Shairi: Kwaheri Nyerere.

Chachasteven

JF-Expert Member
Jul 4, 2014
1,878
1,849
1. Dunia yatetemeka,
Giza hasi lagubika,
Mshumaa ulowaka,
Ghafla umezimika

2. Ua lililochipuka,
Juani limenyauka,
Nyota iliyomrika,
Ukungu waifunika

3. Ni majonzi Tanzania,
Sura nyingi zasinyaa,
Kilio juu chapaa,
Mwangwi anga wapasua.

4. Mitima imepasuka,
Barafu imeyeyuka,
Twiga wanasononeka,
Machozi yabubujika.

5. Kifo mithili ya mwiba,
Uchomao mara saba,
Uchungu usiyo haba,
Ubongoni watukaba.

6. Zawaka dimu nyekundu,
Hisiani bandu bandu,
Kifo kimeshika mundu,
Sumu yake kama tandu.

7. Mwenzetu kifo adui,
Kama ugonjwa wa dui,
Apuliza koroboi,
Atunyonge kama tai.

8. Kifo wabeba shujaa,
Watukatisha tamaa,
Kizani wazima taa,
Wafuasi twazagaa.

9. Napotazama mawingu,
Waongezeka uchungu,
Roho imefungwa pingu,
Namuombea kwa mungu.

10. Taifa lashika tama,
Roho zetu zasimama,
Majonzi yanarindima,
Ndani na nje ya chama.

11. Machozi yatiririka,
Hadi mito yafurika,
Kilio kinasikika,
Kambarage katutoka.

12. Ameshafariki baba,
Kiongozi wa nasaba,
Taifa lina msiba,
Nani pengo taliziba?

13. Wanawake wazimia,
Waume twamlilia,
Kovu kwenye hisia,
Kifo kimetuachia.

14. Upweke kama makapi,
Rohoni sawa na upi,
Oooh mwalimu uko wapi?
Tuonane mwaka gani?

15. Tuko sote kimaisha,
Kifo chatutenganisha,
Pichani wanikumbusha
Hisia zanitatanisha.

16. Yetu machozi yatoka,
Mzalendo kaponyoka,
Tena ni simba wa nyika,
Mtu wa watu hakika.

17. Ubongoni kuna doa,
Kifo kimelidonoa,
Nani ataliondoa?
Macho nitapokodoa.


18. Hakika sijiamini,
Nahisi niko ndotoni,
Kandili yetu gizani,
Yazimika safarini!

19. Falsafa bulibuli,
Na mtizamo mkali,
Lugha yake Kiswahili,
Vishindo alihimili.

20. Rafiki wa kila mtu,
Mwenye chuki na mtutu,
Dhabihu ya nchi yetu,
Kupe hawakuthubutu.

21. Hoja na rai mwanana,
Zatukumbusha bayana,
Ukiwa ulotubana,
Ni donda lisilopona.

22. Siku nyingi sikuoni,
Na fimbo yako kwapani,
Mtima una huzuni,
Kukufata natamani

23. Watuacha njia panda,
Hatuelewi pakwenda,
Wingu majonzi latanda,
Mvua machozi yaranda.

24. Afrika tunalia,
Baba umetukimbia,
Mola ndiye alitoa,
Naye amekuchukua.

25. Ulaya wasikitika,
Asia wakukumbuka,
Hata kule Amerika,
Mwalimu ulipendeka!

26. Enzi zile za msoto,
Ukoloni bado moto,
Chifu nyerere Burito,
Katuzalia mtoto.

27. Kazaliwa Butiama,
Kijiji kiko Musoma,
Imara alisimama,
Tambarare na milima.

28. Mwaka wake wa awali,
Moja tisa mbili-mbili,
Akazaliwa kamili,
Baba wa taifa hili.

29. Jina lake Julius,
Nchi yetu kaasisi,
Japo hayuko nasisi,
Rai zake ziko nasi.

30. Mwalimu mshika chaki,
Kwa kabila Mzanaki,
Mzawa mpenda haki,
Alojali wenye dhiki.

31. Baba mwenye familia,
Mke wake ni maria,
Ni mama msamalia,
Nyerere katutunzia.

32. Mzalengo toka Mara,
Mpenda ‘uzanzibara’,
Hakufanya masihara,
Sekondari ya Tabora

33. Yake elimu si bure,
Hakupata tambarare,
Hayati baba nyerere,
Kasomea Makerere.

34. Siyo mtu wa makundi,
Kasoma Scotland,
Alikopata ushindi,
Bila kukwepa vipindi.

35. Shahada ya Uzamili,
Kakuza wake morali,
Kiupeo kawa mbali,
Sawa na kompyuta kali.

36. Fani yake ya walimu,
Ilimpa Ukarimu,
Hakutaka wadhalimu,
Nchi yetu wahujumu.

37. Hapo Pugu kafundisha,
Elimu kahamasisha,
Maarifa karithisha,
Kujenga yetu maisha.

38. Jadi mithili ya Kinu,
Mwalimu ni yetu tunu,
Kama mwasisi wa TANU,
Kichwani lijaza mbinu.

39. Mwaka hamsini na tano
Alihutubia UNO,
Kwendeleza mapambano,
Bila misuguano.

40. Uhuru kapigania,
Nchini na nje pia,
Mabeberu kuwang’oa,
Mhanga kajitolea.


41. Mwaka sitini na moja,
Akajifunga mkaja,
Uhuru pia umoja,
Kavileta kwa pamoja.

42. Njia ya propaganda,
Mabeberu kawashinda,
Serikali akaunda,
Tukafaidi matunda.

43. Ni Rais wa awali,
Kwongoza taifa hili,
Wengi tunamkubali,
Kwa vitendo na kauli.

44. Mwalimu nae Karume,
Walipatana Kiume,
Mwaka sitini na nne,
Wakasema tuungane.

45. Muungano ukafanywa,
Wazalendo kutonyonywa,
Weupe nao kubinywa,
Waloiba kupokonywa.

46. Haki na Mshikamano,
Matunda ya Muungano,
Tukomeshe malumbano,
Kwa kuwaunga mkono.

47. Kiongozi mjamaa,
Taifa kaliandaa,
Amani kwenye mitaa,
Kwa kweli ametufaa.

48. Msimamo na kauli,
Vitisho ulihimili,
Ukahimiza vikali,
Mgao sawa wa mali.

49. Lichukia ubeberu,
Kasisitiza uhuru,
Kapinga kama kifaru,
Vitendo vya makaburu.

50. Azimio la Arusha,
Na mali kutaifisha,
Kuliboresha maisha,
Mabepari kuwatisha.

51. Kipindi cha uhujumu,
Hakukumwagika damu,
Tutakuenzi mwalimu,
Mwingi wa ubinadamu.

52. Alipanga mikakati,
Kama mwanaharakati,
Kaondoa vizingiti,
Viloleta tofauti.

53. Mwenge alituwashia,
Umlike Tanzania,
Utaifa kuinua,
Tofauti kuondoa.

54. Rais mchapa kazi,
Alopinga ubaguzi,
Magendo na ulanguzi,
Kaondoa kila ngazi.

55. Walojaza utajiri,
Kodi kwao sihiari,
Walomiliki magari,
aliwahoji dhahiri.

56. Hakuwaonea soni,
Makaburu wa kusini,
Wasojali masikini,
Haki na utu barani.

57. Mwalimu akiwa hai,
Kawataja maadui,
Wasongao kama tai,
Japo hatujitambui.

58. Wa-kwanza, umasikini,
Huyu yupo kilingeni,
Kafifisha tumaini,
Mbinyo wake wa zamani.

59. Atufanya ombaomba,
Huku twavaa mitumba,
Chombo kinayumbayumba,
Kwa weupe twajikomba.

60. Pili, adui maradhi,
Huyu katuvua hadhi,
Kaangamiza baadhi,
Si vyema kumhifadhi.

61. Kweli maradhi tishio,
Kila sehemu kilio,
Hata sisi tuishio,
Tumekosa kimbilio.

62. Mwisho, adui ujinga,
Vichwani katia nanga,
Atubeba bila tanga,
Ziwani twatangatanga.

63. Ujinga kutotukaba,
Si nyingi pesa kubeba,
Katika zake hotuba,
Kasema Elimu tiba.

64. Adui hawa watatu,
Waponda taifa letu,
Tuwasage kwa viatu,
Watuacha bila kitu.

65. Tusishupaze mioyo,
Tuache pia uchoyo,
Tukizingatia hayo,
Hatutapiga mihayo.

66. Aliupinga utwana,
Umwinyi pia ubwana,
Mali kutajirishana,
Wengi kufukarishana.

67. Amiri jeshi shupavu,
Mwenye jeshi lenye nguvu,
Idd Amini muovu,
Alipigwa nchi kavu.

68. Kwenye vita ya Kagera,
Akakiliza king’ora,
Nduli aliyetupora,
Kageuza misafara.

69. Vijana walimwadhibu,
Idd katia adabu,
Uganda ndani taabu,
Kaenda bara Arabu.

70. Uganda kawakomboa,
Dikteta kapotea,
Kakomesha na ghasia,
Amani wajivunia.

71. Mengi mema ulifanya,
Mabaya umetukanya,
Nduli hukumpa mwanya,
Mwenye roho kama panya.

72. Wale walojisifia,
Kuwa juu ya sheria,
Macho hukuwafumbia,
Njuga ukawavalia.

73. Rais bora wa watu,
Fahari ya nchi yetu,
Miaka ishirini na tatu,
Meongoza bila kutu.

74. Tulimpa mamlaka,
Hakulewa madaraka,
Kwa hiari kang’atuka,
Bila nguvu kutumika.

75. Miaka ya themanini,
Katoka madarakani,
Ukombozi wa Kusini,
Ukienda ukingoni.

76. Kada chama mapinduzi,
Asiyetaka wapuuzi,
Sera zake za uwazi,
Zilionya viongozi.

77. Mwaka tisini na tisa,
Kumi na nne siku tasa,
Mwezi Oktoba hasa,
Kulia ikatupasa.

78. Njozini naona bucha,
Macho nikayapikicha,
Nahisi hakutakucha,
Ndipo chumba nakikacha.

79. Yalipofika machweo,
Nikafungua redio,
Nachosikia kilio,
Kwenye yangu masikio.

80. Baba aliyejikweza,
Kafia Uingereza,
Taifa laomboleza,
MKAPA akatangaza.

81. Mpendwa wetu Rais,
Hakika hayupo nasi,
Ametoweka kwa kasi,
Hospito ya Thomas.

82. Vazi la rangi nyeusi,
Lanitia wasiwasi,
Wanalo watu kiasi,
Nyumbani kwa Julius.

83. Bendera yetu dhabiti,
Iko nusu mlingoti,
Yaupepea umati,
Wenye simanzi la dhati.

84. Wengi hatukuamini,
Tulidhani tu ndotoni,
Kweli tumo msibani,
Mwalimu yuko peponi!

85. Mcheshi kwenye hotuba,
Mfundi kama ngariba,
Mola wetu kambeba,
Tumkumbuke kwa toba.

86. Mwalimu yuko kuzimu,
Ugonjwa kansa ya damu,
Wazawa hatuna hamu,
Kweli chema hakidumu.

87. Mwalimu mwana fasihi,
Ni mengi alitusihi,
Kutwa hadi asubuhi,
Kifo chake si sahihi.

88. Mtunzi wa mashairi,
Siyependelea shari,
Vitabu katafasiri,
Mwanafasihi mahiri.

89. Kambarage ndiye nguzo,
Suluhisho la mizozo,
Hekima yake kigezo,
Kutatua matatizo.

90. Hotuba zake ni mbiu,
Aliwakanya wadau,
Waachane na dharau,
Mwenendo wa kinyang’au.

91. Kakemea utukufu,
Na hali ya ushaufu,
Wasio waadilifu,
Wasitishe majisifu.

92. Kujidai na ukuu,
Ni hulka kuukuu,
Hasa kwa walio juu,
Kila kutwa sikukuu.

93. Alionya ufahari,
Kwenye yetu jamhuri,
Viongozi mawaziri,
Aliwapa ushauri.

94. Rais mwenye huruma,
Aliyetetea umma,
Walemavu na wazima,
Kwa wote alijituma.

95. Kahimiza ufanisi,
Kwenye jeshi la Polisi,
Kuchunga kwenye ofisi,
Matumizi binafsi.

96. Kabeza rushwa na hongo,
Na tabia za malingo,
Kawanasa kwa mipango,
Mafisadi na waongo.

97. Kaweka Sera nchini,
Kutetea tamaduni,
Hakukosa michezoni,
Kuushika usukani.

98. Mpenda nguvu ya hoja,
Kasisitiza umoja,
Wazawa tupate tija,
Bila vya nje kungoja.

99. Nchi kujitegemea,
Vya-nje kutoagizia,
Madeni kuongezea,
Viwanda kutokomea.

100. Mpole sawa na Panzi,
Busara ya kikufunzi,
Baba yetu toka enzi,
Milele tutakuenzi.

101. Bado tulikuhitaji
Upeo hata kipaji,
Maendeleo ya miji,
Na ujenzi wa vijiji.

102. Mtetezi wa amani,
Burundi na duniani,
Hotuba zake barani,
Tuzitunze kama mboni.

103. Damu zilipomwagika,
Ulisaka muafaka,
Viongozi Afrika,
Mbona vita vyalipuka?

104. Oooh! Safari bado ni ndefu,
Njia inao siafu,
Mchungaji maarufu,
Ni kweli sasa ni mfu!?

105. Kijasho kinanitoka,
Mikono yatetemeka,
Kalamu yaniponyoka,
Namuachia Rabuka.

106. Mwenyezi mwenye huruma,
Ulomwingi wa rehema,
Mlaze mahali pema,
Tutamuenzi daima.
 
Back
Top Bottom