Sheria za nchi yetu zimeganda??

Sheria za nchi yetu zimeganda??

siara

Member
Joined
Jan 4, 2012
Posts
33
Reaction score
4
Tumesoma na kusikia kupitia vyanzo mbalimbali kwamba, nchi yoyote iliyoiva na kukomaa kidemokrasia utawala wake huwa ni wa sheria. Pia tunafahamu kwamba utawala wa sheria huzaa utawala bora katika nchi yoyote ile. Hivyo basi nawiwa kusema 'Utawala bora ni ule utawala wenye kuheshimu na kufuata misingi ya sheria za nchi'. Kwa muktadha huu, nchi yoyote ile inayofuata na kuheshimu utawala wa sheria, watawala wake wanapaswa kutekeleza majukumu yao ndani ya mipaka ya sheria ya nchi husika. Hii ni kwasababu sheria inawataka kufanya hivyo bila kukaidi au kuathiri matakwa hayo, msingi huu wa sheria hujengwa kwenye msingi mkuu wa sheria mama ya nchi husika (yaani Katiba).

Katika utangulizi wangu hapo juu, nimejikuta narudia rudia maneno yanayofanana au kuhusiana sababu ikiwa ni ili wewe msomaji wa makala hii upate kunielewa au kuuelewa ujumbe wangu barabara.
Embu tujikumbushe historia kidogo enzi tukiwa chini ya utawala wa kikoloni yaani Wajerumani katika miaka 1800 hadi miaka ya 1900 na baadae Waingereza katika miaka ya 1900 hadi mwaka 1961 uhuru ulipatikana. Katika tawala zote hizi kulikuwepo na sheria ambazo zilitengenezwa na watawala makusudi ili kufanikisha lengo lao la kunyonya na kukwapua rasilimali za nchi yetu (yaani Tanganyika). Sheria hizi pia zilillenga kuimarisha utawala wao (wa kikoloni) ili kurahisisha usimamizi na uratibu wa shughuli zilizowafanya kuja. Kwakuwa lengo lao lilikua kupata mali ghafi kwa ajili ya viwanda vyao huko ughaibuni kama vile pamba, madini, kahawa, mazao ya wanyama, mkonge n.k . Ilihitajika nguvu kazi ya kuzalisha mahitaji hayo na hivyo sheria zilitengenezwa kuhakikisha kwamba nguvu kazi hiyo inapatikana kwa urahisi bila ya lengo makhususi kukwama. Na endapo yeyote angejaribu kukataa au kukwamisha lengo hilo, sheria zile zingechukua mkondo wake na kutoa adhabu kali ya kupigwa, kufungwa na hata kuuwawa kwa mujibu wa sheria husika.

Kulikuwepo pia na mgawanyo katika ufanyaji kazi kati ya walioenda kufanya kazi kwenye viwanda (processing industries), kwenye mashamba ya mkonge, pamba, kahawa, na kwenye madini bila kusahau wale ambao walifunzwa kuwasimamia wenzao.
Katika kipindi hiki chote, rasilimali zilinyonywa na wakoloni huku watu wakikandamizwa bila huruma kwa msaada wa sheria ambazo ziliitwa 'sheria za kikoloni' (colonial rules) ambazo lengo lake lilikua kutimiza matakwa na haja za watawala na si watawaliwa. Kutokana na mateso waliokuwa wakipata watanganyika chini ya utawala wa kikoloni, waliamua chini ya utangulizi wa baadhi yao Mfano J.K Nyerere, Zuberi Mtemvu,Kasela Bantu, Rashid Kawawa, Abdulwahiid Sykes na wengine kuukataa utawala huu na sheria zake. Hata hivyo hakukua na namna nyingine ya kuondokana nao mbali na kudai uhuru ambao alhamdu Lillah ulipatikana mwaka 1961.

Kwakuwa wote (Watanganyika) walikua na matarajio makubwa juu ya mabadiliko ya sheria kandamizi, unyonyaji, unyanyasaji na ukwapuaji wa rasilimali walifurahia sana kupatikana kwa uhuru huo. Bahati mbaya sana utawala uliochukua nafasi ulijikuta ukiendeleza utamaduni uleule wa kikoloni (colonial bequest) kwa kutumia sheria zilezile na hata kutunga zingine ambazo zilikua mbaya zaidi. Hali iliyopelekea matarajio na furaha yao (Watanganyika) kugeuka kuwa karaha. Serikali mpya ilijikuta ikitengeneza sheria za kulinda madaraka na kuimarasha mifumo ya kiserikali na si vinginevyo. Hii ilipelekea yeyote aliyejaribu kuikosoa serikali kusotwa rumande, kuchapwa viboko au kuwekwa kizuizini. Lakini haikutosha, serikali iliamua kutangaza kuuwawa kwa demokrasia kwa kufuta mfumo wa vyama vingi ambao ulikuwepo hata kabla ya uhuru kupatikana; mfano kulikua na chama cha African National Congress (ANC) chini ya Zuberi Mtemvu na All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT) chini ya Ramadhani Mashado Plantant. Hii ilipelekea kutangazwa kwa mfumo wa chama kimoja ‘Chama kushika hatamu' (yaani TANU).

Tuliendelea na mfumo huu hata baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, katika kipindi cha katiba ya mpito (Interim Constitution) mwaka 1965 na hadi kupatikana kwa katiba ambayo ndio msingi wa sheria zote za nchi mwaka 1977 (sheria mama) inayotumika hadi sasa. Kumbuka katiba hii haikutokana na matakwa ya Watanganyika wala Wazanzibari au wote kwa pamoja.
Hali hii iliendelea hadi kufikia miaka ya 1980 ambapo mashirika ya kimataifa yalihamasisha na kutoa sharti kwa nchi zote kutambua na kuheshimu haki za binadamu hali iliyopelekea mswada wa haki za binadamu (Bills of Right) kufanywa sehemu ya katiba yetu ya mwaka 1977. Ilikua ni nafuu tu kwasababu sheria kandamizi ziliendelea kuwepo hata sasa.

Nimependa kujadili kwa ufupi historia hii kuonyesha kuwa kumbe inawezekana kuwa na utawala wa sheria bila kuwepo kwa utawala bora. Nasema hivi kwasababu, haitoshi tu kuwa na utawala wa sheria lakini sheria zipi au gani?. Kama sheria zenyewe ni mbovu (draconian) basi ni lazima kuwa na utawala m'bovu hata kama unafuata sheria kwani unatokana na sheria mbovu. Tumeona mifano halisi pale ambapo watawala wanajitengenezea sheria za kuwapendelea na kuwalinda wawapo madarakani ili waweze kutawala watakavyo bila kusodolewa na kiumbe chochote.

Si hata mwalimu baada ya miaka yake 24 ya uongozi aliwahi kusema "……mara nyingi tumekua tukitumia sheria hizi mbovu kuwakamata wahalifu na waliodhaniwa ni wahalifu, hii ni mbaya kwakuwa tulishindwa kufuata taratibu za kisheria. Tunapaswa kujirekebisha katika hili na nina uhakika kwamba wa kwanza kujirekebisha ni rais ". Hapa alikua akiizungumzia ile sheria ya Prevention and Detention Act, 1962 ambayo iligharimu maisha ya wengi.
Ni dhahiri na ukweli usiopingika kwamba, ili sheria iwe nzuri na ya viwango (standards) ni lazima itokane na watu (umma) ambayo ndiyo wanufaika wa sheria husika.

Tumesoma maandiko mbalimbali ya wanafalsafa au wanazuoni wa kale mfano Socrate na Plato na hata wanazuoni wa sasa mfano Prof Issa Shivji, Prof John Kabudi, Prof Peter (wote wa chuo kikuu cha Dar es Salaam) na wengine, wamelisisitiza hili.
Kwakuwa nilitangulia kusema ‘sheria mama' yaani ‘Katiba' ndiyo msingi wa sheria zote za nchi, basi sina budi kufikia hitimisho kwa muktadha huu kuwa sheria hii (katiba) ndiyo inayopaswa kutokana na watu (umma) ili sheria zingine zote ziweze kujengwa juu ya misingi yake.

Nachelea kusema, uwepo wa sheria mbovu na ambazo zimekua zikiliingiza taifa letu kwenye michezo ya maigizo zimetokana na ukweli kwamba katiba yetu ya sasa haijatokana na watu (umma). Ubovu wake pia umekua ukitumiwa na watawala kama pitio na mlango wa kufanya watakavyo.
Tumeshuhudia kwa nyakati tofauti viongozi wa nchi yetu wakitoa matamshi kwa makusudi, kuhamasisha vyombo vya usalama na ulinzi kutekeleza wajibu wake kama wanavyotaka wao na si kwa mujibu wa sheria za nchi ili kulinda maslahi yao binafsi. Vilevile tumeshuhudia vyombo vya ulinzi na usalama (polisi) vikiikanyaga sheria na kutumia nguvu pasi lazima dhidi ya raia na hivyo kuwajeruhi, kuwabambikizia kesi, kuchukua mali zao kwa nguvu, kuwapuuza na hata kuwaua kinyume kabisa na mipaka ya kazi yao kwa mujibu wa sheria. Kwa nyakati tofauti tumeshuhudia viongozi wa serikali (mfano wakuu wa mikoa na wilaya) wakijichukulia hatua mkononi kwa kuwaua raia, kuamuru wakamatwe na kushika mali zao kinyume na sheria bila ya mtu yoyote kuwachukulia hatua.

Tumeshuhudia Watanzania wakiibiwa rasilimali zao adhimu na kutoroshwa ughaibuni chini ya usaidizi wa serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama bila ya sheria yoyote kufanya kazi. Nasema hivyo kwasababu rasilimali hizi zimekua zikisafirishwa kupitia viwanja vikubwa vya ndege ambavyo vinamilikiwa na serikali. Kwa mfano vyombo vya habari vya hapa ndani na hata vya kimataifa (local and international media) vimekua vikiripoti taarifa za wizi wa rasilimali zetu kama vile pembe za ndovu, wanyama, mazao ya wanyama kama vile ngozi na madini. Hivi karibuni imeripotiwa kwamba nchi inayoongoza kwa kuuza Tanzanite nje ni India ikifuatiwa na Kenya huku Tanzania ikiwa ya tatu angali ndiyo nchi pekee iliyogundulika kuwa na hayo madini.


Tumeshuhudia wananchi wakinyang'anywa ardhi yao waliorithi toka kwa mababu zao (Inheritance land) na kupewa manyang'au toka nchi za Magharibi na Mashariki ya mbali kwa kisingizio cha uwekezaji. Utadhani nchi yetu haina sheria inayolinda ardhi ya wazawa (indigenous land rights). Cha ajabu, wao huachwa kama yatima wasiojua pakwenda kwenye nchi yao.


Tumeshuhudia mapigano ya wakulima na wafugaji kutokana na ardhi ambayo kila upande unajitutumua kuimiliki. Haya yanatokana na usimamizi mbovu wa sera za ardhi na sheria zake.


Tumeshuhudia rushwa iliyokubuhu ikichukua nafasi katika nchi yetu kwa mapana na kuathiri mfumo mzima. Hivi sasa ukitaka kuwa kiongozi ni lazima utoe rushwa, ukitaka kupata haki mahakamani ni lazima utoe rushwa na ukitaka pia kupata haki isiyo yako unapata kwa kutoa rushwa. Ukitaka kupata huduma nzuri na kwa urahisi lazima utoe rushwa.

Vilevile kumekuwepo na ukwapuaji mkubwa wa fedha za umma kwa watu wachache walioshika madaraka. Mbaya zaidi na cha kuhuzunisha ni pale ambapo wenye nia njema wafichuapo uozo huo ili wahusika washughulikiwe wanakua wameweka maisha yao rehani kwani hutishiwa maisha na kukejeliwa na wahusika bila hata ya haya. Ni dhahiri jeuri walionayo inatokana na ukweli kwamba hawatofanywa kitu.
Hata hivyo tumeshuhudia kuibuka kwa vikundi mbalimbali nje ya utaratibu wa sheria huku zikijipambanua kufanya kazi ya kulinda itikadi zao na maslahi yao. Vyama vya siasa vimeunda vikosi vya ulinzi vya chama na mara kwa mara vimekua vikiripotiwa kupewa mafunzo ya kijeshi bila ya serikali kuchukua hatua za kisheria kuvikomesha. Mfano mzuri ni Green Guard ya CCM na Red Brigade ya CHADEMA.

Vilevile tumeshuhudia vikundi vya kidini vinavyojipambanua kulinda maslahi ya dini na serikali kama kawaida kulifanyia mzaha. Mfano kikundi cha Uamsho. Hili linaashiria mambo mawili; mosi ni kwamba taasisi hizi zimepoteza uaminifu kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na mienendo yao, na Pili ni kwamba taasisi hizi zimeona hakuna wa kusimamia sheria ili kuvikomesha kwani msimamizi mwenyewe ameoza.


Sambamba na hili tumeshuhudia kwa nyakati tofauti viongozi wa vyama vya siasa wakitoa matamko kuvitaka vikosi hivyo kufanya kazi ya kukilinda chama kikamilifu. Ni majuzi tu kiongozi mmoja ambaye ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, aliamuru kikosi cha chama chake (Green Guard) kuwakamata na kuwapiga wanachama wa chama hicho waliokuwa wamehudhuria mkutano wa chama (Kampeni) ambao kwa bahati mbaya hawakupendezwa na kauli alizokua akizitoa mwenyekiti wao jambo lililopelekea wamzomee. Kikosi hicho kilitii amri ya mkuu wake na kuanza kuwashambulia wananchi kuwapiga bila huruma na kuwapeleka kituoni. Wakati haya yanatokea polisi walikuwepo na hawakuchukua hatua yoyote.

Vilevile kwa nyakati tofauti tumesikia vikundi hivi vikituhumiwa kusababisha vurugu pindi upande mwingine unapofanya mkutano wa hadhara yaani CCM au CHADEMA.
Haya yote yaliojadiliwa hapa juu ni udhibitisho pasi shaka kwamba utawala wa sasa hautekelezi majukumu kwa mujibu wa sheria bali kwa mujibu ya watawala.

Pamoja na mapungufu makubwa yaliopo kwenye sheria mama (Katiba) na kupelekea sheria zingine kuwa na mapungufu, lakini bado kujumuishwa kwa muswada wa haki za binadamu (bills of rights) kumepelekea uwepo wa vipengele ambavyo vingeweza kuzuia haya yasitokee. Mfano ibara ya 12 hadi 29 huzungumzia haki za msingi za binadamu na ambazo serikali inapaswa kuziheshimu na kuzilinda lakini hali imekua tofauti kwani serikali yenyewe ndiyo imekua ikizivunja na kuzipuuza.

Je nani atayazuia haya yasitokee.?
Aya hii hapa inaonyesha uwezekano wa kuwepo kwa sheria nzuri zenye kulinda maslahi ya umma na si za watawala lakini bado watawala wakatawala nje ya mipaka yake. Wakati ukifika sheria za nchi zikagandishwa uwepo wake usionekane, basi ujue utawala wa kiimla unachukua nafasi yake (The time when the States' laws freezes, autocracy regime unbolt its way).

Hata hivyo utawala huu kwa uzoefu hauchukui muda kwani watawaliwa hupitia madhwaibu makali katika kipindi cha uwepo wake na hivyo huamua kuchukua hatua mathubuti dhidi yake. Tuna mifano mizuri ya madikteta ambao yawekezekana hawakuwahi kudhani wangeng'olewa lakini wameng'olewa.

Tumewasoma/kuwasikia kina Idd Amini Dada (Uganda), Adolf Hitler (Ujerumani), Generali Muamar Gadafi (Libya), Generali San Abacha (Nigeria), Siad Barre (Somalia) Mobutu Sese Seko (DRC) na wengineo. Hawa wote wametawala kwa mabavu bila kufuata sheria na mwisho wa siku wakaondoshwa kwa aibu na hata wengine kuuwawa.


Turudi kwenye matokeo mengine hasi yatokanayo na kuganda kwa sheria za nchi, leo hii nchi nyingi za Afrika na Mashariki ya mbali ziko kwenye sintofahamu kutokana na sheria za nchi husika kuganda na kukosa nguvu. Tunashuhudia Somalia, tunashudia DRC Congo, tunashuhudia Afrika ya kati, Upande mmoja wa Nigeria, tumeshuhudia Mali, Syria, Sierra Leone n.k. Katika nchi zote hizi kumekuwepo na kila mtu kujiamulia cha kufanya bila ya kuhofia chochote kwani sheria inayomkataza haipo au haifanyi kazi na sasa ushindani wa kupigana na kuuana ndiyo iliyoshika kasi.

Kubaliana na mimi kwamba haya yanayotokea kwa wenzetu, yametokana na sababu zinazofanana au kukaribiana na haya ambayo leo tunayalalamikia kwenye nchi yetu. Kwa maana hiyo hatuna namna tunaweza kujinusuru kutofika huko bila ya hatua muhususi kuchukuliwa kukabiliana na haya yanayoendelea. Swali ni Je nani atayakabili? Serikali haiwezi kukwepa kubeba jumukumu hili kwani ndiyo yenye dhamana ya kulinda katiba ya nchi yetu na kusimamia sheria za nchi. Hata hivyo, kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kuiamini serikali hii tena kwamba itatimiza wajibu wake ipasavyo. Na endapo serikali itashindwa kuyashughulikia haya basi tutajikuta tukifanya ushindani wa kuuana na kuumizana bila kujali.


Rai yangu kwa serikali, kama tunahitaji kuendelea kuzungumza amani isiyo na unafki kwa nchi yetu kama ilivyo sasa, serikali haina budi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria. Idara zote za serikali zisimamie nafasi zao kwa mujibu wa sheria bila kupelekeshwa na matamko ya watu mmoja mmoja waliolewa madaraka. Serikali inapswa kutambua hasara za kuwa na sheria mama isiyotokana na wananchi (umma). Haya yanawezekana kama suala la maadili, uadilifu na uwajibikaji kwa viongozi litapewa nafasi na kuheshimiwa.

KUMBUKA: Taifa lililopotea si lile lililokosa kiongozi, bali ni lile lililokosa utawala wa kisheria. Kupuuzwa kwa sheria haina maana hakuna sheria, ina maana kuna sheria, lakini haitumiki. Hivyo ni kama vile hakuna sheria (A lost nation is not one that lacks a ruler, but one that lacks rule of law. Distortion of law does not mean there is no law, it means there is law, but it is not applied. Thus it is as if there is no law).
 
Back
Top Bottom