Shemsa Mohammed (M/Kiti CCM Simiyu ) Atembelea Kaya 413 Zilizozingirwa na Maji Lamadi

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,992
960

SHEMSA MOHAMMED (M/Kiti CCM Simiyu ) Atembelea Kaya 413 Zilizozingirwa na Maji Lamadi

MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed amefika na kutembelea kaya zaidi ya 400 katika vitongoji vitatu vya Lamadi, Itongo na Makanisani kwenye kata ya Lamadi wilayani Busega Mkoani humo baada ya makazi yao kuzingirwa maji kutokana na kina cha Ziwa Victoria kuongezeka Maji

Akiwa kwenye ziara ya Tarafa kwa Tarafa kwa ajili ya Ujenzi wa Chama na kukagua uhai wake, Shemsa amefika kwenye maeneo hayo na kuiagiza serikali kuchukua hatua za dharura ili kuwanusuru wananchi hao.

‘’Nimeamua nisitishe ziara ya asubuhi ili nije kuwaona, nawapa pole sana…nikuelekeze Mkuu wa Wilaya, kutokana na adha hii tumeona wananchi wanavyoteseka, hatua za haraka zichukuliwe na wenye kuhamishwa wahamishwe kwa haraka’’ amesema na kuongeza.

‘’Hatua za haraka ni kuhamisha hizi kaya na kuziweka sehemu salama ili waweze kupata misaada ya kuishi kwa sasa na misaada hii iende kwa walengwa, nitoe wito kwa viongozi wa vijiji na vitongoji kuhakikisha walipoata majanga wananufaika na misaada itakayotolewa na Dkt. Samia Suluhu Hassan’’

Mkuu wa Wilaya ya Busega Faidha Salum amesema wameanza jitihada za kuwahamisha wananchi hao katika shule za Sekondari Anthony Mtaka na Lamadi.

"Tumeanza jitihada za kuwahamisha kwenda kwenye makazi mengine, tunajipanga kutoa misaada ya vyakula na vyandarua...tunaomba wananchi wananchi waendelee kujihadhari kudumbukia kwenye maji hayo" amesema Faiza.

Kwa upande wake Wakazi wa maeneo hayo wamesema kujaa takataka kwa Mto Lamadi na wananchi kujenga kando ya ziwa ni Moja ya chanzo Cha Maji kujaa katika makazi hayo hali ambayo imesababisha wakose Makazi, Chakula na Malazi.

Wamesema wanaiomba serikali kuharakisha misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, magodoro na madawa ili waweze kunusuri hali iliyopo.

Wameongeza kuwa katika baadhi ya maeneo wanatumia mitumbwi ili kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine huku wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wakikosa kuhudhuria masomo kutokana na hali hiyo.

"Wiki mbili Sasa, vyakula vimelowa maji, hatuna mahali pa kulala, vyoo vimejaa maji na usalama ni mdogo nyakati za usiku kwa sababu ya viboko na mamba...Mto Lamadi umejaa takataka na kusababisha maji kurudi kwenye makazi ya watu, tunaiomba serikali itusaidie kupata mahitaji ya kila siku" amesema Kulwa Lazaro makazi la Itongo.

Naye Monica Mhege amesema wamepata athari kubwa sana kiuchumi na kijamii baada ya nyumba zao kujaa Maji licha ya kutoa taarifa kwa serikali.

Amesema vyoo vimejaa maji Hali ambayo wanahofia mlipuko wa magonjwa ya kuhara na kipindupindu na pia vyumba vya kupanga vimepanda bei kutokana na kaya nyingi kujaa Maji.

"Tumejihifadhi kwa majirani na watoto tunaiomba serikali itusaidie chakula na malazi pia kuboresha miundombinu ya barabara...hatuwezi kufanya shughuli yoyote kwa Sasa, wiki mbili tunapambana na maji, tumeshindwa kupika, magodoro na vyakula vimelowa maji" amesema Monica.

Diwani wa Kata ya Lamadi Laurent Bija amesema wameshapalekea taarifa ngazi ya wilaya juu ya wananchi hao kuzingirwa na maji, na kwamba wanaendelea kuwasihi wananchi kutoingia kwenye maji hayo machafu.

Amefafanua kuwa tayari wameshaanza kuwatambua waathirika katika maeneo hayo ili misaada na takwimu sahihi ziweze kupatikana.
vlcsnap-2024-05-06-12h23m27s003.png
253A1279.JPG
253A1243.JPG
253A1212.JPG
253A1367.JPG

MWISHO
 
Back
Top Bottom