SEHEMU YA 02
Kukutana kwao ilikuwa ni humohumo chuoni, wakati Shadya alipokwenda kujiunga na madrasa hiyo, Ngwali alichanganyikiwa, alijitahidi kuwa naye karibu, kumsaidia na mwisho wa siku kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Sheria za dini hazikuruhusu, hata sheria za madrasa hiyo hazikuruhusu hivyo walifanya mambo yote kwa siri huku wakiwa makini kwenye kuepuka siku za hatari kwa msichana huyo.
Japokuwa watu wengi wa huko hawakuamini kama msichana alitakiwa kusoma kipindi hicho lakini mzee Hamduni alikuwa na jukumu la kumsomesha binti yake ili siku moja aje kuwa na maisha yake, apate kazi nzuri na kulipwa mshahara mnono.
Alimkazania kila siku, alitumia pesa zake kuhakikisha anasoma, tena kwa kufaulu vizuri huku wakati mwingine hata wao wenyewe kama wazazi wakijinyima.
Mbali na huyo Shadya pia kulikuwa na kijana wao mwingine, alikuwa pacha wa Shadya, kijana huyo aliitwa Rahim.
Kwa kumwangalia harakaharaka, Rahim alifanana sana na Shadya, alibarikiwa kuwa na uzuri, wasichana wengi walimpenda, wakatamani kulala naye lakini hakukuwa na kitu alichokuwa akikiogopa kama kulala na mwanamke, kama ni kidume basi aliitwa ‘Joka la Kibisa.’
Pamoja na kuwa na umri wa miaka ishirini na moja lakini Rahim aliogopa wanawake waliokuwa wakijipeleka kwake kimahaba, hakutaka kusikia lolote kuhusu wanawake hao na hata walipokuwa wakimwambia kuwa walimpenda, hilo halikumuingia kabisa akilini.
“Rahim niangalie kwanza,” alisema mwanamke mmoja huku akimwangalia Rahim aliyekuwa kwenye kochi. Siku hiyo alishindwa kuvumilia, alimpenda sana kijana huyo kiasi kwamba alikuwa tayari hata kuvunja ndoa yake lakini mwisho wa siku alale naye.
Alivizia muda ambao mume wake alikwenda kazini ndipo akamleta kijana huyo ndani na kumuweka kwenye kochi. Alivua juba lake na kubaki na sketi fupi laini iliyoifanya miguu yake kuonekana mpaka juu ya magoti kidogo na kumwangalia Rahim ambaye hata kusisimka hakusisimka.