Nilikasirika sana kwa kitendo kile.
Ili kuikomesha tabia ile, niliwashika wale watoto vizuri kisha nikamnyooshea mkono, kidole kimoja nikakikunjua kukielekeza kwake na kukibatulia chini, akaanguka kama gunia, puu!
Aliposimama, nikasonya. Inaonekana alisikia kusonya kwangu kwani alitoka haraka huku akigeuka kuangalia nyuma. Kwa pale nilipokuwa nimekaa palikuwa wazi sana lakini aliyekuwa na uwezo wa kuniona mimi ni mmoja tu. Ni mtu mwenye nguvu za kichawi kama sisi.
Baada ya hapo, mama aliingia. Alikuwa ana watoto wawili, akawaweka kwa kuwachomeka kwangu lakini nilishindwa kuwabeba sawasawa. Aliwaacha hivyohivyo, mama akaondoka. Lakini baada ya dakika mbili alirudi akiwa ameongozana na yule mwanamke mwenzake. Hawakuwa na kitu chochote mkononi. Walipofika, walipiga magoti jirani yangu. Mama alianza kumchukua mtoto mmoja mmoja na kumkabidhi mwenzake ambaye naye aliwachukua na kuwaweka sakafuni.
Mama yeye, alikuwa akimchukua mtoto mmoja, anamuweka mkono kichwani kisha anampindua miguu juu, kichwa chini kabla ya kumpa mwenzake ambaye naye kila alipowapokea, aliwaweka kwa kuwalaza kifudifudi.
Walipowaliza watoto wote, mama alisimama, akanyoosha mkono mmoja juu, akasema:
“Mje mchukue watoto wenu haraka, sisi tunaondoka.”
Kufumba na kufumbua, kweli wanawake waliingia, kila mmoja akamchukua mwanaye, tena walikuwa wakigombeana na kuondoka. Hapa palikuwa na maswali mengi sana na nilipanga kumuuliza mama nyumbani.
Tuliondoka muda huohuo kwa njia ya kichawi hadi nje ya hospitali. Yule mwanamke akasimama getini na sisi pia. Aliangaza kulia na kushoto, akasema twende kwenye mti mmoja wenye matawi marefu na chini yake palikuwa na kivuli kikubwa.
Pale chini ya mti, yule mwanamke alimpa mkono mama na mimi, kisha akasema ameshukuru sana kwa ushirikiano wetu. Akasema ikitokea na sisi tuna shida kama yake au nyingine, tusisite kumwambia muda wowote hata kama itakuwa saa nane za usiku.
Mama alimwambia hakuna shida, akatoa mkono kwangu akauegemeza kichwani, akaniangalia akasema:
“Hakika wewe utafika mbali sana siku za usoni, jitahidi kuwa shupavu kama hivi. Mungu akulinde sana Yusta.”
Tulipofika nyumbani, nilimuuliza mama kama nilivyokuwa nimepanga. Kwamba, wale wanawake waliofika kugombea watoto wao walikuwa wanajijua?
Mama alisema hakuna hata mama mmoja aliyejua mtoto wake amechukuliwa. Ila akasema kwa wale ambao watoto wao walichukuliwa, dalili kubwa kwao ni watoto ‘feki’ waliowashika mikononi walikuwa wakilia sana hata pale mama zao walipowapa maziwa walizidi kulia mpaka kupatwa na kwikwi.
“Sasa mama, pale ulipowaita waje kuwachukua mama zao, kule ndani hospitali wao walijua wanakwenda wapi?”
Mama alinishika kichwani, akanisifia kwamba nina akili sana, kisha akasema:
“Wale hawakujijua chochote. Kila mmoja alipomchukua mwanaye na kurudi naye wodini waliendelea kujiona kama hawakutoka. Ila walijua watoto wao wametulia kulia baada ya kuwabembeleza sana.
ITAENDELEA