Simulizi ya kusisimua: Sitalia tena

Simulizi ya kusisimua: Sitalia tena

Chilojnr

JF-Expert Member
Joined
Jul 5, 2012
Posts
308
Reaction score
1,354
“Where do you live?” (unaishi wapi?)

“Tanzania! You?” (Tanzania! Wewe?)

“Oman.”

“This is my first time to chart with an African girl, you look stunning...” (hii ni mara yangu ya kwanza kuwasiliana na mwanamke wa Kiafrika, umependeza)

“Thank you Kareem.” (Nashukuru Kareem)

Msichana Saida alikuwa kwenye kompyuta yake ya mapajani akiwasiliana na mwanaume aliyekutana naye katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Mwarabu aliyekuwa akiishi nchini Oman.

Muda wote uso wa Saida ulikuwa kwenye tabasamu pana. Kitendo cha kuwasiliana na mwanaume huyo kilimfanya kujawa na furaha tele huku muda wote uso wake ulitawaliwa na tabasamu pana.

Kijana aliyekuwa akiwasiliana naye kipindi hicho aliitwa kwa jina la Kassem Abdulaziz. Alikuwa mwanaume wa Kiarabu aliyekuwa akiishi nchini Oman. Mara ya kwanza walikutana ndani ya Mtandao wa Facebook, japokuwa Saida alikuwa msichana mrembo aliyewaletea mapozi wanaume wengi katika mtandao huo lakini kwa Kareem akashindwa kukataa, alipotumiwa meseji ya kwanza tu, akamjibu na kujikuta wakiwasiliana kila siku.

Moyo wake ukatokea kuvutiwa na mwanaume huyo wa Kiarabu. Alikuwa na sura nzuri, ndevu alizozinyoa kwa staili ya O huku nywele zake akiwa amezipendezesha kwa dawa za nywele zilizomfanya kuvutia na kupendeza machoni mwa msichana yeyote yule.

Saida hakutaka kuishia kuangalia picha moja tu, alichokifanya ni kufungua katika sehemu ya picha za mwanaume huyo na kuanza kuangalia picha nyingine. Akatokea kumpenda lakini hakutaka kuweka wazi, waliendelea kuchati siku hadi siku, wiki hadi wiki pasipo kuonana.

Saida hakutaka kuficha, alichokifanya ni kuwaambia marafiki zake kuhusu Kareem. Kila mmoja alimshangaa. Hawakumshangaa kwamba kwa nini alikuwa na mwanaume huyo, walichoshangaa ni kwa nini alimwamini mwanaume wa mtandaoni.

Marafiki zake wakamwambia kwamba lingekuwa jambo jema kama angeachana naye lakini Saida hakutaka kusikia kwani moyo wake ulitekwa, hakuona kama angeweza kuachana na mwanaume huyo ambaye kwake, tayari alimuona kuwa mwanaume wake wa ndoto.

Alichokifanya ni kuwaonyeshea picha za Kareem, marafiki zake hawakuamini kama kweli duniani kulikuwa na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa Kareem.Nao wakajikuta wakianza kumtamani.

“Ni mwanaume mzuri sana, mpaka nakuonea wivu,” alisema rafiki yake aliyeitwa Grace. Aliishikilia simu ya Saida na kuanza kuangaliapicha za mwanaume huyo.

“Ninampenda sana...” alisema Saida.

“Umemwambia?”
“Anajua hilo nadhani, ila sijamtamkia kwa maneno, naogopa,” alisema Saida na kisha kutoa kicheko kidogo.

Mawasiliano yakapamba zaidi. Kila siku ilikuwa ni lazima kuwasiliana na mwanaume huyo. Mawasiliano hayakuishia kwenye Facebook tu, wakahamia kwenye WhatsApp na kuanza kuwasiliana huko.

Wakawa huru, wakatumiana sana picha mbalimbali. Kwa jinsi alivyoonekana, Kareem hakuwa mwanaume masikini. Alikuwa akipiga picha kwenye magari mazuri, ya gharama ambayo yalimtoa udenda Saida.

Alitamani kumuuliza kuhusu familia yao lakini akaamua kunyamaza, hakutaka kuonekana kama alizipenda fedha zake, alichotaka kumuonyeshea ni mapenzi mazito, hata kama mwanaume huyo angekuwa masikini, basi angempenda hivyohivyo.

“Wewe unaishi Tanzania sehemu gani?” aliuliza Kassem.

“Dar es Salaam.”
“Ooh! Ningependa siku nije huko nikuone. Nitaruhusiwa?” aliuliza Kareem.

“Hakuna tatizo. Karibu!”

Baada ya kuwasiliana kwa miezi mitatu ndipo Kareem alipoamua kutupa karata yake, akaamua kumwambia Saida kile kilichoendelea ndani ya moyo wake, jinsi alivyokuwa akimpenda na kuhisi mapenzi mazito ndani ya moyo wake.

Kwa Saida, hakutaka kuwa na pingamizi, alimpenda mwanaume huyo na hatimaye wakajikuta wakiingia katika dimbwi la mahaba mazito. Wakapendana sana, hakutaka kuwa na mwanaume yeyote yule zaidi ya mwanaume huyo ambaye hakuwahi kuonana naye katika maisha yake zaidi ya kuona picha zake tu na video walizokuwa wakitumiana katika Mtandao wa WhatsApp.

“Naomba nikwambie kitu,” alisema mwanaume huyo.

“Niambie!”

“Lakini naomba iwe siri! Usimwambie mtu, hasa ndugu na marafiki zako!” alisema Kareem, kidogo Saida akashtuka.

“Hakuna tatizo!”

“Umekwishawahi kumsikia mtu anayeitwa Fabrouz Abdulaziz?”

“Hapana! Ndiye nani?”
“Mtafute Google.”
“Sawa.”
Alichokifanya Saida ni kumtafuta mwanaume huyo aliyeambiwa. Kutokana na jina la mwanaume huyo kuwa kubwa, wala Saida hakupata wakati mgumu, akamuona mtu huyo na kuanza kumwangalia.

Akashtuka. Mwanaume huyo alikuwa mmoja wa mabilionea wakubwa katika nchi za Uarabuni. Alikuwa akimiliki kiasi kikubwa cha fedha, visima vya mafuta, migodi na hoteli kubwa nchini Oman.

Saida hakuishia hapo, alichokifanya ni kuangalia familia ya mzee huyo. Hakuamini baada ya kuona kuwa mzee huyo bilionea alikuwa na watoto wawili tu, msichana aliyeitwa Faudhia na mwanaume aliyeitwa Kareem, na alipofungua picha kumuona huyo Kareem, macho yake yakatua kwa mwanaume huyohuyo aliyekuwa akiwasiliana naye.

“Kareem...is it true?” (Kareem...ni kweli?)

“About what?” (kuhusu nini?)

“What I’ve seen,” (kile nilichokiona)

“Please...don’t tell anyone!” (naomba usimwambie yeyote...tafadhali)

Saida akatulia, hakuamini kama kweli alikuwa mpenzi wa mtoto wa bilionea kutoka nchini Oman. Akashusha pumzi ndefu kisha kuanza kuziangalia tena picha za Kareem, akaangalia magari aliyokuwa akipiga picha Kareem na nyumba aliyokuwa amesimama mbele yake, akajikuta akichanganyikiwa akili yake.

“I want you to marry me,” (nataka nikuoe) alisema Kareem.

“Kareem...”

“Please...be my wife..” (naomba uwe mke wangu, tafadhali) alisema Kareem kupitia video fupi katika WhatsApp.

Alitoka katika familia ya kawaida, haikuwa kwenye utajiri wa umasikini. Kipindi hicho ndiyo kwanza alikuwa ameanza chuo, kitendo cha kuambiwa na Kareem kwamba alitamani sana awe mke wake kikamchanganya.

Saida hakutaka kujibu harakaharaka, akatulia na kumwambia Kareem kwamba alihitaji muda na angemjibu kuhusu hilo alilomwambia. Hakutaka kuwashirikisha marafiki zake, alichokifanya ni kutumia muda wake na kuanza kujiuliza kama alikuwa sahihi kumkubalia Kareem au la.

Wakati mwingine akawa anajiuliza kama kweli Kareem yule mtoto wa bilionea Abdulaziz alikuwa huyo aliyekuwa akiwasiliana naye au mwingine. Baada ya kujifikiria sana kuhusu hilo, baadaye akajipa jibu kwamba huyo alikuwa ndiye yeye kwani hata alipomwangalia kwenye Wikipedia, alikuwa yeye.

“Nimkubalie au? Mungu wangu! Naomba jibu lako,” alisema Saida. Ilikuwa rahisi sana kwa msichana kukubali kuwa na mtu kama Kareem, ila kwake, kidogo moyo wake ulikuwa na hofu kubwa.

***

Saida alikuwa kwenye wakati mgumu, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Ni kweli alikuwa kwenye mahusiano mazito na mwanaume ambaye hakuwahi kuonana naye, walijuana kwenye mitandao na kuweka uhusiano mkubwa, ukaribu uliokuwa ambao ulimfanya kila mmoja kuwa karibu na mwenzake.

Akaombwa kuwa mpenzi wake na hivyo kuolewa lakini bado kwake kulikuwa na mtihani mgumu. Alimpenda Kareem zaidi ya mwanaume mwingine yeyote yule, na hakuwa radhi kumuona akiondoka mikononi mwake lakini suala la kumkubalia na kuwa wapenzi, kwake ulikuwa mtihani mwingine mgumu.

Alikaa na kujifikiria kwa kipindi cha siku mbili na ndipo akamwambia Kareem kwamba alikubali kuwa mpenzi wake. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa uhusiano wa kimapenzi baina ya watu wawili hao.

Mawasiliano yakachanganya na kila mmoja akamuona mwenzake kuwa muhimu katika maisha yake. Siku zikakatika huku mapenzi ya mtandaoni yakiendelea kunoga. Baada ya miezi sita mingine, Kareem akamwambia Saida kwamba alitaka kumfuata nchini Tanzania, aende akajitambulishe kwa wazazi wa msichana huyo.

Hilo halikuwa tatizo, Saida akawaambia wazazi wake. Kwanza wakashtuka, walishangaa, hawakuamini kile walichoambiwa na binti yao. Ilikuwa vigumu kumwamini mwanaume huyo kwani kulikwishawahi kutokea wanaume wengi ambao walianzisha uhusiano wa kimapenzi na wasichana kwenye mitandao lakini mwisho wa siku, kulikuwa na mambo mabaya yaliyowatokea.

“Una uhakika huyu ni mtu mwema?” aliuliza baba yake.

“Baba! Siwezi kulijibu swali hilo, ila nahisi ni mtu mwema kwani kwa jinsi tunavyowasiliana, anaonekana ni mtu mzuri sana,” alijibu Saida.

“Halafu yeye akija atataka na wewe uende kwao, si ndiyo?” aliuliza mama yake.

“Ndiyo mama! Tumelizungumzia hilo pia. Ananipenda na ninaomba mumkubali,” alisema Saida.

“Mmh!”

“Nawaombeni jamani! Nataka niolewe na Kareem,” alisema Saida.

Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, machozi yalikuwa yakimlenga, moyo wake ulimpenda sana mwanaume huyo na hakuwa radhi kumuona akiondoka mikononi mwake.

Wazazi wake hawakuwa na jinsi, binti yao alipenda, tena kitu kizuri ni kwamba alimpenda mwanaume wa dini yake hivyo suala la kuoana halikuwa tatizo kabisa. Wakamkubalia na kumwambia kwamba huyo Kareem alikaribishwa kwenda Tanzania na kujitambulisha.

“Nashukuru sana,” alisema Saida.

“Usijali binti yetu. Ila utatakiwa kuwa makini! Hutakiwi kumwamini kila mtu kwenye mtandao,” alisema baba yake.

Saida akamwambia Kareem kilichokuwa kimetokea, ilikuwa ni furaha kwake na alimuahidi kwamba ndani ya wiki moja angekuwa nchini Tanzania. Hilo ndilo likafanyika, kama utani, Kareem akatua nchini Tanzania.

Kitendo cha kumuona Saida uwanja wa ndege kilimfurahisha, akamfuata na kisha kukumbatiana. Huyo ndiye alikuwa msichana wake, aliyempenda kwa moyo wa dhati na ndiye aliyemfanya kusafiri kutoka nchini Oman mpaka Tanzania kwa ajili yake.

“Karibu mpenzi! Siamini kama umekuja kuniona,” alisema Saida, alishindwa kuyazuia machozi yake.

“Nimekuja kwa ajili yako! Nyumbani wazima lakini?”
“Wazima!”

Wakaondoka na kwenda hotelini. Wakafika katika Hoteli ya Nyota Tano ya Caspean iliyokuwa Mikocheni B na kutulia huko. Wahudumu wa hoteli hiyo walipomuona Kareem, hawakuamini kama kwenye dunia hii kulikuwa na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa mwanaume huyo.

Kila mmoja alimpenda, walimuonea wivu Saida na kuona kama alikuwa mwanamke mwenye bahati kubwa, kuwa na mwanaume kama Kareem halikuwa jambo la kawaida hata kidogo.

Kareem akaenda kuoga huku akimwacha Saida chumbani. Alipomaliza, akatoka, akajifuta maji, baada ya dakika kadhaa, wote wakajikuta wakiwa watupu kitandani na ni sauti za mahaba ndizo zilizokuwa zikisikika chumbani humo.

Sauti hizo zilisikika kwa saa moja, wote wakainuka na kuelekea bafuni kuoga, baada ya hapo wakaondoka na kuelekea nyumbani kwa kina Saida.

“Ninatamani kuwaona wazazi wako, inaelekea ni watu wazuri sana mpenzi,” alisema Kareem huku wakiwa ndani ya teksi.

“Bila shaka utawafurahia, wao wenyewe wanatamani sana kukuona,” alisema Saida, hakutaka kuutoa mkono wake kwa Kareem.

Safari hiyo iliwachukua dakika thelathini, wakafika Magomeni Mapipa ambapo wakateremka na kuelekea ndani. Siku hiyo hata majirani walikwenda kwao kwani waliambiwa kuhusu Kareem, hivyo kila mmoja alitaka kumuona.

Kitendo cha kuingia tu, kila mmoja akaanza kupiga makofi. Kareem hakulizoea hilo, alishangaa lakini moyo wake ulikuwa na furaha mno kwani hakuamini kama angepokewa kiasi hicho.

Wazazi wakamfahamu siku hiyo, wakamkaribisha na kutoa baraka zote kwamba binti yao awe na mwanaume huyo. Kwa kuwa familia ya Saida haikuwa ya kitajiri na nyumba waliyokuwa wakiishi haikuwa nzuri, baada ya wiki moja kukaa nchini Tanzania, alichokifanya Kareem ni kuwanunulia nyumba nyingine iliyokuwa Mbezi Beach, nyumba kubwa na ya kifahari.

“Nitataka mke wangu aishi humu kwa sababu ni mkwe wa bilionea mkubwa,” alisema Kareem.

Ilikuwa ni bahati kubwa, maisha yake hayakuwa na mbele wala nyuma lakini ghafla yakabadilika na kuwa ya mtu fulani mwenye pesa nyingi. Kareem alipanga kuibadilisha familia hiyo kwa sababu tu alimpenda mno Saida.

Familia ikapewa hela nyingi na kufungua biashara. Wakatoka Magomeni Mapipa na kuelekea Mbezi Beach huku wakiyaendesha maisha yao huko. Kwa familia nzima, hawakuamini kilichokuwa kikiendelea, wakati mwingine walihisi kama maigizo ambapo baadaye ‘scenes’ zao zingeisha na kurudi Magomeni au kwenye ndoto ndefu nzuri na ya kusisimua na baadaye wangeamka na kujikuta wakiwa vitandani. Hiyo haikuwa filamu, haikuwa ndoto bali kilikuwa kitu halisi kilichokuwa kikiendelea.

Baada ya kukaa nchini Tanzania kwa wiki mbili, Kareem akaondoka na kurudi nchini Oman. Wakati huu baba yake hakutaka arudi na ndege ya abiria ila alichokifanya ni kumtumia ndege binafsi na kurudi nyumbani kwao.

Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa Saida, alitokea kumpenda mno msichana huyo. Aliwahi kuwa kwenye uhusiano na wasichana wengine lakini kwa Saida, alikuwa tofauti, alikuwa msichana mwenye furaha mno, tabasamu pana ambaye alimjali kupita kawaida.

Hakutaka kuondoka, alitamani aendelee kubaki nchini Tanzania kwa kipindi chote kwani kuwa mbali na msichana huyo tayari ikaonekana kuwa kama mateso makubwa. Ndani ya ndege, kazi yake ilikuwa ni kuwasiliana na mpenzi wake kupitia WhatsApp. Kila mmoja alikuwa akimuonyeshea mwenzake jinsi alivyokuwa akimpenda.

“Hakika nitaishi na wewe mpaka kifo kitakapotutenganisha, na siku ya kufa, nitataka nife nikiwa mikononi mwako,” aliandika Kareem.

“Kama Romeo na Juliet...”

“Ndiyo mpenzi! Nitakupenda hata zaidi ya Romeo alivyompenda Juliet. Wewe ni mama wa watoto wangu, nisingependa kuona ukiteseka, katika maisha yako yote, nitakuwa nawe bega kwa bega. Nakupenda mpenzi,” aliandika Kareem.

Waliwasiliana mpaka ndege ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat nchini Oman ambapo akapanda ndani ya gari lililokuja kumchukua na kwenda nyumbani kwao.

Baada ya kulala siku hiyo, siku iliyofuata, Kareem akawaambia wazazi wake juu ya safari yake, aliwaambia namna alivyokutana na msichana huyo huko, alivyopokelewa mpaka kurudi nchini Oman.

Wazazi wake wakawa na furaha mno hivyo walichokihitaji ni msichana huyo afunge safari na kwenda Oman. Hilo halikuwa tatizo kabisa, baada ya wiki kadhaa, Saida akatumiwa tiketi na hivyo kupanda ndege kwa mara ya kwanza na kuelekea nchini Oman.

Alivaa kiheshima, juba jeusi huku kichwani akiwa amevaa ushungi uliozifunika nywele zake. Miguu yake hakuiacha wazi, alivalia soksi kwani alizijua sheria kali za nchi hiyo jinsi walivyokuwa wakikemea mwanamke kutokujisitiri.

Baada ya saa kumi na tano, akafika huko. Alipomuona mpenzi wake, Kareem, akamsogelea na kisha kusalimiana naye kwani alijua kabisa kwamba sheria za kidini za nchi hiyo zilikemea mambo mengi mpaka pale watu walipokuwa wameoana.

Kama alivyopokelewa Kareem nchini Tanzania ndivyo alivyopokelewa yeye nchini Oman. Wazazi wa mwanaume wake walifurahi kumuona na walimkaribisha kwa mikono miwili.

Kutokana na nchi hiyo kutotaka watu kujihusisha na mambo ya kimapenzi kwa kuishi pamoja na wakati hawakuwa wameoana, ilichokifanya familia hiyo ni kumtambulisha Saida kama mfanyakazi kutoka Afrika.

“Ila utatakiwa kuwa makini!” alisema baba yake Kareem.

“Hakuna tatizo baba!”
“Hutakiwi kufanya mapenzi na huyu msichana, si unajua unaweza kumpa mimba kwa bahati mbaya! Ukiona umempa mimba, jua kwamba atauawa kwa kupigwa mawe kama sheria yetu inavyosema,” alisema baba yake.

“Hicho kitu hakiwezi kutokea, siwezi kumpa mimba Saida.”
“Basi sawa. Nashukuru.”

Hicho ndicho alichokijua kwamba asingeweza kufanya mapenzi na Saida hivyo asingeweza kumpa mimba msichana huyo. Ukaribuni wao wa kimahaba ulikuwa ndani ya nyumba tu na wageni walipokuwa wakifika, ilikuwa ni vigumu kugundua kwamba watu hao walikuwa wapenzi kwa namna ambavyo walivyokuwa wakiishi, Saida alionekana kama mfanyakazi wa ndani nyumbani hapo.

Siku zikakatika na hatimaye wiki ya kwanza ikatimia. Hakukuwa na mabadiliko yoyote yale lakini kipindi hicho mwili wa Kareem ukaanza kumuhitaji msichana huyo. Alikuwa mpenzi wake na alikataliwa kufanya naye mapenzi, hakutaka kukubali tena kwani kila alipokuwa naye faragha, msichana huyo alimtamanisha kupita kawaida.

Alichokifanya ni kuanza kuelekea chumbani kwa Saida kila siku usiku. Hakukuwa na mtu yeyote aliyeligundua hilo, huko, walikuwa wakikumbatiana mpaka saa kumi alfajiri ambapo alikuwa akitoka na kwenda msikitini.

Hayo yakawa maisha yao, hakukuwa na siku ambayo Kareem hakuwa akitoka chumbani kwake, walifanya sana mapenzi kisiri, wazazi hawakugundua kitu chochote kile, hawakujua kwamba kila siku watu hao walikuwa wakikutana chumbani kitandani na kufanya mapenzi walivyotaka.

Baada ya mwezi mmoja kutimia tangu Kareem aanze kuelekea chumbani humo, hali ya Saida ikaanza kubadilika. Mwili wake ukaanza kuchoka, kichefuchefu kikamshika na hatimaye kuanza kutapika.

Mara ya kwanza walichukulia ni tatizo la kawaida ila baada ya kuendelea kutokea mara kwa mara Kareem akahisi kwamba mpenzi wake alikuwa na mimba. Akamchukua na kuanza kuzungumza nayye pembeni, alitaka kujua ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea.

“Unasemaje?” aliuliza Kareem kana kwamba hakusikia aliambiwa nini.

“Nina mimba mpenzi! Mimba imeanza,” alisema Saida, hapohapo Kareem akakaa chini. Hakuamini alichoambiwa.

“Unasema kweli?”
“Ndiyo!”
“Mungu wangu! Tumekwisha..” alisema Kareem huku kijasho chembamba kikianza kumtoka.

Aliikumbuka vilivyo adhabu ya kifo waliyokuwa wakihukumiwa watu wengine mara baada ya kupewa mimba. Hakutaka kuona hilo likitokea kwa msichana aliyekuwa akimpenda, tena aliyekuwa na mtoto wake tumboni.

Ilikuwa ni rahisi kumwambia Saida aondoke na kurudi nchini Tanzania lakini ugumu uliokuwepo ni kwamba kulikuwa na sheria ya kuwapima mimba watu wote waliokuwa wakitaka kuondoka nchini humo kwani kabla ya hapo, wengi walikimbia nchi hiyo baada ya kuona kwamba walikuwa wajawazito kwani mbali na kupima, kwa wale waliokuwa wameolewa, walitakiwa kuonyesha vyeti vyao vya ndoa kujua kama walikuwa ndani ya ndoa.

“Kwa hiyo?” aliuliza Saida huku akionekana kuogopa.

“Sijajua! Saida, ninachohofia ni kwamba utauawa kwa kupigwa mawe tu,” alisema Kareem huku akionekana kuwa na hofu moyoni mwake.

“Haiwezekani! Ni lazima niitoe.”
“Utaitoaje? Ukienda hospitali, daktari haruhusiwi, na akijua una mimba, kitu cha kwanza kitakuwa ni kuitaarifu serikali. Saida, nimechanganyikiwa,” alisema Kareem maneno yaliyomfanya Saida kukata tamaa ya kurudi nchini Tanzania, iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuuawa kwa kupigwa mawe.

Je, nini kitaendelea?
Usikose kuungana nami siku ya Jumamosi hapahapa.

Nyemo Chilongani.
 

Attachments

  • gggg.jpg
    gggg.jpg
    70.2 KB · Views: 24
SITALIA TENA-02

Kareem alimpenda Saida, hakutaka kuona akimpoteza msichana huyo ambaye kwake alikuwa kila kitu, kubwa zaidi ni kwamba alikuwa na mimba yake, hivyo kwa namna moja ama nyingine ilikuwa ni lazima amuokoe kutoka katika mkono wa kifo.

Alikuwa chumbani, hakutulia, alikuwa akizunguka huku na kule akifikiria ni kitu gani alitakiwa kufanya. Alihitaji msaada kipindi hicho, akaanza kuwafikiria marafiki zake ambao aliamini kwamba wangemsaidia kumnasua mpenzi wake katika kifo kilichokuwa kikimsogelea.

Alikuwa na marafiki wengi ambao aliamini kwamba wangeweza kumsaidia lakini wakati akiwafikiria hao wote, kichwani mwake alikuja mmoja ambaye alikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba angemsaidia kumtorosha msichana huyo nchini humo.

Rafiki yake huyo alikuwa Al Khalid, mtu ambaye alikua naye tangu akiwa mtoto mpaka kipindi hicho. Alichokifanya ni kuchukua simu yake na kuanza kulitafuta jina lake, alipolipata, hakutaka kuchelewa, harakaharaka akampigia simu.

Simu iliita pasipo kupokelewa, iliendelea kuita mpaka ilipokatika. Hakutaka kukoma, alichokifanya ni kupiga tena kwani mtu huyo alikuwa muhimu sana, alikuwa mtu pekee ambaye angeweza kumuokoa kutoka katika tatizo kubwa alilokuwa nalo kipindi hicho.

“Al Khalid! Can we meet somewhere! (Al Khalid! Tunaweza kuonana sehemu?) aliuliza Kareem mara baada ya simu kupokelewa, hata salamu hakutaka kutoa.

“What is it?” (kuna nini?)
“There is something I want you to help me,” (kuna jambo nataka unisaidie mara moja!) alijibu Kareem.

Hilo lilikuwa jambo dogo kwa Al Khalid, mara kwa mara walikuwa wakipigiana simu na Kareem kuomba kusaidiana katika mambo mengi ambayo kwa namna moja au nyingine yaliufanya urafiki wao kuendelea kukomaa zaidi.

Alimjua Kareem, alikuwa mtu wa kupenda kuyafanya mambo mengi kivyakevyake na kama kulikuwa na kitu alichokuwa akihitaji msaada, basi kitu hicho kilikuwa kikubwa ambacho kwa namna moja au nyingine alikwama kabisa kukifanya.

“Lipi? Baadaye nitakwenda Masjeed, unataka nikusaidie katika lipi?” aliuliza Al Khalid kwenye simu.

“Naomba tuonane kwanza.”
“Ila si unajua kwamba leo tunasubiri mwezi uandame ndiyo tuanze kufunga?”

“Najua! Ila naomba tuonane kwanza.”

Al Khalid na Kareem walikuwa marafiki wakubwa huku wote wakiwa watoto wa mabilionea wakubwa nchini Oman. Waliaminiana kwa kila kitu, walipendana ila tofauti yao ilikuwa moja tu.

Al Khalid alikuwa mtu wa dini haswa, alikuwa mtu wa swala tano, hakutaka kusikia adhana akiwa nje ya msikiti, katika maisha yake yote, alimpenda Mungu na hakutaka kufanya dhambi kabisa.

Kwa Kareem ilikuwa tofauti, hakuwa mtu wa swala, wakati mwingine aliombea misikiti yote ya Oman ibomolewe na kujengwe klabu kwa ajili ya kula bata usiku kama ilivyokuwa Dubai, Qatar na nchi nyingine zilizokuwa katika muunganiko wa Emirates.

Wawili hao wakaonana katika Mgahawa wa Ya Sadeek uliokuwa katikati ya Jiji la Muscat. Wakaonana hapo na kuanza kuzungumza mambo mengine kabisa. Kichwani mwa Kareem kulikuwa na mambo mengi, alikuwa akijiuliza kama lilikuwa jambo sahihi kumuomba msaada Al Khalid au amuache na kuomba msaada sehemu nyingine.

“Nina kitu nahitaji unisaidie,” alisema Kareem.

“Kuhusu nini rafiki?”

Kareem akamwambia ukweli Al Khalid kilichokuwa kimetokea, hakutaka kumficha kitu chochote kile, alikuwa rafiki yake wa dhati, akamuweka wazi kwamba alimpa mimba msichana ambaye alikuwa mfanyakazi wa ndani hivyo alihitaji msaada wa kuweza kumtorosha kutoka nchini humo.

Al Khalid alishangaa, hakuamini alichokisikia kutoka kwa Kareem. Alishangaa kwani lilikuwa jambo lisilo la kawaida kwa Mwarabu kufanya kitu kama hicho, kumpa mimba msichana na wakati alijua fika kwamba adhabu kubwa kwa msichana ilikuwa ni kunyongwa.

“Unanitania Kareem,” alisema Al Khalid.

“Ni kweli! Naomba unisaidie. Mpaka nimekwambia hili ni kwamba ninahitaji msaada wako,” alisema Kareem.

“Mmh! Hebu nikajifikirie, nitajua ni kipi tunachotakiwa kufanya,” alisema Al Khalid na kisha kuagana.

Moyo wa Kareem ukarudi kwenye tumaini kubwa, akaona kwamba hatimaye angeweza kusaidiwa na rafiki huyo na kumtorosha Saida nchini humo. Aliporudi nyumbani, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuonana na msichana huyo kisha kuzungumza naye.

Alimwambia mpango aliokuwa ameufanya wa kumtorosha nchini hapo pasipo mtu yeyote kugundua hilo. Saida akashusha pumzi, ni kweli alitamani kuondoka nchini humo lakini kitu kilichomtisha ni kwamba Kareem alilitoa jambo hilo nje ya nyumba yao, akahisi hapo ndipo kulipokuwa na tatizo.

“Kareem, utamuamini vipi rafiki yako?” aliuliza Saida.

“Usijali! Ni rafiki yangu sana, hawezi kufanya kitu chochote kibaya. Naomba umuamini!” alisema Kareem huku akimwangalia Saida.

Walibaki sebuleni wakizungumza, walionekana kama marafiki wa kawaida na hakukuwa na kitu chochote kilichokuwa kikiendelea. Suala hilo bado liliendelea kuwa siri, hakukuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba aliyelifahamu zaidi ya wao wawili.

Ilipofika saa moja usiku, wazazi wake Kareem wakarudi nyumbani. Kila mmoja alibaki akisikilizia kuona kama mwezi uliandama au la! Kwa siku hiyo, redio zote nchini Oman zikiwemo TunIn Fm, Hi Fm na nyingine zilitangaza kwamba siku hiyo mwezi haukuwa umeandama hivyo ilikuwa ni lazima siku inayofuata kula ila siku nyingine inayofuata ni kufunga.

“Kesho itatubidi twende kufanya manunuzi sokoni kwa ajili ya futari ya keshokutwa,” alisema mama yake.

“Hakuna tatizo!” alijibu Kareem.

Wakatulia sebuleni lakini muda mwingi Kareem na Saida walikuwa wakiangaliana kwa macho ya kimahaba. Ilipofika saa tatu usiku, wakasikia geti kubwa likigongwa. Kupitia kamera za CCTV zilizofungwa kila kona nyumbani humo, wakaliona gari la polisi likiwa limesimama nje ya geti.

Kila mmoja akashtuka, halikuwa jambo la kawaida kwa polisi kufika nyumbani hapo, tena kwa usiku kama huo. Wakamwambia mlinzi afungue geti kwa rimoti maalumu, geti likafunguliwa na polisi wawili waliokuwa na silaha kuingia ndani.

Wakamuulizia mzee Abdoulaziz, wakaambiwa yupo, wakaufuata mlango na kuingia na kuanza kugonga. Kareem akahisi kitu, harakaharaka akasimama kutoka kitini, akamshtua Saida naye asimame, akafanya hivyo na kuanza kuelekea chumbani.

“Kuna nini?” aliuliza Saida.

“Nina hofu na hawa polisi. Mungu wangu! Al Khalid atakuwa amewaambia polisi,” alisema Kareem huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Unasemaje?”
“Nahisi itakuwa hivyo!”

Wakati wakizungumza hivyo chumbani. Mara mlango wa chumba hicho ukaanza kugongwa. Kareem akajiuliza kama alitakiwa kuufungua au la. Wakati huo, Saida alikuwa akitetemeka mno chumbani humo, alitamani kufumba macho na kufumbua awepo nchini Tanzania.

Wakati akijiuliza, akashtukia mlango ukipigwa teke, polisi wawili wakaingia chumbani humo. Hawakutaka kumkamata Kareem, walichokifanya ni kumchukua Saida.

“Kuna nini?” aliuliza Kareem huku akijaribu kuwazuia wasimchukue mpenzi wake.

“Taarifa zinasema ana mimba.”
“Hapana! Hana mimba!”

“Unabishana na wapelelezi wetu. Tumekuja na daktari kwa ajili ya vipimo,” alisema polisi mmoja.

Wakatoka ndani ya chumba hicho huku wakiwa wamemfunga pingu Saida. Kareem alibaki akitetemeka. Saida alikuwa akilia kwa sauti, hakutaka kutoka ndani ya nyumba hiyo, hakutaka kumuacha mpenzi wake lakini kutokana na kutolewa kinguvu, hakuwa na jinsi.

Wakamchukua na kumuingiza ndani ya gari, alikuwa akilia mno, polisi hao hawakutaka kujali, kwao, sheria ya nchi ilipewa kipaumbele kuliko kitu chochote kile. Gari likawashwa na kuondoka mahali hapo, lilipoelekea, lilikwenda katika kituo kikubwa cha polisi hapo Muscat kwa ajili ya kupelekwa mahakamani kesho asubuhi na mchana adhabu ya kupigwa mawe itolewe na kufanyiwa kazi hata kabla mfungo wa Ramadhani haujaanza.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne.
 
Habari mambo naitwa Mr Equator Nimeandika ujumbe huu kuku omba swala moja tu!
Mimi nimetengeza website ya ku share story ambayo ni EquatorStory
Je umekuwa ukipata tabu kupost story zako hapa?
Hili ndo suluhisho lako.
Mimi nataka nkupe nafasi ya kuwa mmoja wapo wa kwanza kutumia hii website
unda account yako na uweze kupost story yako mpya.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom