RUCCI
JF-Expert Member
- Oct 6, 2011
- 1,701
- 1,714
Serikali imesema haitambui utafiti uliofanywa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), kuhusu malalamiko ya wananchi waishio jirani na Mgodi huo kuharibiwa nyumba zao kwa kupata ufa sehemu mbalimbali kutokana na milipuko inayofanywa na Mgodi.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, alikataa kutambua utafiti huo, uliotoa majibu kwamba Mgodi hauhusiki na mipasuko inayolalamikiwa, akitoa sababu kwamba, sio sahihi GGM kama watuhumiwa kujifanyia wao wenyewe utafiti. Badala yake, Dk Kalemani ameuagiza Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kufanya utafiti huo kwa siku tano kuanzia Jumatatu, Februari 29 mwaka huu na kuwasilisha taarifa yake ili Wizara ifanye maamuzi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea baadhi ya nyumba na majengo mengine ikiwemo Shule ya Msingi, zinazodaiwa kuathiriwa na milipuko ya Mgodi, katika maeneo ya Nyamalembo na Katoma wilayani Geita, Dk Kalemani alisema GST, ambao ni Wakala wa Serikali unaohusika na milipuko, watapitia kukagua nyumba na majengo yote yanayodaiwa kuathirika kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali akiwemo Diwani, Wenyeviti wa Vijiji husika pamoja na Wabunge wa maeneo hayo.“Haiwezekani wewe unatuhumiwa kupasua, halafu unaweka mtaalamu kujichunguza mwenyewe,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kalemani alimwagiza Kaimu Afisa Madini wa Geita, Fabian Mshai kuuandikia barua uongozi wa Mgodi wa Geita, kuwataka ndani ya siku 14, watoe taarifa rasmi kimaandishi, kama wanalitumia au hawalitumii eneo ambalo inasemekana Mgodi huo umeweka vigingi na umezuia wananchi wasilitumie kwa shughuli yoyote wakati Mgodi haulifanyii kazi.
Dk Kalemani alisema kuwa, baada ya kukagua alibaini ni kweli Mgodi unamiliki eneo husika na wameweka vigingi kuzuia wananchi wasifanye shughuli yoyote ndani yake, lakini akasema utaratibu unautaka Mgodi kuwaruhusu wananchi kuendelea kutumia eneo hilo kuendeshea maisha yao ikiwa wao Mgodi hawalitumii.
“Huwezi ukaweka vigingi, ukasema hulitumii eneo, halafu humpi fidia mwananchi wa eneo husika na ukamwacha anaendelea kuzubaa asijue nini la kufanya.”
Hata hivyo, Makamu Rais wa GGM anayeshughulikia Mahusiano na Maendeleo ya Jamii, Simon Shayo, alipoulizwa kuthibitisha endapo Mgodi uliandika barua ya kutoa zuio kwa wananchi wasitumie eneo hilo, alikana kuitambua barua hiyo hivyo Naibu Waziri akasema kwa kanusho lile, wananchi wanaweza kuendelea kulitumia kwa shughuli mbalimbali za kilimo, ufugaji na hata ujenzi.
“Wananchi muendelee na shughuli zenu katika eneo hilo kama kawaida mpaka pale Mgodi utakapokubali kuwafidia. Kama hawatawafidia, hakuna zuio la ninyi kutokufanya shughuli zenu. Mkae, muendelee na maisha yenu kama kawaida,” alisema Dk Kalemani.
Aliongeza kuwa, endapo Mgodi utaamua wananchi waondoke katika eneo husika, haitazuia kulipwa stahili za nyuma kutokana na muda waliopoteza.
“Tamko la Mgodi kuwa hawajawahi kuandika barua ya kuwazuia ninyi kuendelea na shughuli zenu, wote tumelisikia hapa. Sasa, tusubiri taarifa yao rasmi kimaandishi kama nilivyoagiza ili ikitofautiana na waliyosema hapa, tuchukue hatua za kisheria,” alisisitiza.
Aidha, Dk Kalemani aliwaagiza GGM kufikia Jumatatu, Februari 29 mwaka huu, wawe wamekarabati Shimo la Maji lililopo ndani ya eneo lao, ili kuzuia athari za maji hayo kufurika hadi nje ya eneo hilo na kufika katika makazi ya wananchi.“Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010, Kifungu cha 14, inawataka muweke mikingamo na kuzuia athari ya maji pamoja na mambo mengine.”
Akizungumzia agizo lililotolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu kutaka wananchi wanaozunguka Mgodi wa Geita wapewe miamba-taka kutoka mgodini, Naibu Waziri alisema, Tume iliyoundwa na Wizara kufuatilia na kutathmini jinsi kazi hiyo inavyoweza kutekelezwa, inakamilisha taarifa yake na utaratibu unatarajiwa kutolewa ifikapo Februari 28, mwaka huu.
Pamoja na maagizo yote aliyoyatoa, Dk Kalemani alizitaka pande zote mbili, yaani wananchi na Mgodi, kuimarisha mahusiano mazuri baina yao kwani kuishi kwa kutumia sheria pasipo kuwa na mahusiano mazuri, haitawasaidia.
Aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mgodi pale wanapofanya vizuri. “Wakifanya vibaya, lazima sheria itachukua mkondo wake.”
Naibu Waziri Kalemani alikuwa katika ziara ya kazi ya siku 10 ambayo aliihitimisha mkoani Geita, Februari 24. Mikoa mingine aliyotembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara yake pamoja na kukutana na wadau wa sekta za nishati na madini ili kujua changamoto zinazowakabili ni pamoja na Tabora na Kigoma.