Simba ilifungwa kwa mengi Lubumbashi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
JUMAPILI iliyopita, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, Simba, walikuwa mjini Lubumbashi kumenyana na TP Mazembe ya huko katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa De Stade la Kenya mjini Lubumbashi.

Matokeo katika mechi hiyo, Simba ililala kwa mabao 3-1 na kujipa kazi ngumu ya kushinda mabao 2-0 katika mechi ya marudiano Aprili 3 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, mechi ambayo wengi wana imani kwamba matokeo hayo yatapatikana.

Nilikuwa miongoni mwa Watanzania wachache walioshuhudia mechi hiyo, na yafuatayo ndiyo yaliyojitokeza:

Kuwasili Lubumbashi:
Msafara wa wachezaji wa Simba ulioongozwa na Mwenyekiti wake Ismail Rage uliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Luano Lubumbashi saa nne kasoro kwa saa za DRC, ambapo ni sawa na saa tano kasoro asubuhi kwa Tanzania.

Mbali na Rage kuongoza msafara huo wa wachezaji, wengine waliowasili Lubumbashi alikuwa mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji, Abdallah Bulembo, Zacharia Hanspope, Majaliwa Mbasa na Charles Hamkah.

Kwenye uwanja wa ndege wa Luano, walilakiwa na Makamu Mwenyekiti Geofrey Nyange
‘Kaburu’ aliyefika siku mbili kabla pamoja na baadhi ya Watanzania wanaoishi Lubumbashi kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Nje ya uwanja huo, kulikuwa na mashabiki wachache wa mjini hapo, ambapo wengi walikuwa
wakionesha mkono mmoja, kuashiria kwamba Simba itafungwa mabao matano na ‘Mamba’ Tp
Mazembe.

Baada ya kuwasili uwanjani hapo na kukamilisha taratibu zote ndipo msafara wa Simba ukaelekea kupanda gari ya Taqwa badala ya kutumia usafiri ulioandaliwa na wenyeji, mmiliki wa timu hiyo Moise Katumbi alitoa mabasi aina ya Toyota DCM mawili kwa ajili ya kupokea wageni wake, lakini kuhakikisha Simba inakwepa hujuma, uongozi uliotangulia huko uliandaa utaratibu mwingine wa usafiri pamoja na hoteli.

Msafara huo ulitoka uwanjani mpaka kwenye Hoteli ya Rose, inayomilikiwa na bosi wa wapinzani wakubwa wa TP Mazembe, FC Lupopo, ambapo baada ya kukamilisha taratibu zote, hatimaye wachezaji walipatiwa vyumba na kuingia ndani kwa mapumziko.

Mazoezini:
Kama ilivyo ada, timu inapowasili nchi husika kwa ajili ya mechi inatakiwa kufanyia mazoezi
uwanja itakayochezea siku moja kabla ya siku ya mechi, na hicho ndicho walichofanya Simba ambapo muda wa saa tisa alasiri kwa saa za Lubumbashi ambapo ni saa 10 kwa Tanzania, msafara wa timu hiyo ulielekea kwenye uwanja wa Stade la Kenya.

Lakini kwa mshangao mkubwa, wachezaji wa timu hiyo waligoma kushuka kwenye gari, kwa madai kuwa eti walichoka kuzungushwa sana na hivyo walihitaji kupumzika. Nikaona hapa tayari timu ilishafungwa!

Kwa sababu inawezekana vipi kuuona na kuufanyia uwanja ambao kesho yake unatakiwa kuuchezea mechi ya kimashindano, kisha mchezaji anasema eti amechoka, nikaona kuna tatizo hapo tayari.

Inawezekana kabisa wachezaji wakawa kweli wamechoka kutokana na kipande kutoka uwanja
wa ndege wa Luano mpaka hotelini, lakini hapo hapakuwa mahala pake kulalamika kuchoka kwani hata lile lililowapeleka pale lilikuwa muhimu, tena muhimu sana.

Kitendo hicho kiliwakera viongozi na baadhi ya wanachama wa kundi la ‘Friends of Simba’
waliokuwepo eneo hilo ambapo walitoa maneno ya ukali kwa wachezaji hao na mwisho waliamua kushuka kwenye basi na kuendelea na mazoezi.

Hilo tu lilinitia shaka na kuona wawakilishi hao wa Tanzania, tayari ‘walishachemka’. Siku ya Mechi: Mechi ilichezwa Jumapili, saa 9:30 a lasiri ambapo kwa saa za Tanzania ni saa 10:30 jioni.

Kama kawaida wachezaji walipata chakula mapema na kuelekea uwanjani mapema tayari kwa
mechi hiyo kubwa. Mechi ilivyoanza dakika za mwanzomwanzo wachezaji walionekana kuwa na woga, lakini baada ya dakika tano walikaa sawa na kurejea katika hali ya mchezo na kuanza kupeleka mashambulizi ya hapa na pale langoni mwa wapinzani wao.

Kwa nilivyoiona TP kama wanavyoiita wenyewe, hata wao walikuwa na woga na mechi hiyo na kuanza ‘kuchangamka’ na kujiamini zaidi baada ya kupata bao la kuongoza katika dakika ya 11.

Lilikuwa bao lililozidisha chachu ya ushambuliaji wa TP na kuinyong’onyesha Simba ambayo
ilionekana kuchanganyikiwa, ikiwa haijakaa sawa ikaongezwa bao la pili katika dakika ya 24, hali iliyowachanganya kabisa.

Lakini Simba ilibadilika dakika chache kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza na ikaendelea hivyohivyo katika kipindi cha pili, ilibadilika na kuonesha imedhamiria kupata bao.

Ndipo kipa wa TP Robert Kidiaba alipoizawadia penalti baada ya kumchezea vibaya Emmanuel Okwi akiwa kwenye harakati za kumfunga kipa huyo mwenye vituko, Okwi bila ajizi alifunga penalti hiyo na kuzaa bao moja kwa Simba na hivyo kupunguza idadi ya mabao inayotakiwa kushinda katika mechi ya marudiano.

Walichokosea Simba:
Walichokosea Simba ni kutowabana TP katika dakika 20 za mwanzo kama walivyokuwa wakishauriwa na baadhi ya wadau. Kwamba timu hiyo imezoea kufunga mabao ya mapema, hivyo isipofanya hivyo ndani ya dakika 20 huchanganyikiwa na hivyo huwa rahisi kwa wapinzani wao kuwafunga.

Ni kweli, tazama mabao yao, la kwanza lilifungwa dakika ya 11, la pili dakika ya 24 la tatu wakalifunga dakika ya 64, baada ya kujiweka sawa kwa mabao mawili ya mapema.

Juma Kaseja, Patrick Phiri:
Naweza nisieleweke katika hili, lakini ukweli ni kwamba, kuna haja ya kufanyika jitihada za makusudi kuwasaidia wawili hawa Simba. Juma Kaseja ni kipa mzuri, hakuna ubishi kwamba ameisaidia sana Simba katika mechi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, si Simba peke yake iliyonufaika na kipa huyo lakini pia hata timu ya Taifa kwa nyakati tofauti imenufaika naye.

Kaseja siwezi kumtofautisha na Kocha wake mkuu Patrick Phiri, naye pia ameipatia mafanikio Simba na ni kocha ambaye Simba waliamini kwamba akipatikana, watamaliza tatizo la kufanya
vibaya kwenye ligi na michuano mbalimbali.

Hilo ni kweli, mfano ni namna ilivyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza mechi hata moja
msimu uliopita, na pia Simba iko katika hali nzuri kwenye msimamo wa ligi kwa sasa.

Lakini ukweli, kwa maono yangu, watu hawa sasa wanahitaji kupumzika, kwa namna Kaseja alivyocheza mechi ile na namna Phiri alivyopanga timu yake, watu hawa wanahitaji kupumzika kiukweli.

Kaseja alishakaririwa kuwa anasumbuliwa na matatizo ya kifamilia, nadhani ni wakati muafaka
kumpumzisha kipa huyu akashughulikia masuala yake ya kifamilia kwanza ili awe sawa kikazi.

Suala hili hata baadhi ya viongozi wa Simba wanalifahamu na ndio maana baada ya kuona
kikosi kinachocheza na TP siku ile kiongozi mmoja alisema: “Nilijua tu kocha lazima atapanga timu itakayotutia wasiwasi”.

Katika kuthibitisha kwamba Kaseja anahitaji kupumzika, Mtanzania mmoja anayeishi Lubumbashi, Mohamed Ally alihoji uwezo wa kipa huyo: “Hivi Kaseja siku hizi kawaje, ndio vile?

Ana matatizo gani mbona zamani alikuwa anacheza vizuri, mpaka kuna rafiki zangu wa Kikongo nilikaa nao uwanjani wakaniuliza hivi kipa huyu ndio kipa wenu namba moja kabisakabisa, hamna mwingine au?.

Kwa upande wa Phiri naye alionekana kuwa na upungufu, hasa katika kufanya mabadiliko, alitakiwa kuwatoa Mbwana Samatta na Mussa Hasan Mgosi mapema na kuwaingiza Nicodemus Nyagawa na Ally Ahmed ‘Shiboli’ ambao kuingia kwao kulizidisha uhai katika timu.

Naweza nisilaumu sana uchezaji wa Samatta siku ile kutokana na kuwa mgeni wa mechi za kimataifa, mechi ile ilikuwa kubwa kwake, lakini kocha Phiri alipaswa pia kumtoa Amri Kiemba kwani siku ile hakuwa kwenye kiwango chake.

Hivyo kwa maono yangu, mabadiliko yanahitajika kwa watu hao ili kuwaepusha na lawama za
hapa na pale kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.

Mashabiki uwanjani:
Ukiwa mgeni kwenye uwanja huo, ‘utachanganyikiwa’ tu, uwe mchezaji ama shabiki kwa namna mashabiki walivyo na bidii ya kushangilia timu yao. Uwanja huo una uwezo wa
kuchukua mashabiki 35,000 walijaa siku hiyo, hata hivyo hilo si neno sana, ila hili la kushangilia mwanzo mwisho, ndio hasa mashabiki wa Tanzania wanapaswa kujifunza.

Nilipoutembelea uwanja wa Amahoro Kigali, niliwapigia saluti Wanyarwanda kwa ushangiliaji
wao, lakini nao hawafua dau kwa Wakongo.

Vikundi vya ushangiliaji maarufu kama kidedea vipo karibu 15 kuzunguka uwanja mzima wengine wakiwa na drums kabisa, hapo ni masebene tu yanapigwa kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya 45 za kipindi cha kwanza na za kipindi cha pili pia.

Kwa hilo wamefaulu, mashabiki wanaonekana kuzipenda timu zao wanacheza kwa madaha huku wakionesha mkono mmoja kwa wapinzani wao wakimaanisha watakula tano.

Simba yaacha gumzo Lubumbashi:
Pamoja na mambo yote hayo, lakini Simba bado imeacha gumzo mjini hapo. Kwa namna ilivyofika uwanja wa ndege na kutopanda mabasi waliyoandaliwa, ilivyokataa kufikia katika hoteli iliyoandaliwa na wenyeji, na mwisho ni kufungwa mabao 3-1.

“Timu yenu inaonekana inajua sana mambo ya mpira, ndio maana walitumia kila kitu chao
baada ya kutumia vilivyoandaliwa na tajiri Katumbi (Moise mmiliki wa Tp Mazembe), alisema Bashiri raia wa Kongo anayejiita mwananchi wa nchi ya Kidemokrasia.

“Hata kufungwa mabao 3-1 mmetutisha sana, tulizoea kuzifunga timu zinazokuja hapa kuanzia mabao matano kwenda juu, sio kushuka chini,”alisema. Kauli hiyo ni kama iliungwa mkono na Kocha wa TP Mamadou Ndiaye aliyekiri kupata upinzani mkubwa kwa Simba.

“Sikutarajia kama ningepata upinzani mkubwa hivi, nilijua nitashinda bao nyingi kama inavyokuwa kwa timu nyingine ninazokuja nazo,”alisema. Je, TP watafungika? Mazembe inaweza kufungika, lakini si kirahisi kama kila mmoja anavyofikiria.

Ndio kwa jinsi nilivyoiona ikicheza, si kama nilivyokuwa nikisikia kwa siku za karibuni na si ile iliyocheza Kombe la Kagame mwaka jana, na ile iliyocheza michuano hiyo ya Afrika iliyopita
pamoja na ile ya klabu bingwa ya Dunia.

Kiwango cha Tp kimeshuka, ingawa hilo siwezi kulisemea sana maana inawezekana hizo ni
mbinu tu ikija kucheza mechi ya marudiano itabadilika, au siku iliyocheza na Simba soka ilikataa kama ilivyo desturi ya mchezo huo.

Lakini kama kweli ile ndio Mazembe ambayo itakuja kucheza na Simba mechi ya marudiano kama, basi Simba inaweza kushinda, lakini si mdomoni, ni kuongeza juhudi, kurekebisha makosa na kujipanga vizuri.

Kwa mfano, silaha kubwa ya Mazembe ni kufunga mabao ya harakaharaka, Simba ikimudu
kuwabana na kuanza kupata mabao ya mapema, watakuwa wameokoka, lakini vinginevyo,
itakuwa inaota.

Simba watambue kuwa wale ni mabingwa watetezi, hivyo si rahisi kuwafunga kirahisi kwani wanafahamu kama watakamiwa na hivyo hawana budi kupigana mpaka dakika ya mwisho kutetea ubingwa wao.

Maandalizi ya mechi hiyo, yalitakiwa yaanze Jumapili ileile baada ya mechi, si kurudi Tanzania na kupiga blaablaa halafu siku mbili kabla ya mechi ndio viongozi waibuke na kutia preshapresha za kushinda.

Je, viongozi wa Simba wameanza kulifanyia kazi hilo? Zimebaki siku chache sana kuelekea kwenye mechi hiyo, kazi kwenu.
 
Mkuu,

Asante kwa Kutujuza yaliyojiri huko kwenye uwanja wa De Stade la Kenya, mjini Lubumbashi, nje na ndani ya Uwanja, kabla na baada ya mechi!!

Kwa hakika wewe ni Simba damu.
 
hahaaaaaaaaaa mimi mwanachama hai inabidi tujipange kwakweli
Mkuu,

Asante kwa Kutujuza yaliyojiri huko kwenye uwanja wa De Stade la Kenya, mjini Lubumbashi, nje na ndani ya Uwanja, kabla na baada ya mechi!!

Kwa hakika wewe ni Simba damu.
 
Back
Top Bottom