Simulizi: Bupe wowowo

Simulizi: Bupe wowowo

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2016
Posts
20,746
Reaction score
25,638
24796617_1901925513183185_5177912437045039521_n.jpg

Nyemo Chilongani
Bupe Wowowo

Ukiniambia nimuelezee msichana huyu, cha kwanza nitaanza na macho yake. Ni msichana mrembo, asiyeisha hamu hata ukikaa na kumwangalia. Alikuwa na umbo namba nane, umbo kali, balaa ambalo kila alipopita wanafunzi wote tulikuwa tunamwangalia.

Aliitwa Bupe! Bupe alikuwa Bupe kweli! Alijua kuringa, alijua kujitingisha, alijua kututega mpaka wanaume tukachanganyikiwa. Kuna watu wengi walimpenda, labda wa kwanza nilikuwa mimi kwa sababu kila siku kabla ya kulala alikuwa mtu wa mwisho kupita akilini mwangu na wa kwanza kumkumbuka kila nilipoamka.

Unaweza kusema sikupenda masomo, hapana, niliyapenda ila hayakushinda upendo wangu juu ya Bupe. Sijui ilikuwaje! Labda alijua kama nampenda! Labda alijua kwamba silali bila yeye, au alijua kwamba kila nilipomuona moyo wangu ulitetemeka sana kwani kila alipopita, alikuwa akijitingisha mno wowowo lake.

Nilimpenda Bupe, niliogopa kumwambia ukweli, nilihisi angenikataa kwa sababu nilikulia Tandale, pale shuleni, nilijitenga kwa kujiona mtoto wa uswahilini, hata kama nilimuheshimu kila mtu lakini waliona kama nawaigizia.

Wanaume hawakutaka kuchelewa, wakaanza kumfuata Bupe na kuwaambia ukweli kuhusu mioyo yao, upendo wao wa dhati juu ya msichana huyo, kitu cha ajabu sana aliwaambia kwamba alikuwa na mpenzi, mzuri, aliyempenda na aliyejua kupenda, alipouliza ni nani, eti akawaambia Nyemo.

Nilishtuka, sikujua kama alikuwa akinitega au la. Alinichanganya! Akanipagawisha! Nikaweweseka! Sikuamini kama Bupe yuleyule ninayempenda eti naye alikuwa akinipenda.

Wengi wakaniuliza, na mimi kwa mbwembwe zangu, kwa misifa yangu nikawaambia”Ndiyo! Bupe demu wangu.” Kuwa na demu kama Bupe nilijisikia fahari sana, nikazugazuga lakini kumbuka kwamba sikuwahi kuongea naye.

Mwisho wa siku nikasema sikubali, siwezi kuwa mshika mapembe huku maziwa wanakamua wengine, sikutaka kula kwa macho na wakati nilikuwa na mikono. Nikapiga moyo konde na kumfuata. Nilipomfikia, nikamwambia “Bupe! Nakupenda, naomba uwe mpenzi wangu! Hakika nitakujali sana!” nilipomwambia hivyo, akaniangalia, akanikazia macho na kuniuliza “Are you serious Nyemo?” Nikamwambia ndiyo na ndiyo maana nilisimama mbele yake.

Akacheka sana! Akaumauma lipsi zake! Akanikonyeza kidogo, kicheko kikapungua na kuanza kucheka kicheko fulani hivi amazing.
“Nyemo! Are serious?” akaniuliza tena, na mimi nikamjibu kwamba nipo serious.
“Una hela?” lilikuwa swali lililonichanganya sana! Aliponiuliza kuhusu hela, alimaanisha nini? Ya kumnunulia chai hapo shuleni au hela gani. Nikajipa moyo kwamba inawezekana alimaanisha hela ya vitafunio. Kama nilikuwa nakula mihogo kumi kila siku, nikimpa mitano na mimi nikabaki na mitano kuna tatizo? Harakaharaka nikamjibu ndiyo! Hela ninayo, tena nyingi sana.

“Hahaha! Ila naupenda mwili wako,”aliniambia, akacheka tena kwa kicheko cha mitego kisha akaondoka zake.

Nilibaki nikiwa nimesimama, nilimwangalia, alijua kwamba wanaume nikiwemo mimi walikuwa wakimwangalia, akaongeza machejo mpaka nikahisi kama wowowo lake linataka kudondoka.

Huyu Bupe alinivuruga sana. Kila nilipokuwa nikikutana naye aliniuliza kuhusu hela, na mimi nilimwambia kwamba hela ninayo kwani nilijiamini kwamba kama siku nyingine nilikuwa nawapa ofa ya mihogo wakina Hassani, ningeshindwa nini kumpa Bupe? Nisingeshindwa, hivyo nilitakiwa kukomaa naye.

Wakati naendelea kumsumbua kwa saundi zangu za uswahilini kwa kumwambia kwamba Diamond nimecheza naye, Madee alikuwa msela wangu, kumbe upande mwingine watu wenye mikono yao yao wakawa wanakula tu, wale wenye meno wakawa wanatafuna huku mimi nikibaki kumuuzia sura.

Mwisho wa siku shule nzima wakajua kwamba Bupe alikuwa demu wangu! Wale waliokuwa wakimfaidi, walicheka sana, walinionea huruma kwa sababu, jinsi alivyokuwa Bupe na mimi, ilikuwa ni sawa na kufika Tandale kwetu na kuona sehemu wanauza Baga, kilikuwa kitu kisichowezekana hata kidogo.

Washikaji zangu wakajua tu kwamba nampenda Bupe, wakaniita na kunishauri kwamba mtoto nimpeleke nyumbani, halafu akifika huko, namaliza kazi.

“Hivi mnaijua nyumba yetu nyie?” niliwauliza, wote wakaangaliana na kuanza kucheka.
“Kwani huna mshikaji wenye kideo ukutani?’ mmoja aliniuliza.
“Ninaye!”
“Huna mwana anayepiga blingblingi akuazime nguo?”
“Ninaye!”
“Sasa tatizo lipo wapi? Ng’oa mzigo kaka!”

Walinipamba weeeee, nikakubaliana nao na kumwambia Bupe. Akaniangalia mara mbilimbili kwa lile jicho lisemalo “Mimi nije kwenu! Tandale Kwa Tumbo! Kule kwenye wezi wa simu! Bupe mimi ninayeishi Tabata! Ni kitu kisichowezekana hata kidogo.”

Nilijua tu kwamba alikuwa akiniambia hivyo kimoyomoyo! Na mimi nikamwangalia jicho la kumwambia “Mbona utakuja tu! Nina geto kali la mchizi, kideo ukutani, Dstv, choo cha kuflashi, mbona utashangaa mwenyewe. Wewe twende kwanza,” macho yangu yalisema maneno hayo.

Kwa mbali nikamuona Bupe akitabasamu, akanisogelea kidogo na kunishika mkono, mapigo ya moyo yakawa juu.
“Nyemo! Kwenu ni vichochoroni?’ aliniuliza huku akiniangalia.
“Ndiyo! Kwa nini umeuliza?”
“Sitaki kukabwa!”
“Nitakuwa pamoja nawe. Hutokabwa.”
“Basi nitakuja Jumapili. Sawa baba watoto?”
“Sawa mamii!’

Kabla ya yote nikawaandaa masela kabisa, nikawaambia mtoto anakuja, cha kwanza nahitaji geto la mwanangu Noel kwa saa mbili tu, akanikubalia, mbali na yeye nikachonga na mwanangu Rajabu, akanipa nguo. Siku hiyo wakati namsubiri, nilikuwa nashaini kinoma.

Jumapili hiyo ikaingia. Bupe ndani ya Tandale. Nilimuona anashuka kwenye ndinga kali sana, ilikuwa ikiendeshwa na mzee mwenye ndevu nyeupe, akaja nilipo, ndinga ile ikaondoka na sisi kusepa kuelekea home kwa msela.

Unajua geto umelifanyia usafi ile kinoma, kunang’aa, viatu vya mshikaji umevipanga vizuri lakini demu alipoingia ndani, niliona kabisa kabadilika.

“Hapa ndiyo kwako?” aliniuliza.
“Yeah! Unataka kinywaji gani?” nilimuuliza huku nikifungua friji. Mtu mzima nilijiandaa, humo niliweka chua za soda za 7Up mbili, ndani nilijaza maji na kukikandamiza kisoda chake. Pia kulikuwa na chupa moja ya Fanta, sikuwa na uwezo wa kununua soda mbili. Nilipotoa, nikawahi chupa ya 7Up manake angeitaka yeye ingekuwa balaa.

“Kunywa soda ya wanawake hiyo! Sisi wanaume tunakunywa 7Up!” nilimwambia kwa mbwembwe huku nikimfungulia, ili asionekane kuitaka ile 7Up niliyoweka maji, nikapiga funda moja fasta.
“Umejitahidi chumbani kwako japo bado kunaonekana local sana,” aliniambia huku akiangalia huku na kule.

Kile chumba ndicho kikali kuliko cha washikaji zangu wote, yeye anasema ni local, je, inamaanisha mageto anayoingia yeye ni hatari sana, yana AC, Tv nchi 50, kapeti unyoya na madude mengine ya hatari.

“Ndiyo tunajipanga mdogomdogo. Ila umependeza! Hiyo nguo umenunua wapi manake imekutoa chicha mno,” nilimwambia harakaharaka huku nikimtoa katika ishu ya kuzungumzia geto manake nilishaumbuka.

“Kariakoo! Nikuulize kitu?”
“Uliza tu!”
“Unanipenda?”
“Hapo umeniuliza au umeniambia?”
“Nimekuuliza!”
“Mimi naona umeniambia. Ninavyokupenda, hakuna mfano! Ninakupenda mno! Angalia macho yako, kama umekula kungu, mtoto una kitumbo fulani hivi amazing, jicho nyanya, shavu laini, lipsi nene, miguu imejaajaa sana! Bupe, kwa kifupi, kila nikikuangalia natamani uuruhusu ulimi wangu ufanye ziara mwili wako wote,” nilimwambia huku nikiachia tabasamu, eti cha ajabu na mimi ninawa narembua macho.

“Hahah! Una maneno matamuuuuuu!”
“Bila shaka ya kumtoa nyoka pangoni, maneno yaliyowafanya wakoloni watuachie nchi yetu,” nilimwambia na kumsogelea zaidi, nikaupeleka mkono mapajani mwake.

“Jamani! Unataka kufanya nini?” aliniuliza kwa sauti fulani hivi nyororoooo...yaani kwa jinsi mambo yalivyokuwa yakiendelea mule ndani, nikasema mtoto kushnei.
“Nataka kufanya nini?”
“Ndiyo!”
“Kuimba wimbo wa CCM Mbele kwa Mbele!”
“Hahaha! Halafu wewe bwana. Unajua mimi nakuchukulia kama kaka yangu wa kuzaliwa tumbo moja,” aliniambia. Yaani maneno yake yalinichefua, nikakunja sura kwa mbali na kumpa bonge moja la mtusi kimoyomoyo. Eti unafika magetoni unaniambia kwamba unanichukulia kama kaka yako, ulivyokuwa akiniita baba watoto shuleni ulimaanisha nini.

“Bupe,” niliita kwa sauti ya chini iliyomaanisha kwamba kuna kitu nakitaka.
“Abee kaka!”
“Daah! Kaka tena!”
“Ndiyo! Kama siyo kaka yangu, niambie una shilingi ngapi!”
“Hela tena!”
“Nyemo! Niangalie jinsi nilivyo, mimi ni msichana mrembo, kila mwanaume ananitaka, napendeza, unahisi nani ananipendezesha? Unadhani ni mama yangu muuza vitumbua ndiye ananipendezesha? Nyemo, acha mawazo ya kiswahili! Yaani unataka kutembea na mtoto mkali huku ukiwa huna hela? Nyie ndiyo wale mnaosema yule nimelala naye, hana kitu, kiuno kama gogo. Mimi si wa hivyo Nyemo, mimi si mwepesi. Ni bora unipe hela, baadaye ukisema kwamba umelala na mimi, pia nami nitasema nilikula hela yako!’

Ebwana siku hiyo Bupe alinipa makavu, alinichamba mpaka nikajuta kwa nini nilimuita. Nilibaki nikishangaa, alihitaji hela na wakati mimi nilijua kwamba ananitunuku baada ya kunipamba sana shuleni.

Huo ndiyo ulikuwa mwisho wangu wa kukaa na kuongea naye. Mpaka leo hii sikuwahi kuongea naye. Namjua! Yupo, namuonaga sana. Kalio lake halipo tena, amekongoroka, niliambiwa na jamaa yangu kwamba kwa sasa anatumia dawa kwani aliambukizwa Ukimwi na pedeshee lililokuwa linamiliki shimo huko migodini Shinyanga.

Makalio yakamponza, uzuri wake hakuutumia vizuri. Wakati mwingine nikawa najifariji kwamba inawezekana alipata matatizo baada ya kuniringia, baada ya kutokuniruhusu kula tunda, labda ningekula mpaka leo hii mambo yake yangekuwa safi tu.

Ndugu yangu! Haka ni kastori fulani ka kutunga lakini naamini kuna mengi umejifunza. Wakina Bupe wapo, tena wengi, wakina Nyemo nao wapo tena wengi. Hutakiwi kubabaika kisa mwili, hutakiwi kubabaika kisa wowowo. Mwanamke! Hutakiwi kubabaika kisa pesa, pesa zinapokuja, zinabeba mambo mengi sana. Hakuna pesa inayotembea peke yake, nyuma ya pesa kuna magonjwa, nyuma ya pesa kuna kifo cha mateso.

Uamuzi ni wako! Kuamua kula kwa macho kama mtu aliyekatwa mikono au kula kiuhakika kusongesha siku ziende. AMUA SASA!

Nb: Kihadithi nimekitunga baada ya kusikia uvivu wa kuandika hadithi ndefu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom