Shairi: Siku Nikipata Demu

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,136
4,298
SIKU NIKIPATA DEMU.
Nasema kinywa kipana , sasa nihofie nini,
Tena nasema kwa vina, kweli kutoka moyoni,
Maneno yatapangana , nitanadi hadharani,
Siku nikipata demu , ulimwengu utajua

Mbona nikipata mwali, mtaona mashauzi,
Nitajifutua kweli,kwa kimwendo cha mapozi,
Mtaniona fedhuli, nikimpata lazizi,
Siku nikipata demu, ulimwengu utajua

Nitakodi tarumbeta, nizurure na vigoma,
Kila kona nitapita, wala sitaona noma,
Nitakua na matata, siku hiyo watakoma,
Siku nikipata demu, ulimwengu utajua.

Nitahonga pesa zote, hadi nyumba ya urithi,
Nitamchumu popote, itakua ni hadithi,
Watanimezea mate , waloniona duyuthi,
Siku nikipata demu, ulimwengu utajua

um'ma wote utajua, siku nikipata demu,
Mbona nitajiashua, niitwe mwendawazimu,
Wataona naugua, waambe sipo timamu,
Siku nikipata demu, ulimwengu utajua.

Sitaacha kujigamba, wajue walo nitema,
Siku hiyo nitatamba, wataicheza tetema,
Midomo wataifumba, watakosa la kusema,
Siku nikipata demu, ulimwengu utajua.

Hapa naweka kamati, nawajuza mjipange,
Siku nikipata Binti, yatawakuta mazonge,
Nitakua madhubuti, anaebisha apinge,
Siku nikipata demu, ulimwengu utajua.

MTUNZI : HAMISI MAGEZY
LAKABU : MAABARA YA TUNGO 📑
DSM, TANZANIA
hamisimagezi@gmail.com
YouTube : malenga wa kiswahili Tz
 
Back
Top Bottom