CHUO KIKUU CHA DODOMA
BUNGE LA WANAFUNZI CHUO CHA SANAA, LUGHA NA SAYANSI YA JAMII
RIPOTI YA TUME ILIYOUNDWA KUFUATILIA SHUGHULI ZA KIFEDHA ZA UTENDAJI WA SERIKALI TAREHE 14/03/2014 HADI TAREHE 22/03/2012
KUSOMWA BUNGENI TAREHE 23/03/2014
SAA 11:00 JIONI
WAJUMBE WAKUU
1. SANGA AYOUB….. ………..MWENYEKITI WA TUME
2. KAPILIMA JAMES…………MWENYEKITI MSAIDIZI WA TUME
3. EDOM ELIA…………KATIBU WA TUME
4. MTONO NORBERTH……..MJUMBE
5. MICHUZI ZAHRA M.…….MJUMBE
Mh. Spika; Awali ya yote napenda kumshkuru mwenyezi mungu kwa kutuweka hai na kutujalia afya njema,sifa na utukufu ni vyake yeye baba. Salam zangu za dhati zilizoambatana na shukrani ziwafikie wanafunzi wenzangu wa chuo cha sanaa ya lugha na sayansi ya jamii.
Mh. Spika; Mosi, Napenda kutumia fursa hii pia kushukuru juhudi nzuri za serikali ya UDOSO- Chuo cha sanaa ya lugha na sayansi ya jamii inayoongozwa na na mheshimiwa Raisi
Bernad Janusi, na kwa hili nasema kua naipongeza serikali nzima nikimaanisha raisi mwenyewe, waziri mkuu na baraza lake lote la mawaziri kwa kutuongoza hadi sasa tulipo.
Pili napenda kuwashukuru wabunge wote wa bunge hili ambao kwa kauli moja walikubaliana na hoja ya kuundwa kwa tume hii, na pasipo kusita wala hofu yoyote waliunga mkono uteuzi wetu na kutupa ushirikiano wakati wowote tulipowahitaji, hasa katika nyakati za mwisho za uandaaji wa ripoti hii kwa kupata mawazo yao wakiwa kama wabunge na si wanafunzi wa kawaida tukiwa nje ya bunge, twasema asanteni sana, nasi tunawakilisha mawazo ya wengi na si wachache.
Tatu tunapenda kwa moyo wa dhati kushukuru watendaji wa serikali ambao kwa namana yao ya pekee bila kujari tofauti zetu za nyadhifa za kisiasa walitoa ushirikiano wao pale walipohitajika. Kadri ya vyeo vyao, napenda kumshukuru mh. Raisi Bernad Janusi, Mh. Makamu wa Raisi Kyando Benedict, Mh. Waziri Mkuu Tata William G., Spika wa Bunge Mh. Kuta T. Kuta pamoja na mawaziri mbalimbali na manaibu wao.
Mh. Spika; Mwisho shukrani zangu ziwaendee viongozi wetu wapendwa wa utawala wa chuo cha sanaa ya lugha na sayansi ya jamii ambao kwa namna moja au nyingine wameweza kufuatilia kwa busara utendaji kazi wa tume hii kuanzia mwanzo hadi siku ya mwisho ya kikao cha mahojiano na waheshimiwa wabunge, Hii imedhihirisha wazi kua tunaviongozi bora wenye kujari uwepo na utendaji kazi wetu katika kutekeleza majukumu yetu ya uwakilishi wa wanafunzi.
UTANGULIZI
Mh. Spika; Bunge lako tukufu lilipokutana katika kikao chake cha kwanza cha muhula huu wa masomo tarehe 14/03/2014, lilikubaliana kwa kauli moja kuundwa kwa tume huru ya bunge itakayo fuatilia madai yote yaliyoibuka bungeni kutokana na hoja binafsi ya Mh. Mpambachile Felix P. (MB-BIASHARA NA UCHUMI) kusaidia bunge lako tukufu kufikia maamuzi yenye busara na manufaa kwa wanafunzi.
Mh. Spika; tume hii ilikua na wajumbe wakuu watano na wajumbe waandamizi wawili ili kukamilisha majukumu yake, hata hivyo baadhi ya wajumbe wakuu wawili walichelewa kuanza kazi katika tume hii kutokana na sababu zao za msingi na hivyo kuwafanya washiriki katika kikao halali na rasmi cha mwisho cha tume na wabunge kilicholenga kupata maoni ya wabunge nje ya bunge.
MSINGI NA MAJUKUMU YA TUME
Msingi wa tume ni wa kikatiba ndani ya ibara ya 16J (1) (J) ya katiba ya UDOSO ambapo bunge hili limepewa nguvu ya kuunda tume mbalimbali na hivyo mnamo tarehe 14/03/2014 tume hii iliundwa na Mh. Spika.
Majukumu ya tume hii ilikua ni kuchunguza tuhuma mbalimbali kama zilivyoletwa na mtoa hoja tarehe 14/03/2014, hivyo ili kutekeleza majukumu yake tume hii ilipanga kufanya kazi zake katika mpangilio ufatao;
1. Awamu ya kwanza ni kukutana kwa wajumbe wakuu ili kupanga hadidu za rejea na maswali ya kuwauliza wahusika tarehe 15/03/2014
2. Awamu ya pili ilikua ni mahojiano na viongozi mbalimbali tarehe 16 & 17/03/2014
3. Awamu ya tatu ilikua ni uandamizi na wajumbe waandamizi,Tarehe 18, 19 & 20/03/2014
4. Awamu ya nne ni kukutana na wabunge mbalimbali ili kupata mawazo kama wabunge wakiwa nje ya bunge. Tarehe 21 & 22/03/2014.
5. Awamu ya tano ni kuandaa na kuandika ripoti ya tume. Tarehe 22/03/2014
MAJIBU YA TUME BAADA YA UCHUNGUZI
Mh. Spika katika kikao hicho hoja mbalimbali ziliibuliwa na hivyo kuhitaji majibu, hoja hizo ni kama zilivyoorodheshwa hapa chini;
1. Awali ni juu ya pesa zilizogunduliwa na tume maalumu ya bunge iliyosomwa tarehe 24/11/2013 na tarehe 07/12/2013, iliyochunguza upotevu wa pesa katika wizara mbalimbali na ofisi za serikali ambazo kiasi cha shilingi 544,100 zilipaswa kurejeshwa.
2. Pili ni juu ya mapato ya serikali yatokanayo na vyanzo vinavyomilikiwa na serikali haswa maduka yalipo block 09 na block 13 huko skuli ya sayansi ya jamii.
3. Ni juu ya mgawanyo wa pesa mbalimbali kama zilivyopitishwa na bunge katika wizara na ofisi mbalimbali.
Mh. Spika tume hii inawasilisha majibu ya uchunguzi huo kama ifuatavyo;
A. AWALI NI JUU YA PESA ZILIZOGUNDULIWA NA TUME MAALUMU YA BUNGE ILIYOSOMWA TAREHE 24/11/2013 NA TAREHE 07/12/2014, ILIYOCHUNGUZA UPOTEVU WA PESA KATIKA WIZARA MBALIMBALI NA OFISI ZA SERIKALI AMBAZO KIASI CHA SHILINGI 544,100 ZILIPASWA KUREJESHWA.
Mh. Spika uchangunuzi wa hoja hii unaeleweka ndani ya bunge kwasababu pesa hiyo iligunduliwa na tume ya mheshimiwa Mpambichile Felix P., na bunge lilikubaliana kwa pamoja kua pesa hiyo irudishwe benki mara moja (Rejea hadidu za rejea za kikao cha bunge cha tarehe 07/12/2013). Katika hali ya kushangaza hoja hii ikarudi kwa mara ya pili ikiwa kama hoja ndogo ya muendelezo wa ripoti ya tume iliyopita.
MAJIBU YA TUME
Mh. Spika; Katika kufanya utafiti tume hii imejidhihirisha kwamba pesa hiyo haijawahi kuingizwa benki na wala haipo kabisa benki(Rejea bank Statementszilizoambatanishwa mwishoni mwa ripoti hii), na hivyo mtoa hoja alikua sahihi.
Mh. Spika; tume hii imegundua kuwa kauli ya Mh.Waziri wa fedha kuwa baadhi ya pesa hiyo imetumika katika kumlipa mbunge ambaye jina lake halikutoka katika malipo ya awali ya pesa za kujikimu za wabunge pamoja na gharama za usafiri wa mh. Raisi kwenda makuru kwenye ajari ni ya uongo na haina ukweli.
Mh. Spika; Mosi, Ili kuthibitisha hilo tume hii imegundua kwamba Mh. waziri wa fedha alilidanganya bunge lako tukufu kwa kutoa matumizi hayo kwasababu matumizi hayohayo ndiyo aliyomwambia Mh. Waziri wa michezo pale alipompa pesa ya bajeti yake nusu (Rejea maelezo ya Mh. Waziri wa michezo ya kupewa shilingi 500,000 kati ya 660,000 kama alivyopitishiwa na bunge kwaajiri ya kununua vifaa vya michezo), hivyo basi kutokana na mgongano wa maelezo hayo, tume imegundua kwamba matumizi hayo ni ya kughushi ili kuongeza matumizi hewa ndani ya serikali.
Mh. Spika; pili kuhusu kauli yam h. waziri wa fedha juu ya baadhi ya pesa hiyo kutumika na Raisi katika dharura ya kwenda makuru, tume hii pia imegundua kwamba matumizi hayo hayakua ya pesa husika kwasababu siku hiyo kuna gari ilitolewa na serikali ilitakiwa ijaze mafuta ya shilingi 15000 na pesa hiyo ilitoka katika mfuko wa Raisi kulingana na bajeti ya ofisi yake.
Hivyo basi, tume baada ya kupitia ushahidi wote tume hii imegundua kwamba pesa hii ipo mikononi mwa mtu/watu wachache au imeliwa kabisa na mtu/watu hao, na hapa pia tume imejidhihirisha kwamba pesa hii kama imeliwa basi imeliwa na mtu wa juu zaidi ya Mh. Waziri wa fedha kwasabau kama ingekua imeliwa na Mh.waziri wa fedha basi Raisi pamoja na Waziri Mkuu wake wangemuwajibisha Waziri husika.
B.
PILI NI JUU YA MAPATO YA SERIKALI YATOKANAYO NA VYANZO VINAVYOMILIKIWA NA SERIKALI HASWA MADUKA YALIPO BLOCK 09 NA BLOCK 13 HUKO SKULI YA SAYANSI YA JAMII.
Mh. Spika; Tume hii ilipewa nguvu ya kuchunguza pato la kodi ya pango la maduka yaliyopo block 9 na block 13 skuli ya sayansi ya jamii. Mtoa hoja alihoji kodi ya pango katika malipo ya awamu mbili yaani kodi ya mwezi wa kumi na moja hadi mwezi wa pili shilingi 900,000 na pili pesa ya kodi ya pango ya mwezi wa pili hadi wa tano shilingi 900,000.
MAJIBU YA TUME
Mh. Spika; Tume hii ilipatwa na wakati mgumu sana katika kuhoji na kufatilia jambo hili na hii ilitokana na mgongano wa maelezo kati ya wahusika wenyewe ingawaje mmiliki wao ni mmoja,mgongano wa maelezo kati ya wahusika na Mh. Raisi., mgongano wa maelezo kati ya viongozi wa serikali. Katika kutekeleza majukumu yake tume hii ilipata maelezo tofauti kutoka kwa watu hao kama ifuatavyo;
I. MGONGANO WA MAELEZO KATI YA WAHUSIKA WA MADUKA WENYEWE
Mh. Spika siku ya kwanza tarehe 18/03/2014, Tume hii ikiwa na wajumbe waandamizi(Mh. Waziri Mkuu na Mh. Waziri wa fedha) ilikwenda mpaka kwa mmoja wa wahusika katika maduka yale. Tume hii ilijitambulisha pamoja na kuwatambulisha wajumbe waandamizi na nyadhifa zao za kiuongozi na hivyo kuruhusiwa kufanya mahojiano. Muhusika wa kwanza ambaye anauza duka la block 09 alihojiwa juu ya ulipaji wa kodi ya pango na alijibu kuwa kodi ambayo serikali inawadai ni kodi ya mwezi wa pili hadi wa tano tuu kwasababu kodi ya pango ya mwezi wa 11 mpaka wa wa pili imekwishalipwa(Rejea maelezo ya kurekodiwa). Mh. Waziri mkuu akiwa kama mjumbe muandamizi alimuuliza muhusika juu ya mfumo wa ulipaji wa pesa hiyo na muhusika alijibu kuwa mfumo wa ulipaji hutegemea na maamuzi ya viongozi wa serikali hivyo wakitaka ilipwe kwa njia ya benki au mkononi wao hufuata. Mh. Waziri mkuu akiwa kama mjumbe muandamizi alimuomba muhusika atuletee mkataba wa pango na muhusika aliuleta na tukaukagua na kugundua kwamba viongozi waliosaini mkataba huo ni Mh. Raisin a Mh. Waziri wa fedha kama inavyotakiwa na Kanuni ndogo za fedha za chuo. Katika hali ya kushangaza Mh. Waziri mkuu alikiri kuwa hata yeye ile ndio ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuuona mkataba ule kwasababu yeye hausiki na mambo ya mikataba ya serikali.
Mh. Spika; baada ya tume hii kupata taarifa hizo iliomba kupewa nyaraka za malipo ya maduka kutoka kwa muhusika huyo na hapo ndipo muhusika huyo aliposema kuwa kulingana na taratibu zao nyaraka zote za malipo hua zinahifadhiwa na muhusika wa duka la block 13 aitwaye Eliza.
Mh. Spika; siku ya pili tarehe 19/03/2014, tume hii ikiongozwa na mwenyekiti Msaidizi Mh. Kapilima James ilienda kwa lengo la kupata nyaraka za malipo na mahojino kwa muhusika wa pili wa duka la block 13 aitwaye Eliza, Katika hali ya kustaajabisha muhusika huyo alisema kua hawajawahi kulipa malipo yeyote ya kodi ya pango la maduka hayo kuanzia November mwaka jana hadi siku ya mahojiano na alipoulizwa sababu ya kutokulipa kodi hio katika kipindi hicho chote akajibu kua alipatwa na mtatizo ambapo aliibiwa pesa mwishoni mwa mwezi December mwaka jana na hivyo alimpigia simu Mh. Raisi mwishoni mwa mwezi December mwaka janaili kumpa taarifa hizo na ndipo aliporuhusiwa na Mh. Raisi kutokulipa Kodi hiyo hadi pale atakapoipata.
Mh. Spika; siku ya tatu tarehe 20/03/2014 baada ya kupewa taarifa za majibu ya muhusika wa pili nilitafakari kwa kina mazingira ya mgongano wa maelezo hayo na ndipo nilipo jadiliana na wajumbe wakuu wenzangu na tukaamua kufanya mahojiano ya pili siku hii. Tume hii ikiwa na wajumbe waandamizi ilifanya mahojiano na muhusika wa pili lakini bado majibu yake yalikua ni sawa kama yaliyopita kwamba hajawahi kulipa kodi yeyote tangu serikali hii iingie madarakani na hii ilitokana na kuruhusiwa na Mh. Raisi baada ya kupatwa na tatizo la kuibiwa pesa kiasi cha shilingi milioni mbili, na alipoulizwa kama aliripoti kesi hiyo polisi alijibu kuwa hakufanya hivyo.
Mh. Spika; Muhusika huyo alipoulizwa lini atalipa kodi ya pango hilo alijibu atalipa pesa hiyo kwa awamu mbili, moja ikiwa tarehe 24/03/2014 na awamu ya pili ikiwa ni tarehe 03/04/2014.Tume imegundua kwamba mpangaji huyo amevunja mkataba hadi sas kwa sababu kutokana na maelezo yake yanayokinzana hajalipa kodi hadi sasa, lakini mpangaji huyo anapata nguvu ya kujitetea kutoka kwa Mh. Raisi.
II. MGONGANO WA MAELEZO KATI YA WAHUSIKA WA MADUKA NA RAISI
Mh. Spika; Tume hii mnamo tarehe 20/03/2014 ilipofanya mahojiano na muhusika wa maduka wa pili aitwaye Eliza ilijibiwa kuwa hajawahi kulipa malipo yeyote ya kodi ya pango la maduka hayo kuanzia November mwaka jana hadi siku ya mahojiano na alipoulizwa sababu ya kutokulipa kodi hio katika kipindi hicho chote akajibu kua alipatwa na mtatizo ambapo aliibiwa pesa mwishoni mwa mwezi December na hivyo alimpigia simu Mh. Raisi ili kumpa taarifa hizo na ndipo aliporuhusiwa na Mh. Raisi kutokulipa Kodi hiyo hadi pale atakapoipata.
Mh. Spika Tume hii ilichukua maamuzi ya haraka ya kumpigia simu Mh. Raisi kupitia simu ya Mh. Waziri Mkuu ili kuweza kuhakiki taarifa za muhusika huyo lakini katika hali ya kushangaza maelezo ya Mh. Raisi yalikinzana na maelezo ya Muhusika wa pili aitwaye Eliza, Raisi zalipoulizwa kama alishawahi kumruhusu muhusika huyo asilipe kodi kwa muda alijibu ndio ni kweli (hapa walifanana), alipoulizwa ni sababu zipi alizopewa hadi akaamua hivyo akajibu aliambiwa na muhusika huyo kuwa amepatwa na matatizo ya kuibiwa pesa na kuharibikiwa na mashine za kutolea kutoa kopi (Maelezo yalitofautiana na sababu za muhusika wa pili), Tume hii ilimuuliza zaidi Mh. Raisi kua alipewa taarifa za uwizi huo lini akajibu kuwa ni November mwaka jana (Maelezo haya yanatofautiana na maelezo ya muhusika wa pili ambaye alisema alimpa taarifa Mh. Risi mwishoni mwa mwezi December mwaka jana) na zaidi alipoulizwa kua alitoa ruhusa ya kutokulipwa kodi hiyo lini alijibu ni mwezi November mwaka jana(Maelezo haya yanakinzana na maelezo ya muhusika wa pili aliyesema alitoa taarifa mwishoni mwa mwezi December mwaka jana).
Mh. Spika tumbe imegundua kwamba mkataba uliopo una mapungufu mengi na hivyo kutengeneza mianya ya rushwa na kuchelewa kwa malipo hayo, hivyo basi tume inaliomba bunge hili kupitia upya mkataba huo na kuurekebisha ili uwe na maslahi kwa mwenye pango si kama ulivyo sasa.
III. MGONGANO WA MAELEZO KATI YA VIONGOZI WA SERIKALI WENYEWE KWA WENYEWE
Mh. Spika; Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 14/03/2014 katika kikao cha bunge, Mh. Waziri Mkuu alipokua akijibu hoja kuhusu pesa hizi alisema kwamba pesa ya kodi ya pango imeshalipwa na kwamba yupo tayari kuambatana na Wajumbe wa tume kwenda benki kufuata bank statement na kwenda kwa mmiliki kuhakiki malipo hayo, na hii ndio ilikua sababu kubwa ya kuundwa kwa wajumbe waandamizi hawa (Rejea hadidu za rejea za kikao cha bunge cha tarehe 14/03/2014).
Mh. Spika; ikumbukwe pia kwamba mnamo tarehe 14/03/2014 Waziri wa fedha alipokuwa akijibu hoja hii bungeni alisema kwamba pesa ya kodi hiyo tayari imeshalipwa(Rejea hadidu za rejea za kikao cha bunge cha tarehe 14/03/2014). Pia ikumbukwe kwamba katika taarifa ya kamati ya fedha ya bunge iliyotolewa bungeni tarehe 14/03/2014 ilithibitisha kwamba Mh. Waziri wa fedha aliiambia kamati kua mpangaji huyo ameshalipa kodi kwa wakati na zaidi yeye ndio anaidai serikali muda wa kukaa pale.
Mh. Spika; Maelezo ya Mh. Waziri Mkuu na Waziri wa fedha yanakizana kabisa na maelezo ya Mh. Raisi ya kujua kutokulipwa kwa kodi ya pango la maduka hayo na hii inazua hali ya sintofahamu kwa tume na kubaki na majibu mawili yanayokinzana. Tume hii imegundua kwamba, kuna mgongano mkubwa wa maelezo juu ya pesa hizi kuanzia kwa wahusika wa madukani wenyewe baada ya mmoja kusema pesa hiyo imekwishalipwa na mwingine kusema pesa hiyo bado haijalipwa, pili mgongano wa maelezo ya viongozi wa serikali ikiwa wengine wanasema pesa imekwishalipwa na wengine wanasema bado haijalipwa.
Mh. Spika; Baada ya mpambanuo huo tume hii inaliachia bunge lako tukufu kuamua maamuzi ya busara na yenye tija na kwa manufaa ya wanafunzi kwasababu tume hii imegundua kuwa pesa hizi zinautata sana na zilishawahi kujadiliwa hata katika baraza la mawaziri na Mh. Raisi alikiri kuzipokea pesa hizo na kuzitumia katika matumizi.
C. NI JUU YA MGAWANYO WA PESA MBALIMBALI KAMA ZILIVYOPITISHWA NA BUNGE KATIKA WIZARA NA OFISI MBALIMBALI
Mh. Spika tume hii pia ilipewa mamlaka ya kuchunguza hoja kuhusu mgawanyo wa pesa katika ofisi na wizara mbalimbali. Katika maelezo ya mtoa hoja alilenga mgawanyo huo katika wizara na ofisi mbalimbali hasa katika ofisi ya Raisi, Ofisi ya Spika, Wizara ya Makazi, Wizara ya Elimu, Wizara ya mikopo, na Wizara ya Makazi.
MAJIBU YA TUME
Mh. Spika; Tume hii katika kufanya uchunguzi wake imegundua na kujiridhisha kwamba ni kweli kuna mgawanyo wa pesa za bajeti usio sahihi katika wizara na ofisi mbali tofauti na viwango vilivyopitishwa na bunge na hivyo kufanya hitimisho kwamba kwa hili pia, mtoa hoja alikua sahihi.
Mh. Spika; tume hii ilifanya utafiti huo na kupata majibu kama inavyooneshwa hapa chini;
1. MAJIBU KATIKA OFISI YA RAISI
Mh. Spika; Tume hii ilifanya mahojiano na viongozi wawili katika ofisi ya Raisi. Kiongozi wa kwanza ni Mh. Makamu wa Raisi ambapo aliulizwa na tume kuwa ofisi yake ilipitishiwa kiasi cha pesa shilingi 75000/= na je amepokea shilingi ngapi?.Tume hii ilipata majibu ya wazi kuwa Mh. Makamuwa Raisi alipokea shilingi 50000/= tuu tofauti na kiwango ambacho bunge hili tukufu lilimpitishia(Rejea mahojiano ya Mh. Makamu wa Raisi na Tume).
Mh. Spika; Tume hii imejiridhisha kwamba katika ofisi ya Raisi bajeti hutoka na kwenda kwa Raisi na hivyo Raisi ndiye huwa anafanya mgawanyo wa pesa hizo, hivyo basi tume hii imegundua kwamba pesa kiwango cha shilingi 25000/= kutoka kwenye bajeti ya Mh. Makamu wa Raisi imeliwa na Raisi.
Mh. Spika; tume hii ilimtafuta katibu mkuu wa serikali kupitia simu ya mkononi akiwa kama mmoja wa kiongozi wa serikali katika ofisi ya Raisi, cha kushangaza katibu mkuu wa serikali alijibu kwamba Mh. Raisi kampigia simu na kumwambia asitoe maelezo yeyote kuhusu mgawanyo wa pesa kwenda kwake.
Mh. Spika; Jibu hilo liliifanya tume iwe katika hali ya sintofahamu na baadae ikagundua kwamba huenda Mh. Raisi hataki kiogozi huyo atoe majibu kwasababu za msalahi yake binafsi na si maslahi ya wanafunzi wa chuo cha sanaa ya lugha na sayansi ya jamii, hivyo basi ni dhahiri kwamba Mh. Raisi alivunja ibara ya 16I. (1)(j) and (L) ya katiba ya UDOSO kwa kuzuia kazi za tume iliyoundwa kwa mamlaka ya bunge na inafanya kazi kama sehemu ya bunge na kutokuheshimu maamuzi ya wabunge wa bunge hili tukufu.
2. MAJIBU KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU
Mh. Spika; Tume hii ilimtafuta waziri Mkuukumpa taarifa tarehe 16/03/2014 ilikufanya mahojiano nawaziri Mkuu juu ya pesa za federation na pesa za malipo ya form za wagombea wa uchaguzi katika uchaguzi wa mwaka 2013/2014. Waziri Mkuu alijibu kuwa hayupo tayari kuhojiwa kwasababu yeye kama mjumbe wa tume hii hakushirikishwa katika mchakato wa kuwahoji waheshimiwa mawaziri.
Mh. Spika; Tume hii ilimfahamisha Mh. Waziri Mkuu utofauti kati ya mjumbe mkuu na mjumbe mwandamizi kulingana na maamuzi ya bunge ya kuunda tume hii, hivyo tume hii ilimuarifu Mh. Waziri mkuu kua ushirikishwaji wake utaanza katika awamu ya tatu ya kazi za tume ambayo ni awamu ya uandamizi wa tume na wajumbe waandamizi kwenda katika maduka na benki kufata bank statements ili kuhakiki.
Mh. Spika; Katika jambo la kushangaza Mh. Waziri Mkuu aliijibu tume kwamba hayupo tayari kuhojiwa na kushirikiana nayo na yupo tayari kuachia ngazi ya madaraka yake muda wowote ule. Katika kuthibitishia hilo, mheshimiwa Waziri Mkuu aliiambia tume kwamba tayari amekwisha mpa taarifa za kujiuzuru mheshimiwa spika na hivyo anasubiri muda wowote ule bunge likiiitishwa aachie madaraka.
Mh. Spika; Tume hii ilimuomba Mh. Waziri Mkuu kutumia busara zake kwenda kutafakari maamuzi yake na hivyo kumuahidi kuwa kunabadhi ya maongezi aliyoyatoa mbele ya tume hayatatumika katika ripoti ya tume hii mbele ya bunge hili tukufu (Maongezi yaliyofanywa kati ya tume na Mh. Waziri Mkuu kwa makubaliano ya kutotolewa bungeni yatawekewa usiri huo kulingana na mazingira yake husika). Mh. Spika siku inayofuata Mh. Waziri Mkuu aliitarifu Tume kuwa yupo tayari kushirikiana na Tume na hivyo alikuja kushirikiana na Tume.
Mh. Spika; kuhusu pesa za serikali inayoidai serikali ya shirikisho, Tume imegundua kwamba pesa hizo zina ulakini wa kutokulipwa kama hakutakua na jitahada za ziada za serikali na bunge kuzifuatilia kwa kupitisha maamuzi ya busara ya kuifanya serikali ya shirikisho kulazimika kulipa pesa hizo.
Mh. Spika; kuhusu pesaza malipo ya form za wagombea wa uchaguzi katika uchaguzi wa mwaka 2013/2014, Tume hii imegundua kwamba pesa hizo hazikuingia katika akaunti ya serikali ya wanafunzi na hivyo pesa hizo ziliingia katika akaunti nyingine (Rejea bank statements zilizoambatanishwa mwishoni mwa ripoti hii). Tume hii ilishindwa kufuatilia akaunti hiyo kwa undani kutokana na kukosa akaunti namba ambapo malipo hayo ndimo yalifanyika, hivyo basi, Tume inamuomba mbunge yeyote mwenye kopi ya "paying slip" ya benki ya malipo yale aitoe ili uchunguzi wa kina ufanyike na serikali.
3. MAJIBU KUTOKA OFISI YA SPIKA
Mh. Spika; Tume hii ilifanya mahojiano na Mh. Spika akiwa ndiye Kiongozi mkuu wa ofisi hiyo.Tume ilimuuliza Mh. Spika ambapo aliulizwa na tume kuwa ofisi yake ilipitishiwa kiasi cha pesa na je amepokea shilingi ngapi?.Tume hii ilipata majibu ya wazi kuwa Mh. Spikaalipewa pesa zake zote za bajeti yake kasoro pesa ya safari ya Spika kwenda nje ya chuo tofauti na kiwango ambacho bunge hili tukufu lilimpitishia.
4. MAJIBU KUTOKA WIZARA YA MICHEZO
Mh. Spika; Tume hii ilifanya mahojiano na waziri wa michezo tarehe 17/03/2014. Waziri huyu aliulizwa na tume kuwa wizara yake ilipitishiwa kiasi cha pesa shilingi 635000/= katika bajeti ndogo ya kununua vifaa vya michezo, na je amepokea shilingi ngapi?. Tume hii ilipata majibu ya wazi kuwa Mh.Waziri alipokea shilingi 500,000/= tuu tofauti na kiwango ambacho bunge hili tukufu lilimpitishia.
Mh. Spika tume hii ilimuuliza hatua alizochukua baada ya kupewa pesa hiyo pungufu, Tume hii iliambiwa kua alipouliza alijibiwa na Mh. Waziri wa Fedha kwamba kiwango kinachobaki kilitumika katika kumlipa mbunge ambaye jina lake halikutoka katika malipo ya awali ya pesa za kujikimu za wabunge pamoja na gharama za usafiri wa mh. Raisi kwenda makuru kwenye ajari(Majibu haya ni sawa na aliyojibiwa mwenyekiti wa kamati ya fedha ya bunge kwenye kikao cha bunge cha tarehe 14/03/2014, alipouliza juu ya deni la shilingi 544,100/= hapa jibu moja linatumika sehemu mbili).
Mh. Spika; tume hii imejiridhisha kwamba serikali hii inayoongozwa na Mh. Raisi Bernad Janusi imebadhiri pesa hizo pasipo kuwa na shaka yeyote.
5. MAJIBU KUTOKA WIZARA YA MIKOPO
Mh. Spika; Tume hii ilimtafuta waziri wa mikopo na kumpa taarifa tarehe 15/03/2014 ilikufanya mahojiano na waziri wa huyo pamoja na naibu wake tarehe 16/03/2014. Waziri huyoalijibu kuwa yupo mjini na ana hudhuru huko kwahiyo hatakuwepo kwa siku hiyo na hivyo akaikabidhi tume ifanye mahojiano na Mh. Naibu Waziri. Mh. Naibu Waziri aliulizwa na tume kuwa wizara yake ilipitishiwa kiasi cha pesa shilingi 542000/= katika bajeti kuu ya wizara yake, na je amepokea shilingi ngapi?.Tume hii ilipata majibu ya wazi kuwa Mh.Waziri alipokea kiasi chote cha pesa Kama alivyopitishiwa na bunge hili tukufu.
Mh. Spika; katika wizara hii utata tume iligundua kwamba kuna safari amabayo ilipaswa kufanyika ndani ya wizara ya kwenda Dar es salaam Bodi ya Mikopo. Tume iligundua kwamba ni kweli safari hii ilifanyika na aliyekwenda ni naibu waziri huyo, lakini Naibu Waziri huyo hakupewa pesa yeyote kama ilivyopitishwa na bunge hili tukufu.
Mh. Spika; tume hii ilimuuliza Naibu waziri huyo hatua alizochukua baada ya kutokupewa pesa hiyo, Tume hii iliambiwa kuwa alipouliza alijibiwa na Mh. Waziri wa Mikopo kwamba atalipwa pesa hiyo hadi pesa ya kujikimu ya wanafunzi (Maarufu kwa jina la boom) ikitoka.Hii inadhihirisha kwamba pesa katika baadhi ya wizara mbalimbali zinatumika na serikali tofauti na maamuzi ya bunge.
6. MAJIBU KUTOKA WIZARA YA ELIMU.
Mh. Spika; Tume hii ilifanya mahojiano na Mh. Waziri wa Elimu kupitia simu tarehe 16/03/2014, Mh. Waziri aliulizwa na tume kuwa ofisi yake ilipitishiwa kiasi cha pesa shilingi 4,225,300/= na je amepokea shilingi ngapi?. Tume hii ilipata majibu ya wazi kuwa Mh. Waziri alipokea shilingi 225,300/= tuu tofauti na kiwango ambacho bunge hili tukufu lilimpitishia.
Mh. Spika; Tume hii ilifanya uchunguzi na kugundua kwamba sababu kuu iliyofanya Wizara hiyo kutokupokea kiwango cha pesa sawa na ilivyopitishwa bungeni ni kutokana na mradi wa kufungua stationary kushindwa kutekelezeka na hivyo pesa yote iliyokua imepitishwa kwajiri ya mradi huo ilisitishwa kutolewa benki, hivyo pesa inayobaki haikutolewa benki
7. MAJIBU KUTOKA WIZARA YA MAKAZI
Mh. Spika; tume hii ilimtafuta waziri wa makazi kupitia simu ya mkononi na kuonana nae yeye mwenyewe ili kumpa taarifa za muda na mahali pa mahojiano, Lakini katika jambo la kushangza Waziri huyo hakutokea katika mahali pa mahojiano na kibaya zaidi alizima simu zake zote. Tume hii haikukata tamaa hivyo kutafuta njia mbadala ya kumpa taarifa waziri huyo kwa kumfata moja kwa moja, Siku ya jumatatu tarehe 17/03/2014, Mwenyekiti msaidizi wa tume alikutana na waziri huyo na kumuliza sababu za kutokuja katika mahojiano na waziri huyo alijibu kua hawezi kuja katika mahojiano sababu mwenyekiti wa tume hiyo hakuwepo siku ya upitishaji wa bajeti yake.
Mh. Spika; Jibu hilo liliifanya tume iwe katika hali ya sintofahamu na baadae ikagundua kwamba huenda Mh. Waziri wa makazi anafanya hivyo akiwa na maslahi yake binafsi nyuma lakini akitumia sababu ya kutokuwepo kwa mwenyekiti wa tume katika kupitisha bajeti yake kama sababu kuu. Tume hii ilijiridhisha kua kutokuwepo kwa mwenyekiti wa tume katika kupitisha bajeti ya wizara ya makazi na ulinzi sio sababu ya msingi ya waziri huyo kutokutii wito wa bunge wa kuhojiwa kupitia tume, hivyo basi ni dhahiri kwamba Mh. Waziri wa makazi alivunja ibara ya 16I. (1)(j) and (L) ya katiba ya UDOSO kwa kuzuia kazi za tume iliyoundwa kwa mamlaka ya bunge na inafanya kazi kama sehemu ya bunge na kutokuheshimu maamuzi ya wabunge wa bunge hili tukufu.
8. MAJIBU KUTOKA WIZARA YA FEDHA
Mh. Spika; tume hii ilimtafuta waziri wa fedha kupitia simu ya mkononi na kuongea nae yeye mwenyewe ili kumpa taarifa za muda na mahali pa mahojiano, Lakini katika jambo la kushangza Waziri huyo hakutokea katika mahali pa mahojiano. Tume hii haikukata tamaa hivyo kutafuta njia mbadala ya kujua sababu za msingi zilizomfanya Waziri huyo kutokuja katika mahojiano, Katika hali isiyo ya kawaida waziri huyo alijibu kwamba hawezi kuja katika mahojiano na hataki kuhojiwa, hivyo basi ni dhahiri kwamba Mh. Waziri wa fedha alivunja ibara ya 16I. (1) (j) and (L) ya katiba ya UDOSO kwa kuzuia kazi za tume iliyoundwa kwa mamlaka ya bunge na inafanya kazi kama sehemu ya bunge na kutokuheshimu maamuzi ya wabunge wa bunge hili tukufu.
CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA KATIKA UTENDAJI WA TUME
Mh. Spika; Katika kutekeleza majukumu yake tume imekumbwa na vikwazo mbali kama ifuatavyo;
Ø Changamoto ya kwanza ni muda kwa wajumbe kwa maana nao pia wanamajukumu mbalimbali na hivyo iliwalazimu baadhi ya wajumbe waache baadhi ya vipindi vya masomo na kufauatilia makujumu yay a tume.
Ø Ukosefu wa pesa za matumizi kwa tume ambapo bunge hili tukufu halikupitisha bajeti ya matumizi ya tume.
Ø Ingawaje tume ilikua na hadidu za rejea na kufanya mambo yake ndani ya mstari wa sharia bila kuvunja sheria au kanuni yeyote, lakini Kuliwepo kwa ujumbe wa tahadhari kutoka kwa ofisi ya mshauri wa wanafunzi kupitia ujumbe wa simu (Kutoka namba 0767035000) kwa kudai kua kikao cha awamu ya nne cha tume si halali wala rasmi(Awamu ya nne ni kukutana na wabunge mbalimbali ili kupata mawazo yao kama wabunge wakiwa nje ya bunge, tarehe 21 & 22/03/2014.
MAONI YA TUME KUTOKANA NA MAJIBU KUTOKA SERIKALINI
Mh. Spika; Tume hii inatoa mapendekezo yafuatayo kutokana na uchunguzi iliyoufanya na majibu ambayo imeyapata, tunaomba waheshimiwa wabunge wayazingatie kwa kuyajadili na kufikia maamuzi yenye tija;
i. Wakati wa kujadili ripoti hii, wabunge wapewe muda angalau wa dakika tano wa kukaa na kujadili maamuzi ya kufikia.
ii. Wabunge wapitishe azimio la kurudishwa kwa pesa kaisi cha shilingi 544,100/= ndani ya siku 2.
iii. Wabunge wapitishe azimio la kurudishwa kwa pesa shilingi 160,000/= zilizoonekana kubadhiriwa ndani ya siku 2.
iv. Wabunge wapitishe Azimio la kumtaka Waziri wa mikopo kumlipa gharama za safari Mh. Naibu waziri wa mikopo ndani ya siku 2.
v. Tume inapendekeza kuwa wabunge kama wataona inafaa wajadili kuhusu kutokua na imani na Mh. Raisi chini ya mshariti ya ibara ya 16 ya katiba ya UDOSO, tume imeona ni busara kupendekeza pendekezo hili kwa sababu zifuatazo;
a. Mh. Raisi amevunja ibara ya 16I. (1) (j) and (L) ya katiba ya UDOSO kwa kuwazuia baadhi ya viongozi kutokuitikia wito wa tume iliyoundwa na bunge hili tukufu na kufanya kazi kama sehemu ya bunge.
b. Mh. Raisi ameonesha dhahiri kutokua na imani ya kifedha baada ya kupokea pesa yote ya Ofisi yake lakini kumpatia Makamu wake pesa pungufu.
c. Mh. Raisi inaonesha alipokea pesa ya pango hiyo toka kwa wahusika wa maduka na ushahidi ni pale alipokiri kuzipokea na kuzitumia pesa hiyo ndani ya kikao cha watu wanne kilichokua na wajumbe muhimu wanne ambao ni Mh. Raisi, Mh. Makamu wa Raisi, Mh. Waziri mkuu, na Mh. Waziri wa fedha na moja ya kikao cha baraza la Mawaziri.
d. Hata kama tukisema pesa hiyo haikulipwa, basi Mh. Raisi amevunja katiba kwa kufanya maamuzi yake binafsi akiwa kama Raisi kwa kuruhusu mpangaji wa maduka yaliyopo skuli ya sayansi ya jamii kutokulipa kodi ya pango kwa wakati bila kushirikisha muhiri wa bungewala kiogozi mkuu wa serikali(Waziri mkuu).
e. Mh. Raisi kaonesha hali ya sintofahamu katika ulipwaji wa pesa ya maduka ya block 09 na 13 yaliyopo skuli ya sayansi ya jamii baada ya maelezo yake kuwa tofauti na maelezo ya muhusika wa pili wa maduka aitwaye Eliza.
f. Mh. Raisi ameshindwa kuwawajibisha baadhi ya Mawaziri kama waziri wa fedha ingawaje alipatwa na hatia za kubadhiri pesa kiasi cha shilingi 544,100/=, kitendo hiki kimeifanya tume kuhisi kuwa huenda pesa hizi zilibadhiriwa na ofisi yake.
g. Utendaji wa Raisi umeonesha kuwa na udhaifu baada yakuonekana anapishana maelezo kati yake na Waziri Mkuu, Waziri wa fedha.
h. Mh. Raisi amebunja katiba kwa kutokuitisha baraza la wanafunzi (College Baraza) ambapo anatakiwa aitishe si chini ya mara mbili kwa kila muhula wa masomo chini ya mashariti ya ibara ya 19 ya katiba ya UDOSO.
vi. Wabunge baada ya kujadili hoja namba (v), waamue kwa pamoja kuwa kiasi cha pesa kinachoonekana kupotea katika ofisi ya Raisi kirudishwe ndani ya siku 2.
vii. Wabunge wapitishe maamuzi ya pamoja kuhusu kufuatilia pesa za malipo ya form za wagombea wa uchaguzi katika uchaguzi wa nwaka 2013/2014, pia wabunge wapitishe maazimio juu ya ufuatiliaji wa pesa tunayoidai serikali ya shirikisho.
HITIMISHO YA UCHUNGUZI WA TUME
Mh. Spika katika kufanya utafiti wetu hicho ndicho tulichokipata na tume inakabidhi ripoti hii kwako ili bunge lako tukufu liweze kuijadili na kutoa maamuzi.
Mh. Spika tunaomba kuwasilisha.