SEHEMU YA 03: JIJINI DAR ES SALAAM
JAMAL TWAHA ambaye baadaye alikuja kufahamika kama JT ni kijana ambaye nyota yake iling’aa kwa haraka sana. Ingawa alikulia katika maisha ya kijijini lakini alipoingia jijini Dar es salaam hakuna kilicho msumbua, alijikuta akifanikiwa kwa kila alicho kifanya. Kunawatu walisema kuwa anatumia kizizi au kuhisi kuwa anadawa fulani hivi.
JT alikuwa na sura ya kuvutia wasichana wengi walivutiwa naye ila yeye hakutaka kuharakisha maswala ya mapenzi. Kwake kazi ilikuwa ni muhimu zaidi na alijua tu kuwa ipo siku atampata ampendaye na kufunga naye pingu za maisha. Kwa muonekano wa nje Jamal alifananishwa na mwanamuziki wa kimarekani aliyeitwa Justin Timberlake, na ndio maana watu wengi walikuwa wakimwita JT.
Jamal hakuwa mtu wa kuchagua kazi, alifanya kazi za kila aina ili aweze kujikimu na maisha ya mjini lakini Mungu hamtupi mja wake Jamal alifanikiwa kupata kazi ya udereva wa daladala. Kwakuwa Jamal alisomea kozi ya udereva na kufanikiwa kupata Leseni ya daraja C ilikuwa ni rahisi kwake kupata kazi hiyo.
“Ndugu yangu Jamal wewe utaendesha hili gari mpaka pale utakapoona inatosha,” Jamal hakuamini ukarimu aliopewa na tajiri mmoja wa kihindi aliyeitwa Patel. “Yaani mtu hanifahamu lakini ananiamini kunikabidhi chombo!” alijisemea moyoni Jamal na kujibu kwa kauli moja tu, “ahsante ndugu yangu.” “Naona una wasiwasi usijali kwani nilipewa sifa zako na marafiki zangu uliowahi kufanya nao kazi, wamenipa sifa zako za ucha Mungu na nidhamu ya kazi nami nimekuamini na kukukabidhi gari hili ulitunze,” alimalizia Patel na kumkabidhi Jamal ufunguo wa garihiyo aina ya Eicher.
Walimalizana na Patel na kuanzia siku hiyo Jamal alikuwa dereva maarufu sana wa Daladala ndani ya jiji la Dar es Salaam, hakuna kondakta, dereva au askari wa barabarani ambaye alikuwa hamfahamu JT. Kuanzia vituo vyote vya mabasi kama Makumbusho, Mawasiliano, Mwenge na sehemu nyingi wote walimfahamu na haswa pia ilikuwa ni ule mfanano wake mkubwa na mkuu mpya wa mkoa wa Dar es salaam aliyeitwa David Adam Billy!
Hata siku moja haikusikika Jamal kukosana au kugombana na bosi wake yule mhindi aliyemkabidhi daladala, kama ni hesabu ya siku aliikabidhi inavyo paswa. “Bosi leo hali ilikuwa mbaya kidogo gari lilipata hitilafu kwahiyo… ehh?!” kabla hajamalizia mazungumzo kwenye simu utasikia Patel akimjibu tu kwa haraka,“oohh Jamal pole sana nimekuelewa usijali utapunguza kwenye hesabu gharama ya matengenezo ya gari hivyo usijali.” Kimsingi ni kuwa walielewana sana na bosi wake na hata siku moja hawakuwahi kukwazana. Jamal alitambua alipotoka hivyo alifanya kazi yake kwa uaminifu.
Taarifa za kuwa kuna kijana dereva wa daladala anayefanana na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ndugu David Adam Billy zilimfikia mkuu huyo wa mkoa. Hivyo mkuu wa mkoa alituma watu kufuatilia na kisha kupata mawasiliano ya kijana huyo. Sikumoja mchana JT alipokuwa kwenye harakati zake za barabarani alishangaa simu yake ikiita na namba ngeni kuonekana, ngrii! ngrii! Simu iliita ilimbidi kupokea ijapokuwa sio kawaida yake kupokea namba ngeni kwani mara nyingi huwa ni za wasichana wanaomsumbua wakitaka awenao kimapenzi.
“Hello, habari unaongea na mkuu wa mkoa ndugu David Billy, hivyo nilikuwa nahitaji kesho asubuhi tuonane ofisini kwangu bila kukosa…” “Eeh sawa, nani…?!” wakati JT anajiumauma simu ilikuwa imesha katwa hapo sasa mapigo ya moyo yakawa yanaongezeka.
****
Jamal aliamka alfajiri mapema na kujiandaa kwakuwa ilikuwa ni siku ya Jumatatu alitaka kuwahi mapema kwa mkuu wa mkoa ili kama akirudi basi aendelee na shughuli zake kama kawaida. Alimjulisha kondakta wake kuwa atachelewa kufika kazini siku hiyo na hivyo amtafute dereva wa muda kwa siku hiyo.
JT alikuwa ni kijana anaye jali muonekano wake, kwa siku hiyo alivaa vizuri sana, suruali nyeusi ya kitambaa na shati jeupe lenye mistari ya bluu na mikono mirefu. Alichomekea vizuri na kwakweli alikuwa anapendeza sana. Alipo ingia pale ofisi ya mkuu wa mkoa maeneo ya Ilala boma jambo la ajabu lilitokea, kuna askari walikuwa wakimpigia saluti wakati wafanyakazi wa kada nyingine wakimpa ukarimu wa hali ya juu.
Ni kweli, Jamal alifanana sana na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ndugu David Adam Billy. Wote hawakuamini baada ya kumuona mkuu wa mkoa anakuja kumlaki JT kwa kumbatio, walikumbatiana na wote wakafurahi sana. Ilikuwa ni kama ndugu walio potezana kwa muda mrefu. “Mkuu huyu ni pacha wako? Nilimfananisha kabisa na wewe pale getini,” alisema yule askari aliyempigia saluti JT pale getini. “Ndio huyu ni ndugu yangu kabisa,” alijibu mheshimiwa Billy huku akitabasamu.
Kiukweli Jamal alikuwa na bahati sana, pamoja na kuwa hakusoma sana lakini mafanikio yake yalionekana dhahiri tangu alipo ingia jijini Dar es salaam. Hata pale mkuu wa mkoa alipo mpa ajira katika ofisi yake Jamal alibaki mdomo wazi. “Kuanzia sasa hivi achana na daladala, kazi yako itakuwa ni kumuendesha huyu afisa wa idara ya ardhi,” aliongea RC David Billy alipokuwa anamkabidhi JT kwa afisa ardhi huyo.
Na ndivyo ilivyokuwa JT akawa ameajiriwa, alifanya kazi kama dereva akihama kutoka kitengo kimoja kwenda kingine. Aliendesha magari ya aina tofauti kuanzia Toyota Harrier, VX, Prado na hata Land Cruiser. Mtaani hakuna aliyetambua kwamba magari hayo JT sio yakwake bali ni ya mabosi wake. Watu wengi walipomwona akibadilisha vyombo vya usafiri walijua kwamba yeye ndiye mmiliki halali wa vyombo hivyo, hali hiyo iliongeza yeye kufukuziwa na wasichana wenye urembo wa kila aina!
Baada ya kufanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja JT alifanikiwa kujenga nyumba maeneo ya Madale na hivyo kuhamia katika nyumba yake. Alifikiria kuwa huo ndio muda wake muafaka wa yeye kutafuta mwenzi wa kufunga naye pingu za maisha, hata wazazi wake kule kijijini walikuwa wakimsumbua katika hilo pia, kila siku maswali ya utaoa lini yalikuwa hayawaishi midomoni mwao.